Bweka jibwa koko bweka, kubweka ndiyo kaziyo
‘Kinguruma ‘tapasuka, mataya na matumboyo
Kunguruma kwa hakika, ni kazi ya simba hiyo
Wewe jibwa ni kubweka!

Wewe jibwa ni kubweka, huwezi kuliko hayo
Kubwa utayatapika, uyale matapishiyo
Waache waloumbika, masimba wangurumao
Wewe jibwa njia shika!

Wewe jibwa njia shika, na ufyate mkiao
Bweka ukinung’unika, na hiyo ndiyo hadhiyo
Masimba yakiinuka, wewe jibwa wende mbio
Wende mbio ukibweka!

Bint Makadara
19 Mei 2015
Zanzibar

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.