Zipo sababu nyingi ambazo naamini chama changu nikipendacho cha Mapinduzi (CCM) kinapaswa kuzitazama na kuzitanguliza mbele kwa maslahi yake na nchi kwa ujumla.

Binafsi nautazama uraisi huu kama kitu kilichotukuka, hivyo si jambo la kuwacha wenye rekodi mbaya waliteke nyara kutokana na ukwasi wa kifedha au utashi wa nafsi zao tu.

Dk. Salim Ahmed Salim
Dk. Salim Ahmed Salim

Tumeona yanayoendelea hadi kufikia mahali baadhi ya wautamanio uraisi kupewa adhabu za kutoshiriki siasa kwa muda hadi waliporuhusiwa karibuni na vikao vya juu vya chama chetu!

Hapa ndipo yaibukapo masuali na khofu dhidi ya watu hao: vipi mtu makini ajiteuwe binafsi na kujikomba kwa michango mbalimbali ili watu wamuone wa maana!?

Na Ahmed Juma
Na Ahmed Juma

Hili mimi silikubali nalo asilani! Silikubali kwa vile naamini kizuri hujiuza chenyewe na kibaya kikajikomba nakujitembeza!

Hili ndilo lijidhihirishalo kwa wenye usongo na uraisi!

Hata hivyo, kulingana na mazingira machafu yenye kubebwa na uhalisia ndani ya CCM yetu, ipo haja na umuhimu mkubwa kurejea kwenye misingi ya chama chetu ambayo ni ukweli na uadilifu.

Tukubali kwamba hizi ni lulu ambazo CCM imezipoteza na sasa chama kimepoteza umaarufu wake!

CCM imegeuka shamba la bibi na sasa kila mchafu huingia humo kufanya apendavyo!

Kutokana na hali hii, ndipo haja ya kuwa na mtu makini msafi wa kusimama kwenye uraisi inapojitokeza.

Lipo pia suala la upande wa Zanzibar kulalamika juu ya uteuzi wa upeperushaji wa bendera hii ya uraisi. Suala linalolalamikiwa ni uteuzi utazamao upande mmoja na kuusahau mwingine. Kwamba Zanzibar haijapewa ipasavyo fursa ya kutowa raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndani ya CCM!

Huu ni ukweli usiopingika na ipo haja kuukubali. Tuukubali ukweli bila kujali nani atafurahi au atanuna!

Tumpe nafasi hii mwanadiplomasia gwiji duniani, Dk. Salim Ahmed Salim, ili aturudishe kwenye umakini tulikokudharau.

Huyu ni msafi na mwenye uwezo wa kukinusuru chama hiki kisiende kaburini. Huyu ana sifa na vigezo vyote kuweza kuongoza na kutukwamua tulipokwama! Huyu ni mzoefu kupita mwingine yeyote ndani ya CCM ya sasa!

Tumpe nafasi ili hadhi na heshima ya nchi irudi mahali pake. Kumuacha Dk. Salim, ni kuwapa UKAWA ushindi wa kimbunga na kuichimbia CCM kaburi kwa mikono yetu wenyewe!

Huo ni msimamo wangu na habari ndio hiyo!!!

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.