Akihutubia mkutano wa hadhara wa chama chake katika viwanja vya Kwa-Mabata, jimbo la Magogoni, kando kidogo ya Mjini Unguja wiki iliyopita, Naibu Katibu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, alinukuliwa akisema kuwa “Ushindi (katika uchaguzi) hautegemei wingi wa mashabiki; ushindi unategemea wingi wa kura ndani ya visanduku vya kupigia kura”.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, akihutubia mkutano wa hadhara Magogoni.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, akihutubia mkutano wa hadhara Magogoni.

Kauli hii inamaanisha kuwa chama kitakachofanikiwa kuandikisha wapigakura wengi na kuhakikisha kuwa wanakipigia chama chao hicho siku ya uchaguzi, ndicho kitakachoshinda. Kwa hivyo, ni rukhsa kuandikisha Wamasai, Watanganyika, Mamluki, Wafu na kadhalika; ilimradi tu chama husika kipate wapigakura wengi watakaokiunga mkono siku ya uchaguzi.

Na Muhammad Yussuf
Na Muhammad Yussuf

Sasa hebu tupige mahesabu rahisi na ya haraka haraka: Tujaaliye kuwa kati ya wapigakura wote walioandikishwa katika daftari la kudumu hadi hivi sasa, CCM inaungwa mkono na asilimia 50 ya wapiga kura wote; na CUF inaungwa mkono na asilimia 50 ya wapiga kura wote. Ili CCM ishinde, inahitaji kupata angalau asilimia 50 na kidogo zaidi. Tujaaliye kuwa CCM itafanikiwa kuandikisha wapigakura wapya na kufikia jumla ya asilimia 55 mpaka 60 ya wapigakura wote, baada ya zoezi la kuandikisha wapigakura wapya litakapomalizika na huku ikitegemea kuwa asilimia 50 ya wapigakura wote iliyonayo kibindoni hivi sasa wataendelea kukipigia kura chama cha CCM siku ya uchaguzi.

Na hapa ndipo wasiwasi wangu unapojitokeza. Kwa kadri hali ya kisiasa ilivyo hivi sasa nchini kufuatia jinsi ambavyo Mchakato mzima wa Katiba ulivyokwenda na hasa zaidi kutokana na misimamo ya wajumbe wa CCM katika Bunge Maalum la Katiba, kuna kila sababu (na ushahidi wa kutosha) ya kuamini kuwa zaidi ya asilimia 60 ya wapigakura wanaoiunga mkono CCM hivi sasa watachagua kukipigia kura chama cha CUF au wataamua kususia upigaji kura na kubakia majumbani mwao siku ya kupiga kura. Idadi ndogo sana ya wafuasi na wapenzi wa CCM katika mikutano ya hadhara inayoandaliwa na chama hicho tawala ni dalili tosha kuwa ushawishi wa CCM katika siasa za Zanzibar unazidi kupungua siku hadi siku.

Kwa vyovyote vile iwavyo, mbinu ya kuandikisha wapigakura haramu haitosaidia chochote katika kuipatia CCM ushindi katika uchaguzi ujao kwa sababu mara hii wananchi wengi watakaopiga kura watalazimika kufanya maamuzi makubwa na mazito katika kuchagua viongozi baina ya wale wenye misimamo wa kulinda na kutetea maslahi mapana ya Zanzibar; na wale wenye misimamo ya kutaka kuendeleza maslahi yao binafsi yenye lengo la madhumuni ya kushibisha matumbo yao.

Mbinu pekee ambayo itaweza kuisaidia CCM, sio kushinda, lakini kupata angalau theluthi moja ya viti katika Bunge na Baraza la Wawakilishi, ni haja ya kuvutia hisia, nyoyo na imani za wananchi; mbinu ambayo CUF inaonekana kuitekeleza kwa mafanikio makubwa.

Huu ni ushauri wangu wa bure kwa CCM.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.