Lakini Afrika haina historia nzuri kwenye ushindani wa siasa za vyama vingi uchaguzini. Vyama vichache vilivyo madarakani ndivyo ambavyo vinafuata busara iliyomo kwenye msemo huo na inapotokezea hivyo huwa ni fakhari na heshima ya hali ya juu kwa chama na mgombea anayekubali na nchi hiyo huandikwa katika vitabu vya historia. Iwapo kulikuwa na vikwazo vilivyoekwa kimataifa, basi husitishwa mara moja na misaada huanza tena kumiminika, imani ya dunia kwa utawala wa nchi hiyo hurejea.
Dk. Ali Mohamed Shein akirudi Dodoma
Rais wa Zanzibar na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Dk. Ali Mohamed Shein.

Sehemu kubwa ya mataifa barani Afrika ni yale yaliyokubali mfumo wa vyama vingi kwa shingo upande na hivyo hadithi ya chama tawala kushindwa haipo na cha upinzani kushinda haifahamiki. Si kwamba vyama hivyo tawala vinashinda kweli kwa kura za wananchi wala si kwamba vyama hivyo vya upinzani vinashindwa kuwashawishi wapiga kura kuwaunga mkono kwenye chaguzi, lakini ni kwa kuwa watawala wanatumia nguvu zote pamoja na vyombo vya dola kuendelea kusalia madarakani.

Hii imejenga saikolojia ya aina fulani kwa pande zote mbili – kwa watawala wamejijengea kiburi cha ushindi, wakijiona kwamba wao si watu wanaoweza kuhimili kushindwa na kwa vyama vya upinzani kumejengeka uvumilivu wa watu woga, wakijiona kwamba wao wanaingia kwenye uchaguzi kila baada ya miaka mitano, wanapiga kura zao, lakini kisha wanatangaziwa kushindwa na kuvumilia kungojea mwaka mwengine bila kuchukuwa hatua yoyote.

Mimi ninataka leo kuivunja saikolojia hii kwa pande zote, maana haikujengwa juu ya ukweli. Tanzania, na hasa visiwani Zanzibar, huo umekuwa mtindo wa kawaida kwa miaka 20 sasa. Je, hali hii itaendelea hadi lini tena? Je, ni kweli chama kikongwe cha ukombozi – kama ilivyo CCM – hakiwezi kuangushwa kirahisi kwa kura tu za wananchi, na lazima itumike nguvu ya ziada kuking’oa wananchi wanapokichoka? Majibu ya maswali haya kwa wale tunaowaita ‘wahafidhina’ ni NDIO. Leo nataka niwape majibu tafauti, tena kwa kuangalia mifano halisi ndani ya Afrika yenyewe.

Nakusudia kuwaambia moja kwa moja  wale wasiokubali kushindwa na upinzani kwamba iwapo uchaguzi utaendeshwa kwa njia ya uhuru na haki na matokeo yakaonesha kwamba wameshindwa, basi wasishangae na kujidhani kuwa watakuwa ndio chama cha mwanzo Afrika kilichopo madarakani kushindwa. Watambue kwamba imewahi kutokea mara tano katika bara hili mpinzani kushinda.

Ilitokea Zambia, ambako Rais Keneth Kaunda na chama chake cha United Nation Party (UNIP) kilichoongoza tangu 1964 waliangushwa kwenye uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1991 na chama cha upinzani cha Movement for Multiparty Democracy (MMD) cha Fredirick Chiluba. Kaunda alikubali kwa amani kabisa kuyatambua matokeo hayo baada tu ya kutangazwa. MMD nayo ikaja kushindwa na mgombea wa upinzani, Michael Sata wa Patriotic Front, mwaka 2011.

Ilitokea Senegal mara mbili, kwanza mwaka 2000 kwa mgombea wa mara nne wa upinzani, Abdoulaye Wade wa chama cha SDP kumuangusha mgombea wa chama tawala SNP, Abdou Diouf, ambaye chama chake ndicho kilichopigania uhuru wa nchi hiyo kutoka Ufaransa. Kisha naye Wade akaja kuangushwa na mgombea wa upinzani wa muungano wa vyama vya upinzani, Macky Sally mwaka 2012 naye akakubali kuwachia madaraka.

Imetokea Machi mwaka huu wa 2015 kwa Rais Goodluck Jonathan na chama tawala cha People Democratic Party nchini Nigeria kushindwa na kukubali kupoteza nafasi hiyo kwa mgombea wa upinzani, Muhammadu Buhari, ambaye naye kama ilivyo kwa Wade wa Senegal alikuwa ameshagombea mara nne.

Hata Zanzibar nayo haiwezi kusema kwa asilimia 100 kuwa ina ugeni na utawala wa wanasiasa wanaotokea upinzani. Tangu kumalizika kwa uchaguzi wa 2010, nchi hii imekuwa chini ya serikali ya umoja wa kitaifa, ambapo CUF sio tena chama cha upinzani bali chama mwenza kwenye serikali hiyo ya pamoja. Ukweli ni kuwa CUF haiongozi serikali kwa maana ya kuwa sio sera wala ilani yake inayotekelezwa na serikali, lakini imo serikalini.

Sasa wakati tukielekea uchaguzi wa 2015, dalili zilizo wazi zinaonesha kwamba CUF ina uwezo wa kuvunja rikodi ya ushindi kwa kuwa sasa kuna wanamabadiliko kutoka kila sehemu ya wananchi wa Zanzibar. Wachambuzi wengi wanakubaliana kuwa uchaguzi wa mwaka huu utakuwa tafauti kabisa na chaguzi zilizotangulia. Umma wa Zanzibar umeungana nyuma ya CUF katika kiwango ambacho hakikuwahi kushuhudiwa hapo kabla.

Sababu za CUF kuwa imara zaidi hivi sasa kuliko huko nyuma ni pamoja na hilo la kuwako serikalini ambalo limekipa chama hicho nafasi ya kufanya siasa kwa utulivu ndani ya kipindi cha miaka mitano mizima. Nyengine ni chama hicho kuendelea kuisimamia ajenda ya Zanzibar mbele ya Muungano wa Tanzania. Na mwisho, inawezekana ni machofu waliyonayo wananchi tangu watawala waingie madarakani pamoja na sera zisizotekelezeka ambazo zimekosesha nchi yetu maendelo ya kweli. Kasi ya mawasiliano hivi sasa inawafanya wananchi kujuwa mengi yanayohusu nchi yao na za wenzao na hivyo kuihukumu serikali iliyoko madarakani kwa kile wanachokifahamu kupitia mawasiliano hayo.

Uchaguzi wa mwaka 2015 si mwaka 1995, 2000, 2005 wala 2010. Tumetoka kule sasa tupo sehemu tafauti na kule. Wanaodhani wana hatimiliki ya kuongoza nchi hii wanajuwa kuwa si kweli kisheria wala kisiasa. Katiba ya nchi yetu inakipa haki ya kuongoza nchi chama chochote chenye usajili, wafuasi na wapiga kura wengi. Kwa Zanzibar, chama hicho ni CUF peke yake.

CCM inapaswa kujitayarisha kisaikolojia kuupokea ukweli huo. Wala isije ikajitia wazimu wa kuiingiza nchi kwenye machafuko kwa kuwa imekataliwa na umma. Ikajipange kwenye upinzani ili isije ikapotea kama KANU ya Kenya au UNIP ya Zambia. Bora kuwa mpinzani mwenye uzoefu wa kutawala, kwa sababu kunaweza kuwapa muda wa kujipanga upya na kujitathmini. Labda wakaweza kurudi tena madarakani kwa kura baada ya chaguzi kadhaa zijazo. Zanzibar ni kubwa kuliko CCM na CCM inapaswa kulikubali hilo.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.