Zapata wiki mbili sasa tangu mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, kuelezea khofu yake ndani ya bunge la Bajeti linaloendelea Dodoma kuwa hakutakuwa na uchaguzi mkuu mwezi Oktoba mwaka huu kutokana na kile alichosema ni kukosekana matayarisho ya uchaguzi huo. Khofu ya Lissu ilijikita kwenye kuzingatia muda uliobakia kufikia tarehe ya uchaguzi na majukumu ambayo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) inapaswa kuwa imeshayetekeleza hadi muda huo inaolinganishwa na ukubwa wa Tanzania.

jinnAwali khofu hiyo ya Lissu ilishapigiwa mstari wa kukozeshwa na Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, ambaye alisema chama chake na muungano wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) walikuwa na taarifa zinazoonesha atiati ya kufanyika kwanza kwa kura ya maoni juu ya Katiba Mpya na kisha uchaguzi mkuu wa 2015 na kwamba kuna dalili za kuifanyia marekebisho katiba ya sasa ili Rais Jakaya Kikwete aendelee kuwapo madarakani.

Na Ali Mohammed
Na Ali Mohammed

Naye, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, akiwasilisha hotuba ya kambi yake hivi majuzi bungeni alisema pia “hakuna maandalizi yoyote yanayofanywa na serikali ambayo yanaashiria wazi kuwa Uchaguzi Mkuu utafanyika Oktoba mwaka huu“. Mbowe alisema ukweli huo umethibitishwa na NEC kwenye ukurasa wa 13 wa randama ya Tume hiyo unaosema: “Kwa upande wa maandalizi ya kura ya maoni na uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, Tume hatujapokea fedha hadi sasa.”

Mbowe alihoji ikiwa serikali haijaipatia NEC fedha kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi mkuu, inategemea miujiza gani kuwa ifikapo Oktoba uchaguzi huo utafanyika. “Ni lini zabuni zitatangazwa kwa ajili ya makandarasi mbalimbali ambao watasambaza vifaa kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu na tarehe ya kuwapata hao wazabuni ni lini?” alihoji, akionya kuwa wakati serikali ikishindwa kuipatia NEC fedha kwa ajili ya kufanya maandalizi ya uchaguzi ili ufanyike katika mazingira ya amani, haki na utulivu, imeamua kuwekeza na kujiandaa kupambana na wananchi wake. “Hii ni kutokana na ukweli kuwa tuna taarifa kuwa Serikali imeamua kuagiza zaidi ya magari 777 kwa ajili ya Jeshi la Polisi, kuanzia yale ya maji ya kuwasha, doria na shughuli za ukaguzi katika mwaka huu wa fedha”.

Hivyo ikitokea khofu ya Lissu ikathibiti kwa kutofanyika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2015, basi ni dhahiri kwamba hadithi ya Kibuyu cha Ajabu aliyowahi kuisimulia Rais Jakaya Kikwete iko katika muendelezo wake. Rais Kikwete aliitoa hadithi hiyo wakati wa ufunguzi rasmi wa Bunge Maalum la Katiba tarehe 21 Machi 2014 mjini Dodoma, ambayo inamuhusisha mtu aliyekuwa akitembea pembezoni mwa ufukwe, ndipo akakuta kibuyu kilichofungwa na alipokiokota na kukifungua likatoka jitu kubwa la kustaajabisha. Kumbe ni jini lililokuwa na njaa na lilipotaka kumla yule aliyeliokota. Jamaa akapiga akili ya haraka haraka aokoke, akaamua kukubali kuliwa lakini kwanza akaliambia jini kwamba angelitaka kuhakikisha kama kweli jini lote lile kubwa liliuwa limetoka ndani ya kibuyu hicho. Ndipo lile jini kwa kutong’amua ujanja wa mwanaadamu, likaonyesha jinsi lilivyoingia kwenye kibuyu, hapo hapo yule jamaa akakifunga na kukirembea baharini naye akanusurika kuliwa.

Kwa Mswahili kama mimi, tangu mwanzo sikupata tabu kuifahamu hadithi hii pale Rais Kikwete aliposimulia bungeni. Kwa wakati huo, taswira ya jini ilikuwa ni Rasimu ya Jaji Warioba yenye pendekezo la muungano wa serikali tatu, na yule jamaa kilikuwa ni Chama cha Mapinduzi (CCM) kinachoongozwa na Rais Kikwete. Hapo ilikuwa wazi kuwa Rais Kikwete alikuwa anawaambia wajumbe wa Bunge hilo la Katiba kutoka chama chake na wale wanaokishabikia chama hicho, kuwa Rasimu ya Warioba ilipaswa kusukumizwa baharini, maana ni jini ambalo lingeliweza kuimeza CCM nzima nzima. Kilichofuatia hapo ndicho ushahidi wa namna Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta, kuliongoza bunge hilo kwenye kukitupa kibuyu baharini na jini wake ndani.

La Sitta na Bunge lake la Katiba likaongezewa maana pale NEC ilipotangaza rasmi kwamba kura ya maoni imeahirishwa kwa muda usiojulikana na sasa yanayosemwa na akina Lipumba, Lissu na Mbowe yanatupa maana zaidi ya Kibuyu hiki cha Ajabu.

Sasa UKAWA inasema NEC haina uwezo wala fedha za kuendesha uchaguzi mkuu kufikia tarehe 25 Oktoba mwaka huu. NEC na serikali zinasema upo uwezo huo. UKAWA unasema Rais Kikwete anajipangia kuongeza muda wa ziada kwa sababu ya kushindikana kufanyika uchaguzi. Ikulu inasema hakuna mpango huo.

Uzoefu wa ukweli wa kile kinachosemwa na viongozi wa upinzani na uongo wa kile kinachosemwa na serikali unatupa majibu zaidi ya Kibuyu cha Ajabu cha Rais Kikwete. Wakati upinzani uliposema Bunge Maalum la Katiba haliwezi kupitisha katiba bila ya ushiriki wa UKAWA, Sitta akaliongoza bunge hilo kuipitisha kibabe, lakini wakati UKAWA waliposema kusingelikuwa na Katiba Mpya kwa kuwa kura ya maoni ya katiba hiyo isingelifanyika na serikali ikasema ingelikuwepo, ni UKAWA iliyoibuka kuwa mkweli zaidi na serikali ikawa imedanganya.

Upeo na uwezo mzuri wa kufikiri na kutathmini mambo ni sifa kubwa ya uongozi. Ule ujumbe kwenye hadithi ya Kibuyu cha Ajabu ya Rais Kikwete unaweza kuwa sasa unakwenda mbali zaidi ya pale pa kuwashajiisha tu wajumbe wa CCM kwenye Bunge la Katiba kuikataa Rasimu ya Warioba. Una pande nyengine mbili: upande mmoja ni kwa Rais Kikwete kusema kuwaambia Watanzania kuwa kuliko kuwajaribu UKAWA waliokwishawatoa kwenye kibuyu, bora wawafungie na kuwasukumiza baharini, na kuendelea na CCM yake yeye akiwa kiongozi wa chama na dola. Upande mwengine, ni ujumbe wa UKAWA kwa wananchi kwamba kulikubali jini lililotoka kwenye kibuyu cha CCM ni kukubali kuliwa na jini hilo, na busara ni kulifungia kwenye kibuyu chake na kulirejesha baharini lilikotoka.

Rais Kikwete akiwa kiongozi mkuu wa nchi na chama tawala ana haki ya kuwa na khofu ya wimbi la upinzani kuchukuwa dola kutokana makosa mengi ambayo chama chake yamekifanya na kushindwa kwake kuchukuwa hatua za kuyasahihisha makosa hayo. Pindipo uchaguzi ukafanyika na UKAWA, ambao wamekuwa imara licha ya figisufigisu zinazofanywa kuwadhofisha, wakashinda, hapa ndio ile khofu ya kuliwa na jini lililomo kwenye kibuyu inapopatikana. Ikiwa haukufanyika, ni sawa na kusema amefanikiwa kumrejesha jini katika chupa hivyo atakayemuokota tena na kumfungua ndiye atakayeliwa na jini aliyemo ndani ya Kibuyu cha Ajabu.

Imehaririwa na Mohammed Ghassani

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.