Na Ali Mohammed Ali
Na Ali Mohammed Ali

I wapi ile ahadi ya kufungua ukurasa mpya, ikiwemo kuendesha shughuli za kisiasa za kistaarabu zisizokuwa na matusi wala bezo yeyote baina ya vyama na wafuasi wake, wakati kila siku tunashuhudia mikutano ya CCM ikitawaliwa na lugha za matusi, chuki na ubaguzi dhidi ya wengine, hasa kwa viongozi wa juu wa chama cha CUF, akiwemo mtu aliyeinusuru nchi kwenye usiku wa matokeo ya uchaguzi wa 2010, Maalim Seif, makamu wa kwanza wa rais, ambaye hata kwa matokeo hayo hayo ya ZEC ana wafuasi nusu nzima ya raia wa Zanzibar?

Ahadi ni makubaliano ya kiimani baina ya pande mbili au zaidi, ambapo upande mmoja huuwaambia mwengine kuwa utafanya kitu fulani katika siku zijazo kwa kipindi maalum walichokubaliana. Kutekeleza ahadi ni kitu muhimu sana si kwa aliyeahidiwa tu, bali pia kwa aliyeahidi. Kwa muahidiwa hupata furaha na faraja kwa kuwa alichoahidiwa kimetekelezewa kama alivyoahidiwa, lakini kwa aliyeahidi humjenga kwenye kiwango cha juu cha uaminifu na uadilifu. Kinyume chake pia ni sawa, yaani pale ahadi isipotekelezwa.

Siku Maalim Seif alipoinusuru Zanzibar na umwagikaji damu uliokuwa karibuni kutokea, alipoyabeba Maridhiano kifuani pake na kukubali matokeo ya uchaguzi wa 2010, kwenye ukumbi wa Bwanani. Na katika picha hii ya kihistoria akimpongeza Dkt. Ali Mohammed Shein kwa 'ushindi wa Wazanzibari.' Je, Dkt. Shein ameyageuka Maridhiano?
Siku Maalim Seif alipoinusuru Zanzibar na umwagikaji damu uliokuwa karibuni kutokea, alipoyabeba Maridhiano kifuani pake na kukubali matokeo ya uchaguzi wa 2010, kwenye ukumbi wa Bwanani. Na katika picha hii ya kihistoria akimpongeza Dkt. Ali Mohammed Shein kwa ‘ushindi wa Wazanzibari.’ Je, Dkt. Shein ameyageuka Maridhiano?

Katika jamii ya Waswahili kama ilivyo ya kwetu ya Zanzibar, ambako rikodi za maandishi kwenye yale tunayoahidiana si kitu muhimu, ni jambo lenye uzito mkubwa kwa mwenye kuahidi kutekeleza ahadi yake, hata kama hakuliweka hilo kwenye maandishi. Imani miongoni mwa Wazanzibari hujengwa kwa imani tu na baadhi ya wakati kuandikiana huonekana kama ni dalili ya kutoaminiana, kitu ambacho ni utovu wa adabu.

Kwenye wimbo maarufu wa taarabu wa Marehemu Asha Simai anauliza “I wapi ile ahadi, wewe uliyoiweka? Umeitupa baidi, hutaki kuikumbuka!“ Ingawa ni wimbo wenye muktadha wa mapenzi na unyumba, mantiki ya swali lake inasafiri kwenye nyanja zote za maisha ya mwanaadamu, ikiwemo siasa kama ulivyo msingi wa makala hii.

Wazanzibari wote ni mashahidi wa ahadi kedekede ambazo tulipeana pale katika Ukumbi wa Salama, Bwawani Zanzibar usiku wa kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa 2010. Ulikuwa usiku wa aina yake kwetu sote, kwa kuwa fumbo la ushindi wa urais kwenye uchaguzi huo lilifumbuliwa kilaini na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), ambaye alikuwa mgombea pia kwenye uchaguzi huo, Maalim Seif Sharif Hamad, kwa kujitolea kuyatambua matokeo ya uchaguzi wenyewe licha ya yote na licha ya vyote. Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ilikuwa kama kawaida imeshafanya madudu yake, na sasa nchi ilikuwa imevimba karibu ya kupasuka. Maalim Seif akajitokeza kuinusuru.

Kujitokeza kwa Maalim Seif kuinusuru hali kumekuja kufahamika baadaye sana kupitia kwa Mzee Hassan Nassor Moyo, mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano, kwamba hakukuja hivi hivi. Kulitanguliwa na mazungumzo ya ndani, ya kina na ya kiutu uzima kati ya mkongwe huyo wa siasa na Maalim Seif. Kwa kauli yake mwenyewe Mzee Moyo ni kuwa kama si busara za hali ya juu alizonazo Maalim Seif na mapenzi ya dhati aliyonayo kwa nchi yake, basi hadithi ingelikuwa vyengine.

Lakini hadithi ikawa njema kwa pande zote. Furaha ikajaa sio tu kwa waliotangazwa kushinda, Chama cha Mapinduzi (CCM), bali pia kwa CUF iliyotangazwa kupoteza nafasi hiyo ya urais kwa mara ya nne mfululizo. Kwa maneno ya Maalim Seif kwenye usiku huo wa aina yake ni kuwa “haukuwa ushindi kwa kundi moja la kisiasa, bali ushindi kwa Zanzibar nzima.”

Haikuwahi kutokea kabla ya hapo katika historia ya Zanzibar na Tanzania, kwa kuwa watu wote waliokuwepo kwenye ukumbi wa kupokea matokeo na hata kwa waliokuwa majumbani kuinuka kwa furaha nyusoni na midomoni mwao kwa wakati mmoja. Na baada ya hapo, midomo ya viongozi wakuu wawili – kwanza Maalim Seif wa CUF na kisha Dk. Ali Mohammed Shein wa CCM – ilifunguka na kutema lulu kama si dhahabu kwa maneno matamu na ya matumaini, ahadi za umoja, ushirikiano, marekebisho na nasaha.

Ndio maana hivi leo nikainuka kuwauliza viongozi wangu hawa iwapo bado wanaukumbuka usiku ule na iwapo bado wanazikumbuka ahadi walizotuewkea sisi kama taifa na raia wa nchi tuipendayo ya Zanzibar.

I wapi ile ahadi aliyohidi kuitekeleza Dk. Shein kutoka kwa Maalim Seif kwamba katika uchaguzi ule hakuna mshindi baina ya CCM na CUF na kuahidi kulinda kauli ile, wakati huu ambapo vyombo vya dola vinaitumikia CCM yake na kulinda maslahi ya chama hicho huku vikijitahidi kumdhoofisha mshirika wake kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa, yaani CUF?

I wapi ile ahadi ya Dk. Shein aliyoitoa usiku ule kwamba atawaunganisha wananchi na kuondoa ubaguzi, katika wakati huu ambapo ubaguzi huo unaendelezwa na CCM kikauli na kivitendo naye akishiriki au akinyamazia?

I wapi ile ahadi ya ya kuendesha chaguzi kwa njia ya amani katika nchi yetu kama ulivyoendeshwa uchaguzi huo wa mwaka 2010, katika wakati ambapo tayari kuna maelfu ya watu wasio wakaazi halali wa Zanzibar wanapewa vitambulisho vya Uzanzibari (ZAN-IDs) na wakaazi halali wananyimwa kwa maagizo na usimamizi wa mtandao wa serikali ya Dk Shein na vyombo vya usalama vya nchi?

I wapi ile ahadi ya kurekebisha Tume ya Uchaguzi (ZEC) ili iwe Tume rafiki kwa wananchi na itakayoendesha uchaguzi kwa uhuru, haki na usawa, katika wakati ambapo mwenyekiti wa Tume hiyo ni mgombea wa uwakilishi kupitia CCM na tayari maafisa na watendaji wake wanashirikiana na Idara ya Vitambulisho na vyombo vya ulinzi na usalama kuandikisha wapigakura hewa?

I wapi ile ahadi ya kufungua ukurasa mpya, ikiwemo kuendesha shughuli za kisiasa za kistaarabu zisizokuwa na matusi wala bezo yeyote baina ya vyama na wafuasi wake, wakati kila siku tunashuhudia mikutano ya CCM ikitawaliwa na lugha za matusi, chuki na ubaguzi dhidi ya wengine, hasa kwa viongozi wa juu wa chama cha CUF, akiwemo mtu aliyeinusuru nchi kwenye usiku wa matokeo ya uchaguzi wa 2010, Maalim Seif, makamu wa kwanza wa rais, ambaye hata kwa matokeo hayo hayo ya ZEC ana wafuasi nusu nzima ya raia wa Zanzibar?

I wapi ile ahadi, Rais wangu Dk. Shein? Ile ya usiku wa kukumbatiana kwa mahaba na kwa umoja na kwa ari ya ushindi wa Wazanzibari?

Na juu ya yote, ziko wapi zile bashasha zilizooneshwa na viongozi wetu usiku ule na zikaashiria mapenzi miongoni mwetu, viongozi kadhaa wa kadhaa wa CCM walionyanyuka na kumfuata na kumkumbatia Maalim Seif kama shujaa na bingwa halisi wa pambano?

I wapi ile ahadi ya Zanzibar moja, imara na madhubuti katika wakati ambapo tunaingia kwenye uchaguzi na nchi imegawika mapande mapande?

Kama hukumbuki ahadi uliyoiweka au kama unaikumbuka lakini unaipuuzia, basi nakukumbusha kuwa wewe ndiye kiongozi mkuu wa nchi hii, na hivyo wewe ndiye mchunga. Kama umesahau yote, angalau kumbuka kuwa kuna Mungu Muumba na kuna siku ya kufufuliwa na kulipwa, nawe mchunga utaulizwa namna ulivyotekeleza dhamana yako.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.