Kwa wengi duniani, kuanzia nchi yake ya asili – Kenya – hadi nchi jirani ya Tanzania na mataifa kadhaa ya Ulaya na Marekani ambako ameishi na kufanya kazi, Abdilatif Abdalla anafahamika kama mshairi na mwalimu wa lugha. Kwa wachache, wanamkumbuka kama kijana wa miaka 22 aliyekwenda jela kwa sababu ya kuandika na kusambaza maoni yake chini ya udadisi wa “Kenya Twendapi?”.

Mimi nilianza kuisikia “Sauti yake ya Dhiki” – mkusanyiko wa mashairi yake akiwa kifungoni – nikiwa na umri wa miaka 16 katika Skuli ya Utaani, Pemba. Hiyo ilikuwa mwaka 1993. Miaka 10 baadaye, nikaanza kuwasiliana naye nikiwa nimeunganishwa na mwandishi bingwa wa kazi za fasihi, Prof. Said Ahmed Mohamed, ambaye alimkabidhi diwani yangu ya kwanza kabisa ya mashairi “Machozi Yamenishiya” aiweke dibaji. Wakati huo, Prof. Said alikuwa akisomesha Chuo Kikuu cha Bayreuth na Abdilatif akisomesha Chuo Kikuu cha Leipzig, vyote viwili nchini Ujerumani.

Sasa mchana mmoja, miaka 12 baada ya kuwasiliana naye kwa mara ya kwanza kwa njia ya barua-pepe, ninakaa naye kitako – mimi nikiwa mwandishi wa habari na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya Deutsche Welle mwenye umri wa 38, naye mhadhiri mstaafu wa lugha ya Kiswahili wa Chuo Kikuu cha Leipzig mwenye umri wa miaka 69. Mahala ni Chuo Kikuu cha Bayreuth, kusini mwa Ujerumani. Na kwenye mazungumzo yangu naye, najikuta kuwa nimemuona “mtu” kwa kila maana halisi ya neno hilo.

Ugunduzi wangu huo ulikuja kuthibitishwa baadaye na Profesa Kai Kresse wa Chuo Kikuu cha Columbia, Marekani, ambaye ameandika “Mapitio ya Kenya Twendapi”, kazi ambayo ilimuwezesha kutumia muda mwingi akiwa na Abdilatif Abdalla. Nilipomtaka amuelezee Abdilatif Abdalla kwa anavyomfahamu, Prof. Kresse akaniambia “Nadhani Abdilatif Abdalla ni utu ndani ya kiwiliwili cha binadaamu.”

One thought on “Kutana na Abdilatif Abdalla “Mtu ndani ya Binaadamu””

  1. Swadakta! Maneno yako ni mahiri kabisa. Mwema kweli kipenzi cha Mungu. Hata Mie nilibahatika kuku tena na Al-Akh Abdalla katika moja ya likizo zake mjini Mombasa na kuwa mstari wa mbele wakati wa usomaji wa mashairi yake kwa mara ya kwanza nchini Kenya baada ya kijana kwake.

    Kwa wale ambao hawajajaaliwa kupata furs a hii adhimu nawaambia Ami Abdulatif Abdalla ni mtu katika watu. Mkarimmu, mcheshi na mzungumzaji aliye na ari msisimko ya kisiasa ambayo hasiti kuipeana ukutanapo nae. In shaa Allah Mungu amueke tukutane tena – Ameen
    Mwalimu Mohamed Koja.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.