Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, amechukua fomu ya kugombea urais wa Zanzibar kupitia chama hicho, huku akisema afya yake ni nzuri na yupo imara kugombea nafasi hiyo na kuongoza nchi.

Katibu Mkuu wa CUF ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad akikabidhiwa fomu ya kuwania nafasi ya urais wa Zanzibar na Katibu wa CUF Wilaya ya Magharibi, Saleh Muhammed Saleh.
Katibu Mkuu wa CUF ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad akikabidhiwa fomu ya kuwania nafasi ya urais wa Zanzibar na Katibu wa CUF Wilaya ya Magharibi, Saleh Muhammed Saleh.

Alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari visiwani hapa baada ya kuchukua fomu hiyo katika ofisi za CUF Bububu wilaya ya Magharibi jana  kwa ajili ya uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu.

“Ingekuwa afya yangu siyo nzuri nisingegombea nafasi hii, lakini kwa kuwa nipo imara kimwili na kiakili na siugui wala siyo mgonjwa nitagombea,” alisema Maalim Seif.
Alisema hakuna atakaemzuia kuwa Rais wa Zanzibar na kuwataka wafuasi wa chama hicho kuwa na umoja na mshikamano ili kuibuka na ushindi katika uchaguzi huo.
VIPAUMBELE VYAKE
Alieleza vipambele vyake endapo atashinda katika uchaguzi mkuu na kuwa Rais wa Zanzibar kuwa ni pamoja na kuwafanyia mambo mema Wazanzibari ambayo yameshindwa kutekelezwa na CCM.
Pia alisema atahakikisha amani na mshikamano na haki sawa kwa watu wote kwa sababu haki hiyo haipo na inatolewa kwa upendeleo.
 Alitolea mfano haki ya kupata vitambulisho vya Mzanzibari mkaazi, akidai haki hiyo inatolewa kwa dhuluma na wenye haki hiyo wananyimwa na kupewa watu wengine ambao hawana haki na wala hawastahili kupewa.
 Alisema pia atahakikisha anaboresha maisha ya wananchi wa Zanzibar kwani hali zao za kimaisha kwa sasa haziridhishi.
 “Rasilimali Zanzibar tunazo lakini hazijatumiwa vizuri, lakini ninaahidi mkinichagua nitazitumia rasilimali zilizopo na vijana mtapata ajira sawa sawa,” alisema Maalim Seif huku akishangiliwa na wafuasi wake.  Alipoulizwa kuhusu endapo atashindwa katika uchaguzi mkuu ujao ataendeela tena kugombea nafasi hiyo katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2020, alisema wakati ukifika ataamua kama alivyoamuwa mwaka huu kuwa atagombea au hatagombea.
Kuhusu wanachama wa chama hicho kutogombea nafasi hiyo ya urais na badala yake kuwa mgombea pekee kila mara, Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais, alisema hajamzuia mtu kugombea nafasi hiyo na kuwataka wafuasi wake kujitokeza kugombea.
 “Chama hiki hakina ubaguzi kila mtu ana haki ya kugombea nafasi hii na wala hakuna anayeniogopa labda niseme kuwa tu wameridhika na mimi nigombee nafasi hii,” alisema.
 Alisema muda bado upo wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kugombea urais na imani yake kuwa watu watajitokeza.
WAFUASI CUF WAZUNGUMZA
Wafuasi wa chama  hicho ambao walijitokeza kwa wingi kutoka maeneo mbalimbali ya visiwa vya Zanzibar kumsindikiza kiongozi wao kuchukua fomu hiyo, walionekana kuwa na furaha na kusherehekea uamuzi wa kiongozi wao na kusema uamuzi huo wa Maalim Seif ni matarajio yao kuona anashinda na watampa kila ushirikiano kuhakikisha anaongoza nchi.
 Khadija Salum Ali (53), mkazi wa Michezani ambaye alifika katika maeneo hayo, alisema kitendo cha kiongozi huyo kuchukuwa fomu kimemfurahisha kwa sababu amewakubalia maombi yao kwani ndiye wanayemtaka kwani wana imani ataikomboa nchi .
 “Maalim Seif anania njema na Wazanzibari na ndio maana wafuasi wake tunamkubali na kumuamini na yale ambayo tunayahitaji. Wazanzibari ndiyo wanaopata tabu katika mfumo wa  Mungano,” alisema Khadija.
Alisema ni matumaini yake Maalim Seif akiwa Rais wa Zanzibar watapata serikali yenye mamlaka kamili na kuwa na Muungano wa mkataba.
Shihabu Ahmmed, mkazi wa Hurumzi, alisema alisema kwa wakati huu hakuna kiongozi mwingine katika chama hicho atakayeweza kukiletea ushindi chama hicho kwa nafasi ya urais wa Zanzibar zaidi ya Maalim Seif.
 Alisema tokea chama hicho kilipotangaza utoaji wa fomu za kugombea nafasi hiyo hakuna mtu aliyejitokeza kugombea nafasi hiyo zaidi ya katibu mkuu huyo kwa sababu hakuna atakayeweza kukiletea ushindi chama hicho.
“Maalim Seif ni mtu wa watu, kwanza ana mvuto, haiba na anakubalika kila kona kwa hivyo watu wanaona kushindana naye ni kujihangaisha tu,”  na kuongeza:
 “Kama yupo mtu anaweza kushindana na mkwaju huu na kuiletea ushindi Zanzibar kwa tiketi ya CUF basi ajitokeze lakini mimi kura yangu ni kwa Maalim Seif.”
CHANZO: NIPASHE

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.