
Tumezisikia tuhuma kutoka kwa Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, wiki mbili zilizopita juu ya uendeshaji wa zoezi zima la uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa Oktoba 2015.
Nimesema “tuhuma” na sio “malalamiko” kwa kuwa pana tafauti kubwa sana kati ya mawili hayo. Mwenye tuhuma ana hoja na anawasilisha kesi yenye ushahidi madhubuti, ilhali mwenye malalamiko analialia akitaka uombezi, ambao hata kama ana haki nao, anakuwa hana hoja nao. Kwa ufupi, tuhuma ni hoja iliyowasilishwa katika mfumo wa mashitaka.

Ikiwa imebaki miezi chini ya mitano, Maalim Seif alikituhumu Chama Cha Mapinduzi na serikali yake, kupitia mamlaka zake zikiwemo zile za ngazi za chini kabisa, yaani masheha, hadi za juu kabisa, yaani wizara, na vyombo vya dola kama Jeshi la Wananchi (JWTZ), mamlaka inayohusika na kutoa vitambulisho vya Mzanzibari (Zan IDs) na hata Tume ya Uchaguzi yenyewe (ZEC). Mbele ya waandishi wa habari wa kitaifa na kimataifa aliziweka tuhuma zote mezani, kila moja ikiwa na rundo la ushahidi.

Kwa mfano, CUF kupitia kwa Katibu wake huyo Mkuu inawatuhumu masheha kuwapatia uthibitisho wa ukaazi kwa watu ambao si wakaazi halali wa shehia zao, akataja majina na akaonesha na picha za wahusika. Pia Maalim Seif aliituhumu ZEC kwa ‘kulichafua’ Daftari la Kudumu la Wapiga Kura (DKWK) kwa maovu kadhaa yenye ushahidi kwa kila moja wao. Miongoni mwao ni:
• kuweka wapigakura wenye umri mdogo
• kuandikisha mpigakura mmoja zaidi ya mara moja
• kuandikisha wapigakura waliokufa
• kupandikiza wapigakura wasiokuwa wakaazi katika maeneo waliyojiandikisha
• kutumia taarifa zisizo sahihi za wapigakura kama vile majina na picha
• kuzidisha idadi ya wapigakura kuliko ile ya vipande vya kura
Makamu huyo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar alielekeza pia tuhuma kwa Idara ya Usajiliwa Wazanzibari ambayo ndiyo hutoa Vitambulisho vya Mzanzibari (Zan-IDs), kwa wakuu wa mikoa na wilaya na, la kusikitisha zaidi, hata kwa vikosi vyetu viitwayo “vya ulinzi na usalama”.
Katika hili la vikosi, Maalim Seif alisema bila kumumunya maneno kwamba kambi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania iliyopo Chukwani, magharibi mwa kisiwa cha Unguja, imeandikisha mamia ya vijana wakiwemo wengi ambao si Wazanzibari na kuwapatia vitambulisho vya Mzanzibari (ZAN IDs) kwa ajili ya kuja kuandikishwa kama wapiga kura. Vijana hawa walikuwa wakipelekwa katika kambi hiyo kwa magari maalum kwa kipindi cha mwezi mmoja uliopita na kuanza wiki iliyopita wameitwa na kuanza kupewa vitambulisho hivyo haramu.
Tuhuma moja wapo ambayo iliwasilishwa kwenye mkutano huo na wanahabari ni ile ya kuandikishwa vijana wanaofikia 20,000 na kupewa Zan-IDs na mamlaka husika ambao wamepangwa kuja kuandikishwakama wapiga kura. Wengi kati ya vijana hao wamehamishwa kutoka nje ya majimbo yao. Kwa mfano, kuna vijana 700 waliochukuliwa katika maeneo mbali mbali ya jimbo la Uzini na kusajiliwa katika jimbo la Bububu.
Tuhuma hizi za CUF ni ishara ya chama hicho kutokuwa na imani na jinsi uchaguzi unavyoandaliwa kabla ya kufika katika kilele chake. Ni kusema kwamba CUF na Maalim Seif hawana imani na serikali juu ya mamlaka zake ambazo imezikabidhi dhamana ya kusimamia na kuendesha uchaguzi, licha ya CUF kuwa mshirika mdogo kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa visiwani Zanzibar.
Hadi sasa, tumemsikia Mkurugenzi wa ZEC, Salum Kassim, akijaribu kujibu tuhuma hizi ingawa hakuvunja hoja ya msingi kwenye tuhuma zenyewe, nayo ni “ZEC kuuchafua uchaguzi”, hoja ambayo kwenye nchi zenye utawala bora inatosha kabisa kuwasweka wahusima jela kwa miongo kadhaa.
Kwa upande wa CCM, ilijibu kwa nayo kutoa shutuma hizo hizo za kutoziamini mamlaka zinazosimamia uchaguzi, isipokuwa tu ilishindwa kusarifu namna ya kuzitoa kwa urefu na badala yake walitumia njia ya mkato kuziwasilisha. Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, aliuambia mkutano wa hadhara uliofanyika Magogoni wiki iliyopita kwamba wao CCM wanajuwa hata CUF nao wametoa vijana Pemba ili kuongezea wapigakura katika majimbo ya Maogogoni, Bububu, Nungwi, Mtoni na maeneo mengine ya kisiwa cha Unguja.
CCM ndiye mshirika mkuu kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa visiwani Zanzibar. Hii maana yake ni kuwa endapo vyama vyote viwili vinavyounda serikali hiyo, yaani CCM na CUF, havina imani na mamlaka zilizowekwa kusimamia uchaguzi wa mwaka 2015, basi lazima kuna tatizo ambalo kutatuliwa kwake kunahitaji mamlaka za juu zaidi au kando ya zile zilizopo sasa.
Kwa hivyo, ujumbe maalum kwa viongozi wakuu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, Rais Ali Mohammed Shein aliyetangazwa kupewa asilimia 50 na wapigakura mwaka 2010 na Maalim Seif aliyetangazwa kupewa asilimia 49 kwenye uchaguzi huo, ni kwamba taasisi zenu kuu hamuziamini na hivyo lazima musake suluhu mahala pengine kusudi muinusuru hii nchi na majanga yanayoweza kutokezea. Ombeni msaada ulimwenguni kwa watu wenye uweledi wa kuendesha uchaguzi kwa uhuru na haki ili watuvuushe salama na kutuepusha na mabalaa.