Migomo na maandamano ni taratibu mbili ambazo hutumika kudai haki pale inapodhaniwa kukosekana ama kunyimwa katika kundi fulani la n kijamii. Taratibu huweza kuwa na maana tofauti,  lakini mara nyingi hufuatana japo si zote. Wanaogomea huishia kwenye maandamano au wanaondamana huishia kwenye mgomo. 

Mabasi ya abiria wa mikoani yakiwa kwenye mgomo katika stendi ya Ubungo, Dar es Salaam.
Mabasi ya abiria wa mikoani yakiwa kwenye mgomo katika stendi ya Ubungo, Dar es Salaam.

Watu hugoma ama kuandamana kwa kuwa ni miongoni mwa haki zao za kibinadamu na ambazo zimeorodheshwa katika Sheria ya Haki za Binadamu za Kimataifa (International Convention) na pia ni haki inayotambulika kikatiba katika katiba na sheria zote hapa nchini – Katiba ya Zanzibar katika kifungu Nambari 20 (1), Sheria ya Vyama vya Siasa Tanzania Nambari 5 ya 1992, Police Force Ordinace ya mwaka 1953, Sheria ya Kazi ya Zanzibar Nambari 11 ya 2005 (Sheria ya Kazi ya Tanzania) na hata Sheria ya Uhusiano Makazini ya Zanzibar Nambari 1 ya 2005 (Sheria ya Mahusiano kazini Tanzania). Zote hizi zinawapa haki raia kupitia makundi yao kufanya migomo na maandamano.

Na Ali Mohammed Ali
Na Ali Mohammed Ali

Tangu kuanza kwa mwezi huu wa Mei, tumeshuhudia Chama cha Madereva wa Usafiri wa Mabasi ya Abiria nchini Tanzania kikitumia haki yao hii ya mgomo kama ni njia moja inayoaminika kudaia haki. Katibu Mkuu wa chama hicho, Rashid Salehe, anasema madai yao makuu kwenye mgomo huo ni pamoja na kutaka kupewa ajira rasmi na waajiri wao, posho za safari na masomo, kufuta kusoma kila baada ya leseni kuisha, pamoja na kupatiwa bima.

Ukiwacha mtafaruku mdogo wa siku ya Jumanne, yaani tarehe 5 Mei, ambapo polisi waliwachawanya wagomaji waliokuwa wanamzunguka Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda, katika kituo cha mgomo huo, stendi ya Ubungo, Dar es Salaam, hadi sasa polisi haijafyatua risasi za moto kutawanya watu wala kupiga watu ovyo na badala yake wanatekeleza wajibu wao kama sheria inavyowataka, yaani ni kutoa ulinzi kwa wanaogoma.

Chama cha Madereva wa Mabasi ni taasisi inayowakilisha kundi maalum lenye maslahi maalum kama vile ilivyo kwa vyama vya siasa na vyama vyengine vilivyopo Tanzania. Lakini cha kushangaza ni hatua ya serikali zote mbili – ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mapinduzi ya Zanzibar – kuinyima haki kama hiyo kwa vyama vya siasa vya upinzani, ambavyo hata vinapojikusuru kuitumia, serikali hutumia vyombo vya dola kuvizuia na matokeo yake kusababisha vifo, vilema na uharibifu wa mali na maisha ya raia.

Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba, akiwa amekamatwa na polisi wilayani Temeke tarehe 27 Januari 2015.
Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba, akiwa amekamatwa na polisi wilayani Temeke tarehe 27 Januari 2015.

Si mara ya kwanza kwa madereva kugoma wakalindwa na angalau kusikilizwa na kupewa ahadi za mdomo. Mwezi uliopita wa Aprili walifanya hivyo, wakiwa na madai haya haya ya sasa. Serikali ikampeleka waziri anayehusika na kuwaahidi kuondoa kero zao na ndipo wakarudi kazini. Si mara ya kwanza pia kwa vyama vya siasa kuitisha mikusanyiko na maandamano kudai jambo, lakini sio tu kuwa serikali haitumi waziri anayehusika na hilo linalodaiwa kuzungumza nao, bali huenda mbali zaidi kwa kutuma polisi na risasi na vifaru na magari ya maji yanayowasha.

Wala isifahamike kuwa ninataka serikali iwatume FFU pale stendi ya Ubungo kwenda kupiga na kuuwa watu kama ambavyo iliwatuma Temeke mwanzoni mwa mwaka huu kuvunja maandamano ya Chama cha Wananchi (CUF) na kuwapiga, kuwajeruhi na kuwakamata wananchi kadhaa akiwamo Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba, ambaye hadi sasa ana kesi mahakamani! Sitaki hilo litokeee, lakini nahoji kwamba mwenye akili zake. lazima ajiulize kwa nini iwe hivi?

Hivi karibuni visiwani Zanzibar, Umoja wa Watoa Huduma ya Nishati ya Mafuta waligoma kuuza mafuta kwa nchi nzima,  wakishinikiza kupandishwa kwa bei ya mafuta. Hakuna mwakilishi wala mshirika wa chama hicho aliyeguswa na vyombo vya dola na badala yake madai yao yalisikilizwa.

Lakini inapokuja kwa vyama vya siasa, hali huwa tofauti hata kama hufuata hatua zinazostahiki tena kwa wakati husika. Hakuna anayewasikiliza serikalini zaidi ya kutumiwa nguvu kuwatawanya wadai haki hao. Inapotokezea mazungumzo yamefanyika baina ya serikali na wadai haki hao, makubaliano yake hudharauliwa na wanaoshika dola kwa maslahi ya Chama Tawala ambacho ni kikundi kidogo kinacholindwa na vyombo vya dola.

Maoni ya wanasiasa wa upinzani, asasi za kiraia na hata wasomi wanaowakilisha raia walio wengi hupuuzwa. Mfano mmoja ni pale Rais Jakaya Kikwete alipoamua kudharau makubaliano yaliyofikiwa kati yake na vyama vya siasa na asasi za kiraia na kidini zinazounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) baada ya kuligomea Bunge Maalum la Katiba.

Undumilakuwili huu wa serikali unapaswa kupatiwa suluhisho kutoka kwa wananchi wenyewe na huo ndio wito wangu wa kumalizia makala hii. Kwamba lazima sisi wananchi tuifikishe mwisho tabia hii ya kinafiki inayofanywa na watawala pale inapokabiliwa na kilio cha haki kutoka kwa wananchi.

Hivyo, kijana mwenzangu, dada yangu, ndugu yangu, mwanangu, na nyinyi wazazi wangu, uwe Mtanganyika ama Mzanzibari, Oktoba 2015 ni wakati wa maamuzi kwa nchi yako uipendayo kuondokana na tatizo hili la kunyimwa haki na uhuru wa kudai haki hiyo. Fanya maamuzi ambayo yatakutoa katika kufanyiwa dharau pindi unapodai haki yako. Ondoa ufisadi uliokithirishwa na watawala waliopo. Ondoa vikwazo vinavyokwaza maendeleo ya raia mmoja mmoja na ya wote kwa pamoja. Ondoa ubaguzi unaofanywa na watawala waliopo. Fanya maamuzi yatakayoweka mustakbali mzuri wa Muungazo wa Tanzania. Tumia kura yako kujenga Zanzibar mpya na Tanzania yenye heshima kwa raia wake.

Imehaririwa na Mohammed Ghassani

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.