Zanzibar ilifanya kosa kuingia kwenye mfumo huu wa muungano na jirani yake, Tanganyika. Kilichotokea Aprili 1964 ni “ajali ya kisiasa” kama zilivyo ajali nyingine zozote. Waswahili husema “ajali haina kinga”, lakini huko kutokuwa na kinga hakumaanishi kwamba ajali ni jambo zuri. Ajali zina madhara – majeraha, kuharibika mali na vyombo na hata vifo.

Ndiyo maana mara baada ya ajali kutokea, jitihada huchukuliwa kurudisha hali ya kawaida, ingawa pia Waswahili haohao husema kuwa “lishalovunjika ni gaye”. Lakini gaye (upande wa nyungu au kaure) linaweza kufanyiwa marekebisho ya hapa na pale.

Kwa miaka ikaribiayo 50 sasa, Wazanzibari wamekuwa wakijaribu kupambana na madhara ya ajali ya kisiasa iliyoipata nchi yao. Hiyo imekuwa miaka 50 ya kulifanya gaye lifae kuwa nyungu ya kupikia.

Je, kama mfumo huu wa Muungano ulikuwa ajali, ilikuwa ajali iliyoweza kuepukwa? Kwetu wengine, jibu lake ni “ndiyo”. Laiti kama kuelekea uhuru wa mwaka 1963, wakati wa zile ziitwazo “Zama za Siasa”, wanasiasa wa Zanzibar wangeliweza kujenga Mwafaka na Maridhiano ya Kitaifa.

Wangelifanya hivyo basi pasingelifanywa Mapinduzi ya Januari 1964 na hatimaye kusingekuwa na Muungano. Kwa Zanzibar, Muungano ulikuwa nyenzo ya kuwalinda watawala walioingia madarakani baada ya Mapinduzi.

Hilo nalibakie hapo kwanza, maana halikuwa lengo la makala haya kuchambua chimbuko la Muungano. Itoshe tu kuthibitisha hoja kwamba Zanzibar iliingia kwenye mfumo huu wa Muungano kimakosa. Na kama lilivyo kosa lolote lile, ni busara kuliepuka. Kama halikuweza kuepukwa kabla ya kufanyika, basi hekima ni kupunguza madhara ya kosa hilo baada ya kufanyika na kujiepusha na mengine mfano wake. Na yako mengine, kwa hakika, baada ya kufanywa, huweza ‘kufanyuliwa.’ La mfumo huu wa Muungano tulio nao sasa, lilipaswa kuwa moja wao.

Lakini je, hata kama hilo la kulifanyua kosa la mfumo wa Muungano likitokea, Zanzibar itakuwa imeyamaliza matatizo yake yote iliyonayo? Kwa hili, jibu ni “hapana” kwa sababu mfumo wa Muungano si tatizo pekee kwa Zanzibar, hata kama ni miongoni mwa matatizo hayo.

Zanzibar inakabiliwa na matatizo mengine mengi na tena makubwa sana. Hayo ni matatizo ambayo hata kama Zanzibar isingelikuwa kwenye Muungano, bado yangelifanya libakie kuwa taifa lililo nyuma sana kimaendeleo mithali yalivyo mataifa mengine yaliopata uhuru wakati ule ule Zanzibar ilipopata wake.

Kama kulivyo kwengine, hasa barani Afrika, Zanzibar pia kuna ufisadi unaofanywa na viongozi wa serikali, kuna ugoigoi wa kijamii na utovu wa nidhamu wa umma. Zanzibar hii leo ingepaswa iwe zilipo nchi kama Sudan, Misri na Ghana, kwa mfano, ambazo kwenye miaka ya ‘60 zilifanana sana na Zanzibar kwa uwezo wao wa kiuchumi, wingi wa wasomi, na nidhamu ya kijamii.

Mkufu wa matatizo shingoni mwa Zanzibar ungeliitundika nchi hii hata kama isingelikuwa kwenye mfumo huu wa Muungano na Tanganyika. Hata nje ya Muungano, Zanzibar isingelikuwa taifa bora lau ingekuwa nao hawa wanasiasa waliobobea katika kufisidi mali ya umma – ardhi, majengo na fedha, ambazo zimegeuzwa kuwa mali ya viongozi hao na familia zao.

Taifa ambalo lina raia wasiotambua haki na wajibu wao kwa nchi, ambao wanaweza kuiibia serikali, kuharibu mali ya umma au kutelekeza wajibu wao kwa kiwango tufanyacho kwetu, haliwezi kuwa zuri zaidi ati kwa kuwa liko huru nje ya Muungano.

Taifa lenye kundi la wanasiasa wanaopigania kusalia madarakani hata kwa mtutu wa bunduki, wakipitia kwenye chaguzi zisizo huru wala zisizo za haki, haliwezi kusonga mbele kiuchumi, hata kama juu yake hakuna kizibo.

Taifa ambalo lina usiri mkubwa sana kwenye mfumo wake wa kijamii, ambapo watoto wadogo wa kike na kiume huharibiwa na walimu, wazee, walezi na wakubwa wao, kisha likashindwa kuwachukulia hatua wahalifu hao kwa sababu yoyote ile iwayo, haliwezi kuzalisha vichwa vya kuliendeleza.

Haya ni matatizo makubwa yanayoikabili Zanzibar. Na matatizo haya – kama yataendelea kuwapo hivi hivi – yasijengewe matumaini kwamba mara baada ya Zanzibar kutoka kwenye mfumo wa sasa wa Muungano, basi itaweza kusimama na kuwa taifa, nchi na dola huru yenye neema kufumba na kufumbua.

Nirudie. Mimi ni mmoja wa wanaoamini kwamba Zanzibar ilifanya kosa kuingia kwenye Muungano. Nimekiita kitendo hicho kuwa ajali ya kisiasa. Ndiyo, ilikuwa ajali, tena mbaya. Ajali haisifiwi wala haikaribishwi. Ajali hukosolewa na huepukwa.

Lakini mwenendo wa mambo ndani ya Zanzibar yenyewe unaonesha kwamba nchi yetu bado ina matatizo mengine makubwa. Ni kwa kuyaweka sawa matatizo hayo tu, ndipo kuwa kwetu nje ya mfumo wa sasa wa Muungano kutakuwa na maana kwa maisha ya Mzanzibari wa kawaida. Na hilo la kuyaondoa matatizo hayo, halitakuwa jambo la siku moja, wala mbili. Utakuwa mchakato wa muda mrefu.

Vuguvugu la umma kwenye mataifa ya Kiarabu limeibua hoja kwamba mataifa kama vile Misri, Yemen na Libya, kwa mfano, sasa yanarudi hatua 100 nyuma kuliko pale yalipokuwa kabla wananchi hawajawapindua viongozi wao wakongwe.

Kuna kitu kilikosewa, ambacho ni taaluma ya kuyasimamia matarajio ya umma. Nitaiita taaluma hii expectology (public expectation management). Hapana shaka, haikuwa halali kwa Hosni Mubarak kuendelea kuwa Firauni wa Misri wala Zein Al-Abidin Ben Ali kuwa dikteta wa Tunisia, kama vile ambavyo si halali kwa Dodoma kuendelea kuwa mtawala wa Zanzibar. Lakini kuyadumisha mapinduzi ya umma wa Kiarabu, wanamkakati walipaswa kuutayarisha umma kwa kipindi kigumu cha kuyasimamisha mapinduzi hayo.

Ya Zanzibar pia ni yayo. Bado Zanzibar haijawa na mageuzi makubwa yanayoonekana kuwa matarajio ya walio wengi. Ninachokusudia ni kuwa hata kama lengo ni kuwa na mfumo tafauti wa Muungano kati ya Zanzibar na Tanganyika, kuelekea huko wanamkakati walenge sasa kwenye taaluma ya expectology, inayojumuisha pia kuyatatua matatizo makubwa ya ndani – angalau kwa kuanza leo kuyazungumzia kwa uwazi.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.