KUNA moja tu litaloweza kukinusuru Chama cha Mapinduzi (CCM) kisiporomoke katika Uchaguzi Mkuu ujao: upinzani uliogawika na unaopigana wenyewe kwa wenyewe badala ya kujumlisha nguvu zao pamoja dhidi ya hasimu yao mkuu.

Na Ahmed Rajab
Na Ahmed Rajab

Kuna uwezekano mkubwa kwamba kisipojiangalia na kujirudi kwa haraka, CCM kinaweza hata kikapasuka na kugawika. Ni upinzani ulio dhaifu usiosimama kama kitu kimoja utaoweza kukipa nafasi chama hicho kiendelee kuwa hai.
Vyama vya upinzani vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vinalielewa hilo. CCM nacho hali kadhalika kinalijuwa hilo na kitafanya kila kiwezacho kuchochea mtafaruku katika kambi hiyo ya wapinzani.
CCM kinaweza kufanya mengi kuzusha mtafaruku huo. Kinaweza, kwa mfano, kikawanunua baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani; kinaweza kikatia chokochoko na kuwafitinisha viongozi wa upinzani; na kinaweza kuzusha uvumi wa kuwakashifu baadhi ya viongozi hao ili wafuasi wao waingiwe na sumu dhidi yao.
Hivi ni vitimbi ambavyo Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimekwishawahi kuvitumia nyakati mbalimbali katika juhudi zake za kuudhoufisha upinzani. Bila ya shaka, kinaona kuwa ni afadhali kutumia hila za aina hiyo kushinda kutumia nguvu.
Hizo nguvu nazo pia hutumiwa, mara baada ya mara, na vyombo vya ulinzi vya dola kwa niaba ya chama kinachotawala.
Chama hicho kilicho kikongwe kushinda vyama vyote vya siasa Tanzania na chenye mitandao ya kisiasa, kiuchumi na ya kijamii iliyotanda nchi nzima, kinatambua kwamba kisipoweza kufanya hivyo kitachezeshwa kindumbwendumbwe mitaani Oktoba 25, mwaka huu.
Si kazi rahisi kukishinda chama kilichojijenga namna kilivyojijenga CCM, na hasa ikiwa chama hicho kimeshika hatamu za kuiendesha nchi kwa zaidi ya nusu karne. Hata hivyo, safari hii kuna sababu nyingi zinazoashiria kwamba CCM huenda kikakiona cha mtema kuni.
Hamna shaka yoyote kwamba chama hicho kimepata mshtuko mkubwa hivi karibuni kiasi cha kuwafanya baadhi ya viongozi wake waanze kutaharaki. Wameingiwa hofu ya kwamba chama hicho kitaathirika vibaya kwa kupata pigo kubwa katika uchaguzi ujao.
Ikiwa jahazi la CCM litapanda mwamba kuna uwezekano mkubwa kwamba viongozi wake kadhaa wataamua kuchupa na kujitosa baharini wakikiacha mkono chama chao. Kazi ya kuliokoa jahazi haitokuwa tena yao. Itakuwa ya wale wataosalia chamani. Mustakbali wa chama utakuwa mikononi mwao na wataweza kuufinyanga watakavyo.
Kitachohitajika ndani ya chama hicho ni mijadala ya fikra na nadharia itayoweza kuibua itikadi mpya itayotumika kwa lengo la kutunga sera zitazoweza kuwanufaisha wananchi wa kawaida. Itikadi hiyo iweze kukiunganisha chama badala ya kutegemea chama kiunganishwe katika umoja wa kulindana viongozi walio na nyendo za kifisadi.
Kwa chama kilichopoteza dira mijadala aina hiyo ya itikadi na sera ni muhimu katika juhudi za kukirejesha chama katika misimamo yake.
Kuna watu ndani ya CCM, miongoni mwao viongozi, ambao bado wanaamini kuwa ni haki yao kuitawala nchi milele. Katika muda wa kama mwaka kutoka sasa chama hicho kitakuwa na mwenyekiti mpya, Dk.John Magufuli.
Tatizo hapa ni kwamba mwenyekiti huyo mpya atakuwa anakiongoza chama kitapokuwa kimejeruhiwa vibaya sana katika Uchaguzi Mkuu ujao. Hilo halina shaka na viongozi wa chama wenye kuona mbele wamekwishalitambua.
Kiongozi huyo mpya itambidi aikubali hali halisi ilivyo nchini. Mwanzo kabisa akubali kwamba wananchi wengi wanataka mageuzi katika mfumo wa utawala. Aidha, itambidi pia aachane na dhana za kujidanganya kwamba hapana mbadala wa chama chao katika kuliendesha na kuliongoza taifa.
Jambo kubwa analopaswa Magufuli alitambue atapoushika usukani wa chama chake ni kwamba atakuwa anakiongoza chama chenye wafuasi wengi wa kizazi kipya walio na hisia na misimamo tofauti na ile ya wazee wao; na kwamba hata na wao wanataka patokee mabadiliko katika jamii yakianzia ndani ya chama chao wenyewe.
Kwa yote hayo, kiongozi huyo mpya, ikiwa atashinda au atashindwa katika uchaguzi wa Oktoba, atalazimika ahakikishe kwamba chama chake kitashinda katika chaguzi zijazo ili kiweze kuleta mageuzi ya maana katika nchi. Mageuzi hayo ni pamoja na ya utawala bora, aina ya utawala ambao utawapatia wananchi maendeleo wanayoyataka ya kiuchumi na ya kijamii.
Katika mchakato wa kuwapata wagombea wake wa chaguzi katika ngazi mbalimbali imethibitika kwamba CCM kimekuwa kikitumia mbinu na hila zilezile kama kilichozoea kutumia wakati wa mchuano baina yake na vyama vya upinzani.
Chama hicho kimekuwa kikitumia pesa (kuwahonga wenye kura zao ndani ya chama) pamoja na vitendo vingine vya ghiliba, vya viini macho. Hivi ni kusema kwamba CCM kinaendelea na mpigo uleule, katika chaguzi za ndani ya chama kama kinachozitumia kinapochuana na mahasimu wake.
Jambo kubwa na linalofanywa kwa uwazi kabisa bila ya kificho wala kuoneana haya ni namna fedha zinazomwagwa kuwahonga wenye kura ndani ya chama. Na fedha zimefanya na zinaendelea kufanya kazi yake katika chaguzi mbalimbali ndani ya chama, chaguzi zenye kuamua nani na nani watakuwa wagombea wa ubunge, viti maalum vya bunge, udiwani, uwakilishi na hata wa urais. Si bure Wahispania wakawa na msemo wao kwamba “Pesa humchezesha ngoma mbwa,” yaani hata mbwa naye huwa tayari kucheza ngoma anapooneshwa pesa. Na ndani ya CCM wapo wasioona haya kujigeuza mbwa, wakiwa tayari kucheza ngoma ya anayewahonga ili wampe kura zao.
Tunaweza kusema kwamba ingawa CCM ni chama cha siasa, kuna baadhi ya viongozi wake wanaotamani kukigeuza chama chao kisiwe chama cha kisiasa. Wangeweza wangetaka hata siasa ziwe si za kisiasa. Wangetaka zizidi kuwa siasa za pesa.
Na ingawa kweli kuna aina fulani ya demokrasia ndani ya CCM lakini kwa kweli demokrasia hiyo ni demokrasia ya pesa. Kinachowashughulisha wanasiasa wa chama hicho ni pesa.
Wanasiasa hawa wana matatizo mengi. Moja ni hilo la kutapia pesa; la pili, na ambao huenda likawa linachangia kuzusha hilo tatizo la pesa, ni kwamba hawaielewi hata historia ya chama chao wenyewe. Wengi wao hawaijui nadharia iliyotumiwa kukizalisha chama chao.
Ingawa kwa sasa chama cha CCM kinaonekana kama kilichoungana hakuna asiyejuwa kwamba kinajikaza kisabuni. Tujuavyo ni kwamba kuna mapambano makali, ya wenyewe kwa wenyewe, yanayoendelea baina ya kambi tofauti za wanasiasa walio ndani ya CCM.
Lenye kuhuzunisha kuhusu CCM ya leo ni jinsi chama hicho kilivyogeuka na kupoteza mwelekeo wake. Kwa msamiati wa kileo chama hicho siku hizi kinafuata sera za ulibirali mamboleo, hususan katika mambo ya uchumi.
Wengi wa wanasiasa wake wameingia katika chama hicho wakiwa na lengo la kupata vyeo na ulwa serikalini. Wanasahau kwamba lengo la wanasiasa wenye msimamo ni kuutumikia umma. Wakijiingiza katika siasa na baadaye wakachaguliwa mawaziri watakuwa wanafuata sera ulibirali mamboleo ambazo ni zenye kwenda dhidi ya maslahi ya umma.
Chama kinahitaji kiongozi jasiri, atayeheshimiwa na kuaminiwa na umma na atayethubutu kukifanyia ukarabati chama hicho.
Katika enzi hizi za “twitter”, za mablogi, mitandao na majukwaa ya mawasiliano ya kijamii taifa hili linahitaji siasa za aina mpya, za mtindo mpya zinazosibu enzi hizi. Mitindo hiyo mipya itasaidia kuzigeuza siasa ziwe siasa za “demokrasia shirikishi” yaani siasa za mfumo wa demokrasia utaowafanya wananchi washiriki kikamilifu katika utungaji wa sera na utekelezaji wa sera hizo.
Haitoshi kwamba tuna taasisi za kisiasa, vyama vya siasa na wanasiasa wanaotakiwa watawale kwa kuwakilisha matakwa ya kisiasa ya wananchi na hivyo kuwafanya watawala wawajibike kwa wananchi. Yote hayo ni muhimu na yanahitajika. Lakini hayatoshi.
Na hayatoshi kwa sababu madaraka yanadhibitiwa na wachache ndani ya vyama vya siasa. Wenye nguvu za madaraka hufanya watakavyo na walio dhaifu wanateseka.
Inahuzunisha kuwaona baadhi ya viongozi wakifanya watakavyo huku wakiyapuuza matakwa ya watu wa kawaida kama tulivyoshuhudia yaliyotokea karibuni na yanayoendelea kutokea ndani ya CCM. Ili kuistawisha demokrasia nchini si CCM pekee bali vyama vyote vya siasa vinahitaji kuwa na viongozi wenye kuiamini kwa dhati dhana ya demokrasia shirikishi na wawe wanafanya kila jitihada ya kuitekeleza dhana hiyo.

 Chanzo: Raia Mwema

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.