KUMBUKUMBU na usahaulifu. Kalima hizo mbili zina umuhimu mkubwa katika fani ya uandishi wa historia. Katika fani hiyo, “kumbukumbu” na “usahaulifu” huwa na siasa zake na nguvu za aina yake.

Uandishi wa historia una miiko na maadili yake. Ni mwiko kwa wanahistoria pamoja na waandishi wa mambo ya kihistoria kupotosha historia kwa kutoa maelezo kinyume na matukio halisi yalivyotukia. Na huo ni mwiko mkubwa.

Miongoni mwa maadili ya uandishi wa historia ni kwanza, kuyafatiisha mambo na kuyachunguza kwa kina; na pili, kutoa maelezo yaliyo sahihi bila ya upendeleo. Hii si kazi nyepesi hasa kwa wale wenye misimamo ya kisiasa.
Kwa hakika, hiyo si kazi nyepesi hata kwa wasio na misimamo ya kisiasa kwa sababu mara nyingine kutokuwa na msimamo wa kisiasa kwenyewe ni sawa na kuwa na msimamo wa kisiasa.
Uandishi wa historia unazidi kutatanisha pale mwandishi anayeandika kuhusu matukio ya kihistoria anapowategemea wasimulizi wenye hakika kwamba ni wao tu wenye ukweli. Wasimulizi hao hutegemea kumbukumbu zao bila ya kusaidiwa na ushahidi wa maandishi wenye kuthibitisha wanayoyakumbuka.
Historia ya wasimulizi hao ndio ile iitwayo “historia simulizi” yaani historia isiyoandikwa, inayotegemea simulizi za wahusika wa matukio au za walioyashuhudia matukio au za walioyasikia tu matukio. Historia ya aina hiyo ina changamoto zake; tena ni nyingi na kubwa.
Changamoto za aina hiyo lazima alipambana nazo Dk. Harith Ghassany alipokuwa akiandika kitabu chake “Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru,” chenye kuhusika na Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964.
Katika daraja za nani wa kuwategemea na kwa kiwango gani cha kuwategemea kati ya makundi hayo matatu, hao wa mwisho, walioyasikia tu, si wa kutegemewa sana wala kupewa uzito mkubwa. Huwezi kuyapa nguvu masimulizi yao kama ya wale walioshuhudia au ya walioshiriki hasa katika matukio yanayohusika.
Lakini hata yale makundi mawili ya mwanzo — ya walioshuhudia na walioshiriki katika matukio — yana mushkili wao. Mushkili huo unatokana na “kukumbuka” na “kusahau.”
Na Ahmed Rajab
Na Ahmed Rajab

Kwa kiwango gani wasimulizi hao watataka kukumbuka na kwa kiwango gani watataka kusahau? Hapo ndipo zinapoingia siasa za kukumbuka na kusahau katika masimulizi ya mambo yaliyokwishatokea.

Kutegemea uamuzi wao, masimulizi yao yanaweza yakawakanganya watu wenye kutaka kuujua undani wa kitu, kwa mfano undani wa matukio yanayohusishwa na mtu au jambo fulani.
Siasa za kukumbuka na kusahau ndizo zinazowakanganya vijana wa leo wasiweze, kwa mfano, kuujua ukweli na undani wa mengi yaliyojiri wakati wa Mapinduzi ya Zanzibar. Kuna namna mbili ya kuyaangalia Mapinduzi hayo.
Njia moja, ni kuyaangalia kama tukio au mfululizo wa matukio. Njia ya pili, ni kuyaangalia kama mchakato ambao baadaye umekuwa na mfumo au umbile la aina yake. Kuna utatanishi kuhusu masimulizi ya aina zote hizo mbili za kuyaangalia Mapinduzi hayo.
Yameandikwa mengi kuhusu tukio na mchakato huo na kila upande unashikilia kwamba masimulizi yake ndiyo yaliyo sahihi.
Hapo ndipo tunapokumbana na tatizo jingine: la fasiri, fasili, tafsiri na ufafanuzi wa maelezo ya masimulizi ya kihistoria. Hata watu wakipewa maelezo sawa ya yaliyotokea bado wanaweza wakawa na fasiri tofauti za maelezo hayo. Ndio maana utata wa masimulizi kuhusu Mapinduzi ya Zanzibar bado unaendelea kutinga.
Msikilizaji au msomaji wa masimulizi ya kihistoria siku zote huwa anapaswa awe makini na atumie akili yake kufikia uamuzi baada ya kuyasikia anayoyasikia au kuyasoma anayoyasoma kuhusu tukio lolote la kihistoria.
Kukumbuka na kusahau mambo yaliyopita ni vitendo muhimu katika kusimulia mambo ya kihistoria, yasio ya hadithi tu. Kwa mwenye kusimulia matukio ya kisiasa vitendo hivyo huwa ni vitendo vya kisiasa; yaani huwa ni vitendo vyenye kuchukua msimamo wa kisiasa.Ama msimulizi anachagua nini cha kukumbuka au anachagua nini cha kusahau.
Wasimulizi wa aina hii wanakuwa wanawafaa sana waandishi wenye msimamo wa kisiasa na wenye kutaka kuuthibitisha kuwa ndio ulio wa kweli. Kuna hoja nyingi katika kitabu cha “Kwaheri Uhuru, Kwaheri Ukoloni” zinazonifanya nifikirie kwamba tangu mwanzo mwandishi alikuwa na dhana fulani aliyokwishaijenga na halafu akatumia nguvu zake zote kutafuta boriti, saruji na mawe kuiimarisha.
Hamna shaka yoyote kwamba alifanya jitihada kubwa ya kuwatafuta watu wataokikata kiu chake cha kujua nini kilichosababisha Mapinduzi na nini hasa kilichotokea.
Bahati mbaya baadhi ya wasimulizi wake walikumbwa na lile tatizo la “kusahau” na kumueleza mwandishi kile ambacho wakihisi mwandishi akitamani aelezwe.
Wakati mwingine huwa ni ajali tu kwamba msimulizi husahau katika masimulizi yake ya tukio au jambo fulani kwani ubongo wa mwanadamu hauwezi kuyakumbuka yote yaliyopita. Ndio maana kuna watu ambao wamejizoesha kuwa na shajara yaani kitabu cha kumbukumbu za kila siku za mambo yao ya kawaida.
Wengine huandika kumbukumbu za mambo makuu tu yanayowakuta maishani mwao.Hufanya hivyo kwa sababu wanatambua ya kwamba kuna uwezekano wa kukumbuka vibaya baadaye. Binafsi nimo katika kundi hili la pili.
Nina kawaida ya kuandika kumbukumbu zangu za mambo makuu niliyoyashuhudia au niliyoshiriki. Miongoni mwa kumbukumbu zangu ni maelezo marefu ya siku niliyokutana London na Abdallah Kassim Hanga, aliyewahi kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Waziri katika serikali ya Muungano. Wakati huo alikuwa ametolewa kwenye Baraza la Mawaziri.
Katika sehemu ya pili ya makala yake kuhusu Hanga iliyochapishwa katika toleo lililopita la Raia Mwema, Mohamed Said amenukuu kutoka kitabu cha “Kwaheri Uhuru, Kwaheri Ukoloni” kuhusu huo mkutano wangu na Hanga nikiwa pamoja na mwenzangu Salim Hamdan, ambaye kwa sasa anaishi Maskati, Oman.
Kiini cha yaliyomo katika nukuu hiyo, yaani wasia aliotupa Hanga,ni sahihi lakini kuna machache yanayohitaji kusahihishwa.
Mkutano huo nilikwishaueleza, ingawa kwa muhtasari, katika Raia Mwema, toleo namba 168 (ZANZIBAR: Siasa za chuki na wasia alionipa Abdallah Kassim Hanga…)
Nachukua fursa hii kuyasahihisha hayo machache yaliyomo kwenye nukuu iliyochapishwa wiki iliyopita.
Oscar Kambona siye aliyetwita kwake.Kusema kweli ingelikuwa nimeambiwa kwamba Kambona alitaka nende nyumbani kwake, pengine ningegoma. Nisingalikwenda.
Siku hizo Kambona akinuka miongoni mwetu tuliokuwa tunafuata siasa za “kimaendeleo” kwa sababu ya ushirikiano wake na wakoloni wa Kireno waliokuwa wakiwagandamiza wananchi wa Angola, Guinea-Bissau na Cape Verde pamoja na Msumbiji.
Mahusiano yetu yalibadilika baadaye kuanzia miaka ya kati ya 1980 alipokuwa mara kwa mara akija ofisini kwenye gazeti la “Africa Analysis” nililokuwa nikilihariri.
Tulikwenda kwa Kambona baada ya mtangazaji mwenzangu wa BBC, Emmanuel Vivian Kassembe, kunambia kwamba Hanga akitaka kuniona mimi pamoja na Wazanzibari wengine wawili, Salim Hamdan na Abdul Latif Mohammed Nura (maarufu kwa jina la Khamis Nura.)
Nura alikuwa ni mtu wa karibu sana na Hanga na alikwenda kusomea sheria Moscow, Urusi, kwa msaada wa Hanga. Niliwajulisha wenzangu hao na tukawa tunajitayarisha kwa Jumamosi kwenda kuonana na Hanga, aliyepita njia kutoka Tanzania akielekea Guinea. (Siku zile ilikuwa kawaida kusafiri kutoka Afrika Mashariki kwenda Afrika Magharibi kwa kupitia ama Paris au London.)
Kabla ya hapo sikujua kwamba Hanga alikuwa London na nilipomuuliza yuko wapi, Kassembe alikataa kunambia. Alitutaka tufike kwenye kituo cha treni ya chini ya ardhi kwenye mtaa wa Belsize Park saa tisa za jioni siku ya Jumamosi. Sikujua kwamba Kambona akiishi mtaa huo.
Mimi na Salim tulifuatana kwenda kwenye miadi yetu pamoja kwa sababu tukikaa nyumba moja. Nura hakutokea kama tulivyoagana. Tulimsubiri kwa robo saa halafu tukamfuata Kassembe kwenda alikokuwako Hanga.
Baada ya Kassembe kugonga kengele ya mlango na mlango kufunguliwa ndipo nilipotambua kwamba kulikuwa kwa Kambona kwani ni yeye aliyetufungulia mlango. Kambona mwenyewe alituvua makoti yetu ya baridi na kuyatundika huku tukilahikiana na akanyosha mkono akisema: “Maalim yuko huko.”
Papo hapo akachomoza Hanga kutoka chumbani; kilikuwa chumba cha pili mkono wa kulia baada ya sebule.Humo sebuleni alikuwamo mtu mwengine ambaye sikumuona na ambaye hadi leo sijui alikuwa nani.
Kambona hakuwa na muda wa kutueleza yaliyoandikwa kwenye nukuu ya wiki iliyopita kwamba alitueleza. Kwa hakika, hatukuijua azma ya Hanga ya kurudi nyumbani mpaka mwisho wa mazungumzo yetu nilipomuuliza anapanga kufanya nini.
Alinijibu hivi: “Unajua mimi nimeoa Guinea na mke wangu amejifungua. Nakwenda kumpa jina mwanangu na halafu nitarudi nyumbani”.
Kusikia hayo nilishtuka kwa sababu Zanzibar ya siku hizo ilikuwa ikitisha.
Hanga akamgeukia Salim na kumwambia: “Mtizame kijana huyu. Niogope nini? Mimi sikufanya kitu. Si kuua, si kuiba”. Halafu akaashiria kwa jicho chumba cha pili walikokuwako kina Kambona na akatwambia: “Angalau huyo ameiba pesa za TANU (Tanganyika African National Union, chama kilichokuwa kikitawala Tanzania-Bara.)
Sijui kama Hanga alitwambia hayo kwa dhihaka au kama alisema kweli lakini tulicheka, tukayaacha.
Kabla ya hayo, mwanzo kabisa wa mazungumzo yetu, Hanga alisema: “Nataka kukuambieni, mimi sina ubaya na Mzee”.
Huyo Mzee aliyekuwa akimtaja alikuwa Sheikh Abeid Amani Karume, Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Tanzania. Halafu akatupa maelezo marefu ya kwa nini Karume alimkalia vibaya kama yalivyoelezwa katika kitabu cha Ghassany.
Miaka kadhaa baadaye niligundua kwamba kulikuwa jengine lililomponza Hanga kwa Karume. Nalo lilihusika na usuhuba wake Hanga na Saleh Saadallah, aliyekuwa waziri wa Karume na ambaye baadaye alifungwa gerezani na kuuawa. Maelezo ya kadhia ya Saadallah ni ya siku nyingine, si leo.
Ni kweli Hanga alitwambia kwamba alitaka kuzungumza nasi kwa sababu, alisema, tutakuwa “viongozi wa kesho” na akatuasa tusiwe na ukabila.
Hanga alitueleza kwamba yeye aliwahi kuwa na chuki za kikabila lakini baadaye aliuona ubaya wake. Alipopelekwa Bara kuwa waziri baada ya kuundwa Muungano, alifanya mpango wa kuwapatia ajira Dar es Salaam waalimu waliokuwa wamefukuzwa kazi Zanzibar.
Takriban wote walikuwa na asili ya Kiarabu. Miongoni mwa aliowataja walikuwa Maalim Shaaban Saleh Farsy, Maalim Salim Sanura na Maalim Amour Ali Ameir.
Hanga akatueleza kwa masikitiko kwamba wapinduzi wenzake wa Afro-Shirazi Party (ASP) huko Zanzibar wakaanza kumsema kwamba akipendelea Waarabu.
“Lakini mimi nilipowaleta Dar sikuwaona kama ni Waarabu, niliwaona kama Wazanzibari,” Hanga alitueleza.
Nakumbuka pia kwamba Hanga alinukuu Qur’an hasa kisa cha Nabii Musa jinsi Mungu alivyomnusuru na wafuasi wake na akamgharikisha Fir’auni na kaumu yake.
Kweli nilimuuliza kuhusu Abdulrahman Babu na alinijibu kwa kusema: “Babu na mimi sote ni Marxists (wafuasi wa Karl Marx) na namtakia kheri. Lakini yeye si tishio kwa Karume kama mimi. Mimi ndio tishio”.
Miaka kadhaa baadaye Kambona alinieleza jinsi Kwame Nkrumah, aliyekuwa uhamishoni Conakry, Guinea, alivyomsihi na kumbembeleza Hanga asirudi nyumbani.
Lakini hakumsikiliza. Yeye mwenyewe Kambona pia alinambia kwamba alimshikilia asirudi lakini hakumsikiliza pia.
Kutoka Conakry, Hanga alirudi nyumbani, akipitia Cairo, ambako alikuwa mgeni wa Ahmed Diria Hassan, Balozi wa Tanzania nchini Misri. Aliporudi Dar es Salaam ndipo Hanga alipokamatwa kwa amri ya Rais Julius Nyerere na akapelekwa Zanzibar ambako aliuliwa kikatili.

One thought on “Tanbihi ya mkutano wangu na Hanga”

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.