WAKATI Rais wa Awamu ya Tano Visiwani, Dk. Salmin Amour Juma alipozuiwa bila kupenda kugombea nafasi hiyo kwa awamu ya tatu na kwa kuvunja Katiba mwaka 2000,matarajio yake ya mbele kwa yale aliyokusudia yaliyeyuka ghafla, akaamua kujiteulia mrithi kwa ushawishi ili kuweza kuyaendeleza akiwa pembeni.

Dk. Mohammed Gharib Bilal
Dk. Mohammed Gharib Bilal

Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) upande wa Zanzibar, ilipoketi Ofisi Kuu Kisiwandui kupendekeza [kwa Halmashauri Kuu ya Taifa [NEC] jina la mgombea Urais wa Zanzibar mwaka 2000; ilikuwa nderemo na vifijo kwenye viwanja vya ofisi hiyo, pale mmoja wa wagombea, Dk. Mohamed Gharib Bilal, alipotajwa mshindi kwa kuzoa kura 44 dhidi ya washindani wake wawili; Amani Abeid Karume, aliyepata kura tisa, na Abdulsalami Issa Khatibu, aliyepata kura chache zaidi.
Kwa matokeo hayo, Dk. Salmin Amour alishusha pumzi kwa furaha kwamba, angalau sasa Urais na Uenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ungekwenda kwa mtu sahihi na mwenye kustahili kuwaongoza Wazanzibar kama alivyotaka iwe.
Awali, Salmin alionekana kukataa kwa kiburi kuachia ngazi licha ya vipindi vyake viwili vya kutawala kikatiba kuelekea ukingoni, na alikuwa katika harakati za mwisho kubadili Katiba ya Zanzibar aweze kutawala kwa awamu ya tatu kama asingenyukwa nyundo nzito ya CCM na kukoma hima kudhihaki na kujaribu kuinajisi Katiba ya wananchi na demokrasia.
Kwa kufurahia na kushangilia ushindi huo wa Bilal hadi gego la mwisho, Salmin na CCM Zanzibar walisahau kwamba uamuzi na uteuzi wao haukuwa wa mwisho; kulikuwa na tanuri la Halmashauri Kuu ya Taifa [NEC] ya CCM mbele mjini Dodoma, yenye uamuzi wa mwisho.
Na ndivyo ilivyokuwa, kwamba majina yote matatu yaliwasilishwa NEC Taifa, ambako kampeni nzito nzito za nyuma ya pazia na “kuchafuana” zikafanyika, na mwisho wa siku, Karume akaibuka kidedea kwa mshangao na ghadhabu kubwa kwa wana-CCM Zanzibar. Hapo Bilal akawa ametoswa kwenye kina kirefu cha maji ya Visiwa vya Zanzibar,kwa teke lenye nguvu kutoka Dodoma.
Matokeo hayo sio tu kwamba yaliwashangaza na kuwakera Wazanzibari, bali pia yalizua tetemeko la kisiasa kwa viongozi wa CCM Visiwani ambao walidai kuwa uteuzi huo wa NEC haukukubalika, lakini wakaamua kuumia kimya kimya.
Kwa uteuzi huo wa NEC, Karume ndiye alikuwa mgombea pekee wa urais Zanzibar kwa CCM, katika uchaguzi wa pili wa vyama vingi nchini; huku upinzani mkubwa ukitoka kwa mgombea wa Chama cha Wananchi – CUF, Maalim Seif Sharif Hamad.

Karume ambwaga Komandoo
Karume alishinda na kusimikwa kuwa Rais wa Awamu ya Sita wa Zanzibar, kuchukua nafasi ya Amour, maarufu Visiwani kama “Komandoo”.
Hata hivyo, ushindi wa Karume ndani ya NEC na kwenye Uchaguzi Mkuu haukuwa rahisi kama ilivyotarajiwa, kwani kambi za “Karume” na “Bilal” ziliendelea kusigana chini kwa chini Visiwani na Bara.
Na hili halikuwa siri ndani ya CCM kiasi kwamba, aliyekuwa Katibu Mkuu wawakati huo, Phillip Mangula, alilazimika kutoa maelekezo na miongozo kwa Makatibu wa Mikoa wa Chama ili “kumwezesha” Karume, akisema: “Na huu ndio mwanzo wa vita ngumu itakayoanza hivi punde kuweza kumuuza Karume”, akimaanisha kwamba, mgombea huyo alikuwa na kibarua kigumu kuweza kupita.
Ushindi wa Karume haukuweza kuondoa mihemko na vifua kujaa miongoni mwa Viongozi wa CCM Zanzibar kutokana na “mauaji” ya Dodoma. Chama kililiona hilo, ambapo miaka mitatu baadaye kiliitisha Semina ya Viongozi wa CCM Zanzibar, kuweka mambo sawa ili kuondoa ukinzani uliokuwa umeanza kukomaza mizizi kati ya CCM Zanzibar na CCM Bara; na kati ya kambi ya Karume na kambi ya Salmin/Bilal Visiwani.
Semina hiyo, iliyofanyika Kisiwandui, Januari 13, 2003 chini ya Uenyekiti wa Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Benjamin William Mkapa, ilitawaliwa na malumbano, vijembe na mipasho juu ya “hadhi” ya Zanzibar, uteuzi wa Dodoma ukirejewa mara kwa mara kama kielelezo.
Mjumbe mmoja [jina tunalo] hakuficha hasira yake kwa yaliyofanyika Dodoma, kwa hisia kali alisema: “Zanzibar ni mahali CCM itakapozikwa pamoja na sera zake; Zanzibar ilizika Chama cha Afro-Shirazi [ASP] mwaka 1977 kwa kuunda CCM, na sasa ni zamu ya CCM kuzikwa Zanzibar isije ikawazika Wazanzibari badala yake”.
Kiongozi huyo, mwenye elimu nzuri, alidai kuwa “hali tete ya sasa inahitaji kuzaliwa kwa chama cha tatu chenye nguvu” [mbali na CUF na CCM] ili kuvunja uhasama wa vyama hivyo, unaowapumbaza wananchi, na Wazanzibari wako tayari kwa hilo”.
Juhudi za Mkapa kujaribu kumdhibiti msemaji huyo azungumzie mambo ya “msingi” tu hazikufua dafu, badala yake zilimpandisha mori na ghadhabu na kusema: “CCM inaporomoka, CUF kina nafasi nzuri, lakini tatizo la CUF ni kwamba wanaendesha siasa za kitoto….”.
Akaendelea, akasema: “Hakuna Mzanzibari asiyejua kwamba Karume [Amani] hakuwa chaguo lao; alichaguliwa kiharamu na kwa njia za kimizengwe ambapo Waasia watatu mashuhuri nchini – wawili kutoka Bara na mmoja kutoka Visiwani, walimwezesha kuvikwa taji bila uhalali wala kustahili; na bado CCM kinawadanganya wananchi kwamba kinapiga vita hongo na rushwa wakati ni kinyume chake”.
Msomi mwingine [jina tunalo] alitaka kumpa somo Karume kuhusiana na kauli yake ya awali dhidi ya Bilal, aliyetahadharisha Wazanzibari juu ya hatari ya kukumbatia utandawazi kichwa kichwa katika uchumi wa nchi, na akataka Wazanzibari waelimishwe vya kutosha. Kwa kauli hiyo ya Bilal, Karume alimpuuza huku akimponda kwa kusema: “Sayansi na Teknolojia haina umuhimu na si lolote”.
Msomi huyo, huku akishambulia kambi ya Karume alisema: “Zanzibar inahitaji kiongozi makini na mwenye upeo mkubwa wa mambo. Inasikitisha kwa kikundi cha viongozi vijana [aliwataja Jakaya Kikwete, Abdulrahman Kinana na Edward Lowassa] kulishambulia kundi la wapinzani wa Karume [kwenye NEC Dodoma],wakiongozwa na Anna Abdallah na Zakiah Meghji mwaka 2000, lakini pamoja na ujabari wa kikundi hicho,wa kujifanya kumtetea Karume, leo wamemtelekeza kabisa”.
Karume akashtuka na kugeuka mtu wa kujiteteana kujihami; lakini kiongozi mmoja akamkata kauli kwa kumwambia, “Ukweli huuma daima”.
Bilal ni msomi mbobevu wa Sayansi na Teknolojia katika “Fizikia ya Nyuklia” na mwenye kutambulika kimataifa, elimu ambayo Karume aliiona kuwa “si lolote”.
Kisha mjumbe huyo akaendelea, akasema: “Kuna viongozi wazuri tu wa CCM wamepuuzwa, wanabaguliwa na hawatakiwi ndani ya chama chenyewe; lakini wamebakia kwa sababu tu hawana mahali pa kwenda……… watu hawa wanahitaji chama cha tatu chenye nguvu, kama alivyotabiri mwanamapinduzi Abdulrahman Babu; wako njia panda; wamekatishwa tamaa na mwenendo wa CUF na wakati huohuo hawatakiwi CCM”.
Msemaji huyo akatahadharisha kwa kusema: “CCM Zanzibar na CUF Zanzibar zinasafiri ndani ya mtumbwi mmoja bila kujua waendako; Zanzibar inauzwa wakati vikundi hivi viwili, kwa ujinga wao, vikiendelea kukashifiana”.
Malumbano haya yakiendelea, kiongozi mmoja wa kambi ya Karume alimlaumu Salmin kwa kusababisha yote haya, hasa pale alipotaka kupindua Katiba kwa lengo la kujiwezesha mwenyewe kubakia madarakani kwa awamu ya tatu na kwa kutaka kujiteulia mrithi wake,Bilal; lakini mbinu zote mbili zikashindwa.
Maneno ya kiongozi huyo, yalitoa picha kamili kwa nini Dakta Bilal alitoswa huko Dodoma licha ya ushindi wa Kisiwandui. Dhambi kuu kwake ilikuwa ni kule kupendelewa” na “Komandoo” Dk. Salmin Amour.
Chama cha Tatu Zanzibar?
Mifarakano ndani ya CCM Zanzibar ilifanya utabiri wa Profesa Abdulrahman Babu utimie: Chama cha SAFINA kiliundwa kuleta suluhisho la uhasama wa CUF na CCM Visiwani ili Zanzibar isonge mbele katika nyanja chanya za maisha, badala ya kuendeleza uhasama na malumbano ya kihistoria.
SAFINA kama kilivyo CUF, kiliundwa na wanachama wa CCM waliokata “tamaa”, hawa wakidai mambo mengi, yakiwamo; Zanzibar kurejeshewa uhuru wake uliopotea kwa kuhodhiwa na Tanganyika; Zanzibar kurejeshewa madaraka ya kuchagua viongozi wake kwa uhuru na kwa mujibu wa Katiba yao, wakidai kuwa CCM ilikuwa na ajenda ya siri dhidi ya Zanzibar. Walidai pia Muundo wa Muungano urejewe upya ili kuwa na Shirikisho lenye Serikali tatu.
Kwa mujibu wa misahafu ya dini za Kiislamu na Kikristo, SAFINA ni jina la meli kubwa iliyotengenezwa na Nabii Nuhu kwa maelekezo ya Mungu kwamba, angetuma mvua kubwa kuangamiza viumbe vyote kwa gharika na kwamba, mvua hiyo ikianza, Nuhu na familia yake pamoja na viumbe vingine vya uteuzi wake, waingie ndani na kuelea hadi gharika litakapokwisha, wakati huo wanadamu na viumbe ambavyo hawakuingia kwenye SAFINA watakuwa wameangamia.
Chama cha SAFINA hakikuweza kupata usajili kwa sababu ya kushindwa kupata wafuasi kwa idadi inayotakiwa Tanzania Bara. Tatizo la SAFINA ni kwamba, kilijielekeza kwa siasa za Kizanzibari zaidi kuliko za Kitaifa. Mmoja wa waumini wake wakubwa, Profesa Abdulrahman Babu alilazimika kujiunga na NCCR-Mageuzi na kuwa mgombea mwenza wa Augustine Lyatonga Mrema katika Uchaguzi Mkuu wa 2000, lakini kura kwao hazikutosha.
Kwa kipindi chote cha mitafaruku na malumbano haya, Bilal alikuwa kimya ametulia tuli, pengine akihangaikia uhai na namna ya kuelea juu ya gharika. Kwa Wazanzibari, na hata kwa viongozi wa siasa za kitaifa Bara, ukimya wake ulitafsiriwa kwa makosa au kwa usahihi kwamba ulificha “kishindo” kwa siasa za Zanzibar na kwa Muungano.
Mchawi mpe mtoto alee?
Kwa ujumla, utawala wa Amour haukwenda vyema na Serikali ya Muungano, hasa ilipohusu “hadhi ya Zanzibar na Wazanzibari” ndani ya Muungano kiasi kwamba wakati mmoja aliwakoromea viongozi wa Muungano waache mchezo wa “kutikisa kiberiti”, kwa maana ya kumjaribu kuona kama yuko kamili ndani na kwa “nchi” ya Zanzibar.
Kwa Bilal, bila shaka, uswahiba wake na Amour ndio uliomponza kwa nafasi ya Urais Zanzibar kwa vigogo wa chama Bara na vigogo wa Muungano kuhofia kuibuka kwa Komandoo mwingine kuwakoromea waache “kutikisa kiberiti” kwa mambo ya Zanzibar.
Msomi huyu wa mambo ya nyuklia alikuwa na nafasi nyingine nzuri ya kugombea Urais wa Zanzibar mwaka 2010, lakini huenda kwa “hofu” ileile ya mwaka 2000 hakupewa mwanya huo, badala yake akapigwa tafu Dk. Ali Mohamed Shein, na yeye Bilal akasogezwa kwa “mzazi” kushika nafasi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano kuona kama alikuwa bado anamiliki uchawi wa kuambukizwa pamoja na ujasiri wa kutosha kuweza kuuwa hadharani “mtoto” aliyekabidhiwa kulea.
Na kwa kuwa uswahiba wa Bilal na Salmin ndio ulimponza mwaka 2000 akakosa Urais Zanzibar licha ya kukubalika kwake kwa CCM Zanzibar, lakini baadaye akaibukia kwenye nafasi kubwa zaidi ya Makamu wa Rais wa Muungano; na kwa kuwa hatujaelezwa popote kwamba [Dakta Bilal] amewahi ”kujisafisha” dhidi ya fikra za Komandoo Salmin ili asihusishwe na “uchawi” wa kuambukizwa; Je, kwa kutoswa na kuibuka hai na kwa madaraka makubwa zaidi kwenye Serikali ya Muungano kunaashiria nini, kama si kile kinachofahamika kama “Mchawi mpeni alee Mtoto”?.
Pili, Makamu wa Rais wa Muungano, kama alivyokuwa Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi kwa Rais Mwalimu Julius Kambarage Nyerere; mara nyingi ana nafasi kubwa ya kurithi nafasi hiyo muhimu ya kidola; lakini kwa historia na matukio haya kama tulivyoona hapo juu; Je, urithi huo uko wazi pia kwa Dk. Bilal,na kwa Awamu ipi kati ya nyingi zijazo?

TANBIHI: Makala ya Joseph Mihangwa kwenye gazeti la Raia Mwema la tarehe 20 Mei 2015

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.