Nimerudi ziara ya wiki tatu ya nyumbani Zanzibar na nina habari njema, kwamba kote nilikopita – Pemba na Unguja – kuna dalili za kusonga mbele kama jamii, kama taifa.

Kwa mfano, kisiwani Pemba nimekuta barabara inayoiunganisha miji midogo ya Mzambarauni Takao, Wingwi Mapofu, Finya na Mzambarauni kwa Kyarimu na ile inayoziunganisha Likoni na Kangagani zikiwa zimemalizika, ingawa barabara ya Konde-Wete imetelekezwa kama ambavyo siku ya kujengwa ya Wete-Chake isivyofahamika.

Mtaa wa Mlandege, Unguja.
Mtaa wa Mlandege, Unguja.

Lakini kando ya barabara zote hizo, ‘mumeota‘ vijumba vizuri vya kudumu vya matufali. Baadhi yake vilizoeleka kushuhudiwa tu kwenye mitaa ya Msasani, Dar es Salaam au Mazizini, Unguja.

Nimeambiwa kasi hii ya ujenzi imechochewa na fidia ya wale waliovunjiwa nyumba zao kupisha ujenzi wa barabara, kupanda kwa bei ya karafuu na pia Wapemba wanaoishi nje ya nchi ambao sasa wameamua kuelekeza nguvu zao nyumbani. Mahala palipoangushwa mbavu za mbwa, pameinuliwa nyumba ya tufali la kuchonga. Hili la tufali la kuchonga tutakuja tulizungumze siku nyengine, kwa sababu nimesikia huko yanakotolewa, kunaachwa mahandaki na uharibifu mkubwa wa mazingira.

Kisiwani Unguja halikadhalika. Maeneo ya mijini yanazidi kushuhudia ujenzi wa majengo mapya, makubwa na ya kudumu. Mitaa ya Michenzani na Darajani kumewekwa taa zinazotumia nishati ya jua. Angalau usiku unakuwa na mwangaza wa kuonana kama si kuoneana.

Kumbuka kuwa nazungumzia miaka mitatu ya kutokuwapo kwenye ardhi ya kwetu. Ni kipindi kifupi mno kurudi nikakuta majengo kama yale ya Mamlaka ya Mapato ya Zanzibar na ujenzi unaoendelea kwa kasi kwenye eneo la Shangani. Maduka ya kisasa Mji Mkongwe na hata jengo jipya la Bandari ya Malindi.

Mote pia – Pemba na Unguja – nimekutana na wavuja jasho wakisaka tonge zao kwa juhudi kubwa. Vijana, watu wazima, wake kwa waume, wanaendelea kufaya kazi za kukimu maisha yao. Hili la ’kuendelea kufanya kazi’ nalisisitiza kupingana na dhana potofu iliyojengeka kwamba watu wa pwani, Wazanzibari tukiwamo, ni wavivu na mamwinyi wasiojiweza, wasiojishika.

Hapana. Nimeikuta mikono dada yangu mwenye umri wa miaka 45 ikiwa imezidi kusinyaa na kuwa migumu kwa kazi za sulubu. Hata nilipoondoka akanifungia pepeta kutokana na mpunga alioulima, akauvuna na akautwanga kwa mikono yake mwenyewe. Nimepikiwa ndizi mbivu ya Mkono wa Tembo iliyolimwa na mama yetu mwenye umri wa karibuni miaka 70 sasa.

Ninalotaka kusema hapa ni kwamba watu wangu, Wazanzibari, si wavivu na hawajasita kufanya kazi. Hawajaacha kujituma.

Ikiwa miundombinu ya barabara na majengo na kuvuja jasho ni dalili ya kusonga mbele kimaendeleo, basi tukubaliane kwamba Zanzibar inaelekea kwenye njia sahihi ya maendeleo. Lakini kuna walakini.

Mtaa wa Kichungwani, Chake Chake.
Mtaa wa Kichungwani, Chake Chake.

Miaka mitatu ya kuishi kando ya jamii yangu imeniwezesha kuyaona yale ambayo kama ningelikuwamo ndani yake nisingeliyaona. Mojawapo ni huku jamii yangu inavyojipima maendeleo yake kwa kutokuendelea kwake. Na hapa nitapiga mifano miwili mitatu.

Kule dikoni kwa samaki Nungwi, kaskazini Unguja, nilikutana na mnada. Wavuvi huwatoa samaki wao moja kwa moja madauni na kuja kuwabwaga chini ya Mkungu. Dalali wa serikali anawatia bei na baadaye mnunuzi mwenye fedha nzuri anakabidhiwa. Samaki hawa wanagaragara mchangani, wanang’ongwa na nzi na kupigwa na jua.

Kando kidogo, serikali ilijenga soko dogo lakini zuri, ambapo shughuli hizo zingefanyika. Lakini hazifanyiki. Bado watu wangu wanaona kuuza samaki sokoni kutawagharimu zaidi, pengine kwa kulipia kodi ya jengo. Hivyo, wanabakia na uholela wa kibiashara.

Mfano huu wa samaki wa Nungwi unazaa mwengine ndani yake. Bei ya samaki imepanda sana. Mtungo wa samaki ambao sasa unagharimu shilingi 20,000, miaka mitatu nyuma ungeuzwa kwa 7,000, ingawa mtu aliyeweza kununua samaki hao kwa bei hiyo ya mwaka 2010 ndiye yule yule anayeweza kuwanunua leo kwa bei hii ya 20,000.

Hili linasema kwamba kipato kimeongezeka, lakini halisemi kwamba maisha ya mtu huyo yameimarika. Sijaulizia wala sijataka kujua kuhusu kima cha pato apatalo mlaji wetu wa samaki wa shilingi 20,000. Nasikia Serikali ya Umoja wa Kitaifa imeongeza mshahara, lakini hauwezi kuwa umeongezeka mara tatu kama alivyoongezeka “Tasi wa Nungwi“.

Hata hivyo, wakati naondoka nikawasikia baadhi ya viongozi wa serikali wakijisifia kwamba hilo la kuongezwa kwa mishahara ni hatua kubwa ya maendeleo ambayo haikuwahi kupigwa kwa miaka kadhaa huko nyuma. Huko ni kuyapima maendeleo kwa kutokuendelea kwetu. Kwa hali hiyo hatutaendelea sana na au tukuwa tunapiga hatua ndogo ndogo kama ngoma ya mbwa kachoka, huku tukijisifu kwamba tunasonga mbele.

Kama nilivyotangulia kusema, nimewakuta watu wakiumuka jua-mvua kusaka tonge yao. Zao la karafuu limeendelea kuzaliwa kwa wingi kisiwani Pemba. Mchana nimewakuta watu wakiwa mitini wameitawa mikarafuu, mapakacha na vingowe vyao juu na mapolo yao chini, watoto wao wanaokota vitawi na au wanachuma zilizo matawi ya chini. Jioni nikawakuta wakizinyambua, asubuhi wengine wakizianika, na wengine wakiwa wamezipakia kwenye magari ya ng’ombe kuzipeleka vituo vya Shirika la Biashara la Zanzibar (ZSTC) kwenda kuziuza.

Katika mtiririko huo sijaona lililobadilika ingawa naambiwa bei ya karafuu imekuwa ya juu sana. Miaka takribani 200 ya kuwa na mkarafuu visiwani Zanzibar, bado mkulima anapaswa kutumia mbinu zile zile za Sultan Barghash bin Said katika kuzivuna, kuzitayarisha na kuziuza.

Licha ya kuwa kwake zao linaloiingizia nchi fedha nyingi za kigeni, bado hakuna maendeleo kwenye sayansi ya ukulima wake. Hatuwezi kupima maendeleo ya kilimo cha karafuu kwa kuangalia bei yake tu, ambayo kwa vyovyote inategemeana sana na soko la dunia na ambalo linaathiriwa pia na aina ya mazao tunayoyapeleka huko.

Tubadilike na tuibadili nchi. Na haya yamo ndani ya uwezo wa akili zetu kama yalivyo kwenye mikono yetu.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.