Tume  ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imepinga kutumika kwa Vikosi Maalum vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwenye shughuli zozote zinazohusiana na uchaguzi mkuu unaotazamiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.

Akizungumza na Zanzibar Daima kwenye ofisi za Tume hiyo zilizopo Maisara mjini Zanzibar, Mkurugezi wa ZEC Salum Kassim Ali alisisitiza kuwa taasisi yake pekee ndiyo inayohusika kwa asilimia zote na uchaguzi na wala si kwa msaada wala ushirikiano wa taasisi nyengine yoyote ya dola ambayo haikupewa jukumu hilo kisheria.

 “Vyombo vya dola, kila chombo kina sehemu yake, sisi tunachotakiwa tutumie jeshi la Polisi pekee. Sheria ya Uchaguzi imeainisha vituo vya kupigia kura na mambo mengine ya uchaguzi yatasimamiwa na vyombo vya ulinzi, yaani Polisi, siyo idara maalum. Vikosi vingine hatuvileti sisi. Hatuna mahusiano na idara maalum hata moja,” alisema Mkurugenzi huyo wa Tume ya Uchaguzi.

Kauli hii ya Kassim inakuja huku kukiwa na tuhuma nzito kutoka kwa wadau mbalimbali wa uchaguzi wa Zanzibar kwamba ZEC si taasisi iliyo huru kwenye kufanya kazi zake na kwamba hupokea amri na kutumika na vyombo vyengine vya dola, ikiwemo Idara ya Usalama wa Taifa na Vikosi Maalum vya SMZ, ambavyo navyo hutumikia Chama cha Mapinduzi (CCM).

Miongoni mwa shutuma hizo ni zile zinazojitokeza kila mwaka wa uchaguzi kwa kuonekana ZEC ndio inayoruhusu vikosi hivyo kutumika sehemu mbalimbali za vituo vya uchaguzi na ambapo vikosi hivyo huhusishwa na uvunjifu wa amani na kushindwa kufuata sheria ya uchaguzi inayolitaka jeshi la polisi pekee kutumika kipindi cha uchaguzi katika kuimarisha ulinzi na kulinda amani na utulivu kipindi chote.

Kassim alisema kuwa Tume yake “inashirikiana kikamilifu na wadau wa uchaguzi kama vile vyama vya siasa, asasi za kiraia na vyombo vya habari na waangalizi wa uchaguzi wa ndani na nje ili kuweza kufanisha uchaguzi huo kwa uhuru na haki.”

Akizungumzia matayarisho ya uchaguzi wa mwaka huu, Kassim alisema ZEC imejipanga kufanikisha uchaguzi mkuu huo kwa kuwatumia maafisa uchaguzi wa wilaya wenye uzoefu, kuepuka ucheleweshaji wa vifaa kwenye vituo vya kupigia kura.

“Kwa sasa tuna maafisa Uchaguzi wa Wilaya ambao wanajua kifaa kipi kinakwenda wapi na saa ngapi na ninahitaji nini katika kazi zangu. Hivyo mpango wa usimamizi wa uchaguzi unakwenda vizuri. Kila mtu anajua majukumu yake na wajibu wake,” alisema mkurugenzi huyo, akiongeza kwamba mwaka huu “usambazaji, uhesabuji na upangaji wa vifaa vya uchaguzi mkuu utawasilishwa mapema iwezekanavyo kwenye vituo vyote vya uchaguzi kote Unguja na Pemba  ili kuepuka usumbufu kwenye vituo vya kupigia kura kwa kutumia uzoefu wa chaguzi zilizopita tangu mwaka 2005, 2010 na kura ya maoni mwaka 2010.”

Lakini wakati ZEC ikijihakikishia kuwa uchaguzi huu utakuwa huru na wa haki na uliopangiliwa vizuri zaidi, Chama cha Wananchi (CUF) – ambacho ni mmoja wa wadau wakuu wa uchaguzi huo – kinasema Sekreterieti ya ZEC inayoongozwa na Mkurugenzi ina matatizo makubwa. Hivi karibuni, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kwamba ZEC inashirikiana na kile alichokiita “mtandao” unaojumuisha masheha, wakuu wa wilaya na mikoa, vikosi vya SMZ na Idara ya Vitambulisho.

Akizungumzia suala la umuhimu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa visiwani Zanzibar, Kassim alitoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kwenye uchaguzi ukuu utakaofanyika tarehe 25 Oktoba, akiwataka wailinde amani na utulivu ulioletwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambapo Tume hiyo ilifanya kazi kubwa kuhakikisha serikali hiyo inapatikana.

Wakati huo huo, imefahamika kuwa Tume inaendelea na uchunguzi wa mwisho wa ugawaji wa majimbo ya uchaguzi kwa mujibu wa mamlaka iliyopewa kisheria. Kikawaida Tume ya Uchaguzi hugawa majimbo kila baada ya miaka minane hadi kumi au baada ya serikali kugawa mipaka mipya ya utawala. Ugawaji huo ulitakiwa ukamilike mwaka uliopita lakini ulicheleweshwa baada ya kile kinachosemekana Tume ilipata taarifa kuwa serikali inajiaandaa kugawa mipaka ya kiutawala.

Tayari Tume imeshatangaza Ratiba ya Uchaguzi itakayoanza utekelezaji wake tarehe 14 Agosti na kumalizika tarehe 28 Oktoba, ikijumuisha uchaguzi mkuu wa rais, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na madiwani. Uchaguzi huo utakwenda sambamba na ule wa rais wa Muungano na ubunge, ambao utasimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa uwakala wa ZEC.

Habari hii imeandikwa na Salum Abdullah Salum, ZJMMC

One thought on “Hatushirikiani na Vikosi vya SMZ – ZEC”

  1. Sasa wewe muandishi mbona hukumuuliza huyo mwenyekiti wa tuma ili atupe majibu kuhusu yale magari ya Jeshi (JWTZ) yanayo onekana yakipakia watu kutoka kwenye matawi ya CCM na kuwapeleka kwenye kambi ya (JWTZ) Chukweli kuwaandikisha ni vipi na picha zao zipo au yale magari ni ya Polici?

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.