Balahau mwenzangu nakukumbusha kuwa miezi michache ijayo, nchi yetu itaingia katika mchakato wa uchaguzi ambao ukimalizika hauji tena mpaka baada ya miaka mitano mingine. Hapo ikiwa bado uhai na uzima ungalipo, wapo watakaoshuhudia, lakini ni wazi kuwa wengine watakuwa au tutakuwa tumeshatangulia mbele ya haki. Tokea kuanza kwa siasa na mapambano ya ‘uhuru wa pili’ wa nchi yetu, tayari tumeshawapoteza wapiganaji mahiri, ambao walipoanza mapambano, tulidhani tutaishi nao hadi kupata ushindi wakiwa hai na wao wakawa viongozi wetu kwenye serikali ya wananchi.

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

Hivi leo nawakumbuka wapambanaji wenzetu akina Balahau Shaaban Khamis Mloo, Balahau Sudi Yussuf Mgeni, Balahau Khatib Hassan, Balahau Suleiman Seif, Balahau Maulid Makame, Balahau Khamis Umbaya, Malahau Hinaya Himidi sambamba na mwandishi mahiri aliyejitolea miaka ya mwisho ya uhai wake, Balahau Ali Nabwa. Mungu awarehemu wote.

Leo pia nawakumbuka waliotufikisha hapa pa kutufanya tuwakumbuke wenzetu walioondoka bila kufikia lengo. Nawazungumzia mabalahali wahafidhina na mawakala wao. Mabalahali wahafidhina wamekuwa wakibadilika kutokana na awamu tokea 1995, lakini kwa kujiamini bila ya kuficha wamekuwa wakisema nchi haitoki kwa vikaratasi. Hiyo ndio sababu mengine yalipita yakiwemo mabomu ambayo mpaka leo maswali yake hayana jawabu. Kwa mfano, siku zote utasikia watu walitoka bomu likaripuka. Au kinyesi kimetiwa kwenye kisima ambacho kipo kwenye kijiji au mtaa ambao wakaazi wake wengi ni mabalahau na mamalahau wa chama cha upinzani. Je, walikuwa wanajitilia kinyesi wenyewe? Kisha wanakuja kukamatwa, kupigwa na kufungwa!!! Nchi hii kwa hakika imepitia mengi katika zama tulizowaita wanaotutesa kuwa ni “Mabalahali Melodi”.

Lakini nawakumbuka pia mabalahali majanjawidi ambao ndio tulionao hadi leo. Nakumbuka mikong’oto yao kwa mabalahau wa Magogoni, Darajabovu, Tomondo, Kwarara, Kinuni na Jang’ombe, kwa kutaja maeneo machache. Safari moja, nakumbuka, kampeni zimemalizika kufungwa rasmi jioni yake na asubuhi ya siku ya pili, ambayo ndiyo ya upigaji kura, jeshi linaanza kazi: mabalahali wa KMKM, wa MAGEREZA, wa JKU na bila kuwasahau wale manyalahali wa UMAWA. Balahau mwananchi wa kawaida ana mbinde kuweza kufika kituo cha kupigia kura na anayefika huko majina yake hayaonekani katika kompyuta, sababu kompyuta za Tume ya Uchaguzi ya Balahali Jecha na Balahali Salumu zina ukakasi kuweza kusoma majina ya Balahau Kombo wa Kombo wa Mwikombo, ingawa huweza kusoma kwa haraka majina ya Malahali. Yanapoonekana majina ya Mabalahau, basi waanakaa hadi saa 7:00 mchana visaduku vya kura havijafika.

Nakumbuka na ya Tume ya Uchaguzi nayo, ambayo kila mara ikipelekewa malalamiko ya kukosekana vifaa au watu kunyimwa haki ya kupiga kura, majibu yalikuwa yale yale: “Kwa sasa tunashughulika na matokeo hatuna majibu rasmi, lakini mbona uchaguzi ulikuwa huru na umeenda vizuri?”

“Kuna watu hawakupiga kura tumewaona,” tukawaambia malahali wakuu wa Tume.
“Walete,” ndio jibu lake. Ukiwapeleka, utawakuta wakuu hao vikaoni kila baada ya dakika 5 kati yao na mabalahali wakereketwa wa CCM. Nia ni kuleta ushindi wa Chama Tawala.

Nawakumbuka na mabalahau na mamalahau wasimamizi wanaotoka upinzani namna walivyokuwa wakishindwa kujua nini kinaendelea na wakiwa kama mfano wa gari iliyokatika “center-bearing” – wanaichaicha tu. Ama kule kunakohisabiwa kura na Balahau Maalim Seif yuko hoi-bin- taabani, akiwa hajui la kufanya kwani hakuwa amejitayarisha mwazoni nini cha kufanya hali itakapotokea tena kama miaka yote.

Nakumbuka kibarua kizito akiachiwa Balahau Said Muhene na Balahau Salim Bimani, nao pia wakiwa hawajui pa kuanzia wala kuishia, kwani jambo lolote linataka matayarisho na wao walikuwa kama hawaamini watu waliowazoea wameweza mwaka huu kuwafanyia tena yale yale. Yote hayo ni 1995, 2000, 2005 na 2010.

Lakini sasa kumbukumbu zangu zinageuka ndoto ya kesho ijayo. Ile kauli ya Balahali Marehemu Salmin Awadi na mgonjwa wa kitandani Malahali Asha Bakari inanijia tena na tarehe ni 25 Oktoba 2015. Hatutoi nchi! Vifaru vinaranda. Jeshi lote limewasili na baadhi ya matokeo yanatolewa jeshini ambako huthubutu kwenda. Kila jimbo linalotangazwa matokeo yake, wapinzani wameanguka. Hebu niambie hali kama hii nini kifanyike? Kwa nia ya kulinda utawala wao, watu mpaka hamsini wameshapigwa risasi. Nasikia wapigaji hawajulikani. Ni wahuni tu! Pengine mtu kama waziri wetu, Balahali Mtumbatu Mshirazi mwezangu akasema: “Hawa wanataka kumrudisha Balahau Sultani hawa, wauweni tu!”

Nini kifanyike sasa? Kama ni mkusanyiko, mji haufikiki tena. Kila kona mabalahau wanazuiwa, kwani wanajuwa kuwa mabalahau na mamalahau wakifanikiwa kujikusanya eneo lote la mjini, basi ile nguvu ya umma kweli itashinda. Sasa shida ni mkusanyiko wa watu, ndio maana huzuiwa wasikusanyike. Nimewahi kushuhudia kwa macho yangu watu wakizuiwa wasije mjini. Hapa panataka matayarisho ya kiume kupokea matokeo, kwani zimwi hili ni zimwi tulijualo na wapi hutokea.

Mara nyingi siku kama hii Mabalahali wote wa CCM huwa lao ni moja tu, nalo ni kuizuia CUF wasishinde. Wamo kwenye Tume, wamo kwenye vikosi, wamo kwenye taasisi za kiraia. Hutumia vikosi vyote vya ulinzi na usalama, huku wengine wakiwa wamevaa nguo za kiraia au fulana za wasimamizi wa uchaguzi na vipande hewa wakirandaranda na vespa na magari. Kama kweli tumekusudia mabadiliko hapa ni sehemu muhimu kwa kuanza kwa mabadiliko katika safari ambayo imetugharimu utajiri wetu, uhai wetu na kututia umasikini na wengine ulemavu wa maisha.

Lazima mipango madhubuti ipangwe. Hakuna siku CCM itamuambia Balahau Maalim Seif umetushinda, chukua nchi uongoze. Firikia Mzanzibari balahau mwezangu siku ya uchaguzi wapi panatakiwa ufa uzibwe. Ninavyoona miye Balahau mwenzio ni kuwa tuna mwaka 2015 tu na hatuna mwengine. Na madhali tushaumwa sana na nyoka, wajibu wetu ni kugutuka. Tukiwa miti iliyokatwa na shoka, tusilisahau shoka lililotukata, kwa maana hata shoka lenyewe bado linatukumbuka lilivyotukata.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.