Mbio za kugombea uteuzi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa wanaotaka kukiwakilisha chama hicho tawala katika nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zimeendelea kuusisitiza ukweli mmoja mchungu kwa Wazanzibari, nao ni kuwa ndani ya vichwa vya wana-CCM wengi hakuna kitu kinachoitwa Muungano wa nchi mbili, Tanganyika na Zanzibar, bali kilichopo ni hali ya Tanganyika kuirejesha Zanzibar kwenye himaya yake, kwani Zanzibar daima imekuwa sehemu ya Tanganyika.

Steven Wassira
Steven Wassira

Msikilize, kwa mfano, mtangaza nia Steven Wassira akielezea vile anavyouelewa Muungano kwenye vidio hii  ambayo ilichukuliwa wakati akitangaza kujiunga na kinyang’anyiro cha kumrithi Rais Jakaya Kikwete akiwa mjini Mwanza.

Ndani ya maelezo hayo ya Wassira, waziri mwandamizi kwenye serikali ya Muungano, muna kedi na ujumlajumla wa kuiangalia Zanzibar kama kwamba wakaazi wake wote wanatoka kwahala kumoja tu, yaani ndani ya ardhi ya Tanganyika.

Lakini kubwa na muhimu zaidi ya yote, ni kwamba kwa maelezo ya Wasira kiasili Zanzibar ni sawa na Mtwara. Kwake yeye, anataka kuhalalisha kuwa hata kidemografia, yaani muundo wa kijamii, Zanzibar ni sawa na mikoa tu ya Tanganyika. Kwa uwazi zaidi, Wassira anachokisema ni kwamba hapa hakuna suala la Muungano, bali lililopo ni kuwa Zanzibar ni sehemu ya Tanganyika isiyotenganishika!

Kama mtu anadhani kuwa kuna siku Mtwara kwa Wamakonde au Rufiji kwa Wandengereko zitakuja zidai kuwa na mamlaka zao kamili, ndivyo anavyoweza kukisia jinsi watawala wa Tanganyika watakavyokubali Zanzibar nayo iwe hivyo. Ndipo nikasema siku moja kuwa mwaka 1964 hakukuwa na UNION (Muungano) bali ilifanyika ANNEXATION, yaani Tanganyika iliitwaa Zanzibar na kuiongezea kwenye eneo lake la ardhi.

Na hapa tafakarini kwa makini ni ipi hekima ya kubaki jina la Zanzibar, kufutwa la Tanganyika na kuja jina la Tanzania wakati jina asili ni Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar!? Jawabu analo Wassira kwenye maelezo yake hapo juu. Kwamba kubaki jina la Zanzibar ni sawa na kuendelea kuwepo majina ya Mtwara, Kigoma, arusha na Tanga. Lakini jiulize kwa nini watawala wa Tanganyika wanakataa katakata kurejeshwa jina lao la asili la Tanganyika?

Jibu ni kuwa likirudi hilo ile dhana ya ANNEXATION itafutika, maana tafsiri ya Tanganyika ni ardhi ya asili ya Tanganyika bila ya Zanzibar lakini Tanzania ni ile ardhi ya asili ya Tanganyika ikiwa imeongezewa na Zanzibar iliyonyakuliwa mfano wa Urusi ilivyoichukuwa hivi karibuni Crimea.

Kama mchakato wa kumpata mrithi wa Rais Kikwete unakwendana na uhalisia huu si jambo baya sana. Wazanzibari wengi wameshang’amua hali halisi kwa muda mrefu sasa. Waliosalia ni wachache ambao nao wamebakia kwenye mzugo wa kikale kwa sababu tu ya maslahi ya kitambo na si ya kudumu.

Ni jukumu la kisiasa hivi sasa kwa Wazanzibari waliokwishafahamu ukweli wa mambo wafanye mambo mawili: la kwanza waliue jina la Tanzania na wairejeshe Tanganyika na kuwaita Watanganyika kwa jina lao na Watanganyika kama sisi wanavyotujua kuwa ni Wazanzibari.

La pili waendelee na jitihada zao za kudai mamlaka kamili ya Zanzibar kwa kuipeleka kampeni yao kwenye ngazi za kimataifa. Ulimwengu ukiri ukweli uliopo na ushirikiane na pande zote husika kuusimamisha ukweli. Baada ya hapo kama itabidi Muungano ubaki, basi urejeshwe kwa jina lake la ASILI, yaani JAMHURI YA TANGANYIKA NA ZANZIBAR. Utapeli wa Tanzania aliouleta Mwalimu Julius Nyerere hauna nafasi tena.

Makala ya Abdufattah Mussa

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.