Kuna msemo maarufu wa Kiswahili usemao: “Siku za mwizi ni arubaini” ukimaanisha kwamba mwizi aibe aibavyo, ajifiche ajifichavyo, akimbie akimbiavyo, adanganye adanganyavyo, lakini safari yake hiyo chafu ya wizi haidumu na humalizikia katika mazingira mabaya sana ya fedheha, aibu na kudhalilika.”Mwizi” sio yule mporaji mali za wenzake pekee, bali ni kila anayedhulumu na akatenda visivyo haki. Ndio maana wengine wakasema “dhulma haidumu” na mwenye kudhulumu siku zote humalizikia mwisho mbaya sana, usiotarajiwa na unaotisha. Mwisho huo ukifika, hakuna wa kuuzuia, hakuna mbinu wala hila ya kuushinda, hakuna sarakasi ya kuukwepa, hakuna nguvu ya kuutoroka, hakuna kipembe cha kujificha, huwa hakuna nusura.

Wacha katuni iseme.
Wacha katuni iseme.

Wengine walisema pia “siku ya kifo cha nyani miti yote huteleza”. Nyani ni mnyama mkorofi na mjanja sana. Huishi kwa kuharibu vipando vya watu na hivyo kudhulumu nguvu za watu.  Kwa ujanja wake, mara nyingi hufanikiwa kushinda mitego midogo na mikubwa inayowekwa dhidi yake. Hata hivyo siku ya kifo chake ujanja wake wote humuishia. Kila staili ya mbinu zake za kushinda mitego hukataa kumsaidia. Uzoefu na umahiri wake kukwepa, kuruka, kuparura, kuchupa, kuchapia, kujificha, kujejea, kuzomea na kadhalika hudumaa na kuvia. Hii ni kwa sababu kifo chake huwa kimefika na hivyo hakuna hila, mbinu wala ujanja unaoweza kumpa nusura. Atakufa tu.

Na Ahmed Omar
Na Ahmed Omar

Misemo hii mitatu inaakisi vyema maisha ya CCM Zanzibar yalivyoweza kudumu kwa kutumia mtaji muhimu wa kuibaka demokrasia na kuendesha chaguzi za wizi, dhulma na za kikandamizaji. Tokea kurejeshwa kwa chaguzi za vyama vingi nchini, CCM Zanzibar katika awamu zote imekuwa ikiandaa majiko yenye gharama kwa kutumia gharama yeyote na wapishi wenye kila aina ya uwezo wa hila, njama, ubabe, dhulma na wizi kuhakikisha ushindi wa CCM unapikwa na unapikika. Tab’an tunaweza kusema hakuna uchaguzi hata mmoja Zanzibar ambao uliweza kuitwa uchaguzi wa kidemokrasia na uchaguzi wa haki tokea kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini. Ni chaguzi za mizengwe, wizi, ubabe, mateso, ukandamizaji na mauwaji.

Dhulma hii ya kiuchaguzi ambayo kwa muda wote huo ilifanikiwa kuibaka demokrasia imekuwa ikitumia itifaki ifuatayo. Kwanza ni matumizi ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kama wakala wa CCM na sio chombo chenye kubeba imani na dhamana ya kuendesha uchaguzi huru na wa haki. Tukianzia na muundo, Tume ya Uchaguzi Zanzibar katika chaguzi zote imekuwa na watendaji wenye mrengo wa CCM na ambao wazi wazi hufanya shughuli zao kwa kufuata maelekezo ya CCM. Kwa zaidi ya asilimia 90, kuanzia Mwenyekiti wa Tume hiyo hadi maafisa waandikishaji wote hawa ni watu wenye utiifu kwa CCM. Huingizwa kwa makusudi kabisa na hukabidhiwa nafasi hizo kwa lengo moja tu nalo ni kuhakikisha wanaipendelea CCM katika kusimamia hatua zote za uchaguzi. Mwenyekiti wa sasa wa Tume ya Uchaguzi ni mwanachama wa CCM ambae uchaguzi wa mwaka 2010 alikuwa mgombea wa CCM katika uchaguzi wa ndani ya chama ambae kwa bahati mbaya alibwagwa.

Tume ya uchaguzi inapolalamikiwa kwa maovu na uchafu wake, wasemaji wa Tume hiyo hukimbilia katika hoja ya uwemo wa makamishna wawili wa Tume ya Uchaguzi ambao wanatoka katika chama cha CUF. Jamii huaminishwa kwa kutumia hoja hii eti CUF haiwezi kuchezewa rafu za kiuchaguzi kwa kuwa makamishna wake hao wawili wamo ndani wakiwa wajumbe wa Tume na kila linalofanyika wanahusika nalo au wanaliona. Hapa lazima ifahamike kuwa makamishna mawili kutoka CUF hawana nguvu ya maamuzi kwa kuwa wao ni wajumbe wawili tu mbele ya wajumbe sita kutoka CCM. Halkadhalika ifahamike kuwa makamishna hao mamlaka yao ni kupitisha sera na miongozo mikuu ya Tume hiyo na sio kusimamia au kutekeleza kazi za Tume za kila siku au za misimu ya uchaguzi.

Masuala ya kiutendaji ya Tume ya Uchaguzi yanaratibiwa, kusimamiwa na kutekelezwa na Sekretarieti ya Tume ambayo inaongozwa na Mkurugenzi wa Tume. Hivyo basi masuala ya kupika hila, njama na wizi wa kiuchaguzi unaofanywa na Tume hiyo unatokana na majukumu na mamlaka ya kiutendaji ya shughuli za kila siku za Sekretarieti ya Tume. Hapa katika Sekretarieti ya Tume ndipo panapotekelezwa ukataji wa mjimbo, utaratibu wa uandikishaji, uajiri wa watumishi na maafisa wa Tume, udhibiti na matumizi ya daftari na uratibu wa mchakato wa upigaji kura na kuhesabu kura, hatua zote hizo hufanywa kwa utaratibu makini wa wizi. Yote hayo ni majukumu ya Skretarieti ambayo hutekelezwa na watendaji ambao ni watiifu kwa CCM na maagizo yake.

Zoezi la kuandaa daftari chafu la wapiga kura linaendelea. Wapiga kura mamluki na wasio na sifa tayari wameshaingizwa kwa maelfu katika daftari hilo. Bado mipango ya kuandikisha wapiga kura wasio na sifa zinaendelea kote Unguja na Pemba. Watu wasio wazanzibari wanakusanywa katika vituo mbali mbali na misafara ya kuwapeleka kupatiwa Zan Id inaratibiwa kila siku huku misafara hiyo ikionekana dhahiri shahiri mchana kweupe.
Pili, wakati ZEC ikifanya uchafu huo, viongozi wa CCM na serikali kutoka CCM upande wa Zanzibar wamekuwa wakiijipanga kimkakati kujenga mazingira ya chuki miongoni mwa wazanzibari. Wamekuwa wakiratibu vitendo vya ubaguzi baina ya wazanzibari ambavyo vina dhamira ya kuzorotesha na kuvunja misingi ya maridhiano.

Ndio maana kila kukicha tunasikia staili mpya za lugha za uchochezi katika mbao za maskani za CCM. Ndio maana ofisi za CUF na baraza za vijana wa CUF zinachomwa moto huku na kule. Ndio maana wanachama na wapenzi wa CUF wakitokea mikutanoni wanavamiwa na kuumizwa vibaya, wengine kupotezewa viungo na wengine kupotezewa maisha. Makundi maalum ya vijana maharamia wanaokabidhiwa silaha zikiwemo nondo, mapanga, chupa, visu na silaha nyengine ambao wanaofunzwa katika kambi maalum za kiharamia huandaliwa kutekeleza hujuma hizo.

Lengo ni moja tu, kuhakikisha amani, utulivu na maelewano yanaondoka badala yake watu waishi kwa hofu, kwa kuchukiana na kuhasimiana. Lengo la haya ni kutengeneza mtaji mwengine muhimu wa CCM ambao ni kuiweka jamii ya wazanzibari katika hali ya kuchukiana na kuhasimiana na hivyo kutengeneza mazingira ya kuelekea katika uchaguzi wenye muelekeo wa mitafaruku, fujo, mapigano na mauwaji. Hii ipo wazi kwani CCM inaamini ndani ya uchaguzi huru, wenye utulivu, masikizano na amani kamwe haiwezi kushinda.

Mipango yote ya mbinu na hila chafu hufanywa kwa usiri na ustadi mkubwa. Hata hivyo CCM wanaendela kupatwa na mshangao kuona kila njama, hila na mbinu chafu wanayoipanga na kuitekeleza inashtukiwa, inafahamika na kuanikwa hadharani na CUF. Hakuna wanapokaa popote wakafanikiwa kupanga mipango yao michafu bila wenzo kuwasaliti. Mwisho wa siku kila uchafu waliojaribu kuupanga na kuutekeleza unaingia ndani ya mikono ya CUF. Jambo hili linazidi kuwaumiza vichwa CCM na viongozi wao na kumtafuta ni nani mchawi wao na ni katika mazingira gani siri za uchafu wao hutoka nje. Jawabu ni moja tu wazanzibari wamechoshwa na CCM. Wamechoshwa na udanganyifu wa CCM.

Wafuasi wa CCM kwa miaka yote wamekuwa wakipewa propaganda chafu dhidi ya CUF. Mara waarabu, mara masultani, mara hivi mara vile. Uzuri ni kwamba sasa wazanzibari wote wameelewa. Hawasikii tena uzushi wowote. Wameungana na wazanzibari wenzao kudai mamlaka kamili ya nchi yao. Wafuasi wa CCM siku zote wamekuwa wakiahidiwa neema baada ya kupiga kura kumi kumi lakini neema hizo huota mbawa. Wamechoka na ahadi za uongo za na sasa wameamua. Wamechoka kutumikishwa dhulma kwa ajili ya kuchumia matumbo ya tabaka tawala na aila zao.

Tatu, ni matumizi ya nguvu na ubabe wa dola kuhakikisha dhulma inakamilika pindipo mipango ya hila na wizi ikishindwa kukamilisha lengo. Matumizi ya nguvu na ubabe ndio mtaji wa mwisho wa CCM kukamilisha agenda yao ya ushindi lazima. Hii ni kwa sababu pamoja na kukamilika kwa mitaji miwili ilioelezwa hapo juu, bado dalili za ushindi katika chaguzi zote zilizotangulia hubaki pale pale kwa Chama cha Wananchi – CUF. Hapo ndipo tena mpango huu wa kutumia nguvu za dola hulazimika kutumiwa.
Mpango huu hutekelezwa na vyombo vya dola vikiwa na silaha nzito nzito tokea siku ya uandikishaji wa wapiga kura, siku za kampeni, siku ya upigaji kura na siku ya utangazwaji wa matokeo. Kwa mfano katika vituo vya uandikishaji na upigaji kura, kwa kufuata maelekezo ya masheha na wana CCM, maafisa waandikishaji hutakiwa kuwakataa waandikishwaji na wapiga kura halali na badala yake kuwakubali waandikishwaji na wapiga kura mamluki. Kwa kuwa afisa wa Tume mwenye utiifu kwa CCM ndie mwenye mamlaka ya mwisho katika kituo cha uandikishaji jaribio lolote la kumpinga afisa huyo hutajwa kuwa ni uvunjifu wa amani kituoni hapo. Hapo tena askari polisi na maafisa wa vyombo vyengine vya dola vikiwemo vikosi vya SMZ, ambao wote wana utiifu kwa CCM kuwakabili walalamikaji au wapigania haki zao na kuwatia nguvuni kwa kuwapiga na kuwaburuza katika vituo vya polisi.

Hapa ndipo lilipo lile jukumu haramu la mwisho la vyombo vya dola kuisaidia CCM. Maafisa wa vyombo hivyo kwa kutumia silaha zao zote na nguvu zao zote husimamia dhulma ikitendeka mbele yao huku na wao kikamilifu wakishiriki na wakihakikisha madhalimu wanafanikiwa. Mitutu ya bunduki huelekezwa kwa wale wenye haki ya kuandikishwa au kupiga kura na huku wakinyimwa haki yao hiyo. Bunduki hizo pia hutumika kuwalinda wale wasio na haki ya kuandikishwa au kupiga kura ili waweze kuchukua haki isio yao na bila ya kubugudhiwa.

Kwa mara zote CUF ikiongozwa na Maalim Seif huwazuia vijana wake kutofanya makabiliano yoyote ya kujibu ubabe huo wa CCM na vyombo vya dola. Vijana wa CUF kwa hakika huwa wako tayari kufa kupona kupambana kwa njia yeyote kuona wanalinda haki yao. Bunduki sio alama ya kushinda vita. Njia za mapambano ni nyingi, wewe ukiijua moja, mwenzako anaijuwa nyengine. Hata hivyo vijana wa CUF huzuiwa kufanya hivyo. Maalim Seif siku zote huwa hayuko tayari kuchukua hatamu za dola huku damu ya wazanzibari ikiwa imemwagika au roho zao zikiwa zimepotea kwa upande mmoja, na kuudhihirishia ulimwengu kuwa CUF kinahitaji kushika dola lakini hakihitaji kuona watu wanadhulumiwa kwa njia yeyote. Ndio maana katika chaguzi zote yeye husema hapana vijana tulieni, waachieni tu, dhulma hii haitadumu. Naam dhulma haidumu na ule wakati wa kumalizika kwa dhulma hii ya CCM umefika.

Vijana sasa tayari wamemuomba Maalim Seif awakabidhi wao dhamana ya uchaguzi wa Oktoba mwaka huu na yeye asubiri kuona nini watafanya kupambana na dhulma ya CCM na kulinda ushindi wa CUF. Maalim Seif sasa ametamka it’s over! Tumechoka kuonewa! Sasa watakalo tunataka! Tayari amekubali ombi la vijana ambalo alilikataa katika miaka yote iliyotangulia.

Naiona hali ni ngumu sana kwa CCM katika kila mazingira ya uchaguzi wa Octoba. Sio hila, sio mbinu, sio ujanja na sio ubabe. Idara zote hizi za dhulma ya uchaguzi zinazotegemewa na CCM tayari zimefeli. Hakuna mbinu inayofanya kazi tena, hakuna hila inayoweza kutimiza lengo, hakuna ubabe utakaoshinda. Sioni tena nusura. Ndio nikasema arubaini ya CCM na dhulma zake sasa imefika na bila shaka ijiandae kufa kifo cha nyani kwani miti yote inateleza.

 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.