Kiswahili kina ghala la tamathali za semi zinazohusu nafasi na hadhi ya mama kwenye jamii. “Nani kama mama?” ni msemo unaoendana na swali ambalo kwa hakika halitaki majibu, isipokuwa limewekwa kwa ajili ya kutilia mkazo kama pale mtu anapokuuliza “Utaniweza mimi wewe?” akiwa hakusudii umjibu kuwa utamuweza au laa, bali kukusisitizia tu kuwa yeye ana uwezo zaidi yako.

Kitendawili kinachosema: “Titi la mama ni tamu, kunyonya halinishi hamu” na ambacho jibu lake ni usingizi, kinaashiria namna ambavyo maziwa anayonyonya mtoto kutoka kwa mama yake yalivyo na ladha isiyosemeka. Usingizi ladha yake ni ya ajabu kabisa. Wengine huufananisha na kifo chema cha muda, ambacho kwacho roho huhama kiwiliwili kwenda kustaaladhi mbali na dunia kisha kurejea.

Msemo mwengine husema: “Mama ni mama” ambao wajuzi wameuongezea kipande cha “…hata akiwa rikwama” ambacho sidhani kama kiliwekwa kwenye uasili wa msemo wenyewe. La muhimu ni kuwa msemo huu unathibitisha kuwa mama ndiye kila kitu kwa mtoto wake. Mimi ni baba na nahisi tamathali nyingi zilizomo kwenye lugha kumuhusu mama peke yake zinanidhalilisha na kutokuionesha nafasi yangu katika familia. Lakini pia zinanikumbusha nafasi ya mama kwangu, maana nami kabla sijakuwa baba, nilikuwa kwanza mtoto.

Tena, kwa bahati kubwa sana, mimi ni mtoto wa mama wawili. Sasa ikiwa wale wenye mama mmoja tu, wanakuwa na tamathali nyingi kama hizo kuwaelezea mama zao, hapana shaka mimi mwenye mama wawili nina hadhi na nafasi kubwa zaidi. Kwamba nina wanawake wawili watu wazima ambao kwao mimi ni mtoto mwenye hadhi na nafasi ya kuwa mtoto wao muda wote na siku zote. Ndicho ninachosema kwenye ushairi huu.

3 thoughts on “Ni Nyie Munipendao”

  1. Kazi nyingi sana fasihi zimekuwa na misemo, nahau na methali nyingi zinazomkuza mwanamke, hata kwenye kazi za fasihi andishi kumekuwa na dhamira ya NAFASI YA MWANAMKE ambapo hakuna nafasi ya Mwanaume katika jamii lengo la kuwepo hii dhamira sio kumdogosha Mwanaume bali ni kumkuza mwanamke na kuonyesha umuhimu wa mwanamke kwani amekuwa ni kiumbe kilichoathiriwa na mfumo dume .
    Hivyo ndio maana mwanamke amekuwa akipewa nafasi kubwa sana katika kazi za fasihi, mwanamke huwa anachorwa katika nafasi mbalimbali lengo tujifunze na tumthani na tumpe kipa umbele, asidharauliwe.
    Mwanaume tayari ni ameshakuzwa kwa kiasi kikubwa kutokana na huku kumpa mwanamke nafasi kubwa katika kazi za fasihi.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.