SASA Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinaweza kufuta propaganda yake dhidi ya Maalim Seif Shariff Hamad ambaye ameapa kuwa pamoja na Wazanzibari awe ndani au nje ya serikali.

Katibu Mkuu wa CUF na Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad.
Katibu Mkuu wa CUF na Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad.

Maalim Seif ameshafunguka. Ametamka kwa mara nyingine kuwa atagombea urais wa Zanzibar, akijibu kilio cha wana-CUF waliomkabidhi fedha ya kutosha kutekeleza utaratibu wa kuchukua fomu wakati utakapofika.

Uongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) wa Zoni ya Mjini, umekusanya fedha na kumpa katika hafla iliyofanyika wiki iliyopita kwenye makazi yake Mbweni, nje kidogo ya mji wa Zanzibar.

Maalim Seif ni Katibu Mkuu CUF na Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar akimsaidia Dk. Ali Mohamed Shein anayeongoza Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Hatua ya wanazoni ya mjini inaondoa propaganda ya muda mrefu ya CCM kuwa Maalim Seif amekuwa mzee asiyefaa kuongoza Zanzibar.

Tena, safari hii kiongozi huyu mpendwa ndani ya nyoyo za Wazanzibari wanaoitakia mema nchi yao, amefanya jamabo asilopata kulifanyika miaka yote – kutamka waziwazi amekuwa akiporwa ushindi wa kila uchaguzi tangu 1995.

Mbele ya wanazoni, Maalim Seif alisema “sitokubali kuporwa tena ushindi wangu. Watake wasitake nitakuwa rais kwa ridhaa ya wananachi wa Zanzibar.”

“Chama chetu tumekuwa tukishiriki uchaguzi mkuu tangu mfumo wa vyama vingi vya siasa na kushinda chaguzi zilizopaita, lakini CUF haipewi haki yake ya ushindi ili kuunda serikali,” akasema kwa msisitizo.

Maelezo yake haya, yanathibitisha msimamo unaofahamika na wengi wanaofuatilia kwa karibu mwenendo wa siasa za Tanzania.

Anathibitisha pia kuwa alichokisema mwanasiasa mkongwe mwenye mvuto mkubwa Zanzibar kwa sasa, mzee Hassan Nassor Moyo, hakikanushiki.

Mzee Moyo, mmoja wa wanasiasa walioshuhudia Rais wa Kwanza wa Zanzibar baada ya mapinduzi ya 12 Januari 1964, mzee Abeid Amani Karume, akiiunganisha Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na ile ya Tanganyika, na kushiriki kuanzishwa kwa CCM Februari 1977, anasema alifuatwa na Mohammed (Eddy) Riyami kumkabili Maalim Seif kutokana na ombi la Rais Amani Abeid Karume.

Bila ya kuelezwa au kuandikiwa angalau maneno ya utangulizi ya kwenda kumshawishi Maalim Seif, Mzee Moyo alimwambia akubali matokeo hayo wakati huo nchi ikiwa imegubikwa na wingu zito la hofu baada ya kufichuka mpango wa siri wa CCM wa kukataa maamuzi ya wananchi ili kulazimisha ushindi.

Mzee Moyo hata hivyo, hajathubutu kueleza bayana kama alijua kuwa Maalim Seif, wakati huo akiwa ameingia kilingeni mara ya tatu, alikuwa ameshinda kihaki uchaguzi, ila tu CCM wakishikilia asitangazwe mshindi.

CCM ilipinda mkia mwaka 1995 pale kada wake, Ali Ameir Mohamed, aliyekuwa naibu katibu mkuu wa chama hicho, alipowaambia waandishi wa habari kabla ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kuwa hawatokubali matokeo yatakayotangazwa.

Yalipotangazwa, na mgombea wake kutaajwa ndio mshindi kwa kura zisizojaa kiganja, kiongozi huyo alitimka maeneo ya Tume na kukimbilia ofisini kwake jengo la CCM Kisiwandui.

Nilikuwa mmoja wa waandishi wachache waliomfuata ofisini kumuuliza anasemaje sasa wakati tangazo la Tume limewapa ushindi, Ali Ameir alijibu, “Niseme nini tena hapo. Kwani ungekuwa wewe ungefanyaje.”

Bado mzee Moyo hajafunguka, licha ya kuulizwa mara kadhaa katika siku za karibuni tangu pale alipoeleza jambo hilo kwa mara ya kwanza akiwa hadharani, mbele ya wananchi waliojazana ndani ya ukumbi wa Salama wa Hoteli ya Bwawani, mjini Zanzibar, kulikofanyika kongamano la masuala ya katiba mpya.

Maalim Seif amepokea fedha huku akisema amefurahi kuoneshwa imani na wananchi wa Unguja na Pemba kwa kuendelea kumuamini kama kiongozi mwema na mwenye utashi wa kujenga matumaini ya kuwapatia maendeleo na maisha bora huku akiipigania mamlaka kamili ya Zanzibar.

Mwanataaluma huyu wa sayansi ya siasa (Political Science) aliyoisomea kufikia ngazi ya shahada katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, aliahidi kiuwa baada ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa, kitatoa uongozi utakaowezesha serikali kutandika misingi ya utawala bora, uimarishaji wa uchumi unaozalisha ajira na kuendeleza umoja na mshikamano miongoni mwa wananchi.

Ahadi nyingine ni kujitahidi kuongoza vizuri ili kurejesha heshima ya Zanzibar na watu wake hadi kwenye jumuiya ya kimataifa.

Tamko lake la kugombea tena urais limekuja wakati muafaka, kwa kuwa viongozi mbalimbali wa CCM wamekuwa wakimhujumu kwa kumsingizia kashfa asizohusika nazo na kumtukana kupitia baadhi ya makada wao vijana akiwemo Naibu Katibu Mkuu wa UV-CCM Zanzibar, Shaka Hamdu Shaka, ambaye kwa Maalim Seif, ni kichuguu anayejifunza siasa.

Wakati Wazanzibari wakijiandaa na uchaguzi mkuu wa 2005, ilienezwa propaganda kuwa CUF ingetangazwa kushinda uchaguzi iwapo chama hicho kingemteua mtu mwingine kugombea nafasi hiyo, badala ya yeye Maalim Seif waliyemueleza kama aliyechuja kwa kukataliwa na wananchi ndio maana ameshindwa uchaguzi mara mbili – 1995 na 2000.

Mmoja wa viongozi wa CUF aliyekuwa akitajwa sana kuwa angekabidhiwa serikali na “CCM” kama angeteuliwa kugombea urais badala ya Maaliam Seif, alikuwa Juma Duni Haji, wakati akiwa naibu katibu mkuu.

Alipopanda jukwaani na kuzungumzia suala hilo, Duni, mchumi kitaaluma, alitangaza waziwazi kuwa kwa wadhifa huo mkubwa wa urais, hawezi hata kwa dakika moja kumpiku Maalim Seif aliyemueleza kama kiongozi makini, muadilifu na mwenye uzoefu mkubwa wa siasa kitaifa na kimataifa.

Mfano hai wa propaganda inayoendeshwa na viongozi wa CCM kumshushia hadhi Maalim Seif katika kipindi hiki cha maandalizi ya uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu, ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Vuai Ali Vuai ambaye 24 Machi, alinukuliwa na waandishi wa habari akisema Maalim Seif asahau urais.

Alisema, “Chama Cha Mapinduzi kitahakikisha Maalim Seif Shariff Hamad hapati nafasi ya kuwa Rais wa Zanzibar katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu. Kazi kubwa tuliyonayo ndani ya chama cha mapinduzi ni kuhakikisha hapati urais, ataendelea kushika nafasi ya makamo wa rais, kama atapenda, au nafasi ya uongozi ndani ya chama chake, si urais.”

Licha ya nguvu kubwa inayotumika kueneza propaganda dhidi ya Maalim Seif, hata mara moja Wazanzibari hawajatilia maanani kampeni ya kumchafua, badala yake wamekuwa wakijitokeza kumpigia kura nyingi lakini mara zote chama chake kimelalamika kuwa uchaguzi unavurugwa kwa nia ya kuinufaisha CCM.

Wiki kadhaa hapo nyuma, Maalim Seif alipata kutamka hadharani kuwa kwa namna CUF ilivyojiandaa mara hii, itashinda uchaguzi kwa zaidi asilimia 70 na imejizatiti kuunda serikali itakayokuwa ya umoja wa kitaifa.

“… Na safari hii uchaguzi utakapowadia, sitakuwa na uwezo wa kuwazuia vijana wa Zanzibar watakapotaka kusimamisha dhulma pale itakapothibitika kuwa tumeshinda uchaguzi kwa kura za Wazanzibari.”

Subira yavuta heri. Muda ndio utaamua.

Makala ya Jabir Idrissa kwenye gazeti la MAWIO 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.