Madhumuni ya maandishi haya mafupi si kumjibu Mzanzibari mwenzangu na kaka yangu Ahmed Rajab, mwandishi maarufu na mwenye kusifika barani Afrika. Nia yangu ni kuweka sawa baadhi ya dhana zake kwa manufaa ya Zanzibar ndani ya wakati huu tulionao.

Mwandishi maarufu wa riwaya, Milan Kundera, aliandika: “mapambano ya binaadamu dhidi ya nguvu [za dola] ni mapambano baina ya kumbukumbu na kusahau.” Suala kuu la kwa kila Mzanzibari aliyeishi kabla au baada ya miaka 50 iliyopita ni, anakumbuka au anakumbushwa nini, anasahau au anasahaulishwa kitu gani, na kwa nini? Suala hilo ni la kwanza kabisa. Suala la chuki, kulipizana kisasi, au kusameheyana bila ya kusahau, ni masuala ya mtitiriko wa suala kuu.

Kwa hiyo, tunapolizungumzia suala la kumbukumbu na kusahau, la kwanza la kujiuliza na kulizingatia ni, tunakumbuka au kusahau kitu gani? Na hicho kinachokumbukwa ni kipi na jawabu yake inatokana na kundi au makundi yepi kati ya makundi matatu (3) aliyoyataja Rajab:

1. La wahusika.
2. La walioshuhudiya, na
3. La walioyasikiya tu.

Na Harith Ghassany
Na Harith Ghassany

Rajab kajiweka kwenye kundi la pili (2) na kuzidi kujiaminisha na aaminike, ameandika kuwa ana ushahidi wa maandishi wenye kuthibitisha yale anayoyakumbuka. Nimefurahi sana kulijuwa hilo kwa sababu tuna mfano mzuri sana wa kufananisha usahihi wa nguvu za historia ya maandishi ya wakati wa tukio na udhaifu wa “historia simulizi” za baadae.

Napenda kumuomba kaka yangu mpenzi atupatie japo kopi ya kumbukumbu za maandishi ya mkutano wake na marehemu Abdalla Kassim Hanga pamoja na Wazanzibari wenzake wawili, ili tupate kipimo cha kuyapima yale ambayo yeye ameyahifadhi kama ni shahidi wa maandishi.

Lakini turudi nyuma kidogo kwenye kumbukumbu na kusahau hata bila ya kujaribu kuyakumbuka au kuyasahau yaliyotokeya katika mkutano wa miaka 47 iliyopita.

Kitabu cha Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru (na si Kwaheri Uhuru, Kwaheri Ukoloni kama alivyoandika Ahmed Rajab kwenye sehemu ya pili ya makala yake ya “Tanbihi”), kina kurasa 496. Kati ya hizo ni kurasa tatu (3) tu, ukurasa 267-270, zenye kuuzungumziya mkutano wa London baina ya Wazanzibari watatu na Hanga. Lakini hizo kurasa tatu (3) ni muhimu katika muktadha wa maudhui ya kukumbuka na kusahau kwa sababu, na Mungu awazidishie afya Ahmed Rajab na Bwana Salum Hamdan ambaye anaishi Maskati, Oman, watu wawili hao wenye kuhusika moja kwa moja na suala la changamoto za kuandika historia, Alhamdulillah, wote wawili wako hai na wana akili zao.

Kwanza napenda kumkumbusha msomaji kuwa Bwana Salum Hamdan ni wa kundi la pili, la waliyoshuhudiya, kama anavyojinasibu nalo Ahmed Rajab. Tafauti yao ni Ahmed Rajab ameweka kumbukumbu ya maandishi ambayo narudiya tena, tutamshukuru sana akitupatiya ili tujifunze namna ya kuzizidhibiti changamoto katika suala zima la kuisajili historia na athari zake mbaya na nzuri za baadae.

Mzee Salum Hamdan ni mzee wa hikma na busara. Nilipokwenda kuonana naye kwa mara nyengine ili nizisajili kumbukumbu zake, aliniambia nisubiri mpaka atakapozungumza na Ahmed Rajab kwa sababu kuna mambo ambayo huenda akawa ameyasahau au hayakumbuki vizuri. Na hapo ndipo msomaji wa kurasa 267-270 katika kitabu cha Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru, atakutana na maneno yafuatayo ya Salum Hamdan yenye kuonyesha kuwa alikuwa shahidi wa mkutano ambaye aliamua kuzungumza na Ahmed Rajab kabla ya kuzungumza na mwandishi (Harith):

“Sasa tulivyokuwa London yeye [Ahmed Rajab] kataja watu watatu tu.” Ukursa 267.

“Nnavyokumbuka mimi Oscar akatwambia sikilizeni bwana.” Ukurasa 268.

“Ndivo navokumbuka mie na ndivo anavokumbuka Ahmed [Rajab].” Ukurasa 268.

“Mimi skumbuki ile nilikwenda railway station. Kile mimi sijakumbuka. Kama ulivosema, mimi nyumba nilikuwa naijuwa, sina haja ya Kasembe kunpeleka. Lakini inaweza kuwa nimekwenda mimi na Kasembe kumpokea Ahmed Rajab. Yeye Ahmed kafikiri tu na mie ni mgeni. Hajajuwa kuwa mimi na Kambona tunajuwana na jirani, na nyumba yangu mie na yake si mbali.” ” Ukurasa 268.

“Yeye Ahmed amekumbuka mambo mimi sijayakumbuka.” Ukurasa 268.

Inasikitisha kuwa mwandishi gwiji na mahiri kama Ahmed Rajab angalau kusema kuwa Salum Hamdan alizungumza na yeye kama mwenzake kuyathibitisha yale walioyashuhudia pamoja na Hanga kabla ya kumpa mkusanyaji (Harith) taarifa za mkutano wa London. Ahmed Rajab kashindwa kuwa mkweli na muwazi na badala yake kaamua kujaribu kunirushia ndoo ya tuhuma yenye uchafu wa “msimamo wa kisiasa”, “dhana fulani”, “kupotosha historia”, “kutoa maelezo kinyume na matukio halisi yalivyotokea”, na kumumunya “wanaoendeleza chuki wakikataa kusamehe.” Hee!

Kama tayari nilikuwa nina dhana fulani, kwanini nilizitupilia mbali simulizi za kina marehemu Ali “Lumumba” na wengineo, na kumfuata Mohamed Said Tanga na kuonana na wazee wazito wa Dar es Salaam? Marehemu Mzee Hamza Aziz ambaye alikuwa Kamishna wa Polisi aliniuliza suala dogo lakini zito. Aliniambia, “Sikiliza kijana. Inataka kwanza ujiulize yale Mapinduzi ya Zanzibar yalipangwa huku kwetu Tanganyika au kule kwenu Zanzibar?” Hapo ndipo nilipoipata ile wazungu wanayoiita “gestalt switch” au “paradigm shift.” Haikuwa dhana wala uhodari wangu. Na hiyo ilitokeya baada ya kupoteza kama miaka miwili Zanzibar kuyatafuta Mapinduzi mchana kwa vibatari na kandili ndani ya vichochoro vya Mji Mkongwe na N’gambu yake!

Hayo yote bado sijayaona umuhimu wake kwa sababu kuna faida au somo gani katika kukumbuka au kusahau kama Oscar Kambona ndiye au siye aliewaita Wazanzibari kwake au kama alimtuma Kasembe? Muhimu Ahmed Rajab alifika kwa Oscar Kambona na angelitaka angeliamua kutohudhuria mkutano baada ya kutambua kumbe Kasembe hakuwaambia alikuwa amewachukuwa kwenda kwa kitimbakwiri na msaliti wa ukombozi wa Afrika – Oscar Kambona. Haingii akilini hata kidogo kuwa Ahmed Rajab abebwe tu na Kasembe kama pakacha la madoriani halafu ajikute anafunguliwa mlango na Kambona!

Narudia tena. Yote hayo si muhimu kwa sababu suala muhimu kwa kila Mzanzibari ni kukumbuka au kusahau namna Zanzibar ilivyotoweka na kupotea au kupotezwa kama ni Nchi yenye Mamlaka Kamili kupitia tukio la tarehe 12 Januari, 1964, na yaliofuatiliya. Suala si nani alikuwa akitawala, uhalali au uharamu wake. Suala ni kupotezwa Nchi kwa kuvamiwa na baada ya muda mfupi kumezwa ndani ya Muungano. Ni kama vile ukamuingiliya kwa nguvu (rape) mwanamke halafu ukaamua kufunga pingu za maisha naye kwa kufanya harusi!

Na ndio maana mazungumzo ya Hanga kwa mujibu wa Salum Hamdan niliyaweka katika mlango wa “Hayeshi Majuto Yao.” Bwana Salum Hamdan ambaye yuhai amemnukuu marehemu Hanga: “…sisi Mungu atusamehe, tumefanya mambo mengi ambayo mabaya, tumedhulumu, tumechukuwa watoto na wake za watu, na Mwenye Enzi Mungu anisamehe na ninajuta kwa haya nlioyafanya.” Ukurasa . 269. Kinyume cha Salum Hamdan, Ahmed Rajab kayasahau maneno ya Hanga yaliyonukuliwa na Salum Hamdan lakini ameyakumbuka maneno aliyojisafisha nayo Hanga kwa kumtusi Kambona.

Salum Hamdan ameeleza “Lakini inasikitisa kuwa tangu wakati ule yeye [Hanga] yupo pale London habari zishafika Cairo. Walioko Cairo maambassador wa pale wameshapeleka habari Tanzania kwa Mzee Nyerere. Ikawa serikali inavosikia wamekaa wakimgojea arejee tu. Yeye Hanga hajajuwa, wala sisi hatujajuwa.” Ukurasa 270.

Anaandika Rajab: “Kutoka Conakry, Hanga alirudi nyumbani, akipitia Cairo, ambako alikuwa mgeni rasmi wa Ahmed Diria Hassan, Balozi wa Tanzania nchini Misri. Aliporudi Dar es Salaam ndipo Hanga alipokamatwa kwa amri ya Rais Julius Nyerere na akapelekwa Zanzibar ambako aliuliwa kikatili.” Ahmed Rajab hajui au hakumbuki kuwa kumbe Hanga alikuwa ameshauliwa kutoka Cairo.
Kitabu cha Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru, si kitabu kilichosimama juu ya midomo ya simulizi peke yake. Kila mlango wa kitabu cha Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru, una marejeo ambayo yanatokana na “primary” na “secondary” sources. Kwenye utafiti wa kihistoria, “primary” sources ni marajeo ya watu ambao walishiriki na waliyashuhudia yale ambayo wanayazungumzia. “Secondary” sources zinaweza zikawa ni vitabu ambayo vinategemea nini watu wengine wameandika na mwandishi mwenyewe si mwenye kuyashuhudia yale yalioandikwa au kusemwa. Simulizi za wazee si zangu mimi bali ni za wazee walioshiriki moja kwa moja au kwa karibu sana na tukio la Zanzibar la 1964. Na ikumbukwe pia, historia ya maandishi inatokana na historia ya simulizi. Yakumbuke ya Jibrili, Wahyi, na kukusanywa kwa Qur’an.

Kitabu cha Kawheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru kina milango ishirini na mja (21). Sasa wacha twende mlango kwa mlango. Kwenye “Mapitiyo kwa Jumla” kuna endnotes (mapitio) 24. 1. Mlango wa Kwanza una mapitio 25. 2. Mlango wa Pili una mapitio 42. 3. Mlango wa Tatu una mapitio 27. 4. Mlango wa Nne una mapitio 6. 5. Mlango wa Tano una mapitio 19. 6. Mlango wa Sita una mapitio 11. 7. Mlango wa Saba una mapitio 15. 8. Mlango wa Nane una mapitio 20. 9. Mlango wa Tisa una mapitio 14. 10. Mlango wa Kumi una mapitio 2. 11. Mlango wa Kumi na Moja una mapitio 16. 12. Mlango wa Kumi na Mbili una mapitio 18. 13. Mlango wa Kumi na Tatu una pitio 1. 14. Mlango wa Kumi na Nne una mapitio 18. 15. Mlango wa Kumi na Tano una mapitio 2. 16. Mlango wa Kumi na Sita una mapitio 6. 17. Mlango wa Kumi na Saba una mapitio 6. 18. Mlango wa Kumi na Nane una mapitio 2. 19. Mlango wa Kumi na Tisa una mapitio 84. 20. Mlango wa Ishirini una mapitio 47. 21. Mlango wa Ishiri na Moja una mapitio 3.

Na ukiingia na ukazama ndani ya hayo mapitio ndipo utakapoweza kuunganisha na kuona wapi penye udhaifu wa sahau na wapi ambapo sahau imepikuliwa na maandishi ambayo hata mwenye sahau utamuona anajikuta hajui au hakumbuki kitu. Wakati kweli nguvu za kukumbuka na kusahau zina uwezo wa kutupiga chenga, jee, maandishi ambayo ni “primary sources” ambayo yako karibu sana ki wakati na tukio lenyewe, hayana uzito wowote kwa gwiji wa fani ya habari na uandishi mtamu kama ndugu yetu Ahmed Rajab? Au tuseme hakuwa na wakati na alizisoma zaidi simulizi za wazee na ndio maana akaona udhaifu katika “methodology” ya uandishi wa Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru? Au alizilenga kurasa tatu (3) tu kati ya kurasa 496?

Kuridhika nako kuna miko yake. Mtu anaweza akakubali lakini asiridhike na jawabu wala ushahidi. La msingi, kama nimekosea au nimedanganywa, kama ni muwongo au nimezuwa; Alhamdulilllah, uhai na uwezo wa wengine kuja na maelezo mbadala na yenye kusimama na hoja zenye ushahidi, bado upo. Suala: kwanini hawakosowi pale wanapoona pametiwa chumvi au pamepotoshwa kwa kulitimiza lengo la mwandishi au la watu fulani? Tumeweke wapi Salum Hamdan? Katika kundi la waliyoshuhudiya au katika kundi walioyasikiya tu na kumkabidhi mwandishi wa makala hii?

Naanza kuamini na kuridhika kuwa kuna tatizo kubwa zaidi hata kuliko kukukmbuka au kusahau. Kitabu cha Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru, kimewashitusha, kimewaporomosha na kuwashusha daraja baadhi ya watu katika majivuno na majigambo waliyokuwa wakijivunia siku zote za Uwao. Kilichowashtuwa zaidi kuwa kimepokewa na kukubalika na hata wale ambao hawakubaliani nacho wameamuwa kukaa kimya.

Kimewashangaza kuona kimefikia kua kigezo cha ushahidi wa kusadikika na kukubalika Bungeni, hiyo ilikuwa fimbo. Walitamani angekuwa kiongozi au viongozi fulani kuipata sifa hiyo. Ahmed Rajab anashaka juu ya nini hali anajuwa kuwa niliyoelezwa yanatokana na mashahidi wa matukio hayo na washiriki wengine bado wahai na hadi leo hakuna aliyeyapinga maelezo yao. Vipi yeye awe na shaka nayo! Yeye na walio kama yeye hawaji na ushahidi au kitu kipya. Ni ushahidi wa kukosoa na kupanga hoja kwa kutumia kipaji cha uandishi na mantiki za kupinduwa hoja.

Katika mapambano baina ya kukumbuka na kusahau, kinachotakinana khasa ni ukombozi wa kiroho kwanza, na wa kiakili baadae, wa kila Mzanzibari, anaeishi ndani au nje ya Zanzibar na vizazi vyao. Ni ukombozi wenye kukubali, tena kwa hoja zenye kusimama juu ya ushahidi juu ya yale ambayo yamekuwa yakiogopwa kuzungumzwa hata kwa siri tena kwa zaidi ya nusu karne. Kinachotakikana ni uongozi mpya wa kizazi kipya ambacho kiko tayari kuinusuru Zanzibar kutokana na maradhi ya ukaidi na kujipambiya sifa ili kujitawadhisha na utawala.

Zanzibar imezungukwa na bahari ya ushahidi wa kuvamiwa kutoka kila upande wa roho na mwili wake lakini bado ina baadhi ya magenerali ambao wameamua kuingia kwenye vita vya kuinusuru huku wakiwa hawana hakika baina ya kuuandama “umimi” au kuyaweka juu kabisa maslahi ya Zanzibar na maslahi ya Wazanzibari ambao wengi wao ni watu wema na wanyonge.

Kizazi kipya hakikubali tena kudanganywa na kuingiliwa na mchwa wa miaka 51 iliopita. Kizazi kipya ni aina ya mbao mpya ambayo mchwa hawezi kuila. Mchwa aliebakiya Zanzibar na nje ya Zanzibar ni yule ambaye ameshaila fimbo ya Nabii Suleiman.

Na hadithi ya Musa ndani ya nyumba ya Firauni haijamalizikia na tukio la kihistoria liliomo ndani ya vitabu vitukufu vya Qur’an na Bibilia. Wakati hauko tena mbali Firauni wa Zanzibar akatoa shahada huku anazama.

Hapo ndipo suala la kukumbuka na kusahau litakapokuwa na maana mpya kwa Zanzibar Mpya na vizazi vyake – Ameen.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.