HEBU tumsome Dk. Ghassany ameandika nini katika kitabu chake Kwaheri Ukoloni Kwaheri Uhuru kuhusu Hanga wakati yuko nyumbani kwa Oscar Kambona anajitayarisha kurejea Tanzania: ”Nnavokumbuka mimi, Oscar akatwambia sikilizeni bwana. Mimi nimekuiteni hapa mje mseme na ndugu yenu na mzee wenu huyu, Hanga, amekuja hapa na anataka kurudi nyumbani.
Hajataja pahala. Na mimi nimemkataza. Nimemwambia huu si wakati mzuri ni bora yeye asiende. Ama angelibaki huko huko West Africa anokotoka kwa mkewe, au abaki hapa London lakini kakataa, anataka lazima arudi. Na mie na hofu maisha yake kuwa akifika kule hatoweza kupata salama. Kwanza kuwa yeye amefikia kwangu, anajulikana yeye na mimi ni rafiki, Nyerere atajua zaidi/uzuri hayo kuwa mimi tangu tuko kule tunasikilizana mimi na ndugu huyu Abdallah. Kwa hali hiyo mimi namwambia. Na yeye Abdallah anasema hana ugomvi na Nyerere.
Waliokaa kutoka kushoto: Marehemu Abdullah Kassim Hanga na Abeid Karume,
Waliokaa kutoka kushoto: Marehemu Abdullah Kassim Hanga na Abeid Karume,

Sasa mimi nimekwiteni mzungumze naye, mseme naye. Akatuchukua akatupeleka kwenye chumba akasema; “Abdallah, hebu zungumza nao hawa jamaa wamekuja kukuamkia.” Tukaingia sie chumbani akatuacha mimi na Ahmed [Rajab] na Abdallah. Peke yetu watu watatu. Ndivyo ninavyokumbuka mie na ndivyo anavyokumbuka Ahmed [Rajab].

Mimi sikumbuki ile nilikwenda railway station. Kile mimi sijakumbuka. Kama ulivyosema, mimi nyumba nilikuwa naijua, sina haja ya Kasembe kunpeleka. Lakini inaweza kuwa nimekwenda mimi na Kasembe kumpokea Ahmed Rajab. Yeye Ahmed kafkiri tu na mie ni mgeni. Hajajua kuwa mimi na Kambona tunajuana na jirani, na nyumba yangu mie na yake si mbali.
Na Mohamed Said
Na Mohamed Said

Ahmed Rajab ndiye anasema, tumefika aliyefungua mlango ni Oscar Kambona, na akatuonyesha chumba. Hajaeleza nini Kambona katuambia. Lakini mimi nakumbuka Kambona katuambia kwanza, “semeni naye.” Yeye kazungumza moja kwa moja, sisi tumekaribishwa tumekwenda kwa Abdallah. Yeye Ahmed amekumbuka mambo mimi sijayakumbuka. Kwa sababu, kasema tulipofika Abdallah Hanga katuambia sikilizeni: nyinyi ni vijana, watoto kwa sasa, lakini kesho nyie ndio mtakuwa viongozi. Nina maneno ninataka kukwambieni. Tukawa sasa tumekaa tunamsikiliza nini atasema.

Anasema nataka kukwambieni juu ya habari ya mapinduzi yetu ya Zanzibar. Kuna mabaya ambayo tuliyafanya na kabla sijasema lolote ninakutakeni jambo moja muhimu mlikumbuke. Msije mkakubali kufuata siasa za ukabila. Siasa za ukabila ndizo zinazotuletea matatizo na ndizo zitakazozidi kutuletea matatizo. Hilo ni jambo la mwanzo ambaye yeye Hanga katuambia.
Akasema mimi (Hanga) nilivyoondoka Zanzibar kupelekwa Dar es Salaam, kuwa Waziri wa kule, badala ya kuwa Vice-President [Makamu wa Rais] huku na Mzee Karume, alivyopelekwa bara, anasema jambo moja katika mambo aliyoyafanya ni kuwasaidia Wazanzibari waliokimbia kutoka Zanzibar wakakaa pale, wale ambao wataalamu, kuwatafutia kazi. Akataja majina. Akamtaja Maalim Salim Sanura, na akawataja wengine, mimi siwakumbuki. Kuwatafutia kazi na wakapewa kazi serikalini. Hata ikafika akaanza kusemwa, akalaumiwa, kuwa Abdalla, mbona unakwenda kinyume sasa? Hawa si ndiyo tuliowapindua, mbona wewe sasa hapa unawasaidia? Unawapokea? Akasema bwana, hapa mimi naona ni Mzanzibari tu hapa. Hawa wote ni Wazanzibari bwana. Na hawako nchi nyingine. Wako na sisi pamoja hapa. Kwa hali hiyo yeye anasema ule ndiyo uzi anataka sisi tuufate. Tusibaguane.
Jambo la pili akasema, sisi Mungu atusamehe, tumefanya mambo mengi ambayo mabaya, tumedhulumu, tumechukua watoto na wake za watu, na Mwenye Enzi Mungu ndiye anaojua. Basi mimi namuomba Mwenye Enzi Mungu anisamehe na ninajuta kwa haya niliyoyafanya. Ahmed Rajab akamuuliza suala. Akamwambia, mzee, lakini wewe na Janab [Babu] mnasikilizana vipi kisiasa? Akamwambia, mimi na Babu sote wawili ni Marxists lakini Babu si tishio kwa Karume. Mimi ndio tishio. Mimi ndio ni tishio juu ya Karume, lakini Babu is not [si tishio]. Hiyo tafauti yangu mimi na Babu, anasema. Kwa Unguja. Sasa ndio tukamuuliza, vipi ikawa wewe ndo tishio? Yeye Ahmed Rajab ndiye aliyemuuliza.
Rome ilijaribu kuingia kati katika ugomvi wa Oscar na Nyerere na ilishindwa. Kambona alinieleza. Hata makanisa yamejaribu. Ugomvi ulikuwa mkubwa na hiyo akijua yeye zaidi Kambona ndio maana akahofu Abdallah asirudi. Ile imani yake ilikuwa kubwa kuwa Nyerere hatamdhuru. Na yeye akiona watu wangapi wamepotea lakini hajafikiria atakuja kuwa yeye.
Tukasema naye tukamwambia kweli hayo maneno anayoyasema Oscar inaonyesha ni bora usirudi kwa sasa. Akasema hapa kuna mambo mawili. Moja, kuna kutosikilizana baina ya Oscar Kambona na Nyerere, Rais Nyerere. Sasa huyu bwana akisema mimi nisirudi anazungumzia kule kutosikilizana baina yake yeye na Rais Nyerere. Sasa anahisi mie nikirudi labda kwa sababu mimi nimefikia kwake au ni rafiki yake Nyerere, anaweza akachukua hatua. Mimi nimeshafanya kazi na Nyerere na namjua vizuri mzee Nyerere, mimi na yeye hatuna ugomvi wowote. Abdallah Kassim Hanga anasema kuwa yeye na Nyerere hawana ugomvi. Na yeye ikiwa anarudi harejei Zanzibar. Atarudi anakwenda zake akakae nyumbani Dar es Salaam. La pili alisema, kuna ukweli wa kuwa mimi na Mzee Abeid Amani Karume kuwa hatusikilizani na kusema kweli si makosa yangu. Akasema Abdallah, jambo dogo sana limemfanya Mzee Abeid anichukie mimi hata ikawa mimi nikienda Zanzibar sasa siwezi kukaa nikalala Zanzibar. Lazima siku ile ile nirudi Dar es Salaam.
Na hili jambo anasema, mimi nilivyokuwa niko Tanzania Bara na Dar es Salaam ni mmoja katika mawaziri, nilikuwa ninakwenda Zanzibar mara kwa mara. Na nikienda nikifia katika nyumba iliyoko Migombani ambayo niliwahi kukaa nilivyokuwa Makamu wa Rais. Wakati mmoja nafikiri baada ya mapinduzi, President wa Zanzibar alikuwa ni Karume na Makamu alikuwa Hanga. Sasa ile nyumba ya Migombani ikawa yeye bado Hanga hajairejesha serikalini kila akienda Zanzibar anafikia pale. Siku katika siku alizokuweko pale anasema yeye kaja kafikia nyumbani pale Migombani na kila akienda watu wakipata habari kuwa Abdallah kaja, watu, jamaa, ndugu na marafiki, walikuwa wanakwenda kumuona na kuzungumza naye, na wengineo wanakuwa nayo mahitaji yao wanakwenda kumuomba awasaidie. Sasa siku moja hiyo Mzee Karume anatokea njia ya uwanja wa ndege kwenda zake mjini akapita pale Migombani akaona magari, akauliza. Kuna nini hapa, mbona magari mengi? Akaambiwa basi lazima Mzee Abdalla Kassim Hanga kaja. “Ala, sasa yeye kila akija lazima iwe namna hii?” Akaambiwa, yeye akija watu wanakuja hapa kumuamkia na kuonana naye. Basi jambo hilo anavyosema Abdalla Kassim Hanga ndilo liloanzisha ugomvi baina yake na Mzee Karume. Karume akawa hataki tena na ikawa na yeye Abdallah akienda Zanzibar hafikii tena katika nyumba ile. Akakataa kabisa.
Lakini inasikitisha kuwa tangu wakati ule yeye yupo pale London habari zishafika Cairo. Walioko Cairo ma-ambassador wa pale wameshapeleka habari Tanzania kwa Mzee Nyerere. Ikawa serikali ninavyosikia wamekaa wakimngojea arejee tu. Yeye Hanga hajajua, wala sisi hatujajua.”
Ukimsoma Dk. Ghassany anavyoeleza jinsi Hanga alivyoonywa asirejee Tanzania na yeye akakaidi unaweza kusema kuwa kifo kilikuwa kinamwita. Hebu sikiliza na kisa hiki kilichotokea Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam siku Hanga alipotua kutoka London kwa Egypt Air. Mpashaji habari wangu anasema:
”Wakati ule mimi nilikuwa meneja wa shirika moja la ndege. Nilikuwa uwanjani nikamuona Bi. Mkubwa. Huyu alikuwa mkewe Hanga, mwanamke wa Kingazija. Nikamuuliza mbona yuko pale akaniambia kuwa alikuwa amekuja kumpokea Hanga. Nilishtuka sana. Mimi ni Mzanzibari na nilijuana na Hanga kwa miaka mingi na nilikuwa nasikia mengi. Hanga alipofika nilikwenda kumlaki na tukatoka sote nje ya uwanja na hapo nikamualika yeye na mkewe chakula cha mchana hapo hapo uwanja wa ndege.
Wakati tunatoka nje ya uwanja nilimuuliza Hanga iweje karejea nchini wakati kama ule. Hanga akanijibu kuwa hapana kitu. Mimi sikuridhika. Tulipomaliza kula na tukawa tanazungumza nilitaka kwa mara nyingine niufungue moyo wangu kwa Hanga. Sikumbuki nilifanya nini lakini niliweza kumtoa mkewe pale mezani tukabaki sie wawili, mimi na Hanga. Hapo nikamwambia Hanga kuwa ni vyema kama akirejea London na ndege ile ile aliyokuja nayo. Hanga hakunisikiliza.
Jioni mimi nikamtafuta Ali Nabwa wakati ule anafanya kazi Tanganyika Standard. Nikampa habari kuwa Hanga yuko mjini. Tulimtafuta mji mzima mwisho tukampata Oyster Bay kumbe kafikia kwenye nyumba ya Kambona. Tukaja hadi Magomeni kwa Maalim Matar tukafanya dua.
Ali Nabwa kumbe alikuwa amewaambia Tanganyika Standard wasubiri habari muhimu wachelewe kidogo kuchapa gazeti. Siku ya pili Tanganyika Standard ikachapa habari ukurasa wa mbele kuwa Hanga amerejea nchini. Haikuchukua siku Hanga akakamatwa.

One thought on “Yaliyotokea kifo cha Abdallah Kassim Hanga-2”

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.