Bwana Mandola ni mhusika kwenye filamu ya kijembe cha kisiasa iliyotolewa na Bollywood mwanzoni mwaka huu wa 2013 kwa jina la Matru Ki Bijlee Ka Mandola. Ni filamu ya vichekesho inawayozungumzia watu watatu – Harphool Singh Mandola, bintiye aitwaye Bijlee na dereva wake, Hukum Singh Matru.

Pankaj Kapur (kulia) kama Harphool Singh Mandola, Imran Khan (kushoto)  kama Hukum Singh Matru na Anushka Sharma kama Bijlee Mandola (katikati) kwenye filamu ya Matru Ki Bijlee Ka Mandola.
Pankaj Kapur (kulia) kama Harphool Singh Mandola, Imran Khan (kushoto) kama Hukum Singh Matru na Anushka Sharma kama Bijlee Mandola (katikati) kwenye filamu ya Matru Ki Bijlee Ka Mandola.

Bwana Mandola ana sifa, au tuseme ila, tatu: ni tajiri mkubwa, ni mlevi mkubwa na ni mwanamapinduzi mkubwa. Lakini hilo la uwanamapinduzi halionekani kwenye haiba yake mpaka kwanza ‘apige maji’ na yamtoshe. Mara tu akishalewa chakari, hapo ndipo Mandola Mwanamapinduzi huibuka ndani yake. Yule tajiri mlafi anayetaka kukigeuza kijiji kizima kilichopewa jina lake kuwa eneo huru la kiuchumi na kuwafukuza kwa dhuluma wakulima wa kijiji hicho, hutoweka.

Mwanzoni mwa mchezo, ni yeye anayewatokea wanakijiji wakifanya mkutano wa kudai mashamba yao kutoka kwake, na ni yeye anayewahamasisha wafanye mapinduzi ya kumpindua mwenyewe. Lakini wakati wanakijiji wameshahamasika, mwenyewe anapitia mlango wa nyuma wa kasri lake, ambako kwa bahati mbaya anatumbukia kwenye bwawa la maji na hivyo ulevi unamtoka na sasa Mandola tajiri mlafi anaibuka ndani yake. Anachukua bunduki na kuwaelekeza wanakijiji wanaoelekea kulivamia kasri lake kutwaa haki yao kwa njia ya mapinduzi ya umma.

Wanakijiji wote wanakimbia, huku wakijiuliza: “Lakini sini huyu huyu aliyetuhamasisha tufanye mapinduzi tukatwae haki zetu kwake sasa hivi tu!?” Kisha Bwana Mandola anamgeukia dereva wake, Matru, na kumuuliza kwa nini amemruhusu (yeye Mandola) alewe mpaka kupitiliza, ilhali anajua kuwa tajiri wake huyo akishalewa hupoteza fahamu na kuwa Mandola mwengine.

Ndipo hapo mtazamaji anapojua kuwa kumbe kazi ya Matru haikuwa udereva wa gari tu, bali pia kuendesha kiraru cha ulevi wa Bwana Mandola. Chama cha Mapinduzi (CCM) ni Bwana Mandola.

Kinapokuwa‘kizima’ hakijalewa, ni chama kilichoshika dola na hatamu za uongozi na chenye ulafi wa kutosha kuhalalisha upapiaji wake wa madaraka. Kimefanya hivyo miaka nenda miaka rudi kwa jina la kukubalika na umma kwa mbinu na kiwango kile kile Bwana Mandola anachofanya kwenye umiliki wa ardhi ya wanakijiji. Ghilba, jeuri na kiburi, kwa kushirikiana na mawakala wake waliomo kwenye asasi na taasisi kilichoziunda chenyewe kutoka unyayo hadi utosi wa nchi.

Lakini CCM ina khulka ya ulevi. Kwa hakika imeshalewa na kulewalewa kwenye madaraka, kiasi cha kwamba baadhi ya wakati andasa za kilevi hupanda kichwani zikaiibua CCM nyengine ndani yake – taasisi ya kimapinduzi hasa kama lilivyo jina lake.

Kipindi cha mwaka mmoja uliopita andasa hii ya CCM ikampanda mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete, ambaye naye akadhukuru “matarajio ya kimapinduzi” kwa kutangaza mchakato wa kuelekea katiba mpya. Ilikuwa andasa ya kilevi ya Bwana Mandola, maana nani asiyejua kuwa miezi michache tu kabla ya hapo CCM hiyo hiyo ilikuwa imeng’ang’ania kuwa katiba iliyopo ‘yatosha’?

Lakini Rais Kikwete akazuka ghafla-bin-vuu akisema vyengine – kwamba katiba hii haitoshi. Panapaswa kuwepo na nyengine. Nchi nzima ikainuka kumpigia makofi na kumpongeza. Bwana Mandola akatunga wimbo na ngoma ya kimapinduzi. Mapinduzi hupinduliwa mtawala. Mtawala hapa ni CCM. Hivyo wimbo wa katiba mpya ulikuwa ni wimbo wa kuipindua CCM. Ikateuliwa Tume ya Jaji Mstaafu Joseph Warioba (pia mwana-CCM) kuusimamia mchakato huo.

Lakini kumbe, kama tulivyokuja kujua baadaye, jukumu la Tume hii lilitakiwa na CCM liwe ni kama lile la dereva Matru wa Bwana Mandola. Sio tu kuiendesha nchi kuelekea Katiba Mpya, lakini pia kuiendesha Katiba yenyewe kuelekea kwenye matakwa ya CCM.

Kumbe Jaji Warioba na wenziwe walikuwa na jukumu la ‘kumdhibiti’ Bwana Mandola asilewe, ama akilewa asipitilize. Haikufanya hivyo. Ikauwacha wimbo wa kimapinduzi kwa jina la katiba mpya ulioanzishwa na mwenyekiti mwenyewe wa CCM usikike, uakisike na mwangwi wake uaminike kwa umma.

Tumejua hivyo baada ya jitihada ambazo zimekuwa zikifanywa tangu pale tume hiyo ilipoitangaza na kuikabidhisha rasimu ya kwanza ya katiba, ambayo miongoni mwa mengi iliyoyapendekeza, lililoikasirisha CCM ni pendekezo la Muundo wa Muungano wa Serikali Tatu.

Tangu hapo, Bwana Mandola ndani ya CCM amekuja juu kama moto wa kifuu. Hakuna tusi alilowachwa kutukanwa Jaji Warioba na wenzake kwenye Tume kwa kuja na pendekezo hilo. Na hata ilipodhihirika wazi kwamba wananchi walio wengi kupitia ama kauli zao za moja kwa moja au kupitia vyama vya siasa, makundi ya kijamii au asasi za kiraia zinazowawakilisha, wanaunga mkono pendekezo la Muundo huo wa Muungano, CCM haikuacha kufanya mbinu na hila.

Ya karibuni zaidi ikawa ni hatua ya wabunge wa CCM kupitisha Mswaada wa Mabadiliko ya Sheria ya Katiba Mpya, kwa kile kilichoonekana wazi ni mapindi ya mwisho mwisho ya kuinusuru nchi isiingie kwenye Muundo wa Muungano wa Serikali Tatu. Sasa tena Bwana Mandola wa CCM amejikuta akilewa chupa nyengine za ulevi. Za mara hii ni baada ya shinikizo la Zanzibar kupitia upande wa Chama cha Wananchi (CUF) ndani ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa na kambi ya upinzani Bungeni.

Kwamba wataishitaki CCM na serikali zake kwa umma kwa kuuteka mchakato wa Katiba Mpya na kuikandamiza Zanzibar. Rais Kikwete ameinuka mwanzoni mwa Oktoba hii akasema ni kweli kuna ulazima wa hili kuangaliwa upya. Huko ni kwenda kinyume na maneno na matarajio ya wana-CCM wenzake, ambao walishaamini kwamba Rais Kikwete angeliusaini mswada kama ulivyo, na hivyo kukengeuka matakwa ya wananchi wengine wengi.

Tena Bwana Mandola amebugia ‘murji’. Na bora asileuke tena hadi Katiba mMpya ipatikane na jamhuri mpya zizaliwe, zikifuatiwa na ushirikiano wa haki baina yao

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.