Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kutoka Chama cha Wananchi (CUF) leo wametoka nje ya ukumbi wa baraza hilo kwa kile wanachodai kuwa ni ukiukwaji wa sheria, ikiwemo kujaza askari Polisi na wengine wakivaa ninja katika uandikishaji wa Daftari la Wapiga Kura unaloendelea visiwani Zanzibar.

Makamu Mwenyekiti wa CUF, Juma Duni Haji.
Makamu Mwenyekiti wa CUF, Juma Duni Haji.

Wakizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Ofisi za chama hicho Vuga mjini Unguja, wajumbe hao walisema wameamua kutoka kwa lengo la kupinga matukio yanayoendelea kutokea katika uandikishaji wa daftari hiyo kwa wilaya ya Magharibi ambayo yanakwenda kinyume na sheria za nchi.

Akizungumza kwa niaba ya wawakilishi na mawaziri wa SMZ kutoka upande wa CUF, Mwenyekiti wa chama hicho, Juma Duni Haji, alisema ni jambo la kushangaza katika nchi iliyokubali demokrasia kuona askari wanavaa ninja bila ya sera zao wakiwatisha watu wanaokwenda kujiandikisha.

“Huu jamani ni uhuni. Unaingiza majambazi katika vituo vya kujiandikisha halafu unasema ni askari wa kulinda amani. Hebu niambieni mumeona wapi mambo hayaa isipokuwa hapa kwetu?” alihoji Haji, akiongeza kuwa tangu kuanza kwa uandikishaji huo kisiwani Unguja, “kumekuwa na vurugu kutokana na Chama cha Mapinduzi (CCM) kuingiza wageni na watoto wadogo kutoka nje ya majimbo husika.

Hata hivyo, Waziri huyo wa Mawasiliano na Uchukuzi kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa inayoongozwa na Rais Ali Mohamed Shein wa CCM, alisema wao wametoka barazani lakini wataendelea kuwa mawaziri na wawakilishi mpaka mwisho wa serikali ya awamu hii.

“Sisi ni mawaziri na tutakuwa mawaziri mapaka Rais atakaposema basi au muda wetu kumalizika, sambamba na kuwa wawakilishi hadi litakapovunjwa Baraza la Wawakilishi hapo tarehe 26 Juni mwaka huu,” alisema Haji.

Haji, maarufu kama Babu Duni, alieleza kuwa wataendelea kuitumikia serikali lakini hawatojishughulisha na shughuli za Baraza hilo kwa kipindi hiki, na hawatohudhuria katika ufungaji wake ambapo Rais Shein atalihutubia na kisha kulivunja rasmi Baraza hilo hapo tarehe 26 Juni.

Kabala ya kugomea shughuli za Baraza hilo, Waziri huyo wa Mawasiliano na Miundombinu alisimama na kutoa malalamiko hayo kwa Spika Pandu Ameir Kificho na baadaye wajumbe wote wa CUF wakatoka nje huku wakiacha bajeti ya Wizara ya Fedha ikiendelea kujadiliwa.

Mapema Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Nassor Ahmed Mazrui, mwenyewe akiwa Waziri wa Biashara na Viwanda, alisema ameziona kambi za jeshi tatu zanzibar zinatumika katika kuwapatia watu vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi (Zan IDs) kinyume na utaratibu.

“Nimekwenda mpaka kwenye kambi ya Chukwani, nikakaaa kwenye geti, nikaziona gari tatu namba ninazo, wanaingia na vijana ambao ni watoto wadogo na watu kutoka Tanzania Bara kwa ajili ya kupewa vitambulisho vya Zan IDs,” alisema Mazrui.

Kwa mujibu wa mwakilishi huyo wa jimbo la Mtoni, Wilaya ya Magharibi, Unguja, tayari CUF ilishamueleza Rais Jakaya Kikwete, ambaye ndiye Amiri Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania juu ya namna Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) linavyotumika katika siasa wazi wazi, lakini bado hali haijabadilika na badala yake jeshi hilo linaendelea na mchakato huo kama kawaida.

Alisema kwa ushahidi walionao kambi za jeshi Chukwani, Mwalimu Nyerere, Bububu na Dunga iliyooko Wilaya ya Kati, ndizo ambazo zinahifadhi vijana kwa ajili ya kuandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kinyume na sheria za nchi.

Akijibu suali la endapo CUF itashiriki kwenye uchaguzi mkuu baada ya yote hayo, Waziri Mazrui alisema licha ya uharibifu wote unaotokea, hawatosusia uchaguzi na watashiriki kwa gharama yoyote.

“Hapa hapana dezo kuwa tuwaachie CCM wachukue serikali hivi hivi tu. Tutashiriki uchaguzi kwa vyovyote vile itakavyokuwa,” alisema Mazrui, akiongeza kuwa kwa mazingira yoyote yatakayokuwa, chama chake kimejipanga kuwakomboa wananchi na dhuluma iliyodumu muda mrefu.

Kitendo hicho cha kususia kikao cha Baraza kilionekana kuwakasirisha wawakilishi wa CCM waliokuwemo wakati huo na kuwafanya wote kutaka GNU ivunjwe. Akichangia bajeti ya Wizara ya Fedha, mwakilishi wa Kwamtipura, Hamza Hassan Juma, aliliomba Baraza hilo kuongeza siku tatu ili aweze kupeleka hoja binafisi ya kuwataka wananchi kupiga kura ya maoni kuamua kuwepo au kutowepo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
“Waziri ndiye anasusia shuhuli za serikali ndani ya Baraza hili. Kwa kweli ni hili gumu na si vyema kuendelea na Serikali ya Umoja wa Kitaifa, kwani wenzetu hawaitaki,” alisema Juma, aliyewataka pia mawaziri wote waliotoka kurejesha magari ya serikali wanayoyatumia.
Hivi karibuni, Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Salum Kassim Ali, aliwaambia waandishi wa habari kwamba Tume yake haina mafungamano na taasisi yoyote ile katika ufanyaji kazi wake na wamekuwa wakifanya kazi zao kwa ustadi mkubwa. CUF, kwa upande, iliwasilisha mbele ya waandishi wa habari kile ilichokiita ushahidi wa kuwepo kwa mtandao mkubwa unaoishirikisha ZEC, vyombo vya dola, masheha, wakuu wa wilaya na mikoa pamoja na Mamlaka ya Vitambulisho katika kuisadia CCM kwenye uchaguzi.

Habari hii imeandikwa kutokana na mitandao mbalimbali ya kijamii.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.