Kwa wale walaji wa mikate ya kiasili ya Kizanzibari, maarufu kama boflo, wanafahamu ambacho hutokea pale mkate huo unapovamiwa na umma wa sisimizi. Hususan pale mlaji wa mkate huo anapokuwa na njaa kali, hujaribu kukata kipande na kukipigapiga chini mara kadhaa ili sisimizi watoke. Lakini wapi! Huwa hawatoki, bali huzidi kujificha ndani kwa ndani.

Boflo ya CCM Zanzibar imeshaingia sisimizi? Mkutano wa hadhara uliokusudiwa kukusanya wanachama na wafuasi wa CCM wa mikoa miwili ya Unguja uliofanyika viwanja vya Mabata, Magogoni, Wilaya ya Magharibi siku ya Alhamisi, tarehe 14 Mei 2015.
Boflo ya CCM Zanzibar imeshaingia sisimizi? Mkutano wa hadhara uliokusudiwa kukusanya wanachama na wafuasi wa CCM wa mikoa miwili ya Unguja uliofanyika viwanja vya Mabata, Magogoni, Wilaya ya Magharibi siku ya Alhamisi, tarehe 14 Mei 2015.

Mara nyengine mlaji hujaribu kuupasha moto, ili kuona kama athari ya sisimizi hao itapungua aweze kuula mkate wake, lakini hakuna kinachobadilika. Badala ya sisimizi hao kubaki ndani ya mkate wakiwa hai, sasa hubaki wakiwa wafu. Ni yale yale, mkate umezidiwa na sisimizi. Hauliki.

Boflo hii iliyojaa sisimizi ndio hali inayokikabili chama kikongwe cha kisiasa kwa upande wa Zanzibar hivi, Chama cha Mapinduzi, CCM, mshirika mkuu kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa visiwani humu. Sababu kubwa ni kuacha kwake misingi kilichoundiwa. Badala ya kutekeleza kazi na urithi kilioachiwa na mtangulizi wake, Afro-Shirazi Party (ASP), ambayo ni kukamilisha malengo ya kupigania uhuru wa visiwa hivi, chama hicho kimeukengeuka kabisa wajibu huo. ASP ilipigania uhuru wa wazanzibari ikimaanisha kumkomboa mwananchi kutokana na kila aina ya idhlali na unyonge ili wana wa visiwa hivi vitukufu waweze kuishi katika maisha bora, na yenye heshima.

Na Ahmed Omar
Na Ahmed Omar

ASP ilipigana na hatimae kuung’oa utawala uliohodhiwa na wachache na hatimae mamlaka ya nchi yakawa ndani ya mikono ya wengi. Ilifanikiwa kuondoa kila aina ya ubaguzi wa rangi, kabila, asili na kadhalika, hatimae wazanzibari wote wakawa na haki sawa, heshma sawa na hadhi sawa. Ilifanikiwa kwa kiasi kikubwa kuondoa umasikini wa kipato, chakula, mavazi na makaazi na wazanzibari kuwa watu wenye kuheshimika ndani ya nchi yao.

CCM Zanzibar, mrithi wa ASP, imesaliti wajibu wake wa kuyaenzi na kuyaendeleza mazuri hayo ya ASP. Badala yake imekuja kujengea misingi mipya miovu na kuweka mazingira mapya ya kuyaendeleza yale yote yaliyopigwa vita na ASP. Utawala wa nchi hii umetolewa ndani ya mikono ta wazanzibari na umekabidhiwa kwa majirani zetu, Tanganyika, kwa kisingizio cha Muungano kandamizi. Watanganyika wanautumia vyema Muungano huo na fursa zake kuijenga nchi yao na kuiimarisha kiuchumi na kisiasa huku Zanzibar ikidhalilika na ikitokomea pole pole kutoka katika ramani ya ulimwengu.

CCM imerejesha upya ubaguzi miongoni mwa wazanzibari wenyewe kwa wenyewe kwa misingi ya rangi zao, makabila yao na asili zao na kuifanya kazi kubwa ya ASP ya kufuta laana hiyo ya ubaguzi kuwa ni bure. Nyimbo zile za zama zile za uarabu, uafrika, ubwana, utwana, na kadhalika ambazo sisi vijana wa leo tumezikuta vitabuni na katika masimulizi ya walimu wetu maskulini, sasa tunazisikia zikitoka ndani ya midomoya viongozi wa CCM na katika mabango ya maskani za CCM. Ni jambo la kushangaza sana.

ASP iliikomboa ardhi na kuweka sera na sheria ambazo ziliwezesha wanyonge wa nchi hii kuweza kuitumia na kuimiliki ardhi ya nchi yao pamoja na udogo wake. CCM imerejesha tena kadhia hii ya laana ya kuimilikisha ardhi katika mikono ya wachache na kuipora kutoka kwa masikini na mafukara walio wengi. Ardhi ni raslimali muhimu kwa nchi ndogo ya Zanzibar ambayo wananchi wake wanaongezeka kila siku. Badala ya kuwekewa sera na sheria nzuri na madhubuti za umiliki na matumizi yake, viongozi wa CCM wanawapora masikini ardhi yao na kujimilikisha wao na watoto wao. Sehemu nyengine ya ardhi inauzwa kifisadi kwa matajiri na wawekezaji na kuwawacha raia masikini wakikosa hata sehemu ya kuzikiwa. Nchi yetu inanuka migogoro ya ardhi kila upande kuanzia Nungwi hadi Mkoani Pemba.

Wananchi wa Zanzibar wanaishi bila matumaini. Njaa itokanayo na ukosefu wa kazi za kufanya na kipato kisichokidhi mahitaji ndio kilio kikubwa kinachosikika katika kila kona ya nchi. Visiwa hivi vilivyojaaliwa wingi wa raslimali na utajiri wa kila aina havionekani kuwa na mvuto na utulivu kwa wananchi wake. Watu wanaishi kwa rehma za Mwenyezi Mungu. Hakuna anaethubutu kula akipendacho, kuvaa nguo aipendayo au kuishi ndani ya nyumba aipendayo. Yote hayo sasa kwa wazanzibari yamekuwa ni ndoto. CCM imewapiga wazanzibari wamepigika. Wanaishi kama wakimbizi, kama omba omba ndani ya nchi yao.

Matokeo ya usaliti huu, CCM Zanzibar imepata pigo kubwa. Nguo ya umaarufu na heshma ambayo ilijivalisha kutoka kwa mrithi wake, ASP, sasa inavuliwa maana haistahiki tena kuivaa. Inainukisha kupuu na vundo. Ngome zake zote zinabomoka. Ikijaribu kwenda kujenga palipobomoka kidogo jana, kesho yake kunabomoka kwengine zaidi ya jana. CCM inahamwa kama mji uliokumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe. Haina tena hata ile kauli mbiu ya kujifakharisha na kujipamba na historia ya uombozi ambapo Mapinduzi daima! sasa husikika katika majukwaa ya CUF. Waasisi na wanamapinduzi wanaonyesha wazi wazi kuwa Chama hicho kinawaaibisha na hivyo wanakikimbia.

Badala ya CCM kujitathmini na kufahamu kwamba imekwisha kisiasa, inanuka mbele ya wazanzibari na haina pakushika ili ijizoezoe kunyanyua upya mguu wake na kujaribu kupiga hatua mbele, imeamua kufanya maigizo ikidhani itasalimika. Inaitumia Tume ya Uchaguzi ya Zabzibar, ZEC na Mamlaka ya usajili wa wazanzibari wakaazi kama mitaji yake. Inakimbilia kwa ZEC na usajili wa wazanzibari wakaazi kupata nusura ya kuokoka. ZEC kwa maelekezo ya CCM inaandikisha wapiga kura mamluki, wasio na sifa za kuwa wapiga kura. Inaandikisha watoto wadogo walio chini ya umri wa kisheria. Inaandikisha wafu na inaandikisha mtu mmoja zaidi ya mara moja kwa kutumia picha na majina tofauti, alimradi tu CCM iweze kubaki madarakani.

CCM pia inayatumia mamlaka ya usajili wa wazanzibari kupitia vitambulisho vya mzanzibari mkaazi (ZAN Id) kama mtaji wake mwengine. Maelfu ya watoto wadogo walio chini ya umri wa miaka 18 wamepatiwa vitambulisho hivyo kinyume na sheria. Maelfu ya wakaazi feki katika maeneo ambayo CCM imezidiwa kisiasa wamepatiwa vitambulisho hivyo ili kuwahalilisha kuwa wapiga kura katika maeneo hayo. Maelefu wa wageni wasio wazanzibari wamepatiwa vitambulisho hivyo ili kuwa wapiga kura katika maeneo mbali mbali kwa lengo la kuisaidia CCM.

Kama yote hayo hayatoshi, CCM kwa kutumia wizara ya Tawala za Mikoa na idara maalum ya SMZ, inayoongozwa na Mheshimiwa Haji Omar Kheir imepitia upya mipaka ya wilaya, wadi na shehia na kutangazwa mipaka na majina ya wilaya, wadi na shehia hizo katika gazeti la serikali. Ukataji huo wa wilaya, wadi na shehia uliotangazwa unaakisi vyema wazi wazi ramani ya kisiasa na sio kijeografia wala kidemografia.

Ukataji huo umepunguza jumla ya wadi 30 kutoka katika wadi zilizokuwepo huku wadi 25 zikipunguzwa kutoka kisiwa cha Pemba peke yake. Ukataji umezichukua shehia zisizooana au zisizolingana kijeografia na kuzifanya wadi moja, huku katikati yao zikitenganishwa na shehia za wadi nyengine. Lengo la ukataji huo ni kuweka ramani itakayoiongoza Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kupitia na kukata upya majimbo ya Uchaguzi kwa upendeleo wa kisiasa (gerrymandering).

Inasemekana Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ilikwishakamilisha kazi ya kupitia na kukata upya majimbo ya Uchaguzi mapema sana lakini hata hivyo ukataji huo ulipingwa vikali na CCM wakidhani hautakuwa na faida na chama chao. Badala yake Tume ya Uchaguzi ikalazimishwa kusubiri ukataji wa mipaka ya wilaya, wadi na shehia utakaofanywa na wizara ya Mheshimiwa Haji Omar Kheir ili iwe kigezo na muongozo kwa ajili ya ukataji wa majimbo ya uchaguzi utakaoipendelea CCM.

Kwa mujibu wa sheria inayofuatwa na Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC), ukataji wa majimbo hautafanyika katika kipindi kilicho chini ya miezi sita kabla ya Uchaguzi Mkuu. Ikizingatiwa pia Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ni wakala wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, majimbo ya Zanzibar pia ni majimbo ya Uchaguzi katika uchaguzi wa Jamhuri ya Muungano, hivyo basi nayo hayapaswi kuguswa chini ya kipindi cha miezi sita. Mpango wowote au jaribio lolote la Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kupitia na kukata upya mipaka ya majimbo ya Zanzibar bila shaka ni kinyume na sheria, kwa sababu moja tu, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar inashea majimbo hayo hayo na Tume ya Uchaguzi ya Taifa.

Hata CCM ikifanikiwa kukata upya majimbo ya Zanzibar kinyume na sheria na kwa kutumia ramani yake ya upendeleo wa kisiasa ishayoitengeneza chini waziri Haji Omar Kheir bado haitapata nusura na haitaokoka. Mimi nahisi haitasaidia kwani hakuna tena ngome ya CCM, hakuna tena pakukata wala pakuacha. CCM haipo tena popote. Hakuna ilipobakia, sio kaskazini, sio kusini, sio mawioni wala machweoni. Ndio maana tunasema CCM Zanzibar mkate wenu umeshajaa sisimizi wote. Hauna pakukata tena, kilichobaki ni kufumba macho na kuumeza.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.