WENGINE wakimwita “Maalim Salim”, wengi wakimwita “Sheikh Salim” na wakisikia anaitwa “Maalim” wakishangaa kwa sababu walikuwa hawajui kwamba Salim Mzee, aliyefariki dunia Ijumaa iliyopita akiwa na umri wa miaka 99 na miezi mitatu, ujanani mwake alikuwa mwalimu.


Wengi waliotambua kwamba aliwahi kuwa mwalimu wakidhani kwamba akisomesha katika skuli za kawaida. Lakini Salim Mzee, aliyepata umaarufu Afrika ya Mashariki nzima katika fani ya utangazaji wa redio, akisomesha katika Skuli ya Mafunzo ya Polisi (Police Training School).
Juu ya hayo, utangazaji wa redio ndio uliomjenga; naye, kwa upande wake, alikuwa miongoni mwa wachache walioijenga fani hiyo Zanzibar. Kuna waliojaribu kuyaiga mahadhi yake ya utangazaji wasifanikiwe.

 

Na Ahmed Rajab
Na Ahmed Rajab

Salim Mzee akijua namna ya kuchagua maneno ya kuyatumia, wapi pa kuyatilia mkazo na lafudhi yake siku zote ilinyooka. Hakuwa na ulimi ulioyaponda maneno. Utaona raha namna alivyokuwa akilitamka jina “Zanzibar” si kama baadhi ya watangazaji wa leo wanavyolitamka: “Zanzibaa.”
Si lafidhi yake ya Kiswahili tu iliyokuwa nzuri bali hata za Kiarabu na Kiingereza. Watu wengi wamesahau na pengine wengine hata hawana habari kwamba kabla ya Mapinduzi ya 1964 Sauti ya Unguja pia ilikuwa ikitangaza kwa Kiarabu, Kiingereza na Kihindi.
Kwa upande mmoja, ubingwa wake wa utangazaji ulitokana na ugwiji wake wa lugha za Kiswahili, Kiarabu na Kiingereza. Ugwiji huo aliupata kutoka kwa waalimu waliomsomesha Zanzibar ilipokuwa na mfumo wa elimu uliosifika Afrika ya Mashariki.
Waalimu wa enzi hizo, kwa mfano, hawakusomesha masomo ya kawaida tu bali pia wakifundisha maadili na mwenendo mzuri. Nadhani kufuata mafundisho ya waalimu wake ndiko kulikomfanya awe “mtu mwenye kustahiki kuheshimiwa,” kama alivyomwelezea rafiki yangu mmoja juzi.
Salim Mzee alizaliwa Unguja na alikuwa miongoni mwa kundi la pili au la tatu la wanafunzi wa Zanzibar walioanza kusomeshwa katika skuli za kawaida. Skuli ya mwanzo ya serikali ilifunguliwa visiwani humo 1905 kwa jitihada za Sultan wa siku hizo, Seyyid Ali bin Hamoud (aliyetawala kutoka 1902 hadi alipojiuzulu ufalme 1911 na akaenda kuishi uhamishoni Paris alikofariki 1918, akiwa na miaka 34.)
Baada ya kumaliza masomo yake ya msingi, Salim aliingia Skuli ya Kujifunza Ualimu (Teachers’ Training School, kwa ufupi TTS), taasisi pekee ya elimu ya juu iliyokuwako Zanzibar siku hizo. Huko TTS alisomeshwa na magwiji. Miongoni mwao alikuwa L.W. Hollingsworth, Mwingereza aliyeishi Zanzibar kwa miaka 13 na ambaye baadaye aliandika kitabu kuhusu historia ya Zanzibar na kingine kuhusu Kiswahili.
Mwalimu wake mwengine wa Kiingereza alikuwa Mohamed Salim Barwani (maarufu kwa jina la Jinja), aliyebobea kwa ‘umombo,’ na aliyewahi kuwa mwanafunzi wa Hollingsworth.
Jinja, ambaye ni babu mzaa mama wa mwanasiasa Mansour Yusuf Himidi, alikuwa mtu mwenye hisia za kizalendo aliyehitimu baadaye katika Chuo Kikuu cha Oxford, Uingereza.
Si ajabu kwamba Salim Mzee aliondokea kuwa na lafudhi nzuri ya Kiingereza kwa sababu waalimu wake wa Kiingereza walikuwa ndio hao — Hollingsworth na Jinja.
Mwalimu wake mwengine anayetajika ni Maalim Abdallah Hadhrami, aliyekuwa mwanafunzi wa mwanzo kutiwa skuli Zanzibar 1905. Binafsi nilibahatika kwamba alikuwa mmoja wa waalimu wangu wa Kiarabu katika King George VI Grammar Secondary School (ambayo sasa inaitwa Lumumba College).
Abdulla Hadhrami alikuwa na njia zake za kusomeshea zilizokuwa nje ya zile alizopangiwa kwa mujibu wa minhaji (silibasi). Kwa mfano, nakumbuka alikuwa hatufundishi sarufi na nahau ya Kiarabu tu au mashairi ya al-Mutanabbi, mshairi wa kale wa Kiarabu, lakini akisimama mbele ya klasi mawazo yake yakitembea kwingi kwani alikuwa ameogelea katika bahari tofauti — za lugha, fasihi, historia, siasa na masuala ya kijamii.
Kwa vile akipenda kusoma magazeti na kusikiliza redio, Abdulla Hadhrami akiweza kutuchambulia matukio mbalimbali ya ulimwengu.
Siwezi kusahau siku moja 1960 namna alivyoyachambua matabaka ya Uingereza alipoposwa Princess Margaret, mdogo wa Malkia wa Uingereza, na mpiga picha Antony Armstrong-Jones, aliyekuwa mtu wa kawaida na si wa aila ya kifalme.
Wengine waliomsomesha Kiarabu Salim Mzee walikuwa Mmisri aliyekuwa akiitwa Abdul Bari al-Aziji, Maalim Abdulla al-Kindi na Sheikh Burhan Mkelle, mtaalamu wa lugha hiyo ambaye moja ya vitabu alivyotunga ni kitabu cha sarufi ya Kiarabu kwa mashairi ya Kiarabu na cha utangulizi wa kujifunza Kiarabu, “Tamrin al-Atfal,” kilichochapishwa Cairo, 1918. Sheikh Mkelle alisomea Cairo na kati ya vitabu vingine alivyotunga kwa Kiarabu katika miaka ya 1920 ni “Al Burhaniyat”, mkusanyiko wa mashairi, na “Tarikh Jazirat al-Qamar al-Kubra” (Historia ya Ngazija).
Waalimu wengine wa Salim Mzee walikuwa Ibrahim Kassim (bingwa wa hisabati), Kassim Abdul Hafidh pamoja na Amour Ali Ameir, ambaye baada ya adha za Mapinduzi ilimbidi akimbilie Oman ambako aliujenga msingi wa elimu wa taifa hilo.
Katika Zanzibar ya miaka ya 1930, mtindo uliokuwapo ulikuwa kwamba wanafunzi waliohitimu TTS wakitafutiwa kazi na Hollingsworth katika idara za serikali. Salim Mzee alipomaliza masomo March 1934 alipelekwa kufanya kazi ya ukarani katika idara ya forodha, akisubiri kuajiriwa kuwa mwalimu.
Fursa hiyo aliipata Novemba mwaka huohuo ilipofunguliwa Skuli ya Mafunzo ya Polisi (PTS). Huko alisomesha Kiingereza na akawa Mkuu wa PTS (1936-1954) akimrithi mzungu. Miongoni mwa askari aliowasomesha ambao baadaye walishiriki katika Mapinduzi ya 1964 ni Eddington Kisasi, Ramadhan Haji (aliyewahi kuwa waziri kiongozi) na Ibrahim Amani, aliyekuwa mjumbe wa Baraza la Mapinduzi.
Wakati redio ya Sauti ya Unguja ilipofunguliwa na kuendeshwa na serikali, Salim Mzee aliingiwa na shauku ya kutangaza. Mara ya mwanzo alipoomba kazi hiyo bahati haikuwa yake; alikataliwa.
Bahati ilimwangukia ama 1954 au 1955 alipoomba tena naakakubaliwa. Wakati huo mtangazaji aliyekuwa aking’ara kwa sauti yake tamu alikuwa Ali Buesh, aliyekuwa pia mwanamuziki. Buesh baadaye alikwenda Misri kusomea fani ya muziki.
Alipoondoka Buesh ndipo Salim Mzee akawa yeye mbele katika fani ya utangazaji naSauti ya Unguja ilistawi kwa ajili yake. Alikuwa miongoni mwa watangazaji wa mwanzo wa redio katika Afrika ya Mashariki. Miongoni mwa watangazaji wa Kizanzibari walikuwako wawili wengine, David Wakati na Ahmed Rashad Ali, waliokuwa wakivuma miaka hiyo ya mwanzo ya utangazaji wa redio katika Afrika.
Lakini David Wakati, ambaye kama Salim Mzee, alikuwa “mtangazaji wa watangazaji” kwa sauti yake ya kuvutia, akilifanyia kazi Shirika la Utangazaji la Tanganyika (TBC) na pia BBC, London, isipokuwa kwa muda mfupi baada ya Mapinduzi aliporudi kwao akateuliwa Mkurugenzi wa Utangazaji. Ahmed Rashad naye baada ya kufanya kazi Sauti ya Unguja akinguruma kwenye “Sauti ya Afrika kutoka Cairo” na alijipatia umaarufu kwa matangazo yake ya kuupinga ukoloni.
Miongoni mwa watangazaji aliofanya nao kazi Salim Mzee ni Yusuf Mohamed, Joseph Asama, Sanura Shakhsi, Mdungi Usi, aliyekamatwa na kuuliwa bila ya kufikishwa mahakamani katika awamu ya mwanzo ya Mapinduzi.
Watangazaji wengine mashuhuri aliofanya kazi nao ni Septi Suleiman, Haidar Jabir, Ramadhan Ali (mtangazaji mstaafu wa Sauti ya Ujerumani) na Zeyana Seif, ambaye baadaye alikuwa mtangazaji wa mwanzo wa kike wa idhaa zote za BBC, za Kiingereza na lugha nyingine, kusoma taarifa ya habari.
Salim Mzee aliwapiku watangazaji wengi kwa sauti yake tamu, lafdhi ya matamshi yake na upeo wa aliyokuwa akiyajua. Ni mtangazaji aliyekuwa akipewa dhamana ya kutangaza mambo muhimu na makubwa ya kiserikali toka siku za utawala wa kikoloni hadi baada ya Mapinduzi.
Alifundishwa kazi na maofisa wa idara ya habari, wakiwemo Yahya Alwi na Mohamed Saleh Farsi. Halafu alipelekwa Nairobi kujifunza zaidi tasnia ya uandishi habari wa redio katika Kenya Institute of Mass Communications (KIMC). Alipohitimu alitunukiwa stashahada.
Mwaka 1964 Salim Mzee alipata fursa ya kuwa miongoni mwa waandishi wa habari kutoka barani Afrika waliotembelea nchi kadhaa za Ulaya ya Mashariki kwa miezi michache wakihudhuria semina mbali mbali.
Salim Mzee alishikilia vyeo kadhaa vya utangazaji kama vile Mkuu wa Habari na mwisho akawa Mkurugenzi wa Utangazaji. Alistaafu 1978.
Baada ya kustaafu alipumzika kwa muda wa kama miezi mitatu halafu Rais Aboud Jumbe alimtaka arudi kuutumikia umma alipokuwa anatayarisha kuliunda Baraza la Wawakilishi (BLW). Salim Mzee akateuliwa msaidizi wa Katibu wa Baraza hilo na mwisho akawa kaimu wa Katibu mpaka alipostaafu 1990.
Mbali na kazi zake rasmi, Salim Mzee akijishughulisha na mengine pia. Alikuwa mjumbe wa Baraza la Kiswahili la Tanzania na kuna wakati akiwafundisha watu wazima kuandika na kusoma katika mtaa wa Mtendeni.
Miongoni mwa wanafunzi wake walikuwa wazegazega na wauza kahawa waliokuwa wakitafahari walipoanza kusoma na kuandika.
Salim Mzee akiwavutia wengi katika baraza zake hususan ile ya karibu na jengo la Manispaa, Darajani, iliyobandikwa jina la utani la “Baraza la Wawakilishi.” Hapo alikuwa kinara wa kustawisha “barza”. Watu wakivutiwa kwa ujuzi wake mkubwa wa lughana kwa maarifa yake.
Miongoni mwa watu wa baraza hiyo alikuwa Rais Jakaya Kikwete kabla hajawa Rais alipokuwa akikitumika chama chake Zanzibar. Wengine walikuwa mawaziri, wanasiasa, watumishi wa serikali na wasomi.Ndo Salim Mzee akawa“msomi wa wasomi” hususan kuhusu siasa, taarikh (historia) — hasa ya Zanzibar, ya Afrika ya Mashariki na ya ulimwengu wa Kiislamu.
Baraza yake ya mwishoni mwa uhai wake ilikuwa ya “Kwa Calypso” iliyo kwenye duka moja katika eneo hilo la Darajani.
Miaka hii michache iliyopita alipokuwa akishindwa kutoka nje watu wakimwendea kwake kuchota viwili vitatu kutoka kwenye kisima cha hazina ya kumbukumbuku na maarifa yake.
Siku zote, juu ya meza, ubavuni mwake, kulikuwa vitabu na magazeti mbali mbali, pamoja na Raia Mwema ambalo alikuwa halikosi. Akisoma vitabu vya Kiswahili, Kiarabu na Kiingereza na vya kila aina — riwaya, siasa, historia na dini.
Nakumbuka kumtembelea ofisini mwake alipokuwa Mkurugenzi wa Utangazaji kabla hajastaafu 1978. Alinyosha mkono wake kunionesha safu ya vitabu. Vyote vilikuwa vimeandikwa na Karl Marx, mwanzilishi wa falsafa ya Umarx. Halafu kwa dhihaka akanambia: “Mwambie Abdulla, nimeviramba vyote hivi!”
Abdulla ni mwanawe na rafiki yangu mkubwa. Sifikiri kama “aliviramba” kweli vitabu vyote; nadhani akitufanyia tashtishi kwani alikuwa akizipinga siasa zetu.
Nayajuwa hayo kwa sababu alikuwa mtu asiyebania mambo, kama hapendi kitu akikwambia wala hakuwa mtu wa porojo na chokochoko. Ndio maana akipendeza kwa watu naalipokuwa akizungumza akivutia. Alikuwa muungwana na mtamaduni.
Kwa vile hakujidai kwamba akijuwa kila kitu hakuwa akiona haya kuuliza asichokijua. Lakini ingawa kwa kawaida alikuwa mtu mpole na wa mizaha wakati mkibishana na akihisi kwamba unasema upuuzi hamaki zikimpanda. Hata hivyo, hamaki hizo zikizimika mabishano yalipokwisha.
Sheikh Salim Mzee, gwiji wa utangazaji wa redio na msomi wa wasomi, alikuwa miongoni mwa watu wa kupigiwa mfano Zanzibar. Atasalia kuwa mtu wa kupigiwa mfano na hapatotokea mwengine mfano wake kwani alikuwa mtu pekee wa aina yake.

 

Chanzo: Raia Mwema

 

 

2 thoughts on “TAABINI: Salim Mzee, “mzee wa Calypso” 1916-2015”

  1. Nimevutika sana na makala haya yaliomuelezea Maalim Salim Mzee. Katika maelezo haya wengi watapata kuwajua ijapokuwa kwa ufupi walimu wa daraja la Hollingsworth waliowasomesha wazee ambao bila shaka ni tunu ya Taifa letu. Napenda kusahihisha jambo moja: Ali Buesha hajawahi kuwa mtangazaji Sauti ya Unguja. Aliyefanya kazi na maalim Salim alikuwa ni ndugu yake Saleh Buesh. Naye alisifika vile vile kwa sauti yake. Wote hao watatu walikuwa ni marafiki. Wenzangu wa Mchangani wanaweza kuthibitisha hili.

    A. Abdalla

  2. Makala nzuri sana Bwana Ahmed Rajab.Zanzibar ilikuwa na kila ya aina ya watu wenye ujuzi na maarifaya ya fani tofauti.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.