Wengine tutauchukulia mwezi huu wa Novemba kuwa wa aina yake visiwani Zanzibar kwa sababu ya matukio mawili, tunayoyaona ni muhimu kwa maendeleo ya kidemokrasia na kiutawala visiwani humo.

Moja ni kujizoazoa kwa Serikali ya Mapinduzi (SMZ) na kuja juu dhidi ya vyombo vya habari “vitakavyotumia vibaya uhuru wa habari na kuchapisha au kutangaza habari zenye lengo la kuvuruga amani.”

Hayo yalisemwa na waziri anayeshughulikia habari, Said Ali Mbarouk, katika kile kilichotajwa na vyombo vya habari vya Tanzania kuwa ni mkutano wa waziri huyo na wakuu wa vituo vya redio vya Zenj FM na Coconut FM, vyote vya Zanzibar.

Ujuu iliokuja nao SMZ katika hili ni kutoa onyo kwamba ama vyombo hivyo viache kupandikiza mgawanyiko wa Pemba na Unguja au vichukuliwe hatua kali. Hatujui ukali wa hatua hizo kali, lakini mazoea ya serikali zetu yanatupa mwelekeo wa makisio – vitapigwa faini, vitafungiwa, lakini havitapelekwa mahakamani. Vikipelekwa mahakamani itakuwa ni hatua nyengine kubwa ya kupongezwa katika ukuaji wa demokrasia na utawala wa sheria nchini mwetu.

Isifahamike kwamba makala haya yanapingana na onyo hilo la Waziri Said. La hasha. Kwa hakika, yanakubaliana nalo kabisa na yangelipenda hata liongezwe nguvu zaidi, yaani sio tu vyombo hivyo vikabiliane na adhabu iwapo vikiendelea, bali viwajibike sasa kwa yale ambayo tayari vimeshayatangaza.

Ikiwa msingi wa kuchukuliwa kwao hatua hapo baadaye ni athari za matangazo yao dhidi ya Umoja wa Kitaifa wa Wazanzibari, basi tayari umoja huo umeanza kuathiriwa. Sikiliza kauli za viongozi wajiitao wa shehia, wazee na vijana wa Unguja kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM) wakifoka hadi mapovu kuwatoka dhidi ya watu wenye asili ya kisiwa cha Pemba. Hapa nimewaita “wajiitao” na namaanisha hivyo hivyo “wajiitao wa Unguja.”

Hao niwaitao “wajiitao wa Unguja” wanasikika wakitamka kwamba Wapemba hawapaswi kuendelea kubakia kisiwani Unguja kama wanapingana na mfumo wa Muungano wa Serikali Mbili uliopo sasa. Wasikie hao “wajiitao Waunguja” wakikumbusha mauaji yaliyofanyika wakati wa Mapinduzi na wakiapa kwamba wako tayari kwa mapinduzi mengine kama hayo ili “kuweka heshima na adabu.”

Chuki, hasira na kisasi kinaonekana wazi kwenye maneno yao kama zionekanavyo kwenye nyuso na dhamira zao. Kauli ya vita, damu, mauaji, majeruhi, unaweza kuihisi kwa mbali. Makala haya yanadhani kwamba hatua zilipaswa kuchukuliwa leo, mfano wa vile viongozi wa Uamsho walivyochukuliwa hatua na Serikali hii hii, ikiwa kweli Serikali ilikuwa na haki ya kufanya vile wakati ule.

Ila kama panangojewa hadi watu washikiane mapanga, kama ilivyotokea Rwanda baada ya Redio Intarahamwe kutumika kuchochea mauaji dhidi ya kabila la Watutsi na Wahutu wenye msimamo wa wastani, basi natusubiri ule uitwao kwetu pwani “ushahidi wa Kinyamwezi”.

Nimeiita hatua hii ya sasa ya Serikali kwamba imekuja baada ya kujizoazoa. Nakusudia kwamba ni hatua nzuri iliyokuja baada ya Serikali kuchelewa sana na kuwachelea wakubwa. Palikuwa pamezoeleka kwa wale wanaojinasibisha na Mapinduzi na Chama cha Mapinduzi, hata kama ni mijitu mijahili, mijinga na mikatili, kuogopewa na SMZ. Ni kituko, lakini ndio ukweli kwamba Serikali ya Mapinduzi inawaogopa wajinasibishao na Mapinduzi, hata kama hawana uwezo wala njia za kupindua tena.

Si haba kwamba angalau kwa mara ya kwanza hao wajinasibishao na Mapinduzi – na kwa hakika ukichungua historia utawakuta wengi wao hata hawakuhusika nayo – sasa wanaambiwa kwamba Zanzibar si yao mali yao, wala yao peke yao.

Novemba hii pia itaingia tena kwenye historia ya maendeleo ya kisiasa visiwani Zanzibar, kwani kwa mara ya kwanza tangu kurudi kwa mfumo wa vyama vingi, Serikali iliamua kusimamia haki ya kisiasa ya kila raia kwa kukiruhusu Chama cha Wananchi (CUF) kufanya siasa za wazi kwenye jimbo la Donge, ambalo kwa miaka yote 20 na ushei ya siasa za vyama vingi wanasiasa wahafidhina wa chama tawala wamejenga mazingira ya kulitenga na sehemu nyengine za Zanzibar kama kwamba Donge ni nchi pekee.

Nakumbuka mwaka 2005, kundi letu la wanahabari lilipojikuta likilazimika kuripoti risasi na mabomu pale Mahonda baada ya polisi kuwazuia wana-CUF kwa mara nyengine. Matokeo yake, yalikuwa majeruhi na mauaji. Uvunjwaji wa haki za binadamu ukaendelea hata baada ya hapo.

Lakini ukweli ni kwamba mambo yana zama na zamu. Ndivyo alivyosema Rais Mstaafu wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour Juma, siku akitoa hotuba ya kusisimua juu ya umoja wa Wazanzibari, Ikulu ya Mnazimmoja kwenye mkesha wa Mwafaka wa kwanza wa kisiasa kati ya CCM na CUF mwaka 1999.

Sasa zama zimebadilika na mabadiliko haya yanawaumiza wanasiasa ambao walivuta pumzi, walikula na walikunywa uhasama wa kisiasa. Donge imefunguka na kujiunga tena na sehemu nyengine za Zanzibar.

Wala kujiunga huko si lazima kumaanishe kuiacha mkono CCM na kuikumbatia CUF. La hasha. Kunamaanisha kwamba sehemu hiyo nayo sasa iko tayari kusikiliza hoja na kuzipima ndani ya ardhi yake kisha ikafanya uamuzi baada ya kuzipokea hoja hizo. Wanaotaka kujiunga na CUF wakafanya hivyo kwa mujibu wa walichoelewa na wanaotaka kusalia CCM wakafanya hivyo kwa mujibu huo huo. Lakini si kinyume chake.

Mantiki muhimu hapa ni kwamba kubwa kuliko yote Donge nayo ni Zanzibar, imekuwa hivyo na itakuwa hivyo milele. Kama ilivyo Pemba, kwa ujumla wake, ndivyo ilivyo Donge kwa udhati wake. Zote ni sehemu za Zanzibar, zimekuwa hivyo na zitabaki hivyo milele.

Wale wanasiasa waliopigania kuitenga Donge na Zanzibar na ambao sasa wanahubiri utengano wa Pemba na Unguja, “imekula kwao” kwa kutumia lugha ya vijana wa kileo.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.