Msiba mkubwa wa historia za viongozi wa Afrika ni kuwa wao hutaka historia ziandikwe zitakazowakweza wao na si kinyume cha hivyo. Historia ya Zanzibar haikusalimika na tatizo hili. Hadi kilipotoka kitabu cha Dr. Harith Ghassany, “Kwaheri Ukoloni Kwaheri Uhuru,” historia ya mapinduzi yaliegemezwa katika ujuzi wa mipango ya ASP na Makomredi wa Umma Party. Historia ikisema kuwa hawa ndiyo waliofanikisha mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964. Ikiwa tutachukulia hii kuwa ndiyo historia ya kweli basi Kassim Hanga hawezi kuwa kinara wa mapinduzi ya Zanzibar. Historia itamtaja Abeid Amani Karume, Abdulrahman Babu, Yusuf Himidi na wanamapinduzi wengine. Hii ni picha moja.

John Okello (aliyekaa katikati) anatajwa kuwa aliongoza kundi hili kufanya mashambulizi yaliyopelekea Mapinduzi ya Zanzibar ya tarehe 12 Januari 1964, lakini kitabu cha Kwaheri Ukoloni Kwaheri Uhuru kinathibitisha mikono mingine mingi nyuma ya Mapinduzi hayo.
John Okello (aliyekaa katikati) anatajwa kuwa aliongoza kundi hili kufanya mashambulizi yaliyopelekea Mapinduzi ya Zanzibar ya tarehe 12 Januari 1964, lakini kitabu cha Kwaheri Ukoloni Kwaheri Uhuru kinathibitisha mikono mingine mingi nyuma ya Mapinduzi hayo.

Ikiwa tutafunua picha nyingine kuwa mapinduzi ya Zanzibar yalikuwa na mikono mingi itabidi tuitafute hii mikono imetoka wapi. Hapa ndipo anapoingia Dr. Harith Ghassany na utafiti wake uliompitisha maktaba nyingi Marekani na Uingereza na mwisho kuishia katika mashamba ya mkonge ya Sakura na Kipumbwi, Tanga. Hapa ndipo lilipotoka jeshi la Wamakonde waliovushwa hadi Zanzibar na kusaidia katika mapinduzi. Katika mashamba haya ya mkonge ndipo anapoingia Abdallah Kassim Hanga.

Na Mohamed Said
Na Mohamed Said

Kipande hiki cha historia kwa karibu zaidi ya miaka 46 kilikuwa hakijatajwa popote si na wanamapinduzi wenyewe wala watafiti wa ndani na nje ya Tanzania. Dr. Ghassany ndiyo alikuwa mtafiti wa kwanza kuja na habari ya Jeshi la Wamakonde katika mapinduzi ya Zanzibar. Hili jeshi nani aliliunda na kwa idhini ya nani na nani walikuwa wasimamizi wa mpango ule? Ukifika hapa ndipo sasa utaiangalia historia ya mapinduzi ya Zanzibar kwa hii picha ya pili.

Jeshi lile lilikuwa katika ardhi ya Tanganyika huru na kiongozi wa Tanganyika anafahamika kuwa ni Julius Kambarage Nyerere. Iweje nchini kwake liwepo jeshi ambalo lilivuka mikapa ya nchi yake kwenda kushiriki katika kuvamia nchi jirani. Hapa ndipo unapokutana na Abdallah Kassim Hanga na Oscar Kambona. Marafiki hawa wawili ndiyo waliokuwa wapangaji wa mipango ya mapinduzi ya Zanzibar. Kambona wakati ule alikuwa na sauti kubwa katika TANU na serikali yake. Hanga na Kambona hawakuwa peke yao. Vyombo vya dola vya Tanganyika viliwapa kila aina ya msaada ili mpango huu ufanikiwe.

Hapa ndipo unapokutana na Ali Mwinyi Tambwe na Jumanne Abdallah viongozi wa ngazi ya juu katika serikali Mkoa wa Tanga wakati wa mapinduzi. Hapa ndipo unapokutana na wahusika wengine wakuu katika mpango ule kama Victor Mkello na Mohamed Omar Mkwawa. Orodha bado ndefu. Wapo wengine katika Tanganyika katika ngazi za juu ndani ya TANU na vyombo vya usalama wote walihusika katika kufanikisha mpango wa mapinduzi na Dr. Ghassany kawataja wote kwa majina yao katika kitabu chake.

Hanga hakupata kutia mguu Sakura na Kipumbwi lakini Jimmy Ringo alifika Tanga kukagua mipango. Mkono wa Hanga ulikuwa chini ya mkono wa Kambona wakati wote wa kukamilisha mpango wa mapinduzi. Unaweza sasa ukajiuliza mkono wa nani ulikuwa juu ya mkono wa Kambona? Waarabu wana msemo: “Ukiijua sababu huondoka ajabu.” Sishangai kuwa hawa wote waliotajwa na Dr. Ghassany katika kitabu chake kuwa ndiyo wapangaji wa mapinduzi leo wametolewa katika historia ya mapinduzi.

One thought on “Msiba uliyoikumba historia ya Zanzibar”

  1. Thanks for your self determinations towards Zanzibar, it is good thing to see some one use his her knowledge to emancipate people. the question is what the focus of Zanzibar right now especially for the next election?

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.