Hivi majuzi ulifanyika uchaguzi mkuu katika Muungano wa Ufalme (United Kingdom) tunaoufahamu zaidi sisi kwa jina la Uingereza, ambao ulishuhudia ushindi wa kishindo wa vyama viwili vya Wahafidhina (Conservatives) na cha Utaifa wa Uskochi (Scottish National Party) kwa kifupi SNP. Wahafidhina, ambao katika uchaguzi uliopita walilazimika kuungana na Wademokrati wa Kiliberali (Liberal Democrats) kuunda serikali ya mseto, mara hii wameweza kuzoa jumla ya viti 331, ambavyo vimewawezesha kuunda serikali ya peke yao. Amma Chama cha Utaifa wa Uskochi ambacho katika uchaguzi uliopita kiliambulia viti sita tu vya eneo hilo katika bunge la Uingereza, mara hii kimesomba viti 56 kati ya viti vyote 59.

First Minister of Scotland and Scottish National Party leader Nicola Sturgeon, center, celebrates with the results for her party at the count of Glasgow constituencies for the general election in Glasgow, Scotland, Friday, May 8, 2015. The Conservative Party fared much better than expected in Britain's parliamentary election, with an exit poll and early returns suggesting that Prime Minister David Cameron would remain in his office at 10 Downing Street. The opposition Labour Party led by Ed Miliband took a beating, according to the exit poll, much of it due to the rise of the separatist Scottish National Party.  (AP Photo/Scott Heppell)
Waziri Kiongozi wa Scottland na kiongozi wa chama cha Scottish National Party,  Nicola Sturgeon (katikati), akishangilia ushindi mkubwa wa chama chake kwenye uchaguzi wa tarehe 8 Mei 2015, ambapo SNP ilitwaa viti 56 kati ya 59 vya ubunge katika Scottland. (Picha ya AP/Scott Heppell)

Kwa wenzetu hawa, ushindi wa vyama katika chaguzi huchangiwa na mvuto wa ilani na sera zao wanazotangaza kwa wapiga kura wakati wa kampeni. Miongoni mwa sera, na tena ya ahadi aliyotoa kiongozi wa Chama cha Wahafidhina, ambaye ni Waziri Mkuu wa sasa wa Uingereza David Cameron ni kwamba endapo chama chake kitapewa ridhaa kamili na wapiga kura kwa kupata ushindi mkubwa wa kuiwezesha kuunda serikali ya pake yake, moja kati ya yatakayofanywa na serikali ya Wahafidhina ni kuitisha Kura ya Maoni ya kuwauliza Waingereza wenyewe kama wanataka nchi yao iendelee kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya (EU) au ijitoe katika jumuiya hiyo. Cameron alitangaza uamuzi huo mwaka 2013 na kuahidi kuitisha kura hiyo ya maoni mwaka 2017. Kwa upande wa chama cha SNP, kama jina lake linavyojionyesha, hiki ni chama kinachopigania Uskochi kuwa taifa huru na lenye mamlaka yake kamili na kujiondoa kwenye Muungano wa Ufalme wa Uingereza Kubwa (Great Britain) ambao imekuwemo ndani yake tangu mwaka 1707 yaani kwa zaidi ya karne tatu sasa.

Katika wakati huu ambapo Watanzania, yaani Watanganyika na Wazanzibari, wanajiandaa na uchaguzi mkuu wa Oktoba 2015, ambao wengi wanauchukulia kuwa ni uchaguzi muhimu zaidi tangu ulipoanzishwa mfumo wa vyama vingi, suala la hatima ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar linaonekana kuwa nafasi muhimu zaidi katika kuamua hatima ya uchaguzi huo, hasa kwa upande wa Zanzibar. Na hii ni kutokana na misimamo inayokinzana ya sera za vyama viwili vikuu vya siasa nchini au visiwani humo (kutegemea na mtazamo wako kama Zanzibar ni nchi, visiwa, sehemu….), yaani Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF). Wakati CCM inataka muungano wa Tanganyika na Zanzibar uendelee kuwa wa serikali mbili (na yumkini kuelekea moja) , unaoendelea kuifanya Tanganyika nchi kamili kwa kutumia jina la Tanzania na Zanzibar kuendelea kukasimiwa mamlaka ya mambo yake ya ndani tu, CUF inataka Zanzibar irejeshewe mamlaka yake kamili iliyokuwa nayo kabla ya kuungana na Tanganyika mwaka 1964 na kuundwa Jamhuri ya Tanganyika na Zanzibar, iliyokuja badilishwa jina baadaye na kuitwa Tanzania.
Haya yote yametokana na suala la Muungano kutawala kwenye mchakato, kuanzia wa utoaji maoni hadi utungaji wa rasimu ya Katiba mpya ya Tanzania, iitwayo Katiba Inayopendekezwa, japokuwa wakati alipozindua mchakato huo, Rais wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete aliweka mwiko wa kutojadiliwa au kutohojiwa Muungano, na kujaribu kuliwekea vizuizi na pingamizi mbalimbali suala hilo.

Utiaji saini wa hati za Makubaliano ya Muungano. Abeid Karume wa Zanzibar (kulia), Julius Nyerere wa Tanganyika (kushoto).
Utiaji saini wa hati za Makubaliano ya Muungano. Abeid Karume wa Zanzibar (kulia), Julius Nyerere wa Tanganyika (kushoto).
Madhumuni ya kuyaleta hapa mawili haya, ya Uingereza na Uskochi na ya Tanganyika na Zanzibar ni kujaribu kusafisha kiwingu cha upotoshaji kinachotandazwa na baadhi ya viongozi, makada na wanachama waandamizi wa CCM wanaojaribu kuwadanganya wananchi wa kawaida hasa wa Zanzibar kwa kuwaeleza kwamba muungano, ndilo jambo linalopiganiwa na mataifa yote katika dunia ya leo, na kwa hivyo ni ukosefu wa nadhari kwa Watanzania kufikiria kupunguza nguvu ya mgandanisho uliopo baina ya Tanganyika na Zanzibar katika muungano wa serikali mbili kwa kutaka kuanzisha ule wa serikali tatu au hata wa Mkataba. Miongoni mwa makada wa CCM niliobahatika kuwasikia zaidi ya mara moja akipigia upatu dhana hii kupitia televisheni ya ZBC na katika mahojiano na vyombo vya habari ni Balozi Ali Abeid Amani Karume, ambaye kwa kutumia hadhi yake ya uzoefu katika uga wa kidiplomasia na uhusiano wa kimataifa amekuwa akijaribu kuonyesha kuwa ili kupata maendeleo, mataifa mbalimbali duniani, yanafikiria kukaribiana zaidi kiushirikiano badala ya kutengana. Na hii ni kutokana na hofu kwamba hatima ya muungano wa serikali tatu au wa Mkataba ni ATI kuvunjika muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Anachopaswa kuelewa Balozi Ali Karume na wengine wote wenye mtazamo kama wake – ikiwa unatokana na uzalendo au ghilba za kutaka kuwazubaisha Wazanzibari wa kawaida – ni kwamba si MUUNGANO wala si UTENGANO wa kutaka kujitawala, ni kitu kizuri au kibaya mutlaki au kwa nafsi yake. Uzuri na ubaya wa kila moja kati ya mawili hayo unatokana na MATOKEO yaani tija na maslaha yanayopatikana kwa kuungana au kutengana pande mbili au zaidi husika. Huo ndio muhatasari wa maneno. Lakini kwa ufafanuzi zaidi ni kuwa, iwe ni katika mahusiano ya mtu na mtu, kikundi cha watu, jamii au nchi na nchi, msingi wa kuungana na kushirikiana unazingatia ridhaa ya kweli na maslahi ya kila upande. Sote tunajua kuwa wakati madhila ya mume yanapomfika kooni, mke hudai talaka ili angalau abaki kuwa binadamu mwenye heshima na utu wake halisi, hata kama ni katika maisha ya kujikimu kwa dhiki katika hali ya ujane! Methali ya Kiswahili imesibu iliposema “Umoja ni Nguvu na Utengano ni Udhaifu”, lakini tusipotoshe ukweli wa methali hii, kwani umoja uliokusudiwa hapa ni ule ambao tija na matokeo yake, ni kwa pande zote mbili kufaidika na nguvu iliyokusudiwa, si kutotonoka upande mmoja na kuukongoa mwengine.
Uhalisia wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar?
Uhalisia wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar?
 Na katika masuala ya nchi na nchi, hili halijali uwezo wao, ukubwa wao, mfungamano wao wala historia yao! Uingereza, ambayo ni moja ya madola makubwa ya Ulaya inafikiria sasa kama ibaki au ijiondoe kwenye Umoja wa Ulaya, kama ambavyo Uskochi iliyo ndani ya Muungano wa Muungano wa Ufalme, nayo pia inataka iwe nchi huru yenye kujitawala. La kuvutia zaidi ni uamuzi wa hivi majuzi wa baadhi ya wakaazi maeneo kadhaa ya kaskazini mwa England, yakiwemo ya Manchester na Liverpool, waliosaini waraka wa kutaka kujitenga na nchi hiyo na kujiunga na Uskochi itakayokuwa na mamlaka kamili.
Nimesema hivi kwa sababu, hoja kuu inayotolewa na viongozi wa CCM hasa wa Tanganyika kung’ang’ania kuendelea kuidhibiti Zanzibar kwa kutumia muundo wa serikali mbili, ni hofu ya kuvunjika muungano endapo utakuwa wa serikali tatu au wa Mkataba wakati muungano wa Tanganyika na Zanzibar ndio muungano pekee wa kielelezo cha UMOJA wa bara la AFRIKA (Pan Africanism) uliodumu kwa muda mrefu zaidi wa miaka 51. Kwa hakika mimi ni miongoni mwa watu wanaoshangazwa sana na hoja hii, ninapoangalia misimamo ya viongozi wa Tanganyika wa huko nyuma na hata wa sasa waliokalia kiti cha Urais wa Muungano, katika masuala ya muungano na umoja wa Afrika. Mwaka 1968, Mwalimu Nyerere aliunga mkono uamuzi wa jimbo la Biafra nchini Nigeria kujitenga na kujitangazia mamlaka yake ya kujitawala. Na wakati Sudan Kusini ilipojitangazia uhuru wake mwaka 2011, Rais Jakaya Kikwete alikuwa miongoni mwa viongozi waliotoa pongezi zao kwa uamuzi huo.
Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania (katikati) akipeana mkono na mwenzake wa Sudan Kusini, Salva Kiir, katika mkutano wa upatanishi jijini Arusha, huku hasimu wa Kiir, Riek Machar (kulia) akiangalia.
Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania (katikati) akipeana mkono na mwenzake wa Sudan Kusini, Salva Kiir, katika mkutano wa upatanishi jijini Arusha, huku hasimu wa Kiir, Riek Machar (kulia) akiangalia.
Kihistoria, Biafra haikuwa nchi huru iliyoungana na Nigeria, wala hakuna kumbukumbu za kihistoria zinoonyesha siku Sudan na Sudan Kusini zilipoungana na kuwa nchi moja. Vipi viongozi wa Tanganyika wanakuwa wakali wa kuulinda kwa nguvu zote muungano wa nchi mbili huru zilizoungana miaka 5i tu iliyopita, kwa hoja ya kuenzi muungano wa kipekee kwa bara la Afrika, lakini wao wao wameridhia nchi za Kiafrika kumeguka na kuanzishwa taifa jengine ndani ya taifa moja ilhali umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu? Msemo huu umuhimu wake ni kwa muungano wa Tanganyika na Zanzibar tu si kwa mataifa mengine ya Afrika? Hata wakati huu ambapo imefufuliwa tena Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Tanzania imekuwa mzito kukubali kusabilia mambo kadhaa ya msingi kwenye mfumo wa Shirikisho la Afrika Mashariki likiwemo la ardhi kwa sababu ya kulinda MASLAHI yake na mamlaka yake. Kwa nini basi isiwe ya mbele kuyasabalia mamlaka yake ili kuwa na shirikisho imara zaidi la EAC?
Haya yote na yanayojiri Uingereza yanatupa tafsiri moja tu, nayo ni kwamba muungano au utengano unazingatia kabla ya jambo lolote, MASLAHI ya wanaoungana; mengineyo ya historia, udugu na ujirani ni vichapuzo tu kwenye dhifa ya karamu. Uingereza inataka kujitoa kwenye Umoja wa Ulaya kwa hofu ya kupoteza mamlaka yake ya kujitawala ndani ya jumuiya hiyo. Uskochi inataka ijitawale hivi sasa baada ya kupita miaka 308 tangu ilipoungana na England, wala si 51 tu kama zilivyo Tanganyika na Zanzibar. Wala Zanzibar haijataka kuvunja Muungano wake na Tanganyika. Inachotaka ni muungano wenye MASLAHI, ambao ni muungano wa haki sawa kwa pande mbili. Lakini hata kama itataka kujitoa kwenye muungano huo haitokuwa kioja wala dhambi.
Muungano na Umoja ni jambo zuri sana, kama alivyosema muimbaji nguli wa Reggae, Bob Marley aliposema kuhusu Afrika “Africa unite, for the benefit of your people! “Afrika unganeni kwa faida ya watu wenu”. Lakini Bob Marley huyo huyo akasema:” Every man gotta right to decide his own destiny. And in this judgement there is no partiality”, yaani “Kila mtu ana haki ya kuamua majaaliwa na hatima yake. Na katika uamuzi wa hili hakuna upendeleo”. Kama Biafra na Sudan Kusini zilikuwa na haki hii, ambayo Uingereza na Uskochi pia zinafikiria kuitumia kwa maslahi ya watu wao, hakuna mwenye haki ya kufanya upendeleo kwa hili dhidi ya Zanzibar! Hakukuwepo kabla nchi iitwayo Biafra aliyoiunga mkono Mwalimu Nyerere ili iwe na mamlaka ya kujitawala, wala nchi iitwayo Sudan Kusini aliyoipongeza Rais Kikwete, lakini Zanzibar imekuwepo karne na dahari, na inshallah itaendelea kuwepo.
Makala ya Abdulfattah Mussa.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.