Siku mbili baada ya Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, kuituhumu Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kutumiliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM)  kuendeleza hujuma dhidi ya uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu kwa kushirikiana na mtandao mpana unaowajumuisha wakuu wa mikoa, wilaya, Idara ya Vitambulisho na vikosi vya ulinzi na usalama, na siku moja baada ya ZEC na CCM kukanusha vikali tuhuma hizo, wananchi kisiwani Pemba wakiongozwa na wabunge na wawakilishi wao wameanza kuchukuwa hatua kuhakikisha kuwa wanapatiwa vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi, turufu muhimu ya kuandikishwa kuwa mpigakura, inasema ripoti hii ya gazeti la MTANZANIA kutoka kwa mwandishi wao aliyeko Pemba.

Mbunge wa Mkanyageni (CUF), Mohammed Habib Mnyaa, aliyewaongoza wananchi kwenye ofisi za Idara ya Vitambulisho ya Wilaya ya Mkoani, Kusini Pemba.
Mbunge wa Mkanyageni (CUF), Mohammed Habib Mnyaa, aliyewaongoza wananchi kwenye ofisi za Idara ya Vitambulisho ya Wilaya ya Mkoani, Kusini Pemba.

HALI ya siasa visiwani Zanzibar imeanza kuwa tete baada ya wabunge na wawakilishi wa Chama cha Wananchi (CUF), kuwaongoza wananchi katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mkoani kisiwani Pemba waweze kupewa vitambulisho vya Mzanzibari.

Hatua hiyo imechukuliwa baada ya tangazo lililotolewa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Hemed Suleiman Abdallah, la kuwataka wabunge na wawakilishi kwenda kuwahamasisha wananchi wakachukue vitambulisho vyao.

Kutokana na hali hiyo Mbunge wa Mkanyageni, Habib Mohamed Habib Mnyaa na Waziri asiyekuwa na Wizara Maalumu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) Haji Faki Shaali, ambaye pia ni Mwakilishi wa Mkanyageni (CUF) ilibidi waingilie kati.

Akizungumza na waandishi wa habari huku akiwa na wananchi wapatao zaidi ya 800 waliojitokeza kwenda kuchukua vitambulisho vyao, alisema anasikitishwa na hatua ya Ofisa Vitambulisho wa Pemba, Omari Ngwali, kuwa na lugha za kupishana katika utoaji wa vitambulisho hivyo.

Alisema ofisa huyo amekuwa akiwaambia watu wakachukue vitambulisho vyao kila Jumatatu; amekuwa akishindwa kufika ofisini kwa mujibu wa utaratibu.
“Tumefika hapa nikiwa na wenzangu, tukampigia simu akasema vitambulisho havipo lakini kuna ofisa wao ametumwa Unguja yuko kwenye meli itafika leo (jana), jioni. Lakini ni uongo kwani kwa mujibu wa ratiba hakuna meli inayokuja leo Pemba.

“Nilikuwa mimi, Mbunge wa Mkoani Ali Khamis Seif, Waziri asiye na Wizara Maalum Haji, Haji Faki Shaali, Mwakilishi wa Mtambile Mohamed Haji Kingunde, Mwakilishi wa Chambani Mohamed Mbwana, Katibu wa CUF Wilaya ya Mkoani Saidi Aweso pamoja na Mkurugenzi Abas Juma Muhunzi.

“Pamoja na kumpa taarifa zote lakini DC hakuamini taarifa hizo akasema hana habari za vitambulisho hivyo. Je, haki iko wapi kwa wananchi? Tumetoka mashambani kuja kuchukua vitambulisho vyetu na hakuna shughuli iliyofanyika,” alisema Mnyaa.

Alipotafutwa na mwandishi kwa simu kutoka Dar es Salaam jana, Ofisa Vitambulisho vya Mzanzibari, Omari Ngwali, alisema anaomba apewe muda aweze kuzungumza.

“Mimi sikujui kwanza kama wewe ni mwandishi nataka nikufahamu, nipe dakika moja nipo katika sehemu mbaya kidogo,” alisema na kukata simu.

Hata hivyo, alipotafutwa baada ya muda, simu yake iliita bila kupokewa.

CHANZO: MTANZANIA

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.