HADI sasa, hakuna aliyetangaza wazi kugombea urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ingawa miongoni mwa waliowahi kutajwa ni Shamsi Vuai Nahodha na Balozi Seif Ali Iddi.

Kwa mwelekeo huu, inawezekana Dk. Ali Mohammed Shein aliyeingia madarakani Novemba 2010, anaweza kubakia mgombea pekee wa CCM, chama ambacho pasipo msingi huamini katika kumuachia rais aliyepo madarakani amalizie kipindi cha pili cha miaka mitano.

 Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai, akitambulisha Ujumbe wa Viongozi wa CCM wa Mikoa ya CCM Zanzibar wakiti ulipofikwa kwa mazungumzo na Dkt. Salmin Amour maaruf wakati wa Uongozi wake akijulikana kwa jina la Komandoo. (Picha/ZanziNews)
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai, akitambulisha Ujumbe wa Viongozi wa CCM wa Mikoa ya CCM Zanzibar wakiti ulipofikwa kwa mazungumzo na Dkt. Salmin Amour maaruf wakati wa Uongozi wake akijulikana kwa jina la Komandoo. (Picha/ZanziNews)

Nayasema haya kwa kuwa kuna watu, kwa kujifanya wapambe wema wa Dk. Shein, wanashinikiza kuondolewa kwa Maalim Seif Shariff Hamad katika wadhifa wa Makamu wa Kwanza wa Rais ili ateuliwe kada wa CCM.

Ni watu wasiojua hata Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 inavyoelekeza kuhusu uteuzi wa makamu wa kwanza wa rais. Wanasahau kuwa Rais akishamteua mtu kushika wadhifa huo, hawezi kumuondoa.

Kundi la watu hao limekwenda hadi kwa Dk. Salmin Amour Juma (Komandoo), Rais Mstaafu wa Zanzibar, eti kupata rai na ushauri wa kumuangusha Maalim Seif anayegombea tena urais katika uchaguzi mkuu ujao.

Na Enzi Talib
Na Enzi Talib

Nyumbani kwa Dk. Salmin, Migombani, mjini Zanzibar, kumegeuka baraza ya vikao maalumu vya wanaojiita makada na walinda mapinduzi, chini ya uenyekiti wake. Mmoja aliyepata kuwa waziri wakati akiongoza serikali na ambaye amehudhuria vikao hivyo, amesikika akisema kuwa ” wameitwa kupewa maagizo kuwa lazima CCM ishinde”.

Waziri huyo amemnukuu Dk. Salmin akisema, “ingawa sijaanza kuona vizuri, nimewaiteni kwa kazi moja muhimu, kujipanga katika medani za kivita. Uchaguzi ni vita inayohitaji makomando, silaha na mipango ya kusambaratisha maadui. Ni lazima tupambane na wapinzani wa mapinduzi yetu ili kulinda urithi wetu.”

Lakini, kwa siasa za sasa Zanzibar, maapizo haya ya Dk. Salmin, hayawezi kukisaidia chama chake. Siasa za ukamandoo hazina nafasi katika demokrasia iliyopevuka. Wananchi wamechoshwa na siasa za mabavu na vitisho ambazo alizisimamia wakati akiongoza. Wamechoshwa na ubaguzi. Wamechoshwa na vurugu, ugomvi na siasa za kutukanana na kukashifiana.

Wazanzibari wamechoshwa na mtindo wa viongozi wa CCM kugeuza uchaguzi kuwa uwanja wa vita. Wanataka amani, umoja, heshima, utu na uchumi imara. Haya huletwa na siasa za kiungwana na uongozi adilifu.

Wananchi wanataka viongozi wanaojali ujenzi wa uchumi unaohimili utoaji wa huduma za jamii kwa ufanisi; kuimarishwa kwa elimu na kuwa na uhuru mpana wa kujieleza na wa serikali yao kujiamulia mambo yake kwa maslahi ya wananchi. Mabavu ya utawala wa Dk. Salmin yalizikwa na mrithi wake, Amani Abeid Karume, miaka 10 iliyopita.

Dk. Salmin aliyeongoza 1990 mpaka Oktoba 2000, alijisahau kama ni kiongozi; akajigeuza Chifu na Sultani wa Zanzibar. Alifikia hatua ya kutaka kuibadilisha katiba ili asiondoke madarakani.

Kiburi chake hicho kilimuondelea sifa Dk. Mohammed Gharib Bilali, aliyekuwa waziri kiongozi wake, pale alipogombea urais wa Zanzibar kupingana na Rais Karume. Jina lake liliondolewa na Kamati Kuu ya CCM.

Katika uchaguzi wa mwaka 2000, Dk. Bilali alimshinda Karume katika kura za maoni zilizopigwa na wajumbe wa Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM. Karume alipata kura tisa, Dk. Bilal alipata kura 54. Badala ya kuutambua ushindi wa Dk. Bilal, CCM ilimpitisha Karume.

Ulipofanyika uchaguzi mkuu, Karume alitangazwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) mshindi kwa kupata asilimia 67.04 ya kura. Mwaka 2005 alipata asilimia 53.18 tu ya kura zilizopigwa. Zipo taarifa kuwa upungufu huu wa kura kwa Rais Karume, ulitokana na baadhi ya viongozi kutoka kambi ya Dk. Salmin kumfanyia hujuma ili kumzorotesha kimamlaka.

Hata hivyo, Karume alipambana kishujaa na kushinda mbinu na hujuma hizo. Kimkakati kabisa, alimteua Ali Juma Shamhuna, aliyekuwa kipenzi kikubwa na nguzo ya utawala wa Dk. Salmin, kuwa waziri na baadaye akampa wadhifa wa naibu waziri kiongozi usiokuwepo kwenye Katiba ya Zanzibar. Shamhuna alikuwa mkosoaji mkubwa wa serikali ya Karume.

Uamuzi huo mwanana kimkakati, ulituliza siasa za umbea dhidi ya rais Karume ambaye katika kipindi chote cha miaka 10 ya uongozi wake, hakuchukua ushauri wowote kutoka kwa Dk. Salmin, hasa katika suala la udhibiti wa fedha za serikali.

Alisimamia mwenyewe wizara ya fedha na akafanikiwa kurudisha imani ya watumishi wa serikali waliokuwa hawalipwi mishahara kwa wakati. Alilipa mishahara kila mwezi, tofauti na ilivyokuwa wakati wa Dk. Salmin walipokuwa wanakopwa kwa wiki kadhaa.

Serikali ya Dk. Salmin ililaumiwa kwa ubadhirifu na matumizi ya anasa ya fedha za umma. Aliyekuwa waziri wa fedha, Amina Salum Ali, hakupata ushirikiano wa kutosha na alinyimwa taarifa hasa za matumizi ya fedha na katibu mkuu wake, Omar Sheha Mussa, ambaye alikuwa na nguvu kubwa na akipokea maagizo ya matumizi ya fedha moja kwa moja kutoka kwa  Dk. Salmin. Hata pale Amina alipoomba Sheha aondolewe, kwa kuwa ameshindwa kufanya naye kazi, alipuuzwa.

Dk. Salmin hakuwa na wasaa wa kusikiliza matatizo ya utendaji serikalini. Alitumia muda mwingi kupambana na Maalim Seif na kuendesha siasa chafu. Salmin alijijengea maadui wengi nchi nzima. Alivunja nyumba za wafuasi wa CUF. Aliwafuta kazi wazaliwa wa Pemba. Aliwanyima ajira mpya waliostahili kupata. Walimu wengi walifukuzwa kazi ;na waliobanwa, waliacha wenyewe.

Ubaguzi huu na ubabe mwingine, ndivyo vilisababisha Maalim Seif kukataa kumtambua Dk. Salmin na serikali yake baada ya uchaguzi wa 1995 ambao CUF ilisema iliporwa ushindi. Maalim alikituhumu CCM kuiba kura kwa kumlazimisha mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, kutangaza matokeo batili.

Kupaa kwa Amani Karume na kuungwa mkono hata na jumuiya za kimataifa, ikiwemo Marekani iliyotoa ushirikiano mkubwa kwa serikali yake, si tu katika maridhiano ya kuunda Serikali ya Umoja wa kitaifa ( SUK), lakini pia ufundi wa kisheria uliotumika kuiweka na kuitambua serikali hiyo ndani ya Katiba ya Zanzibar.

Ndani ya Katiba ya Zanzibar, kumewekwa kifungu kinachomtambua aliyepata nafasi ya pili ya kura za urais, kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais. Katika mgawanyo wa mawaziri, Katiba inamuelekeza Rais lazima, vilevile, ateue mawaziri kutoka upande wa mgombea urais aliyeshindwa uchaguzi. Mfumo huu wa uundaji serikali, umeleta amani na utulivu na ni mwiba kwa siasa chafu zilizoasisiwa na CCM. Ndiyo hawa wanaouandama kwa maslahi binafsi.

Lakini ujasiri wa Maalim Seif wa kumtambua Dk. Shein kuwa Rais halali wa Zanzibar na kukitambua CCM kuwa ndio chama tawala baada ya uchaguzi nwa 2010, ingawa hakubaliani na sera za chama hicho, vilisaidia sana katika jitihada za kuimarisha siasa za maridhiano Zanzibar.

Hakika Maalim Seif amebadilika kutoka yule aliyekuwa akishawishi serikali inyimwe misaada. Wa leo, ni kiongozi mwema na anayeshika ipasavyo kamba ya mshikamano wa kitaifa. Ndiye hasa anayezuia jitihada za kuirudisha Zanzibar shimoni kama vile ilivyokuwa chini ya utawala wa Dk. Salmin.

CHANZO: Gazeti la Mawio

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.