Siku moja baada ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad kutoa tuhuma nzito dhidi ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), kuandikisha wapigakura wasio na sifa, tume hiyo imeibuka na kukanusha vikali.

Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Salum Kassim Ali.
Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Salum Kassim Ali.

Mkurugenzi wa ZEC, Salum Kassim Ali alisema jana kuwa hakuna majina ya marehemu yanayoendelea kutumika katika Daftari la Kudumu la Wapigakura hivyo CUF iache kuipotosha jamii.

Alikuwa anajibu madai ya Maalim Seif kuwa ZEC iliandikisha na kuruhusu wapigakura wenye umri chini ya miaka 18, walioandikishwa mara mbili, wasiokuwa wakazi na waliotumia ama majina au picha za watu wengine.

Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF, alisema madai hayo yamebainika katika utafiti uliofanywa na chama hicho ili kubaini hujuma zilizofanywa na SMZ na taasisi zake ambazo zinaweza kufanyika pia katika uchaguzi ujao.

Katika majibu yake, Ali alisema sheria na taratibu za uchaguzi kabla ya kupiga kura, yaani daftari huhakikiwa na majina kubandikwa hadharani katika vituo vya kupigia kura zilifanyika, hivyo kama kungekuwa na dosari, zilipaswa kuwekewa pingamizi.

Alisema sekretarieti ya ZEC inafanya kazi zake kwa maelekezo ya makamishna wake wakiwamo wawili kutoka CUF ambao wanafanya nao kazi kwa ushirikiano mkubwa na hayakuwahi kujitokeza malalamiko hayo.

Alisema kabla ya kuanza uandikishaji mwezi huu, ZEC ilikutana na wadau vyama vya siasa na kuwaeleza mambo manne yatakayofanyika ambayo ni uandikishwaji wa mwisho kwa wapiga kura, kuhakiki daftari la wapigakura, ikiwamo kuondoa waliokufa, kubadilisha taarifa na kuhamisha taarifa za wapigakura.

Alisema endapo kungekuwa na kasoro, makamishna hao wa CUF ndiyo wangekuwa wa mwanzo kulalamika kwa vile wapo jikoni na siyo viongozi wa chama wanaolalamika kwenye vyombo vya habari.

“Kama kweli ana ushahidi wa kile anachokizungumza, kwa nini haleti malalamiko yake ZEC badala yake analalamika kwenye vyombo vya habari?” alihoji.

Mkurugenzi wa Idara ya Usajili wa Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi, Mohamed Juma Ame alisema viongozi wenye dhamana wanapaswa kufanya utafiti na kupata ukweli kabla ya kutoa shutuma nzito ili wananchi wapate taarifa sahihi.

Alisema kwa mujibu wa Sheria ya Mzanzibari Mkaazi, mtu yeyote kabla ya kusajiliwa, anatakiwa awe na cheti cha kuzaliwa, barua ya sheha na haiwezekani mtoto mwenye umri chini ya miaka 18 kupewa kitambulisho hicho.

Alisema kabla ya kuandikishwa kuwa mpiga kura, lazima mtu awe na kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi na masharti ya kukipata lazima awe na cheti cha kuzaliwa na sheha amtambue.

Mkurugenzi huyo alikanusha madai ya kuwepo kwa kambi ya jeshi inayotumika kuandikisha na kuwapatia watu vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi bila sifa, akisema idara yake haina uhusiano wowote na kikosi wala jeshi lolote hapa nchini.

Alisema Maalim Seif ni Makamu wa Kwanza wa Rais, hivyo ana uwezo wa kumwita ofisini kwake wakati wowote kumwelezea madai yake, lakini hajawahi kufanya hivyo isipokuwa mara moja baada ya mtoto wake wa kumlea kukwama kupata barua ya sheha ya kumwezesha kupata kitambulisho cha Mzanzibari mkaazi.

Alisema utafiti wa CUF una kasoro kubwa kwa vile mamlaka inazozishutumu hazikupewa nafasi ya kujieleza dhidi ya malalamiko hayo, jambo ambalo ni kinyume na taratibu za utafiti.

Kuhusu madai kuwa baadhi ya wafuasi wa CUF hawapatiwi vitambulisho vya ukaazi, alisema kuna zaidi ya vitambulisho 20,000 ambavyo havijachukuliwa na wahusika, wengi wao kutoka Pemba.

Kuhusu Shein

Akizungumzia madai kuwa Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein anatakiwa kuanza kujitayarisha kisaikolojia kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai alisema Maalim Seif hana ubavu wa kuiangusha CCM visiwani hapa.

Alisema kama alishindwa akiwa kijana hawezi kufikia malengo hayo akiwa mzee.

Vuai alisema Dk Shein ana kila sababu za kushinda kutokana na kutekeleza vyema ilani ya uchaguzi, kulinda misingi ya amani na umoja wa kitaifa na ndiyo maana Serikali ya Umoja wa Kitaifa imeendelea kuwapo na kuhudumia wananchi wake.

Vuai alisema endapo Maalim Seif haridhishwi na utendaji wa ZEC alitakiwa kuzungumza ndani ya Baraza la Mapinduzi na si kwenye vyombo vya habari, jambo ambalo linazorotesha malengo ya maridhiano yaliyozaa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Chanzo: Gazeti la Mwananchi la tarehe 12 Mei 2015

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.