HEBU turudi nyuma kidogo ili kuipa mashiko hii hoja ya anguko la asilimia 20 linalokikabili Chama cha Mapinduzi (CCM) kwenye uchaguzi wa mkuu mwaka huu. Kwa kutumia takwimu zilizotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), mwaka 1995 Benjamin Mkapa alishinda urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa 61%, ambazo zilikuwa ndogo mno kwa wakati ule kwa sababu kadhaa.

Rais Jakaya Kikwete aliingia madarakani kwa mara ya kwanza mwaka 2005 kwa ushindi wa asilimia 80.28, akarejea kwenye muhula wa pili kwa ushindi wa asilimia 62.83 akiwa amepoteza nguvu za awali na sasa anaiwacha nchi huku CCM ikihofiwa kupoteza asilimia nyengine 20.
Rais Jakaya Kikwete aliingia madarakani kwa mara ya kwanza mwaka 2005 kwa ushindi wa asilimia 80.28, akarejea kwenye muhula wa pili kwa ushindi wa asilimia 62.83 akiwa amepoteza nguvu za awali na sasa anaiwacha nchi huku CCM ikihofiwa kupoteza asilimia nyengine 20.

Moja, CCM ilikuwa iko madarakani tangu uhuru (kwanza kama TANU kwa Bara na ASP kwa Zanzibar, kisha kama CCM yenyewe) kama chama pekee na ikifuata siasa za “Chama kushika hatamu”, ambapo kila taasisi ya umma na kiraia ilikuwa inatii mawazo ya mtu mmoja tu. Pili, wakati ule CCM ilikuwa bado inaye huyo “mtu mmoja” ambaye mawazo na fikra zake ndizo zilizodumishwa na wengine wote, yaani Mwalimu Julius Nyerere, ambaye alitanga nchi nzima kumpigia debe Mkapa. Tatu, chama hiki kikongwe kilikuwa kikifaidi  ugeni wa Watanzania kwenye mfumo wa vyama vingi na ujinga wao kwa siasa za mageuzi. Nne, wakati huo, CCM ilikuwa chama pekee kilichokuwa kimejisambaza kutoka kileleni hadi mashinani – mijini mpaka vijijini – na ndicho kilichojulikana zaidi. Tano, hadi mwaka 1995, mfumo wa mawasiliano na upashanaji habari haukuwa umesambaa nchi nzima. Kwa mfano, ni mijini pekee ndiko kulikokuwa na simu za mikononi, televisheni na redio iliyoweza kufika mijini na vijijini ilikuwa moja, huku mtandao wa intaneti ukiwa kama haupo kabisa.

Na Ali Mohammed
Na Ali Mohammed

Lakini hata katika chaguzi nyengine mbili baada ya hapo, bado CCM iliendelea kupata ushindi mkubwa dhidi ya wapinzani, licha ya kwamba vyama vya upinzani sasa vilikuwa vinajuilikiana zaidi. Kwa mfano, katika uchaguzi wa mwaka 2000, Mkapa aliongeza asilimia 10 zaidi kwenye ushindi wake kwa kupata asilimia 71.74, na katika mwaka 2005, mrithi wake, Jakaya Kikwete, aliingia madarakani katika muhula wake wa kwanza kwa asilimia nyengine kumi zaidi ya , akiwa na 80.28%.

Kwa maslahi ya mjadala huu, tukubaliane kwamba katika mara zote hizo, NEC ilifanya uadilifu na hivyo iliowatangaza na ilivyotangaza ndivyo wapigakura walivyokuwa kweli wameamua kwa haki na uwazi. Ushindi wa mwaka 2005 wa Kikwete unaweza kuwa uthibitisho kuwa mtangulizi wake alifanya mambo mazuri sana kama kujenga barabara za lami, madarasa, kukua kwa uchumi, kuongezeka kwa pato la taifa na kadhalika. Inawezekana hayo ndiyo yaliyoifanya mizani ya mema ipae juu na kuididimiza mezani ya maovu aliyoyafanya na kuzijenga imani za Watanzania waitoe CCM kutoka asilimia 61.82 mwaka 1995 na kuifikisha asilimia 71.74 mwaka 2000 na 80.28 mwaka 2005.

Ikiwa tunakubaliana kuwa CCM iliendelea kuongeza asilimia 10 kwenye kila uchaguzi kuanzia mwaka 1995 hadi 2005 kwa sababu ya sifa za serikali ya chama hicho kutenda mema kwa Watanzania, basi inaonekana kuwa mambo hayo mema yalioijengea sifa CCM yalianza kukoma na utawala wa Rais Kikwete ulioanza 2005. Hapo ghafla mambo yakageuka na sifa mbaya na chafu za CCM zikaanza kuibuka moja baada ya nyengine na zikaanza kidogo kidogo kuwachukiza Watanzania. Kashfa ya Richmond na Dowans ikawang’oa serikali baadhi ya watendaji wake wakuu, mfumuko wa bei ukapanda maradufu, mauaji ya albino, uchunaji ngozi na ukataji viungo yakakithiri, bila kutaja kashfa ya EPA ilivyoijeruhi vibaya serikali ya Rais Kikwete.

Lakini kubwa kuliko yote ni kuwa umma wa Watanzania ulikuwa sasa unajiinuwa kutoka usingizi mzito wa miaka mingi. Mzimu wa Mwalimu Nyerere haukuwepo tena, kasi ya mawasiliano na upashanaji habari ilikuwa imeongezeka, vyama vya upinzani vilijichawanya kiasi kushuka chini vikiondokana na siasa za mijini pekee. Kwa ujumla, hayo ndiyo yaliyoifanya CCM kuingia katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 na kuanguka kwa asilimia takribani asilimia 20, kwa kupata asilimia 62 tu kama zile za miaka 15 nyuma alizozipata Mkapa kwenye muhula wake wa kwanza.

Sasa, unapochukuwa yaliyojiri kutoka mwaka 2005 hadi 2010 na ambayo yaliipelekea CCM kupoteza asilimia 20 ya ushindi wake ndani ya kipindi cha miaka mitano tu, na ukayalinganisha na mambo kama hayo yaliyojiri kuanzia mwaka 2010 hadi 2015, basi ni rahisi kuhitimisha kwa kusema kuwa CCM hii hii na kwa sababu ya yale yale, itapoteza asilimia nyengine 20. Yaani kutoka ushindi wa asilimia 62 kwenye ngazi ya uraisi mwaka 2010, CCM inaweza sana kushuka hadi asilimia 42 ya kura.

Kwa nini? Ndani ya kipindi hicho yameibuka mambo yaliyowanyima raha na imani wananchi juu kwa utawala wa CCM. Moja ni sakata la Escrow ambalo limeimomonyoa serikali ya Kikwete hadi mifupa yake. Kushindwa kwake kuwawajibisha ipaswavyo viongozi wa kichama na serikali na badala yake kupigania kuwasafisha kunatoa mchango mkubwa katika kuzipotezea CCM hizo asilimia 20.

 

Pia CCM kupitia serikali yake imekosa mbinu za kusuluhisha matatizo na migogoro itokeapo. Kwa mfano, mzozo wa wafugaji na wakulima maeneo kadhaa ya Tanzania Bara. Vile vile, suala la mauaji ya albino ambayo bado yanaendelea na hadi sasa hakuna njia sahihi hasa ya kuwanusuru viumbe wenzetu hawa. Hivi karibuni imetangazwa na vyombo vya habari, kwamba hata CCM wenyewe wanahusika na kadhia hiyo, pale mwenyekiti wake wa Marampaka alipokutwa na fuvu la albino pamoja na viungo vingine.

Anguko hio la asilimia 20 kwa CCM linaweza pia kuchangiwa na Operesheni Tokomeza Ujangili iliyosababisha mateso, ukatili, udhalilishwaji, upigaji na hatimaye vifo vya wananchi na aibu kubwa kwa taifa letu. Nako huko pia, CCM na serikali zake inaelekea kuwasafisha wahusika na kuwawajibisha wasiohusika kwa sababu ya kulindana na kutaka ushindi wa uchaguzi.

Kudharauliwa kwa maoni ya wananchi kupitia mchakato wa katiba nako pia ni kichocheo cha kuifanya CCM kudondosha asilimia 20 zaidi ya ilizokuwa nazo kwenye uchaguzi wa 2010. Wananchi walijenga imani na Tume ya Jaji Mstaafu Warioba, walipoteza muda wao kwa kuacha shughuli zao za kimaisha, walijitokeza kwa wingi kutekeleza haki yao ya kikatiba, wakatoa maoni yao, lakini baadaye kupitia CCM ikaupindisha mchakato mzima, maoni ya raia yakapuuzwa, ubabe ukatumika, waliodai haki hiyo ya raia wakabezwa, kukejeliwa na hadi kutukanwa ndani ya chombo kitukufu cha kutunga sheria Bungeni Dodoma, na kodi za wanyonge zikateketea bure na sasa hakuna Katiba Mpya iliyopatikana. Watanzania watakuwa wapumbavu wasipoiadhibu CCM kwa kupunguza angalau asilimia 20 kwenye ushindi wake.

Isitoshe, kuna pia matumizi ya nguvu yanayofanywa na vyombo vya dola. Watanzania wa Bara na Zanzibar wameona jinsi vyombo vya dola vilivyotumia nguvu nyingi dhidi ya watetezi wao, kama ilivyo kwa viongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu visiwani Zanzibar, ambao kwa mwaka wa pili sasa wamewekwa ndani, kosa lao kubwa ikiwa kutetea hadhi na heshima ya Zanzibar kwenye Muungano.

Juu ya yote, kuna kuzidi kupanda bei bidhaa muhimu kwa maisha na kushuka kwa thamani ya shilingi, ambako kunamfanya Mtanzania wa kawaida azidi kuwa masikini, huku deni la serikali likipaa kama limefungwa mashine ya kuongeza mwendo. Kubwa zaidi ni kuwa kasi ya mawasiliano na upashanaji habari hivi sasa inaifanya CCM iwe tupu kwa aibu zake kuwekwa hadharani kila uchao. Vijana wengi ambao ndio wapiga kura wanaichukia CCM kutokana na kuisoma tabia na matendo yake mitandaoni na kusikia kwenye vyombo vya habari.

Sasa, kwa kuwa CCM haikusoma makosa yake na kujirekebisha kama vile ilivyoonesha kwenye uchaguzi wa vitongoji na vijiji, basi wajitayarishe kuporomoka tena kwa asilimia 20 nyengine kutoka 61 ambazo Rais Kikwete aliingilia katika muhula wake wa pili. Kwa sasa, CCM wajitayarishe kupokea asilimia si zaidi 40 kutoka kwa Watanzania na kuwapa nafasi UKAWA kuvuna asilimia zaidi ya 50% na kufanya iunde dola na kuiongoza Tanzania kwa muhula wa miaka mitano ijayo.

Hayo ndio malipo ya matendo ya CCM isiyosoma wala isiyosikia.

Imehaririwa na Mohammed Ghassani

2 thoughts on “Hili anguko la 20% la CCM Oktoba 2015”

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.