Msomi mtafiti yoyote alie makini hawezi kuipuuza Sakura. Ile ndiyo “Sierra Maestra” ya kuingia Zanzibar na “Granma” yake ndivyo vile vyombo vilivyokuwa chini ya ulinzi wa bahari ya dola huru ya Tanganyika.

Majibu ya ndugu yangu mpenzi Muhammad Yussuf nimeyapitia ila hoja yake yenye kusema marehemu Hanga hakuwa kinara wa Mapinduzi ya Zanzibar kwa sababu tu hakuwa na wadhifa wowote ndani ya ASP si hoja ya kutolewa na – MashaAllah – mtu mzito kama yeye.

Waliokaa kutoka kushoto: Marehemu Abdullah Kassim Hanga na Abeid Karume,
Waliokaa kutoka kushoto: Marehemu Abdullah Kassim Hanga na Abeid Karume,

Hanga aliekuwa si chochote, si lolote, vyereje aje kufanywa Waziri Mkuu kwa siku mbili au tatu baada ya Mapinduzi ya 64, halafu aangushwe na kipenzi chake marehemu Mzee Abeid Amani Karume? Ateremshwe kutoka Uwaziri Mkuu Hanga hadi Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, na kichupa cha udi hichohicho kikavushwa bahari na kurudishwa Tanganyika kwenye mzimu ule ule ambao mwanzoni ulimtabiria uongozi wa juu kabisa Zanzibar!

Sikatai kuwa mwanzoni Karume alimpenda sana Hanga ila mapenzi yake yaligeuka shubiri baada ya Karume kuutambuwa ukweli kuwa kama Hanga na Kambona waliweza kupinduwa Serikali basi yeye Karume hatokuwa salama. Kilichomsaidia Mzee Karume ulikuwa umaarufu mkubwa aliokuwa nao kutokana na wafuasi wa ASP na ukaribu wake na Kamati ya 14, vitu ambavyo Hanga na wenzake walishindwa kuvitathmini ipasavyo.

Na Harith Ghassany
Na Harith Ghassany

Wachambuzi makini huwa wanapendelea kusimama juu ya ushahidi usiotetereka na wale wenye kuamua katika kukiamini wakipendacho basi huna ushahidi wa kuwapa wakuamini. Suala la nani kinara wa Mapinduzi ya Zanzibar ni suala ambalo limejitika katika ufakhari na kujiadhimisha unaotokana na ulwa wa kisiasa na wa kidunia. Ila suala hilo hilo linaweza likachukuwa sura nyengine iwapo litaangaliwa kwa jicho la ubinaadamu zaidi lenye kuongozwa na hisia kuwa wazee wetu walikuwa na nia njema lakini walifika mahala fulani na walipoteza njia/dira.

Bado sijakutana na kiongozi au mfuasi mzuri wa ZNP, ASP, au UMMA, ambaye amekubali kukiri hadharani kuwa chama au viongozi wa chama chake walifanya makosa ambayo ndiyo yaliosababisha na kuifanya roho ya Zanzibar na Wazanzibari kukosa utulivu kwa nusu karne nzima. Hakuna hata mmoja na kama yupo basi atazungumza pembeni au ndani ya mtungi wa kichwa chake na hapo pia ni pahala pazuri pa kuwepo binaadamu ambaye pia ni Mzanzibari.

Nafikiri bado tatizo letu kubwa Wazanzibari ni kule kutokubali kwetu kuwa mabara yote mawili, la Afrika na la Arabuni, yote mawili ni mabara yetu kidamu na kiutamaduni – si kiutawala. Zanzibar ya tarehe 10 Disemba 1963 haikuwa na mahusiano yoyote na Oman na wala hapakuwa na ujumbe kutoka Maskati/Omani ulioalikwa kuhudhuria sherehe za Uhuru wa Zanzibar. Tanganyika ilipeleka ujumbe wake kwenye sherehe za Uhuru wa Zanzibar huku Sakura ikijiandaa kuivamia Serikali Huru ya Zanzibar ambayo ilifanya makosa ya kiusalama na ya kiulinzi na ndio sababu kubwa iliosababisha Uhuru wa Zanzibar kwenda na maji.

Ilipofika tarehe 14 Julai 1964, Balozi wa Kiingereza Tanganyika alipeleka kwao salamu kuhusu kambi za Msumbiji za Megame, Kisarawe na Mewala, na kumalizia kwa kusema kuwa mtazamo wa Serikali ya Tanganyika juu ya kuziweka kambi za ukombozi katika ardhi yake huenda ilitokana na ushindi wa mapinduzi ya Zanzibar ambayo yalipangwa Tanganyika. Sasa Tanganyika haijapatapo kukiri mahala popote pale kuwa Mapinduzi ya Zanzibar yalipikwa Tanganyika na kupakuliwa Zanzibar kwa sababu kwa kulikubali tendo hilo Tanganyika itakuwa imekubali kosa la jinai ya kimataifa na itakuwa imehusika na maafa yote yaliotendekeza Zanzibar kwa miaka 50 iliopita. Hapo sasa ni pakubwa sana kuliko Hanga, Karume, Babu, Kamati ya 14, na kadhalika, na kadhalika….

Na la muhimu zaidi kuliko yote si nani wa kuhukumiwa kwa sababu kazi ya kuhukumu si yetu bali ni ya Mwenyewe Mwenye Enzi Mungu ila tu…Suala la Mapinduzi ya Zanzibar lina wenyewe, lina vichwa na lina mikono yake. Vichwa Zanzibar vilikuwepo, na mikono pia, ila vichwa na mikono ya Dola iliosimama kuiangusha Dola ya Zanzibar ilikuwa ni ya Dola ya Tanganyika. Hilo halikataliki na mwenye kulikataa basi na ajiulize kwa makini kwanini Tanganyika haitaki kuiwachia Zanzibar? Kwa sababu Mapinduzi na Muungano, vyote viwili ni wakfu wao Tanganyika ambao wameiwachia Zanzibar wautumie mpaka Zanzibar itakaporudi kwao na kuwa Nchi Moja na Tanganyika.

Majini sugu ya ukabila, ya Uwarabu na ya Uafrika, ya utwana na ubwana, hayapungiki ila lazima uyapate na mapema na kabla hayakubaleghe! Marahemu Hanga na Karume, Ali Muhsin na Babu walikuwa na mazuri yao ila waligubikwa na mengi na kubwa lao lilikuwa ni kujiweka karibu sana na dola nyengine. Hanga na Tanganyika ilioipinduwa Zanzibar. Karume na Tanganyika ya kumlinda. Ali Muhsin na Masri (Egypt), na Babu na China. Na wote kati ya hao walijuta na kupoteza maisha yao yote baada ya 1964 katika kupigania kuirudisha Zanzibar walioipoteza kwa mikono yao wenyewe, na kati ya hao roho za maelfu ya Wazanzibari pamoja na Hanga na mlezi na mpenzi wake marehemu Mzee Karume walipoteza roho zao.

Ama kweli. Kumbe haya majini mwalimu wao yuko Kipumbwi na Sakura! Tena majini haya yana hila. Hawataki chano kengine ila kitoke Tanganyika kwani huko ndiko aliko yule mbuzi wa kafara (Zanzibar) aliekuwa hataki kufa na yule chatu (Tanganyika) wanasubiri hirizi (Katiba) ya kuuendeleza au kuimaliza migogoro isiokwisha.

Sakura na Kipumbwi ni sehemu ya historia na zimeshapita ila darasa zake bado ziko na sisi na katika chaguzi zote za Zanzibar. Marehemu Ali Muhsin aliupenda Uhuru wa Zanzibar na aliupata. Marehemu Hanga aliitamani Jamhuri na aliipata kupitia Jamhuri ya Tanganyika. Marehemu Karume aliitaka Zanzibar Huru ya Ali Muhsin lakini ndani ya Jamhuri lakini hakuiwahi. Babu aliitaka Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, aliipata lakini ya siku mia tu!

Miaka 51 baada ya kuupoteza Uhuru wa Zanzibar na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, Wazanzibari tumerudi pale pale penye mfundo: penye Uchaguzi Mkuu na Zanzibar Kwanza!

InshaAllah tutaipata iwapo hatutoudharau mzimu wa Sakura.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.