Muktadha wa makala haya ni mchakato unaoendelea wa kuipata Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao sasa umebakiwa na viunzi viwili vya mwisho kukamilika – Bunge la Katiba na Kura ya Maoni. Anwani ya makala haya imekopwa kutoka jina la kitabu kiitwacho “Uhasidi wa Marekani kwa Mapinduzi ya Zanzibar” kilichoandikwa na Dk. Amrit Wilson – mmoja wa wasomi walioitumia sehemu kubwa ya uandishi na usomi wake kuitetea heshima ya Zanzibar.

Zanzibar inabadilika na kwenye kubadilika huko inaelekeza kutokuridhika kwake.
Zanzibar inabadilika na kwenye kubadilika huko inaelekeza kutokuridhika kwake.

Hasidi ni hasidi tu kama alivyowahi kusema Mwalimu Julius Nyerere alipokuwa akipingana na sera mpya za mageuzi ya kiuchumi, baada ya yeye mwenyewe kushindwa kuikwamua nchi kiuchumi na “kumpakatisha maiti” Mzee Ali Hassan Mwinyi mwaka 1985: “Kaburu ni kaburu tu, haidhuru kama ni mweupe au ni mweusi.” Sababu ni kwamba ukaburu, kama ulivyo uhasidi, ni sera kwa dhati yake na tabia kwa utekelezwaji wake. Hauna rangi wala kabila, hauna dini wala jinsia.

Si jambo la sadfa hata kidogo kwamba jambo hili limewapambanua mahasidi na mahabubu visiwani Zanzibar. Pengine kwa maslahi ya Maridhiano ya Wazanzibari, si hekima kupiga mstari baina ya matapo hayo mawili, lakini kama tunataka kweli kuacha kunafikiana na kuangaliana machoni tuambizane ukweli, hiyo ndiyo hali halisi – kwamba wako wanaoipenda Zanzibar ukomo wa mapenzi yao na wako wanaihusudi Zanzibar ukomo wa hasadi zao.

Si jambo la sadfa hata kidogo, kwa mfano, kwamba wale ambao baada ya Rais wa wakati huo, Amani Karume, kukutana na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, Novemba 2009, walighadhabishwa na kuanza kupita chini kwa chini kupinga hatua hiyo iliyoyazaa Maridhiano, ndio hao hao waliokuja kupiga kampeni ya “Hapana” kwenye Kura ya Maoni ya Julai 2010.

Si jambo la sadfa hata kidogo kwamba baada ya kushindwa kwenye kampeni yao hiyo, tena kwa kuwa tu kiongozi wa juu ya Zanzibar alikuwa amesimama kwa dhati kuhakikisha kwamba Maridhiano hayarudi nyuma, kundi hilo hilo likajipanga kuwa na mgombea wao wa uraisi, ambaye hakuwa Dk. Ali Mohamed Shein. Kwa hakika, watu hao walimpinga vikali Dk. Shein asipeperushe bendera ya CCM kwa sababu moja tu kubwa – yeye ni Mpemba asiye na mizizi kwenye Afro-Shirazi (ASP).

Hata katika hotuba yake ya awali katika makao makuu ya CCM Zanzibar, Kisiwandui, Dk. Shein alipaswa “kujizikua“ upya kuwaonesha wasiomjua mafungamano yake na ASP, tangu akiwa kijana mdogo katika mitaa ya Kidongo Chekundu, Mjini Unguja. Kwa hakika, akikaribia kusema kwamba yeye ni wa Unguja zaidi kuliko kuwa wa Pemba, maana hadi leo kwenye CCM Zanzibar, kuwa na asili ya Pemba ni alama moja ya mbaya kwenye wasifu wako.

Nakumbuka CUF ilijiingiza kufanya kazi ya ziada kupitia wanamikakati wake kwa kuichora picha nzuri zaidi ya Dk. Shein akiwa kama mgombea wa CCM, kwa hoja tu kwamba kama ikibidi CCM kushinda tena, basi bora iwe na rais atakayeyalinda Maridhiano, ambayo ilikuwa tunu iliyokuja baada ya miaka 50 ya kusakwa kwa udi na uvumba, kwa jasho, damu na usaha.

Wengine wakawa wanahoji kwamba CUF ilikuwa inapiga hisabati ya kisiasa tu ili awekwe mgombea dhaifu na asiye na mvuto, ambaye angezigawa kura za CCM na hatimaye mgombea wao kupita kirahisi. Lakini wanaozijuwa siasa za Zanzibar, wanafahamu kuwa CUF hawafuati mkumbo kiasi hicho. Baada ya chaguzi tatu mutawaliya, ilishaisoma saikolojia na stretejia ya CCM.

Kwa maneno ya mmoja wa waliokuwa wanamikakati mkubwa wa CCM: “Mgombea yeyote wa CCM alipaswa kushinda si kwa sababu ya kuwa na kura halali za Wazanzibari, lakini kwenye uchanga wa Maridhiano, ilikuwa afadhali zaidi kuwaibia waliozowea kuibiwa, kuliko kuiangusha chali CCM ambayo imezowea ushindi. Kishindo cha kuitangaza CCM imeshindwa kingeliyavunja Maridhiano siku ile ile ambayo angelitangazwa Maalim Seif kuwa mshindi, na Zanzibar ingelirudi miaka 50 nyuma.”

Si jambo la safda hata kidogo kwamba kundi hili hili ndilo ambalo mara baada ya kushindwa kumrudisha mgombea wao kutoka Dodoma, na ambaye walishampa jukumu kubwa kabisa la kuyakata roho Maridhiano, lilijibadilisha kama kinyonga na kumzunguka Dk. Shein.

Kundi hili ndilo ambalo sasa huwa la mwanzo kukutana na uso wa Rais Shein asubuhi akiamka, na wa mwisho kuagana na uso huo usiku akilala. Mawazo yao ndio yanayozunguka kwenye ubongo wa Rais Shein. Ukitaka kupima nadharia hiyo, chunguza kauli zake kila mara anaposimama hadharani baada ya kimya kirefu.

Si sadfa hata kidogo kwamba kundi hili hili lililoyapinga Maridhiano, likapiga kampeni ya “Hapana“ kwenye Kura ya Maoni, likampinga Dk. Shein kwa sababu ya Upemba wake, likamzungukia na sasa kumzunguka Makamo Mwenyekiti huyo wa CCM na Rais wa Zanzibar, ndilo hilo hilo lililoratibu kampeni ya aidha “kubaki na Serikali Mbili“ ama “kuuvunja Muungano wa Unguja na Pemba“ wakati wa kukusanya maoni ya kupatikana kwa Rasimu ya Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano.

Hayo yote hapo juu si ya sadfa. Yalipangwa moja baada ya jengine. Kila Plan A iliposhindwa, Plan B iliingia kuelekea kwenye shabaha kuu, ambayo ni kuendelea kuwa madarakani kwa namna yoyote iwayo. Hiyo namna yoyote iwayo itafsiri hivyo hivyo, maana ndani yake muna kila “namna ya kuwa“.

Lakini jambo la sadfa ni kwamba sasa kundi hili limejipanga kwenda kwenye Bunge la Katiba kwa hoja kwamba Muundo wa Muungano wa Serikali Tatu utaimaliza Zanzibar.

Hii ni sadfa kwa sababu la kuinusuru Zanzibar isimalizwe haijawahi kuwa ajenda ya kundi hili tangu machweo. Mtu hawezi kupinga Maridhiano, Umoja wa Kitaifa na Mamlaka Kamili, ambavyo ndicho kifurushi kizima cha Ajenda ya Zanzibar, halafu akasema ameibeba Ajenda hiyo mbele ya umma kuitetea. Huko ni kubeba buyu lisilo mbuyu ndani yake. Kupinga yaliyomo ndani ya seti ya Ajenda ya Zanzibar ni kupinga Ajenda yenyewe.

Hili ni kundi ambalo hadi jana usiku lililala likiweweseka kuizidi kuisakiza Zanzibar kwenye makucha ya Muungano, izidi kupoteza kila chake na kila lake, alimradi tu liendelee kubakia madarakani kwa kulindwa na Serikali ya Muungano. Ni sadfa sana kwamba leo hii wapinge Zanzibar “kumalizwa“ kwenye Katiba Mpya.

Kundi hili halipingi kumalizwa kwa Zanzibar. Linachopinga ni kumalizika kwa enzi za utawala wao visiwani Zanzibar. Na huo ndio uhasidi wao.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.