Katika Toleo la 405 la Gazeti la Raia Mwema la tarehe 13 Mei 2015, Mwandishi Mohamed Said, katika makala yake yenye kichwa cha maneno “Yaliyotokea katika kifo cha Abdulla Kassim Hanga”, kwa ufasaha mkubwa ameandika hivi: “Kuwa Hanga ndiye aliyekuwa kinara wa Mapinduzi ya Zanzibar hili si jambo lenye utata tena. Ikiwa hivyo ndivyo Hanga hatoweza kuutua mzigo wa roho zilizopotea katika mapinduzi hayo. Ikiwa Hanga atalaumiwa kwa vifo vya maelfu ya Wazanzibari nani alaumiwe kwa mauti yaliomfika Hanga tena kwa kuuliwa kikatili kwani hapana neno zaidi ya hilo linaloweza kutosheleza kuelezea jinsi Hanga alivyouliwa”.

Picha hii iliyochukuliwa tarehe 16 Januari 1968 inamuonesha Mwalimu Julius Nyerere akihutubia mkutano wa kumuumbua Abdullah Kassim Hanga (aliyekaa baina ya maaskari wawili) na hiyo inaaminika kuwa siku ya mwisho Hanga kuonekana hadharani.
Picha hii iliyochukuliwa tarehe 16 Januari 1968 inamuonesha Mwalimu Julius Nyerere akihutubia mkutano wa kumuumbua Abdullah Kassim Hanga (aliyekaa baina ya maaskari wawili) na hiyo inaaminika kuwa siku ya mwisho Hanga kuonekana hadharani.

Kusema kweli, kauli hii inayodai kuwa Abdulla Kassim Hanga alikuwa kinara wa mapinduzi si sahihi na haina ukweli wowote. Si sahihi kwa sababu Hanga hajapata kushika wadhifa wowote ule katika Afro-Shirazi, (hata uenyekiti wa Tawi la ASP), seuze kuwa “Kinara wa Mapinduzi”. Ukweli wa mambo ni kuwa Hanga hakupanga wala hakushiriki katika mapinduzi ya Zanzibar. Aliteuliwa kuwa Makamu wa Rais baada ya mapinduzi ya 1964 kutokana na mapenzi aliyokuwanayo Mzee Abeid Amani Karume kwake. Karume alimuona Hanga kama mtoto wake binafsi; alisaidia sana, kwa hali na mali, kumpeleka masomoni USSR na Chicago, USA, kwa masomo ya juu baada ya kuhitimu mafunzo ya ualimu katika chuo cha TTC pale Beit el Ras, Unguja.

Na Muhammad Yussuf
Na Muhammad Yussuf

Kwa hivyo, kama ilivyokuwa kwa akina Othman Sharif, Abdulaziz Kassim Twala, Aboud Jumbe, Idris Abdul Wakil na wasomi wengine ambao walipewa nyadhifa mbali mbali katika serikali na baraza la kwanza la mapinduzi, Hanga hakuhusika kwa namna yoyote ile na vifo vya Wazanzibari wakati wa/na baada ya mapinduzi ya Zanzibar.

Kwa kweli, inahuzunisha sana kutambua kuwa Hanga ni mmoja miongoni mwa wahanga wengi wa mapinduzi ya Zanzibar ambaye amedhulumiwa roho yake kwa kuuawa kikatili kama walivyodhulumiwa akina Othman Sharif na Wazanzibari wengine wengi wakati wa/na baada ya mapinduzi. Mimi binafsi nilimjua Hanga kwa karibu sana kwa sababu kaka yake wa mama mmoja, Ali Hassan Ngwenge, alimuoa mama yangu mkubwa, Ashura bt. Haji Dau. (Mama yangu mzazi akiitwa Talha Haji Dau). Hanga hakuwa na ubavu wala ujasiri wa kumuua hata nzi, seuze binaadamu yoyote.

Kwa mnsaba huo, hapana shaka yoyote ile kuwa, siku moja, historia itamkumbuka Hanga, Othman Sharif, Abdulaziz Twala, Mdungi Ussi, Jaha Ubwa, Khamis Masoud, Aboud Nadhif, Idrisaa Majura na wengineo, kwa jinsi na namna ambayo wanavyostahiki kukumbukwa.

Allah azilaze roho zao mahala pema Peponi – Amin.

One thought on “Hanga hakuhusika na mauaji ya 1964”

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.