Na Dk. Azaveli Lwaitama
Na Dk. Azaveli Lwaitama

Wakomunisti wa Afrika ya Kusini waliingia ubia na ANC ya mabwenyenye weusi ili kutokomeza kwanza ukaburu na mapambano na ubepari yaje baadaye.

Katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, wakomunisti walishirikiana na mabwenyenye wa mrengo wa kulia na kati kutokomeza janga kubwa zaidi wakati huo la ufashisti, yaani ubepari wa mrengo wa wa kulia kupitiliza.

Hivyo hivyo, mapambano ya kuleta uhuru wa Tanganyika yalivyounganisha nguvu za mabwenyenye Wazungu na Waasia pamoja na zile za wakulima na wafanyakazi wa rangi zote kwa azimio lile la mkutano wa mkuu wa TANU wa 1958 pale Tabora.

Hivyo hivyo, Nelson Mandela na ANC waliingia “urafiki wa mashaka” na Fredrick de Clerk kiongozi wa makaburu ili kuondolewa ukaburu kuwe kwa amani ya “kula matapishi” ya kuwalaani huko nyuma kuwa ni wabaya wa Mwaafrika!!

Mabadiliko ya haraka haraka yanayoendelea hapa Tanzania yenye lengo la kuondoa CCM madarakani kama chama dola kinachodumaza na kudhoofisha ushindani wa kisiasa miongoni mwa mabwenyenye watabaka tawala Tanzania ni mabadiliko yatayoleta neema kwa Watanzania wote.

Ile tu CCM kudhoofishwa na kujiunga UKAWA kwa Edward Lowasa ni kuvuja kwa pakacha ambayo ni nafuu ya mchukuzi… Ni kuondoa kizingiti kikuu cha kushamiri kwa demokrasia pana na maendeleo endelevu Tanzania, ambacho ni kuhodhiwa na ukiritimba wa chama dola cha CCM kinachojinadi kama chama cha mrengo wa kushoto wakati ni chama cha mrengo wa kulia kama vyama vyote vya siasa Tanzania kwa sasa.

Kumeguka kwa CCM-Mambo Leo kama taasisi ya kakundi kawana mtandao ulioingiza serikali ya sasa ya Tanzania madarakani mwaka 2005 ni faraja kwa wote wenye kuitakia mema nchi hii na ni kiashiria cha kukomaa kwa vuguvugu la ukombozi wa pili wa Tanzania utakaochukua sura ya demokrasia zaidi ilikuwa na na maendeleo endelevu zaidi yapatikane kupitia kupatikana nafasi chanya zaidi ya kupitishwa kwa Katiba Mpya kama ilivyopendekezwa ndani ya Rasimu ya Pili ya Tume ya Rais iliyoongozwa na Jaji Warioba.

Kwa mara ya kwanza vyama vy siasa vya upinzani kiuhalisia (tofauti na vile ambavyo vimebebwa na watawala wa sasa kwa lengo la kuua upinzani wa kisiasa kijanja kijanja kama ACT- Wazalendo) sasa vimeunganishwa na kupigania Katiba Mpya iliyotokana na maoni ya wananchi yaliyokusanywa na Tume ya Jaji Warioba (UKAWA) badala ya kuunganishwa na kutaka kuondoa CCM madarakani pekee.

Ghafla mwanasiasa mwenye nguvu nyingi ndani ya chama cha kifisadi cha CCM, mwanasiasa ambaye umaaarufu wake umetokana na kuongoza mtandao uliouweka utawala wa sasa wa CCM madarakani, Ndugu Edward Lowasa, amekasirishwa na kukatwa jina lake na aliodhani ni rafiki zake ndani ya CCM na kuamua kusema basi na lolote liwe kwa kujiunga na vuguvugu la kupigania katiba mpya!!

Naye sasa kang’amua kuwa katiba ya sasa na ile Pendekezwa ni za ovyo maana haziruhusu kuwepo mgombea huru bila mizengwe. Hasira za Lowasa zimezaa tunda zuri la kung’amua kuwa Watanzania wanaitaji mabadailiko kupitia Katiba Mpya iliyobebwa ndani ya Rasimu ya Pili ya Tume ya Rais iliyoongozwa na Jaji Warioba. Hasira hizi za mkizi ni furaha ya kunguru na ni busara kwa viongozi wa Chadema na UKAWA kwa ujumla kutoongopa “kula matapishi yao” kwa kumkaribisha Ndugu Lowasa …huyu huyu waliomwita fisadi… kujiunga na UKAWA na kugombea urais. Nafasi ya kihistoria imejitokeza ya kukiondoa CCM madarakani kwa amani!!

Sishangai wasaliti wa vuguvugu la kukiondoa CCM madarakani wanatushauri sisi Watanzania wenye shauku ya kuutumia upenyo huu wa mpasuko ndani ya CCM kukiondoa CCM madaraka!!! Eti tuombe radhi kwa” kula matapishi yetu” wote tulio wahi kumwita Lowasa fisadi! Wao wanataka tuendelee kuvumilia kutawaliwa na CCM labda kwa miaka mitano au zaidi hivi mpaka chama kipya cha watakatifu kiitwacho ACT-Wazalendo kitakapo kuwa tayari kututawala badala ya CCM!!

Sishangai kusikia ushauri huu kutoka kwa wasaliti hawa ambao kazi yao hata huko nyuma imekuwa nikuudhoofisha upinzani dhidi ya CCM na kukisaidia CCM kiendeleee kuwa madarakani!! Hawa jamaa ni wasomi sana na ni wajanja sana, ilo lazima kulikiri!!!

Sitashanga kama haya ninayoyasema yatapigwa madogo na wasaliti hawa!! Historia itakapoandikwa baada ya UKAWA kupata viti vingi zaidi Bunge lijalo au hata kuuchua urais na kupata Katiba Mpya iliyobebwa ndani ya Rasimu ya Pili ya Tume ya Rais iliyoongozwa na Jaji Warioba itawapa hukumu yao stahiki, wajanja na welevu hawa!

Bila shaka wanaoomba UKAWA ishindwe kupata viti vingi Bunge lijalo na iukose urais na hivyo tuendelee kutawaliwa na CCM na wao wapate viti vya kutosha kuwa viongozi wakuu wa eti upinzani muruwa wenye maadili ya Azimio la Arusha Tanzania!! Ni haki yao ya binadamu kuendelea na matumaini haya kama na sisi tulivyo na haki ya kuendelea na matumani yetu ya uwezakano wa ushindi mnono chini ya UKAWA dhidi ya ukiritimba wa chama kimoja chama dola cha CCM!

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.