NILIPONUKUU maneno aliyoniambia Samwel John Sitta kupitia simu ya mkononi (rudia makala iliyopita), sikujua bwanamkubwa huyu ana kiburi cha kupindukia mpaka.

Mshangao niliopata kuhusu hulka yake hiyo baada ya kumsikiliza Septemba 2014, haujapungua uzito. Sikuwahi kumjua kwa sura yake halisi. Na tatizo zaidi linakuja ninapojiuliza hivi mtu huyu mwenye hadhi kubwa kisiasa kutokana na kupata vyeo vikubwa serikalini, anajisikiaje anapoporomosha maneno ya chuki na ubabe? Najisumbua. Mtu na hulka yake inafanana na mbwa na bwana wake – wanapatana na kurandana nyakati zote, iwe jua iwe mvua. Ni hakika kabisa Sitta ana hulka ya kiburi na jeuri hata pale anapojua fika anaowaonesha sifa hizo mbaya ni watu wanaofikiri sawasawa na kwa kiwango.

Sasa amejifunua zaidi na amejikaanga kwa mafuta yake. Ni kama pweza – kujikunja kadiri anavyoguswa na uzito wa moto huku akizidi kuteketea. Pweza, samaki mtamu na ambaye mchuzi wake una rutuba muhimu kwa ujenzi wa mwili wa mwanadamu, huangamia kila anapojipinda akifikiri anapambana na moto anapochomwa. Ajabu Sitta anavyojifanya msahaulifu.

Na Jabir Idrissa
Na Jabir Idrissa

Amesahau kishindo alichopata ukumbi wa Sekondari ya Haile Sellasie, mjini Zanzibar, mwaka 2011, aliposhuhudia upinzani wa Wazanzibari kuhusu muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba aliokwenda nao kwa lengo la kuuelimisha. Hakustiriwa chembe, bali alioneshwa waziwazi kuwa Wazanzibari walio wengi hawataki kuburuzwa na kufanywa kama vile watu wasiojitambua au watoto wasioelewa historia ya nchi yao, mila na desturi yao, na kwa jumla, utamaduni wao. Muswada aliopeleka ulichanwa mbele yake na ujumbe wake akiwepo Samia Suluhu Hassan ambaye alikuja kuwa makamu mwenyekiti wake katika Bunge Maalum la Katiba.

Sitta alitakiwa kurudi kwa waliomtuma Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kilichochuja na kukataliwa Zanzibar, na sasa Tanganyika ambako kimekuwa kikiamini kingali na mvuto. Nilisema Sitta hastahili kuheshimiwa wala kufikiriwa kuwa kiongozi na kutarajia kura za Wazanzibari. Nikamweka kundi na Bernard Kamilius Membe, ambao wanapatana.

Sitta ametangazia vita Wazanzibari wenye asili ya Pemba. Ameonya wasimchezee na kwa wale wanaojitia kupinga Muungano, anasema, ole wao, watakiona cha mtemakuni. Amewaweka wananchi hao kundi moja na viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) akisema atawashughulikia kwa nguvu zake zote atakapokuwa Rais wa Tanzania. Swadakta. Ujumbe wake umewafika Wazanzibari. Wazanzibari wanaoupinga muungano wa mfumo wa serikali mbili unaolelewa na CCM, si Wapemba tu, hata Unguja. Wanataka Muungano wa serikali tatu, tena wa kuipa Zanzibar mamlaka yake kamili.

Wakati Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilipokuwa ikipita majimboni kukusanya maoni ya Wazanzibari kuhusu wanavyotaka Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano iwe, walijadili kwa upana mustakbali wa Muungano. Walitaka mabadiliko ya mfumo, na ikibidi kama hautabadilishwa, basi walihiyari uvunjiliwe mbali. Hivyo basi, kwa upinzani wa muungano wa mfumo unaolelewa na CCM, Sitta na wenzake waliokusudia kuwavurumishia mizinga na maji ya kuwasha Wazanzibari, watambue si Wapemba tu watakaokutana nao. Sitta amedhihirisha asivyo muungwana bali mwanasiasa jeuri na mpenda uongozi wa mabavu.

Anapenda kulazimisha watu kutaka atakalo na atakavyo; kuamini anavyoamini na anavyofikiria. Hataki mawazo yasiyoendana na yake. Mhafidhina. Ameapa atavunja ngome ya CUF kisiwani Pemba. Huyu mwanasiasa anayetafuta kupewa dhamana ya kuongoza jamhuri ambayo Zanzibar ni sehemu muhimu, anachekesha. Unavunjaje ngome ya CUF iliko asili yake? Sitta amefika Zanzibar kutafuta wanachama wa CCM wa kumdhamini katika fomu zake za kuomba ateuliwe kugombea wadhifa wa urais wa Tanzania ifikapo Oktoba 2015.

Anafika Pemba ambako ni sharti kwa kila muombaji wa uteuzi huo kufika na kupata wadhamini, kati ya wale 450 wanaotakiwa kwa mujibu wa kanuni za chama chao. Maneno yake hayo ndiyo ujumbe anaowaachia wananchi wa Pemba. Na kwa mantiki ya mjadala huu, ndio ujumbe anaowaachia Wazanzibari – “ole wao, nitawaonesha cha mtemakuni.” Ina maana Sitta amedhamiria kuongoza kwa chuki na hasira dhidi ya wananchi wasioukubali Muungano kwa mfumo unaolelewa na kung’ang’anizwa na CCM, kama vile kilivyofanikiwa kuubakisha mfumo huo kwenye Katiba Inayopendekezwa, iliyopitishwa kiunajimu na Bunge Maalum la Katiba aliloliongoza.

Alikuwa Sitta aliyeapa kutimiza kura za kufikia theluthi mbili ya mahitaji ya kuidhinisha katiba kuwa imeridhiwa na bunge hilo. Kweli alifanikiwa kufikisha matakwa ya sheria, lakini kila mjumbe wa bunge na yeye mwenyewe wanajua kwa uhalisia, ghushi iliyotumika. Na ajuwe iko siku ukweli wa kilichotokea utawekwa wazi na yeye na wenzake kuchukuliwa hatua. Sitta amewakosea Wazanzibari na ameikosea nchi yao. Ameidharau historia ya Zanzibar na utamaduni wa Wazanzibari kupenda ukweli na utamaduni wao. Ameandika historia ya kishetani isiyosahaulika na historia.

Aliowatuma wamfanyie kazi ya kishetani wanasema walichokitenda. Wanasema walichokipata. Hata kama hawasemi hadharani, wanasema na nyoyo zao. Wanasema. Kwa kuwa walichokifanya baada ya kutumwa kukifanya chini ya maelekezo yake Sitta, ni kibaya kisichokubalika kisheria na kimaadili, dhamira zao zinawaumiza hata kama wanapotezea. Sitta mwenyewe hawezi kujiangalia sawasawa kama mtu muadilifu. Amejifutia ile dhana yake ya utendaji wa kiwango na kasi. Haikustahili kasi na kiwango katika kupanga maovu. Hata kidogo.

Dhana hii ilipaswa na inapaswa kutumika kutengeneza kitu kizuri kinachosaidia kuandika historia ya maendeleo ya kweli ya mwanadamu na siyo uchafu na uhalifu. Hata chembe. Sitta amejibiwa na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad ambaye anasubiri tu muda achukue fomu ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kuwania tena kiti cha urais wa Zanzibar. Sitta anamjua Maalim Seif. Anakumbuka majibu yake alipokwenda kumshawishi asaliti Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) eti kwa kumuahidi cheo na fedha.

Masikini Sitta ameshindwa kusoma alama za nyakati. Alikubali vipi kubeba mzigo mchafu na kumfikia mwanasiasa anayefahamika alivyo muungwana, muadilifu, muaminifu na makini kiuongozi na kidhamira? Hajui Maalim Seif amechukua ahadi kuwa na Wazanzibari itakavyokuwa. Kwa kuwa Sitta hatarajiwi kupika wala kupakua yanapokuja masuala wanayoyaamini Wazanzibari kuwa ni haki yao, ajue alijiumbua na kuumbuka mwenyewe. Amejishusha.

Kilicho kibaya zaidi ni kuendelea kujishusha kwa kujitwisha mfupa uliomshinda fisi – kuyabadili matumaini ya Wazanzibari kuhusu kupata mamlaka kamili. Tofauti na anavyoeneza chuki za kidini na usultani. Walishindwa waliomtangulia, atashindwa binafsi na CCM anayoiabudu imteue.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.