MUUNGANO wa Tanganyika na Zanzibar umetimiza miaka 51 kwa kero na homa za vipindi, lakini pamoja na hayo umedumu na unaendelea kudumu katika hali hiyo.

Ingawa imedaiwa mara nyingi kwamba Muungano huo ulikuwa [mkakati] kama hatua moja kuelekea Muungano wa Bara zima la Afrika, hadi leo, hakuna dalili kuonesha kwamba mtizamo huo ulikuwa sahihi kufikia lengo hilo.

Hakuna asiyefahamu kwamba, kwa kipindi chote cha miaka 51, Muungano umekuwa ukiumwa; na badala ya kutibu ugonjwa tumejaribu “kutibu” dalili za ugonjwa badala ya kutibu wala kutaka kujua ugonjwa wenyewe.

Kama tungetaka kujua chimbuko la ugonjwa wa Muungano wetu, tungeanzia pale mmoja wa waasisi wa Muungano, hayati, Sheikh Abeid Amani Karume, alipoukatalia ujumbe wa watu wawili, waliotumwa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wa Tanganyika kumshawishi juu ya Muungano, Machi 1964, na tena Aprili 27, 1964 pale alipotishia kutohudhuria sherehe za kukabidhiana Hati ya Muungano, kwa madai ya “kutegeshewa” baadhi ya mambo aliyoyatilia sahihi bila yeye kujua.

Madai ya Karume yalikuwa kwamba, wakati Mwalimu alitia sahihi Mkataba chini ya Ushauri wa Wanasheria wake makini, yeye (Karume) alilazimishwa ampe Mwanasheria wake, Wolfgang Dourado, likizo ya siku saba hadi Mkataba wa Muungano uwe umetiwa sahihi. Makala haya yanajaribu kufanya rejea fupi jinsi ilivyokuwa.

Kufuatia Mapinduzi ya Zanzibar ya Aprili 12, 1964, Mwalimu Nyerere, ambaye alipewa jukumu na viongozi wenzake wa Kenya na Uganda [kwa baraka zote za Uingereza na Marekani] kuratibu shughuli za kuundwa kwa Shirikisho la Afrika Mashariki, alijaribu mara nyingi kumshawishi Karume ajiunge.

Mara ya kwanza aliwatuma Bibi Titi Mohamed [Waziri mdogo na Mjumbe wa Kamati Kuu ya TANU] na Oscar Kambona, Waziri wa Mambo ya Nje, wamshawishi Karume, lakini akarejesha jibu kwamba alihitaji muda wa kutosha kufikiria, na muda wa kutosha pia kurekebisha mambo ya ndani ya nchi yake.

Kabla ya Kambona na Bibi Titi kuondoka Zanzibar, waliwaona Saleh Saadallah na Kassim Hanga, kuwasihi waendelee kumbembeleza Karume akubali kujiunga na “Familia ya Afrika Mashariki”.

Ujumbe wa pili ulikuwa na mawaziri waandamizi; Tewa Saidi Tewa na Job Lusinde, ambao nao walirudi mikono mitupu.

Kuhusu aina ya muungano uliokuwa ukifukuziwa tangu mwanzo, Nyerere amenukuliwa mahali fulani baadaye akisema: “Sikuwa na dhamira ya [kuendelea] kuwa Kiongozi wa Tanganyika; dhamira yangu ilikuwa moja tu; ya kuwakilisha nchi yangu [iitwayo] “Afrika Mashariki” [Shirikisho la Afrika Mashariki] kwenye Umoja wa Mataifa”.

Azma hii ya Nyerere tangu mwanzo, ilikuwa ni kutekeleza Azimio la Wanaharakati Wazalendo wa Vyama vya Kudai Uhuru Afrika Mashariki na Kati [PAFMECA] miaka ya 1950/60; ambapo katika Mkutano wa Nchi huru za Afrika [kabla ya OAU] mwaka 1960, mjini Adis Ababa, Nyerere amenukuliwa akitoa msimamo kwa kusema: “Lazima tuikabili Ofisi ya Kikoloni kwa kudai, si Uhuru wa Tanganyika, kisha Kenya, na Uganda na baadaye Zanzibar; bali tudai Uhuru wa Afrika Mashariki kama kitu kimoja cha kisiasa” (Soma: The Tanganyika Standard, 16 Nov. 1964).

Mtazamo huu wa Mwalimu ndio uliofanya atamke kuwa, alikuwa radhi kuchelewesha uhuru wa Tanganyika hadi Kenya na Uganda zipate uhuru kamili ili nchi hizi ziweze kuungana kuunda shirikisho la kisiasa.

Ni harakati hizi chini ya uratibu wa Mwalimu Nyerere ambazo, Juni 5, 1963, katika Mkutano wa Viongozi wa Nchi za Kenya, Tanganyika na Uganda mjini Nairobi, zilizaa tamko la uundaji wa Shirikisho la Afrika Mashariki, pale viongozi hao waliposema: “Sisi, viongozi wa wananchi na Serikali za Afrika Mashariki …. Tunaahidi kwa viapo vyetu, kuunda Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki …. Hii ni siku yetu ya vitendo, tukiongozwa na imani na maadili katika umoja na uhuru ambao tumeusumbukia (Tamko la Serikali za Afrika Mashariki, No 13/931/63 PDT/1/1 la Juni 5, 1963).

Na kuhusu Zanzibar, “tamko” hilo lilisema: “Ingawa Zanzibar haikuwakilishwa katika mkutano huu, tunatamka wazi kuwa, inakaribishwa; kwamba, mara itakapomaliza chaguzi zake (Julai 1963), serikali yake itakaribishwa kujiunga”.

Kisha tunashuhudia Mwalimu akimwambia Karume, Machi 6, 1964; “Tazama (Karume), nimewaeleza Waziri Mkuu [Jomo] Kenyatta na Waziri Mkuu [Milton] Obote, kwamba wao wakiwa tayari kuanzisha Shirikisho la Afrika Mashariki, sisi [Tanganyika] tuko tayari”.
Kisha akaendelea, “Na sasa nakwambia na wewe (Karume); mtakapokuwa tayari kuunda Shirikisho, sisi tuko tayari”. Inasemekana, Karume naye alijibu: “Sisi tuko tayari hata leo”; lakini Mwalimu Nyerere alimwambia, ilihitaji muda kidogo.

Katika hali iliyoonekana ya kushindwa kwa juhudi za Nyerere za kuunda Shirikisho la Afrika Mashariki, huku viongozi wenzake wakimsaliti na kumsambaa, Mwalimu aligeukia muungano mdogo zaidi hatua za mwisho hapo Aprili 19, 1964, kati ya Tanganyika na Zanzibar.

Kwa nini Kenyatta na Obote walighairi wazo la shirikisho?. Kenyatta anatoa jibu, miezi minne baada ya Muungano akinukuliwa na Gazeti la “The Times of London”, la Agosti 3, 1964 akisema, “Kwa kifupi, sikuwa tayari kupiga magoti kwa Nyerere na Tanganyika”.
Kufuatia kushindwa kwa mazungumzo juu ya Shirikisho la Afrika Mashariki, Aprili 11, 1964 na Aprili 18, 1964; tunajulishwa juu ya mazungumzo ya simu kati ya Nyerere na Karume hapo Aprili 21, 1964, na Karume kuondoka Zanzibar ghafla siku hiyo hiyo kwenda Dar es Salaam kukutana na Nyerere, kisha kurejea tena Zanzibar siku hiyo.

Tunaelezwa, aliporejea Zanzibar, Karume aliwaagiza wasaidizi wake, kuandaa mapokezi ya Mwalimu Nyerere, Unguja Aprili 22, 1964; ambaye aliwasili na Mkataba wa Muungano mkononi na kutiwa saini na wote wawili, kisha naye akarejea Dar es Salaam siku hiyo hiyo.
Aboud Jumbe, katika kitabu chake “The Partner-ship” [Uk 15], ametambua hali ngumu aliyokuwamo Karume wakati wa kutia saini mkataba huo; akitaja matatizo ya ndani likiwamo tishio la kupinduliwa na mahasimu wake; na shinikizo la nchi za nje, katikati ya vita baridi kati ya Marekani na Urusi.

Anachosema Jumbe hapa ni kwamba, Karume alitia sahihi Mkataba wa Muungano kwa shinikizo la kimazingira; nami sina sababu hapa ya kuyachambua yote hayo kwa kuwa nimefanya hivyo mara nyingi katika gazeti hili. Itoshe tu kusema hapa kwamba, mazingira hayo ndiyo yaliyofanya Muungano huu uanze kutekelezwa kwa mikwara.

Mkwara wa kwanza ulikuwa pale Karume alipotishia kususia sherehe ya makabidhiano ya Hati/Sheria za Muungano, Aprili 26, 1964, eti kwa sababu tu gazeti la chama cha TANU, “The Nationalist”, lilitangaza Muungano mapema [siku tatu] kabla ya taratibu kukamilika. Washauri wake walimpoza, naye akakubali kuhudhuria, lakini kwa shingo upande.

Mkwara wa pili ulitokana na Nyerere, kama Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, kuutambua ubalozi wa Ujerumani Magharibi [FRG] kama mwakilishi halali wa Ujerumani nchini Tanzania, na si ubalozi wa Ujerumani Mashariki (GDR) ambayo ilikuwa na ubalozi kamili Zanzibar, na moja ya nchi za kwanza kabisa kuitambua Serikali mpya ya Karume, kufuatia Mapinduzi ya 1964, kabla hata Mwalimu Nyerere mwenyewe hajafanya hivyo.
Katika kipindi hicho cha vita baridi, kati ya Magharibi na Mashariki; na kwa uhasama kati ya FRG na GDR katika nyanja za uhusiano wa kimataifa, ni kwamba, chini ya kanuni ya kihasama [doctrine] ya Hallstein, FGR iliweza kuvunja uhusiano na nchi yeyote iliyoitambua au kuwa na uhusiano na GDR.

Wakati Nyerere alisisitiza FRG iwe na ubalozi kamili nchini, kama nchi rafiki kabla ya Muungano, iliyotoa misaada tele kwa Tanganyika [kifedha, elimu na ufundi]; Karume kwa upande wake, alishikilia msimamo mkali kwa GDR kuwa na ubalozi kamili Zanzibar, kama shukrani kwa misaada kwake wakati wa siku za mwanzo za serikali yake kufuatia mapinduzi.
Licha ya kwamba Mambo ya nchi za Nje lilikuwa jambo chini ya Serikali ya Muungano, na chini ya mamlaka ya Rais Nyerere, Karume hakukubali kwa kile alichokiita “heshima ya Zanzibar kama nchi huru”, na hivyo nusura Muungano uvunjike.

Mtafaruku huu ulimalizwa kwa kuruhusu GDR kuwa na ubalozi mdogo Zanzibar na FGR kuendelea kuwa na ubalozi kamili Dar es Salaam na Muungano ukasalimika; lakini Serikali ya GDR, kwa hasira, ikaondoa na kufuta kabisa misaada yote kwa Tanzania Bara.

Mkwara wa tatu kwa Muungano, ulikuwa ni ule wa Serikali ya Zanzibar kukataa kwa kiburi na kwa makusudi kuhamishia baadhi ya mambo ya kimuungano kwenye Serikali ya Muungano. Kwa mfano, wakati mambo ya Ulinzi na Uhamiaji yalikuwa chini ya himaya ya Serikali ya Muungano, Zanzibar iliendelea kudhibiti Jeshi lake la Ulinzi, Usalama wa Taifa, Polisi na Idara ya Uhamiaji bila kuitika kwa Serikali ya Muungano.

Vivyo hivyo, ingawa mambo ya fedha inayopatikana kutokana na biashara ya Nchi za Nje ni ya muungano, Serikali ya Zanzibar haikuiruhusu Serikali ya Muungano kugusa akiba kubwa ya fedha zake za kigeni kutokana na biashara ya karafuu, zilizohifadhiwa kwa uangalifu kwenye benki moja ya Urusi mjini London.

Pamoja na hayo, ingawa mamlaka juu ya mambo ya Nje, Polisi, Benki, Kodi ya Mapato na Ushuru wa forodha yalikuwa chini ya Serikali ya Muungano, Serikali ya Zanzibar iliendesha mambo haya kivyake bila hofu ya kuulizwa wala kuwajibishwa na mamlaka ya Kitaifa.

Na katika nyanja za mipango ya maendeleo, Zanzibar haikutaka kupikwa chungu kimoja na Serikali ya Muungano. Kwa mfano, mwaka 1965, Bunge la Muungano lilipitisha Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano wa kwanza kwa utekelezaji; Baraza la Mapinduzi liliukataa; badala yake likapokea kwa utekelezaji, Mpango mbadala wa miaka mitatu ulioandaliwa na mchumi mmoja wa Ujerumani Mashariki [GDR], na ambao haukupata kuwasilishwa kwenye Bunge la Muungano.

Ingawa chini ya Muungano, Tanganyika na Zanzibar ziliungana na kuwa nchi moja, lakini Zanzibar iliendelea kudhibiti uhuru wa wananchi wa Tanzania Bara kuingia Zanzibar na wa Zanzibar kwenda Bara na kuzua mivutano na fadhaa.

Hali hii ilifanya mamlaka za usalama Tanzania Bara zisituke na “uasi” huo visiwani, kiasi cha kumshauri Mwalimu Nyerere kuahirisha ziara yake ya kwanza ya kiserikali visiwani humo.

Mamlaka ya Rais wa Muungano, yaliingia majaribuni kwa mara nyingine, pale alipomteua Othman Sharrif (hasimu mkubwa wa Karume) kuwa Balozi wa Tanzania nchini Marekani mwaka 1965; lakini siku chache tu aliporejea baadaye Zanzibar, Karume akamtia kizuizini bila Nyerere kujua wala kupewa taarifa. Na ingawa hakuna tuhuma zozote zilizoelekezwa kwake, Nyerere alilazimika kuingilia kati kumwokoa Sharrif; Karume alikataa katakata kumwachia, licha ya kumwita [Karume] Ikulu kujadili tukio hilo.

Sharrif aliachiwa miezi mingi baadaye, baada ya Nyerere kukubali sharti la Karume la kumtaka kubatilisha uteuzi [wa Sharrif] kuwa balozi; badala yake, Nyerere alimteua kuwa Ofisa Mifugo wa Mkoa wa Mbeya.

Hata hivyo, miaka minne baadaye hapo 1969, wakati Nyerere akiwa nje ya nchi, Othman Sharrif alikamatwa akiwa Tanzania Bara na kurudishwa Zanzibar ambako aliuawa bila kushitakiwa pamoja na wengine, kama kina Abdullah Kassim Hanga na Ali Mwinyi Tambwe na wenzao.

Huu ni uthibitisho tosha kwamba, Serikali ya Zanzibar na kiongozi wake mkuu, tangu mwanzo, ilikuwa haitaki kamwe kuheshimu wala kuachia sehemu kubwa ya madaraka yake kwa Muungano, licha ya Karume mwenyewe kutia sahihi Mkataba wa Muungano (kwa hiari) kwa utekelezaji.

Pendekezo la kuunganisha vyama vya Afro-Shirazi [ASP] na Tanganyika African National Union [TANU], lilikuja kwa kasi ya radi, Septemba 1975, pale Mwalimu Nyerere alipopendekeza hivyo kwenye kikao cha Halmashauri Kuu za Vyama vya ASP na TANU Mjini Dar es Salaam, zilipokutana kujadili uchaguzi wa Rais.

Sheikh Aboud Jumbe, wakati huo Rais wa ASP, alilipokea wazo; lakini akasema, alihitaji muda wa kutosha kwa chama chake kucheua pendekezo hilo. Hatimaye Oktoba 1976, vyama hivyo vilifikia makubaliano, pamoja na mengine, kwa masharti kwamba, chama kipya kiwe na neno ”Mapinduzi” ili Zanzibar isipoteze historia yake ya Mapinduzi, na hivyo kikazaliwa “Chama cha Mapinduzi” – CCM. Muungano wa vyama hivyo pia ulifanyika Februari 5, 1977; siku na mwezi wa kuanzishwa kwa chama cha ASP.

Furaha ya ndoa kati ya TANU na ASP [CCM] iliendelea vizuri kati ya mwaka 1977 – 1983, hadi pale Nyerere alipotoa pendekezo lingine la kuifanyia marekebisho Katiba ya Jamhuri ya Muungano, yaliyotafsiriwa na Wazanzibari wengi kama mtego wa kutaka kuimeza Zanzibar.
Malalamiko hayo yalitolewa waziwazi, hadharani na kupitia vyombo vya habari – Redio (kipindi cha “Kiroboto Tapes”) na magazeti, katika hali iliyoonyesha kuwapo ridhaa ya serikali kwa yote hayo.

Daudi Mwakawago [hayati], Waziri wa Habari na Utangazaji wa wakati huo, alijaribu kuingilia kati kwa kumtaka Waziri wa Habari mwenzake, akomeshe “uasi” huo, lakini jibu alilopata lilimfanya asithubutu tena kufuatilia “uasi” huo.

Wanajeshi wa Zanzibar walioshiriki katika Vita vya Kagera dhidi ya Nduli Idi Amin nao walilalamika juu ya kutotekelezwa kwa ahadi ya kupewa “bonasi maalum” baada ya vita, wakidai kwamba wenzao wa Bara walilipwa na kupewa heshima kama “Mashujaa wa Vita”.
Pemba nayo iliulalamikia Muungano kwa kuendesha njama kati yake na Unguja, ya kutaka kuitenga kabisa; ikitaja matatizo yasiyoshughulikiwa ya umeme na maji; wakati zaidi ya nusu ya pato la Zanzibar linatoka kisiwa hicho.

Kutokana na malalamiko haya ya Wazanzibari, serikali yao ilionyesha “huruma” na kuomba mawazo/ushauri wa Makatibu Wakuu wa Wizara na Watumishi wengine Waandamizi Visiwani, juu ya nini kifanyike kuokoa hali, ambapo wote waliunga mkono wazo la kuwa na Serikali tatu – Serikali ya Tanganyika, Serikali ya Zanzibar [kwa mambo yasiyo ya Muungano] na Serikali ya Muungano ili kulinda maslahi ya Zanzibar katika Muungano.

Akihutubia kwenye kilele cha Sherehe za Siku ya Mapinduzi mjini Unguja, zilizohudhuriwa pia na Rais Nyerere, Januari 12, 1984; Rais wa Zanzibar, Sheikh Aboud Jumbe, aliwaomba Wazanzibari wawe watulivu wakielewa kwamba Serikali yao ya Mapinduzi ingetafuta suluhisho la Kikatiba na Serikali ya Muungano; na kwamba, kama suluhu isingepatikana, angelipeleka suala hilo kwenye Mahakama maalum ya Katiba kwa utatuzi wa Kikatiba.

Hotuba hiyo inatufikisha kwenye mkwara wa tano, kwamba, katika kutekeleza hilo, Jumbe, alimrejesha kwao, Tanzania Bara, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Damian Lubuva, na kumteua raia wa Ghana, Bashir K. Swanzy, kuchukua nafasi yake.

Kufuatia uteuzi huo, Swanzy aliomba na kupewa uraia wa Zanzibar [sio wa Tanzania] bila ridhaa ya Serikali ya Muungano, na bila kujali kwamba uraia ni jambo la Muungano.
Swanzy, kwa agizo la Jumbe, aliandaa hati kupeleka kwenye Mahakama Maalumu ya Katiba [angalia Katiba, ibara 125] kutaka ifafanue muundo na aina ya muungano uliokusudiwa kwa mujibu wa Hati/Mkataba wa Muungano uliotiwa sahihi Aprili 22, 1964; na nafasi ya Zanzibar katika muungano huo.

Hata hivyo, katika hali ya kushangaza, hati hiyo ilipotea katika mazingira ya kutatanisha kabla Jumbe hajatia sahihi, na hatimaye ikaibukia mikononi mwa Mwalimu Nyerere.
Hoja zikapikwa, kwamba Jumbe alitaka kuvunja Muungano; Halmashauri Kuu ya CCM ikaitishwa haraka mjini Dodoma kujadili; hali ya hatari, ya “kuchafuka kwa hewa ya kisiasa Zanzibar” ikatangazwa.

Jumbe akahojiwa na mwisho wa yote, akavuliwa nyadhifa zote za chama na serikali kwa kosa la kuthubutu kukanyaga “mahali patakatifu”, yaani kutumia haki yake ya kikatiba kutaka kujua Muundo sahihi wa Muungano.

Mimi na makada wenzangu wa CCM kutoka Tanzania Bara, tulishuhudia hali hiyo ya hewa iliyochafuka. Lakini ukiachia mbali maswali mengi yaliyoulizwa, swali moja gumu lilikuwa: “Imekuwaje Rais [Jumbe] wa nchi [Zanzibar] kutekwa nyara na kuvuliwa madaraka ya nchi [yake] ugenini?”.

Maswali kama hili, yenye kuonyesha kutoeleweka vyema kwa muundo sahihi wa Muungano uliokusudiwa, yataendelea kuulizwa, kama hatutakaa chini kutafakari na kufafanua vyema matakwa sahihi ya Muungano wetu na mgawanyo wa madaraka ndani ya Muungano.

Maswali kama haya si ya kupuuza; yanapaswa kupata majibu sahihi kwa misingi ya kikatiba, badala ya misingi ya kivyama vya siasa; bila hivyo tutaendelea kujaribu kutibu dalili tu za ugonjwa wa Muungano, badala ya kutibu ugonjwa wenyewe.

Chanzo: Makala ya Joseph Mihangwa kwenye gazeti la Raia Mwema

 

 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.