KUNA usemi na usemi huu ni wa Kichina ambao tafsiri yake ni: “Nyayo iliyonyoka haikiogopi kiatu kilichopindika.” Maana ya usemi huu ni kwamba mtu mwenye maadili yaliyonyoka haogopi umbeya au udaku. Yaani, huwa haogopi kusengenywa au kutiwa hewani, kama wasemavyo mitaani.
Madhali anachofanya au anachosema mtu huyo ni cha haki na cha kweli kisicho ila wala waa, madhali ameongoka na amenyoka hapaswi kuwa na hofu ya kutiwa midomoni.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mizengo Pinda.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mizengo Pinda.

Kwa bahati mbaya, baadhi yetu wenye uchu ya kuwapiga darubini wanasiasa, hususan wale wenye madaraka, hatukosi wa kuwatia hewani kila uchao. Wanajitakia wenyewe.
Hayo husababishwa na hulka yao kwanitabia moja waliyo nayo wanasiasa, wa mirengo na rangi mbalimbali za kisiasa, ni ya kuupindapinda ukweli. Hufanya hivyo wakijuwa kwamba wanadanganya na kwamba wanaowadanganya wanajuwa kwamba wanadanganywa.Lakini hawawezi kujizuia wasidanganye.
Inawezekana kwamba wanapodanganya, nafsi zao huisuta midomo yao. Hatujui. Tujuacho ni kwamba wamezoea kudanganya na kwao kudanganya kumekuwa kama mchezo. Kama kucheza bao chini ya mwembe.
Mtu huwa na mengi ya kujiuliza anaposimama Waziri Mkuu mzima bungeni kama alivyosimama Waziri Mkuu Mizengo Pinda wiki iliyopita na kusema, akiwa na macho makavu na bila ya kuyapepesa, kwamba hayajui yaliyowafika mashekhe 24 wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu, kwa ufupi Uamsho, waliokamatwa Zanzibar na kupeleka kufungwa gerezani Bara kwa tuhuma za ugaidi.
Mahabusu hao wanashtakiwa kwa makosa mane ya ugaidi na kesi yao iko katika Mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam. Washtakiwa wamekuwa wakihoji kwamba mashtaka hayo ni ya “bandia” na kwamba kilichowachongea ni msimamo wao wa kuupinga Muungano na wa kupigania Zanzibar irejeshewe mamlaka yake kamili.
Wamekuwa wakidai kwamba huo msimamo wao ndio ulioikera serikali na kuifanya “iwabambikie” mashitaka ya ugaidi.
Katika nyakati tofauti walipofikishwa mbele ya Mahakama mahabusu hao walieleza, bila ya kubania, unyama wanaodai kwamba walifanyiwa wakiwa gerezani.Shutuma hizo zimeenea nchini, zinazungumzwa mitaani, barazani na zimetajwa kwenye vyombo vya habari.
Inawezekanaje kwamba Waziri Mkuu awe peke yake asiye na fununu yoyote ya shutuma hizo? Itakuwaje mtu mwenye wadhifa wa kuongoza serikali, kama alionao yeye,asijulishwe pale vyombo vinavyomsaidia kusimamia sheria vinapotuhumiwa kuwa vimepotoka?
Na hata kama hajapashwa habari na wasaidizi wake, huwa hasomi magazeti na kufuatilia mambo kwenye vyombo vya habari? Hana afisa maalum anayeshughulika na habari na anayemjuza yanayojiri nchini kila siku? Haingii akilini kwamba Waziri Mkuu msomi kama yeye hana utaratibu huo.
Walipofikishwa awali Mahakamani washtakiwa hao walidai kwamba walipokuwa gerezani walipigwa, waliteswa na baadhi yao waliingiliwa kimwili kinyume na maumbile. Kwa ufupi, walilawitiwa. Huu ni unyama usio kifani, ni unyama wenye kulivunjia heshima taifa la Tanzania, serikali yake na viongozi wake.
Huo ndio unyama ambao Waziri Mkuu anatwambia kwamba hana habari nao ilihali uliripotiwa kwa kina na waandishi wa habari waliokuwapo mahakamani wakati shutuma hizo zilipokuwa zikitolewa.
Kwa vile hizo ni shutuma nzito ambazo baadaye zimekuwa zikizungumzwa mitaani, barazani na kwenye vyombo vya habari unakuwa na haki ya kujiuliza Waziri Mkuu huyu anaishi nchi gani? Anaongoza serikali ipi?Anawatumikia wananchi wepi?
Wala hutolaumiwa ukifikiria kuwa labda yeye ni miongoni mwa wale wenye masikio yaliyozibwa kwa vizibo maalum ili yasisikie yasemwayo.
Au pengine anahisi kwamba hana ubavu wa kuwakosoa wanaotuhumiwa kukiuka haki za binadamu? Labda ana uungwana wa kutoweza kufanya hivyo kwani si yeye aliyewahi kuwaruhusu polisi wawatie adabu waandamanaji kwa kuwapiga?
Hatujasahau yaliyojiri Bungeni wakati mmoja pale Pinda alipokuwa akimjibu Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Murtaza Mangungu, aliyelilaumu jeshi la Polisi kwa nguvu linazotumia linapopambana na wananchi wanapokuwa wanaandamana.
Pinda alimjibu Mangungu kwa kusema: “Ukifanya fujo umeambiwa usifanye hiki ukaamua wewe kukaidi utapigwa tu maana hakuna namna nyingine maana wote lazima tukubaliane nchi hii tunaiendesha kwa misingi ya kisheria sasa kama wewe umekaidi hutaki unaona kwamba ni imara zaidi, wewe ndio jeuri zaidi watakupiga tu na mimi nasema muwapige tu, kwa sababu hakuna namna nyingine maana tumechoka sasa.”
Hapo Pinda amekiri mwenyewe kwamba amewashajiisha polisi watumie nguvu badala ya sheria kupambana na waandamanaji akijuwa vyema kwamba wananchi hao hawakuhalifu sheria na kwamba wamekuwa wakitumia haki walizopewa na Katiba ya nchi.
Sasa ikiwa Pinda amewaamrisha polisi wawapige wananchi wenye kutumia haki zao za kikatiba za kukusanyika na kuandamana atawezaje kuwakemea polisi wa magereza wakiwatesa wamahabusi wanaotuhumiwa kwa ugaidi?
Ndio maana Mei 21 kwenye kikao cha maswali ya papo kwa papo Bungeni alijifanya kama mtu aliyejibanza nyuma ya miti na asiyeona wala kusikia yaliyo bayana mitaani.
Kwenye kikao hicho Mbunge wa Mji Mkongwe, Muhammad Sanya, alimtaka Waziri Mkuu aunde Tume Maalum ya Uchunguzi itayochunguza tuhuma za “ukatili na unyama” zilizotolewa na viongozi wa Uamsho walio gerezani Tanzania Bara.
Sanya alitumia neno “unyanyasaji” lenye maana ya kutesa, kudhalilisha au kuonea. Na ikiwa tuhuma za Sheikh FaridHadi Ahmed, mmoja wa mahabusu hao, zina ukweli, basi hivyo ndivyo walivyofanyiwa wengi wao gerezani huko Bara: waliteswa, walidhalilishwa na walionewa.
Vitendo vyote hivyo ni vyenye kukiuka haki za binadamu, ni vyenye kwenda kinyume na maadili ya utawala bora na ni sababu za kutosha zinazoweza kuwafikisha wenye kuvitenda mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai mjini Hague, Uholanzi.
Alichopaswa kukifanya Pinda na mawaziri wake wa sheria na wa mambo ya ndani mara tu baada ya kuibuka shutuma hizo Mahakamani ni kuunda jopo maalum la kuzichunguza au walau kutoa taarifa rasmi ya kiserikali kuzikanusha kama ni shutuma zisizo na mashiko.
Iwapo shutuma hizo zina ukweli, hata ikiwa ni nusu ya chembe ya ukweli, basi ilikuwa wajibu wake kuwachukulia hatua zifaazo wenye kuhusika. Katika hali hiyo mawaziri wa sheria na wa mambo ya ndani wangewajibika kujiuzulu pamoja na maofisa wa ngazi za juu wa magereza.
Waliotambulika kuwa ndio waliotesa wangefikishwa Mahakamani wakashtakiwa na kupewa adhabu inayostahiki, watapopatikana na hatia.
Pinda hakuchukuwa hatua zozote alizostahili achukuwe.Badala yake alikimbilia msituni kujibanza nyuma ya miti akijidai kwamba hakuwa akijuwa Sanya akisema nini.
Alisema alikuwa hajui Sanya anawazungumza kina nani seuze kujuwa iwapo wamo gerezani, wala hakujuwa wamekamatwa kwa kosa gani licha ya kwamba walishafikishwa kabla mahakamani zaidi ya mara moja.
Lenye kutisha zaidi ni kwamba hawa ni watu wanaoshtakiwa kwa makosa ya ugaidi, si kosa moja, ni makosa manne na Waziri Mkuu anasema hana habari nao. Tena katika kesi ya kwanza ya aina yake nchini.
Wala hakuwa akijuwajinsi mahabusi hao walivyoteswa.Na ikiwa hujui kitu ndio hujui, unakuwa huna dhambi.Huna lawama wala hulaumiki.Ikiwa Pinda ametumia mantiki hiyo basi ametumia mantiki finyu iliyopindika.
Ukweli wa mambo ni kwamba hatuwezi kumtoa lawamani Pinda kwani ni muhali kabisa ya kuwa hajui yaliyowafika hao mashekhe wa Uamsho.
Mwisho hivi majuzi tu Mei 11, Farid aliyaeleza Mahakama kwa ufasaha na uwazi namna walivyotendewa. Miongoni mwa aliyoyasema ni kwamba tukiwaacha wao 24 walioshtakiwa kwa kesi moja kwa jumla kuna Wazanzibari wasiopungua 50 walio katika magereza ya Bara wakishutumiwa kwa makosa ya ugaidi.
Farid alieleza jinsi wengi wao walivyochukuliwa majumbani mwao saa nane za usiku, wengine walivyovunjiwa milango yao na kusafirishwa kutoka Zanzibar kupelekwa Tanganyika, hatua ambayo, alisema, ni ya udhalilishaji kwa vile Zanzibar ina Mahakama yake Kuu yenye hadhi sawa kama Mahakama Kuu yaliyo Bara.
Aidha, Farid alisimulia namna walivyokuwa wakihojiwa “kishenzi, kikatili” walipofika Bara.
Alitoa mfano wa jinsi alivyokuwa akisailiwa mshtakiwa mwenzake Sheikh Msellem bin Ali, aliyemuelezea kuwa ni mtu mwenye kuheshimika, kiongozi wa Jumuiya ya Taasisi ya Kiislamu na mfasiri wa Qur’an Tukufu. Alisema kwamba Msellem alihojiwa akiwa uchi kama mnyama.
Aliongeza kwamba takriban wote walihojiwa namna hiyo. Kwa mujibu wa Farid, Msellem baadaye alihojiwa akiwa ametundikwa huku akifungwa pingu hali akiwa uchi.
Farid na mwenzake Salum Ali walimueleza Hakimu kwamba wenzao wanne wamegoma kula chakula na hali zao ni mbaya na ndio maana hata hawakudiriki kufika Mahakamani. Kati ya waliohudhuria walikuwepo waliokuwa wakichechemea kwa sababu ya kuteswa, walidai kina Farid.
Kiongozi huyo wa Uamsho aliongeza kudai kwamba kesi yao ni ya kisiasa kwa sababu, alisema, walitiwa nguvuni kwa vile wamekuwa wakidai Zanzibar irejeshwe heshima yake na kwamba pawepo usawa baina ya Zanzibar na Tanganyika.
Farid, aliyesema: “…hatuwezi kudhulumiwa haki yetu tukakaa kimya” alimwambia Hakimu kwamba yeye na wenzake wanahitaji Jaji Mkuu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri wa Katiba wa Zanzibar, waende gerezani kuonana nao.
Ni ajabu kuona kwamba yote hayo yakijiri Waziri Mkuu anasema kwamba yeye hajui chochote kuhusu kadhia hiyo.Lazima kuna kitu ambacho Pinda anakiogopa. Amegeuka nyayo isiyonyoka na ndio maana anakiogopa kiatu kilichopindika.

 

Chanzo: http://raiamwema.co.tz/waziri-mkuu-anaposema-hajui#sthash.4wAAOUj5.dpuf “Waziri Mkuu anaposema hajui”

 

 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.