OTTO von Bismarck alikuwa mwanasiasa wa kihafidhina wa Ujerumani aliyefariki dunia Julai 30, 1898 akiwa na umri wa miaka 83. Historia inamtambua kuwa ndiye aliyeijenga Ujerumani ya leo iliyoungana.

Otto Eduard Leopold maarufu kama Otto von Bismarck aliyezitawala siasa za Ujerumani na Ulaya nzima baina ya miaka ya 1860 hadi 1890.
Otto Eduard Leopold maarufu kama Otto von Bismarck aliyezitawala siasa za Ujerumani na Ulaya nzima baina ya miaka ya 1860 hadi 1890.

Wanahistoria wameandika mengi, na wanaendelea kuandika mengi, kumhusu Bismarck. Kuna wanaomsifu na kuna wanaomponda.Lakini hakuna anayebisha kwamba alikuwa gwiji wa siasa. Pengine alikuwa hata zaidi ya gwiji.Labda alikuwa“mchawi”wa kisiasa.

Kwa namna alivyokuwa akizicheza karata zake za kisiasa, ilikuwa taabu kung’amua iwapo ilikuwa ni Bismarck aliyezivaa siasa au siasa zilizomvaa yeye.
Tukiuweka kando umahiri wake wa kisiasa na jinsi alivyokuwa amebobea katika siasa, hulka yake Bismarck ilikuwa ya kukanganya kwa sababu alikuwa na tabia zilizokuwa zikipingana.
Kwa mfano, ijapokuwa alikuwa pandikizi la mtu kila mara akiitilia shaka afya yake, akifikiria kwamba labda alikuwa mgonjwa.
Udhaifu wake mwingine ni kwamba alikuwa hajui kumsamehe mtu. Akipenda kulipiza kisasi wala hakuwa akijali hisia za wengine, iwapo vitendo vyake au matamshi yake yaliwakera au kuwaumiza.
Kwa upande mwingine, Bismarck huyohuyo alikuwa na haiba kubwa. Alikuwa mcheshi, mwenye moyo mkunjufu na mwenye huruma.
Alikuwa na tabia nyingine za kushangaza. Kwa mfano, ingawa alikuwa dikteta katili inasemekana kwamba kulikuwa nyakati ambapo akiangua kilio na machozi yakimtoka.
Jengine la kukanganya ulikuwa msimamo wake kuhusu makoloni. Awali alikuwa akipinga Ujerumani isiwe na makoloni, akihoji kwamba makoloni yatakuwa mzigo mkubwa kwa Ujerumani.
Lakini ghafla baina ya 1883 na 1884, Bismarck huyohuyo alibadilika na akanyakua makoloni katika eneo la Pacific ya Kusini na barani Afrika (Tanganyika ikiwa moja ya makoloni yake barani humo).
Ijapokuwa alikuwa mpinzani mkubwa wa Usoshalisti na wa sera zozote za kijamaa, hata hivyo ni yeye aliyeanzisha mpango wa mwanzo katika dunia ya kisasa wa serikali kutoa huduma za kijamii bure, bila ya malipo.
Bila ya shaka alianzisha mpango huo ili wafanyakazi wamuunge mkono yeye badala ya mahasimu zake wa Kisoshalisti.
Bismarck alikuwa mwandishi mzuri lakini barua zake na kumbukumbu zake haziaminiki kwa sababu ya ila yake ya kudanganya. Alianza kumwambia mamake maneno ya uwongo tangu utotoni mwake na aliendelea na tabia hiyo hadi kufa kwake.
La ajabu ni kwamba hiyo hulka yake Bismarck ya kuwa na tabia zilizopingana ni moja ya mambo yanayowafanya waandishi wa leo wavutiwe naye.
Kuna na jingine lenye kuwafanya watu wavutiwe naye. Nalo ni matamshi yake yenye kuonekana kuwa ni maneno ya busara au yasiyosahaulika. Na Bismarck katika maisha yake ya kisiasa amewahi kutamka maneno mengi ya kukumbukwa.
Ijapokuwa yeye mwenyewe alikuwa na sifa au ila ya kusema uwongo, safari moja aliwahi kusema kwamba hakuna wakati ambapo watu husema sana uwongo kama “baada ya mawindo, wakati wa vita au kabla ya uchaguzi.”
Kweli, hayo ni maneno ya mtu aliyekuwa mwongo lakini Watanzania hawana budi ila kuyatia maanani kwa wakati huu kwa vile uchaguzi mkuu tayari unanukia nchini. Kwa mujibu wa Bismarck, na kwa hili hajakosea hata kidogo, wakati huu wa kabla ya uchaguzi ndipo uwongo mwingi husemwa.
Tutaraji basi kuyasikia mengi ya udanganyifu naya uwongo mwingi kutoka kwa wanasiasa wetu, wa kambi zote. Ingawa kuna kuzidiana, lakini kamwe tusisahau kwamba wanasiasa ni wanasiasa na moja ya tabia zao ni hiyo ya kusema yasiyo ya kweli.Kwa kawaida, uwongo husemwa zaidi na wale wenye hofu ya kushindwa katika uchaguzi.
Siku hizi katika baadhi ya nchi za Kiafrika, Tanzania ikiwa mojawapo, kuna mtindo wa watu kukimbilia kujiingiza katika siasa kwa upande wa vyama venye kutawala wakiwa na lengo moja kubwa: kujineemesha. Watu hao huzitumia siasa kama ngazi za kupandia kuelekea juu kwenye ufanisi wa kila aina.
Hivyo,lakini, sivyo ilivyo katika nchi zote. Katika nchi mbalimbali za Kiafrika na zilizo nje ya mipaka ya Afrika kuna wanasiasa wengi wanaozikumbatia siasa kwa sababu za kiitikadi. Huwa wanataka kuchangia katika maendeleo ya nchi zao na kuzifanya nchi hizo ziwe ni pahala pazuri penye neema na ustawi.
Shughuli kubwa ya wanasiasa katika nchi zenye mfumo wa demokrasia ni ya kushinda katika uchaguzi. Huwa hawawezi kuzitekeleza sera zao iwapo hawatochaguliwa, na wanapochaguliwa kazi nyingine kubwa wanayojipa ni “kujipigia debe” wachaguliwe tena ili waendelee na kazi yao ya kuleta maendeleo katika nchi.
Ndipo wanasiasa wakawa wanawania viti katika mabunge na mabaraza mengine ya utungaji sheria.
Kadhalika vyama vya siasa navyo vinakuwa vinawania vipate viti vingi katika mabaraza hayo ili viweze kuunda serikali na kutawala.
Matokeo ya yote hayo ni kwamba wanasiasa wengi, nasema wengi, sio wote, lakini wengi huwa tayari kujiuza kwa Ibilisi ili kuyarefusha maisha yao ya kisiasa. Hujihisi kwamba wanakabiliwa na mawili: ima waseme uwongo wanyakue kura au washindwe katika uchaguzi.
Nchini Tanzania, tangu siasa ziwe siasa za ushindani wa itikadi au za mchuano wa vyama vya siasa, wanasiasa wamezidi kusema uwongo. Ama hutoa ahadi za uwongo au huwapaka tope mahasimu zao wa kisiasa.Hizo ndizo hila kubwa zinazotumiwa na wanasiasakuwania kura.
Mambo hayo yako pia hata katika nchi zinazojigamba kwamba zimepevuka kidemokrasiana yanazungumzwa huko. Mbali ya kuzungumzwa kunafanywa jitihada za kuyapatia ufumbuzi matatizo hayo, kwa sababu hayo ni matatizo na ni vizingiti vinavyoweza kuusambaratisha mfumo wa demokrasia hasa katika nchi kama zetu zenye taasisi zisizo imara za kulinda haki za wananchi.
Kwa mujibu wa sheria za Uingereza, kwa mfano, ni marufuku kwa mgombea uchaguzi kusema uwongo kuhusu wagombea wengine walio wapinzani wake.
Kwa upande mwingine, nchini Marekani, nchi ya maajabu mengi, kuna wenye kuhoji kwamba wananchi wawe na haki ya kikatiba ya kusema uwongo na kwamba sheria zilizopo katika baadhi ya majimbo ya Marekani zenye kuharamisha uwongo wakati wa kampeni na uchaguzi zifutwe.
Kuna wenye kuiunga mkono hoja hiyo. Wao wanasema kwamba wapigaji kura toka hapo hawaamini kwamba wanasiasa wanasema kweli na kwamba ni watu waaminifu. Wanahisi kwamba hulka yao ni kudanganya tu, na kwa hivyo hawawezi kubabaishwa na uwongo wao, yaani uwongo wao hauwezi kuwashawishi wawapigie kura.
Huku makwetu, wapigaji kura wanakabiliwa na hatari mbili. Kwanza, huo uwongo wa wanasiasa tuliokwishautaja na pili, upendeleaji wa vyombo vya dola ambavyo kila siku huwa vinakipendelea chama kinachotawala.
Nchini Tanzania, kwa mfano, sikupata kusikia polisi wakikizuia chama kinachotawala kisifanye mkutano wake. Wala sijapata kusikia polisi wakiuingilia mkutano wa chama hicho na kuwafurusha na kuwapiga marungu wanaohudhuria.
Inaweza kuwa kwamba chama kinachotawala ni kiangalifu zaidi na kinafuata kanuni zinazotakiwa za kuandaa mikutano. Lakini sidhani.
Wala tusidanganyike tukadhani kwamba polisi na vyombo vingine vya usalama huwa havijui vinafanya nini vinapoingilia kuchafua mikutano ya wapinzani au kuwatia nguvuni wapinzani.
Ukweli wa mambo ni kwamba polisi wanapotumiwa na wanasiasa wanakuwa wanakijuwa nini hasa wanachokifanya.
Ndio maana kila mara tunahitaji kujiuliza tena na tena kila vyombo vya dola vinapowatia nguvuni wapinzani iwapo hatua hiyo ni ya halali. Tuachane na dhana kwamba kila hatua ya polisi ni halali au kila anayefunguliwa mashtaka na polisi ni mhalifu wa sheria.
Vitendo vya polisi katika wakati huu unaokaribia uchaguzi vinapaswa vizidi kupigwa darubini na wananchi pamoja na asasi za kiraia zinazoshughulikia haki za binadamu na uwajibikaji wa vyombo vya dola.
Hii ni kazi muhimu sana kwani tunayoyasikia yakizungumzwa na kupangwa na wanasiasa wa duru fulani huko Zanzibar yanatisha. Hiyo ni dalili tu ya uchovu uliozagaa huko Zanzibar.
Tuna wajibu wa kutahadharisha ama sivyo, tukikaa kimya, na sisi pia tutakuwa tunafanya dhambi.
Kimya chetu kitatufanya tuwe sawa na wanaoshiriki katika uovu wowote unaopangwa na kuanza kupikwa tangu sasa.
Tunatambua kwamba katika siasa lisilowezekana, huwezekana.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.