Misamiati hii mitatu iliyobeba anwani ya makala hii inastahiki kwanza kufafanuliwa kabla ya kuingia kwenye hoja yenyewe. Kwanza ni neno ujahili, ambalo katika maana yake ya kawaida linamaanisha ujinga, yaani hali ya kutokujuwa jambo au mambo fulani, lakini katika matumizi yake linamaanisha sio tu hali ya kutokujuwa bali pia ukaidi wa kutotaka kujuwa na au vitendo vya kujizuwia na kuwazuwia wengine wasijuwe. Kwenye historia, kuna nyakati ziliitwa “zama za ujahili” au “zama za giza”.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mizengo Pinda.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mizengo Pinda.

Pili ni neno upuuzi, ambalo katika maana yake ya kawaida ni hali ya kutokuwa na maana au jambo lisilofaa kutendwa ama kusemwa, lakini nalo kwenye matumizi yake husimama baina ya upumbavu na uwendawazimu kwa kuwakilisha jambo lisilokubalika kwa akili ya kawaida ya kibinaadamu. Ingawa kama alivyo mpumbavu na mwendawazimu kufanya mambo yasiyo maana, mpuuzi hufanya lisilo maana lakini mwenyewe akiwa na maana, akiwa dhamira maalum ya kuwapumbaza wale anaowafanyia au kuwapotosha. Upuuzi hufanywa na watu wenye akili zao, ilhali upumbavu na uwendawazimu hufanywa na wasiokuwa nazo. Ndio maana Waswahili hutumia hekima mbili tafauti katika kushughulika na makundi haya mawili. Kwa mpuuzi, hekima husema “mpuuzi mpuuze”, lakini kwa mpumbavu husema “pumbavu likipumbaa pumbaa nalo, likiingia msituni shika njia wende zako.”

Tatu ni msamiati wa uhalifishaji wa siasa, ambayo ni hali ya kuzifanya siasa za kawaida kuwa ni sawa na uhalifu na hivyo kuzichukulia na kuzihukumu kama uhalifu na anayezitenda siasa hizo kuwa naye ni muhalifu. Kinyume chake ni kuusiasisha uhalifu, ambapo uhalifu unaotendwa na wahusika huchukuliwa na wengine kuwa ni jambo la kisiasa tu na hivyo kuuhukumu kisiasa.

Tuje sasa kwenye kiini cha makala yenyewe, tukianza na ujahili wa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mizengo Kayanza Pinda, kwenye jibu lake la tarehe 21 Mei 2015 wakati wa kipindi cha masuala ya papo kwa papo bungeni kwa suala la Mbunge Muhammad Sanya wa jimbo la Mji Mkongwe, aliyetaka iundwe tume ya uchunguzi kwa tuhuma za kunyanyaswa viongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu wakiwa gerezani Tanzania Bara.

Ikiwa maana ya ujahili ni ujinga na ikiwa maana ya ujinga ni hali ya kutokujuwa, basi Waziri Mkuu Pinda alikiri kuwa yeye ni jahili katika hili, maana alisema hakuwa akijuwa ni akina nani waliokuwa wakiuliziwa na hata alikuwa hajuwi walikuwa wanazuiliwa gerezani kwa kosa gani na, kubwa zaidi, hajuwi ikiwa hata watu hao wameshawahi kufikishwa mahakamani.

Inawezekana kuwa waziri mkuu, ambaye ni mtendaji mkuu wa shughuli za kila siku za taifa lenye watu milioni 48, hajuwi kuwa nchi yake inaendesha kesi ya kwanza ya ugaidi inayowajumuisha watu wengi kwa wakati mmoja ndani ya kipindi cha miezi 24 sasa.

Inawezekana pia Waziri Mkuu Pinda hajawahi kupatiwa maelezo kutoka taasisi yoyote kati ya zile anazozisimamia na wala hajawahi kusoma, kusikia wala kuona popote jambo hilo likiripotiwa kwenye vyombo zaidi ya 30 vya habari katika nchi yake na au chombo chochote cha nje ya nchi yake. Ikiwa mawili hayo yanawezekana na ndivyo yalivyokuwa, basi kwa hakika huo utakuwa ni ujahili hasa kwa maana yake ya kihistoria, yaani Waziri Mkuu Pinda atakuwa anaishi kwenye “zama za kiza”.

Lakini, endapo kiongozi huyu mkuu wa shughuli za siku kwa siku za serikali amefikishiwa taarifa kutoka kwa taasisi anazoziongoza, na endapo amejuwa kutoka chombo chochote cha habari, au kwa namna yoyote akafahamu kuwa nchi yake inaendesha kesi ya kwanza ya ugaidi katika zama hizi za “vita dhidi ya ugaidi” na yeye akawa amesema tafauti, basi Waziri Mkuu Pinda atakuwa anaingia kwenye kigawe chengine cha maana ya neno “ujahili” – nacho ni kiwango cha matumizi ya neno hilo kwa maana ya ukaidi wa kutotaka kujuwa na vitendo vya kujizuwia au kuwazuwia wengine wasijuwe.

Sifa za mtu jahili nimezitaja kwenye shairi langu la tarehe 11 Julai 2014, ambalo unaweza kulisikiza hapa, kuwa ni kuona kila jambo na kujifanya hakuona, kusikia kila jambo na kujifanya hakusikia, na kujuwa kila jambo na akajifanya hakujuwa.

Tumuache Waziri Mkuu Pinda hapo.

Tuugeukie sasa upuuzi wa Naibu Mkurugenzi wa Upepelezi wa Makosa ya Jinai katika Jeshi la Polisi Zanzibar, Kamishna Msaidizi Salum Msangi, ambaye siku moja baada ya Waziri Mkuu Pinda kuyasema hayo bungeni, yeye aliwaita waandishi wa habari kwenye chumba cha mikutano Makao Makuu ya Polisi kuwatangazia wananchi kukamatwa kwa vijana wawili, Said Ali Abdullah mwenye umri wa miaka 26 mkaazi wa Kiwani, Pemba, na Hussein Mageni Hussein mwene umri wa miaka 27 mkaazi wa Pangawe, Unguja, kwa makosa ya kuwatukana Rais Ali Mohamed Shein na makamu wake wa pili, Balozi Seif Ali Iddi, wakitumia mitandao ya simu.

Upuuzi wa Kamishna Msaidizi Msangi upo kwenye ngazi nyingi, na hapa nitazitaja tatu: kwanza, kwenye kutupambaza sote, akitaka tuamini kuwa kilichofanywa na jeshi lake kilikuwa kitu sahihi kwa kuwa tu kinachoshukiwa kufanywa na vijana hao hakikuwa si sahihi. Kwa mfano, kijana Said ambaye anatajwa kwengineko kuwa ni kiongozi wa Jumuiya ya Vijana ya Chama cha Wananchi (CUF) wilaya ya Mkoani, Pemba, amekamatwa kwa kosa la kumtukana Balozi Seif kwa kumtaka asiende kisiwani Pemba kufanya mikutano ya Chama cha Mapinduzi (CCM). Lakini kwenye vidio ambayo ilisambazwa kwenye mitandao ya kijamii na ambayo ndiyo ushahidi pekee wa Kamishna Msaidizi Msangi, Said anasema pia kuwa mjumbe wa kamati kuu ya CCM, Balozi Seif, asijaribu kuwazuia wanachama wa CUF kufanya mikutano kwenye jimbo la Kitope lililo Kaskazini B kisiwani Unguja, kwa kuwa wao CUF hawamzuii yeye kufanya mikutano Pemba, ambako CCM haina jimbo hata moja. Kwa hivyo, Msangi anatupumbaza kwa kutuambia nusu ukweli na nusu uongo. Hasemi kuwa kauli hiyo ni majibizano ya kisiasa kati ya vyama vya siasa.

Pili, upuuzi unakuja pale jeshi la polisi linapotangaza kuwachukulia hatua vijana hawa wa CUF, lakini likiwaacha vijana na viongozi wa CCM ambao wanaowatukana viongozi wakuu wa CUF kwa matusi makubwa kuliko hayo yaliyoripotiwa kusemwa na Said. Hapa upuuzi unamaanisha kutenda jambo lisilo maana, kwa sababu hatua hii inayochukuliwa na taasisi yenye jukumu la kusimamia usalama wa aria na mali zao imekosa maana yoyote ya kiusalama kwa kuchukuliwa kwake inachukuliwa kibaguzi. Inakuwaje kumtukana Katibu Mkuu wa CUF na Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad, kwa mfano, kuwe si jambo la kuchukuliwa hatua za kiusalama na polisi, lakini lichukuliwe hatua inapotokezea aliyetukanwa na mjumbe wa kamati kuu ya CCM na Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Iddi?

Alipoulizwa kuhusiana na hilo, Msangi alisema polisi hawajawahi kuwakamata wale wanaowatukana viongozi wa CUF kwa kuwa wenyewe viongozi wa CUF hawajawahi kuwashitakia makosa hayo, akitaka tuamini kuwa Rais Shein na Balozi Seif walikwenda kufungua jalada la malalamiko makao makuu ya polisi, Madema. Huu ni upuuzi uliopitiliza.

Tatu ni upuuzi kwa kuwa umesemwa kipuuzi. Kwa mfano, kwenye maelezo yake Kamishna Msaidizi Msangi anawataja vijana hao kuwa ni wahalifu na anaelezea kushangazwa kwake kuwa kuna mawakili walikwenda kutaka kusimamia mahojiano yao, akiwemo mwakilishi wa jimbo la Kiwani kwa tiketi ya CUF, jimbo ambalo ndilo analotokea kijana Said. Ikiwa maadili ya kipolisi na sheria za mwenendo wa mashitaka anazijuwa na si mpuuzi, basi Kamishna Msaidizi huyu anajuwa tafauti baina ya neno “mtuhumiwa” na “mhalifu” kama anavyojuwa pia haki ya kila mtuhumiwa kuwa na wakili. Mtuhumiwa anabakia kuwa na haki zote za utuhumiwa na si mhalifu hadi hapo mahakama iamuwe hivyo.

Sasa tuhitimishe kwa kuyahusisha yote mawili, yaani ujahili wa Pinda na upuuzi wa Msangi, na hali ya kuzigeuza siasa kwenye nchi yetu kuwa ni uhalifu – kuihalifisha siasa. Kanuni zinatuzuwia kuzungumzia kesi inayoendelea mahakamani dhidi ya viongozi wa Uamsho, lakini hazituzuwii kuzungumzia siasa zilizomo na zinazoizunguka kesi hiyo. Kwa mfano, si mara moja wala mbili, viongozi wakuu wa CCM na wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kusikikana wakisema kuwa yanayowapata viongozi wa Uamsho yana mkono wao, huku wakiapa kuwa madhila kama hayo yatamfika Mzanzibari mwengine yeyote ambaye atafanya walichokifanya Uamsho.

Uamsho walifanya nini? Kwa muda wa mwaka mmoja mtawaliya kuelekea kukusanywa maoni ya Katiba Mpya, viongozi wa Uamsho walipita sehemu zote Unguja na Pemba kuwahamasisha Wazanzibari kuupinga mfumo uliopo wa Muungano na kupigania mamlaka kamili ya Zanzibar ndani ya Muungano. Hiyo ilikuwa ni siasa asilimia 100. Wito wao wa kisiasa uliopitishiwa jukwaa la kidini ukapokewa na tangu hapo hadi leo, Wazanzibari walio wengi wamesalia na msimamo huo. Kwa hivyo, ni wazi kuwa ni siasa ndiyo iliyowafikisha viongozi wa Uamsho walipofikishwa na wala si uhalifu.

Lakini serikali za CCM zimeamua kuzifanya siasa hizo za kuupinga mfumo wa Muungano na kuipigania Zanzibar kwa Mzanzibari kuwa ni uhalifu. Imewatendea hivyo takribani viongozi na Wazanzibari wote waliowahi kufanya hivyo huko nyuma na inaendelea hivyo hivi leo. Tangu zama za Rais Aboud Jumbe Mwinyi hadi kwa Waziri Mansoor Yussuf Himidi, hakuna Mzanzibari aliyewachwa salama “asihalifishwe” kwa kuitetea Zanzibar na kupinga mfumo wa Muungano. Ajabu ni kuwa Tanzania Bara haiwahalifishi wanasiasa na viongozi wake wanaoupinga mfumo wa Muungano. Huwavumilia na, katika baadhi ya mifano, hata kuwatunza.

Sasa kama CCM na serikali zake imeshajiamulia kuwa kila mpinga muundo wa Muungano ni mhalifu na itamtendea hivyo, inapaswa kuongeza bajeti ya magereza yake kwa kuwa idadi ya wapinzani wa mfumo huu wa Muungano wanazidi kuongezeka kila uchao, na hakuna siku waliowahi kupungua.

Bahati mbaya ni kuwa wakati CCM inazihalifisha siasa, huwa pia inausiasisha uhalifu, kwa maana ya kuyachukulia matendo ya kihalifu kuwa ni ya kisiasa na hivyo kuyahukumu kisiasa. Ndivyo ambavyo inayashughulikia masuala ya kashfa za wizi wa mabilioni ya fedha za umma. Wizi ni uhalifu. Ufisadi ni uhalifu. Lakini kwa kuwa unafanywa na wanasiasa wa CCM, huhisabiwa kuwa ni siasa. Ndio maana kuna jitihada za kuwasafisha wahusika wa kashfa ya Tegeta Escrow, kwa mfano, kwa kuwa uhalifu wao unatakiwa uangaliwe kuwa ni siasa tu.

Hakuna taifa lililosonga mbele duniani kwa kuzihalifisha siasa na kuusiasisha uhalifu.

2 thoughts on “Ujahili wa Pinda, upuuzi wa Msangi na uhalifishaji wa siasa”

 1. Nihakika siasa kwa Zanzibar imefanywa kuwa uhalifu na uhalali wa kuwa mhalifu uwe cuf au unahitaji Zanzibar yako kama yaliyomtokea Othman masoud, kosa lake ni kukataa katiba inayooendekezwa wakati serikali ya suk kutokuwa na msimamo ila msimamo ulikuwa wa ccm, uhalifu wa othman kutounga mkono chama

  Kamishna msangi na jeshi la polisi wanashangaza kwA mengi mana kwenye mtandao wamepatA wahalifu ila waliopigwa wamekosa kumjua mhalifu, kuna kila dakili ya jeshi la polisi hasimu wake mkubwa kwa Zanzibar ni cuf na wakapinga muungano

  Naungana nawe ni upuuzi kusema Dr shein kafungua jalada la kesi, Dr shein hafati upuuzi wala hana muda wa kusikiliza wapuunzi na hivyo kwamwe hatafungua kesi ya kipuuzi na Kitoto na kijinga namna hiyo
  Polisi duniani huwsa kama kioo cha dola na kuwakilisha image ya taifa, au kwa sababu Zanzibar inaonekanwa sio taifa ndo mana mtazamo huo haupo? Imefika wakati polic waache ukereketwa mana ccm munayoikingia kifua imeshakataliwa Zanzibar, kuwakamata cuf c kuondoa tatizo, mana namezoweAa kila chaguzi kuingia jela
  lakini nirudi kenye hoja waliokamatiwa ya matusi, balozi seif iddi ni mwanasiasa hata cheo chake ni cha kisiasa hawezi epuka majibizano ya kisiasa na wanasiasa, katibu wa juvcuf ni mwanasiasa anahaki ya kutekeleza siasa na wanasiasa, na lamko lake nimetokea kwa tukio hivyo alijibu tukio tena la kisiasa lisilo aina yoyote na matusi, neno usije kwangu c tusi kama ninajibishana na mtu nae alienambia nisiende kwake

  Kama kamishna msangi anatafuta wanaotoa matusi kwa viongozi basi bila ya kumhoji wala kutakiwa kujibu borafya silima angekuwa wa mwanzo na sadifa, mana tuseme borafia ni mtu msima sawa lakini sadifa anatowa natusi ya nguoni dhidi ya makamo wa kwanza wa rais mtu anaemzaa tuseme maalim c kiongozi sawa lakini anamzaa na polic wapo leo wanakwenda kumkamata mtu mtandaoni wanamuacha wa hadharani!

  Kwa mfumo huu kuna haja ya kupanua magereza kama ya segerea au kilimani mana ukweli dhidi ya uonevu wowote hatutakaa kimya tutasema tu.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.