Leo tuongee uchumi kidogo. Kuna watu wanapenda namba lakini hawajui hesabu. Kama na wewe ni mmoja wao, tafadhali usisome makala hii.
Wabunge wengi na mawaziri wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ni wagonjwa wa namba. Wanapenda namba lakini hawajui hesabu. Kwa kuwa viongozi wako hivyo, wamewaambukiza hata na wananchi wa kawaida, wakiwemo hata wale wanaoitwa kuwa ni wafanyakazi, ambao hutakiwa wawe tabaka la kati. Ukitaka wakushangilie, wewe ongeza tarakimu tu kwenye namba. Wanapenda namba lakini hawajui hesabu!
Kama ulikua unamlipa mtumishi mshahara wa 500,000 (laki tano) mwaka jana, mwaka huu mlipe 700,000 (laki saba). Atashangilia na kukushukuru. Kumbe hajui upande wa pili gharama za maisha zimeifanya hiyo 700,000  iwe sawa na 100,000 (laki moja) tu ya mwaka jana. Yeye atakushukuru tu, kwa sababu anapenda namba lakini hajui hesabu!
Naona wengi hamjanielewa. Ni hivi kuna faida gani kulipwa mshahara wa shilingi 2,000,000 (milioni mbili) halafu ukauziwa sukari kilo moja shilingi 3,000? Si bora ulipwe 500,000 tu lakini sukari uuziwe shilingi 500 kwa kilo? Kama unapenda namba lakini hujui hesabu, huwezi kunielewa.
Twende kwenye historia kidogo. Mwaka 2005, wakati Rais Benjamin Mkapa anaondoka madarakani, bajeti ya serikali ilikuwa shilingi trilioni 7. Mwaka huu wa 2015, yaani miaka kumi baadaye, ni shilingi trilioni 22. Wanaopenda namba lakini hawajui hesabu wameshaanza kushangilia eti “Bajeti imekua!” Huu ni ujinga wa kiwango cha shahada ya juu ya uzamifu (Phd) kabisa!
Ukweli ni kwamba bajeti haijakua ila imezidi kuporomoka. Na hapa tukokotowe hesabu pamoja.  Ni hivi: mwaka 2005, bajeti ilikua trilioni 7 na thamani ya dola moja ya Kimarekani ilikuwa sawa na shilingi 650 za Kitanzania. Hivyo, ukichukua shilingi trilioni 7 ukazigawanya kwa shilingi 650, utapata dola 10,769,230, yaani dola milioni kumi na laki 7. Mwaka huu, bajeti ni trilioni 22 na thamani ya dola moja ya Kimarekani ni shilingi 2,250 za Kitanzania. Ukichukua trilioni 22 ukazigawanya kwa hizo shilingi 2,250, utapata dola 9,777,777, yani dola milioni 9 na laki 7.
Hii ina maana kuwa bajeti ya mwaka huu wa 2015 (dola milioni 9) ni ndogo kuliko bajeti ya mwaka 2005 (dola milioni 10).
Maana yake ni kwamba kwa miaka 10 yote tumepiga hatua 9 mbele tukarudi nyuma hatua 10. Wanaopenda namba lakini hawajui hesabu, hawawezi kunielewa!
Haiwezekani bajeti ya mwaka 2005 iwe kubwa zaidi kuliko bajeti ya mwaka huu, wakati mwaka huu mahitaji ni makubwa zaidi kuliko ya 2005. Watumishi ni wengi zaidi, miradi ya maendeleo ni mingi zaidi na hata idadi ya watu ni kubwa zaidi. Hivyo tulitegemea bajeti ya mwaka huu iwe kubwa zaidi. Kubwa maradufu kuliko ya mwaka 2005. Lakini cha ajabu imekua ndogo kuliko ya 2005. Halafu wabunge wa CCM wanaopenda namba bila kujua hesabu wanashangilia eti bajeti imepanda.

Tafsiri hii ya bajeti inamaanisha kuwa kwa miaka 10 ya utawala wa Rais Jakaya Kikwete wa CCM, tumeshindwa kwenda mbele japo hatua moja. Badala yake tumerudi nyuma kwa hatua moja (10-9). Kwa lugha rahisi ni kuwa maisha ya leo yamekuwa magumu zaidi kulinganisha na maisha ya miaka 10 iliyopita.
Yaani mtumishi aliyekuwa analipwa mshahara wa shilingi 300,000 (laki tatu) mwaka 2005, aliishi maisha mazuri zaidi kuliko mtumishi anayelipwa shilingi 1,000,000 (milioni moja) hivi leo. Unajua kwa nini? Kwa kuwa mwaka 2005, kilo moja ya sukari ilikuwa shilingi 500, kwa hivyo kwa mshahara huo wa 300,000, mtumishi huyo alikuwa una uwezo wa kununua kilo 600 za sukari kwa mwezi. Leo sukari kilo moja ni shilingi 2,200, kwa hivyo kwa mshahara wa shilingi 1,000,000 anaweza kununua kilo 454 tu za sukari. Hapa tunasema nguvu ya ununuzi ya shilingi imeporomoka maradufu. Wanaopenda namba lakini hawajui hesabu hawawezi kunielewa!

Mwaka 2005 mfuko mmoja wa saruji uliuzwa baina ya shilingi 4,500 hadi 5000. Kwa maana hiyo, mtumishi aliyelipwa mshahara wa shilingi 300,000 aliweza kununua mifuko 66 ya saruji. Leo mfuko mmoja wa saruji ni baina ya shilingi 20,000 hadi 25,000. Hivyo mtumishi anayelipwa shilingi 1,000,000 ana uwezo wa kununua mifuko 40 tu ya saruji.
Mfumko wa bei kuanzia mwaka 2005 hadi sasa 2015 ni wa kiwango cha asilimia mia nne (400%). Maana yake ni kwamba bidhaa zimepanda mara 4 ya bei yake kwa kipindi cha miaka kumi tu. Nyama iliyokua inauzwa kilo moja shilingi 1,000, sasa hivi inauzwa baina  ya shilingi 4,000 hadi 6,000. Mchele uliokua ukiuzwa shilingi 350 kwa kilo moja, sasa hivi ni shilingi 1,500. Nauli ya daladala iliyokuwa shilingi 100, hivi sasa ni shilingi 400. Lita ya mafuta ya taa ilikuwa shilingi 350, hivi sasa  inakaribia shilingi 2,000. Kimsingi kila bidhaa imepanda bei mara nne au zaidi ya bei yake ya mwaka 2005. Hiyo ndiyo tafsiri ya kwamba mfumko wa bei ni wa kiwango cha zaidi ya 400%.
Katika uchumi, mfumko wowote wa bei unaoanzia na tarakimu tatu na kuendelea huitwa “hyper-inflation”, yaani mfumko wa bei wa kiwango kibaya zaidi unaoweza kuathiri uchumi wa nchi kabisa. Kama ni lazima kuwe na mfumko wa bei, basi nchi inapaswa kuwa na mfumuko wa bei wa kawaida (moderate inflation) ambao ni wa tarakimu moja. Yaani mfumko ukiwa wa kuanzia asilimia moja (1%) hadi tisa (9%), huo ni mfumko wa kawaida na hauna athari kubwa kiuchumi.
Lakini sisi tuna asalimia 400 za mfumko wa bei. Hii ni hatari sana. Hivi punde tutawakaribia Zimbabwe au Somalia na kuanza kutembea na hela kwenye matoroli. Hata wao walianza hivi hivi!

Thamani ya shilingi inaporomoka kila siku na watu wanashangilia. Huu ni uzwazwa wa kiwango cha Phd. Jiulize, embe lililokua likiuzwa shilingi 50 pale sokoni Buguruni, leo linauzwa baina ya shilingi 500 hadi 1,000. Mara 20 zaidi. Kwa mtindo huu, ukitaka kujua bei ya embe miaka 10 ijayo chukua bei ya sasa (shilingi 1,000) halafu zidisha mara 20, utapata shilingi 20,000. Kwa hivyo, tukipata rais kama Rais Kikwete, miaka 10 ijayo tutanunua embe moja kwa shilingi 20,000. Wallahi, itabidi tuwe na noti ya shilingi 100,000.
Kama embe limepanda bei mara 20 tangu mwaka 2005 hadi 2015, tutegemee lipande tena mara 20 kuanzia 2015 hadi 2025, ikimaanisha mwaka 2025 bei ya embe itakuwa 20,000. Ukitaka kununua embe kumi utakuwa unaenda na shilingi 200,000. Sasa sijui wale wafanyabiashara wa embe wanaonunua kwa fuso watalipa bei gani? Bila shaka watalipa mabilioni kadhaa kwa fuso moja. Yaani unaenda kwa mkulima na fuso lako limejaa noti na mkulima anapakua noti akimaliza anapakia maembe. Huko ndiko serikali ya CCM inakotaka kutufikisha.
Nisiongee sana maana napata tu hasira bure na huenda hata hamnielewi.

Chanzo: Makala ya Malisa GJ kwenye mtandao wa WhatsApp – Mhariri

One thought on “CCM wapenda namba lakini hawajui hesabu”

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.