Na Foum Kimara
Na Foum Kimara

Wanapropaganda wa chama tawala, CCM, na wanamkakati wa chama hicho kilichoshindwa kuiongoza Zanzibar kuelekea kwenye maendeleo na uwezo wa kujitegemea na kujiendesha kwa miaka 50 sasa, wamo kila pembe kumwaga propaganda zao za vitisho, ukatishaji tamaa na upandikizaji chuki kama silaha zao mwisho kabla ya uchaguzi wa Oktoba mwaka huu. Soma jawabu ya Foum Kimara kwao. – Mhariri

Mabadiliko yamewadia na hakuna wa kuyazuwia.
Mabadiliko yamewadia na hakuna wa kuyazuwia.

Nimekaa na ndugu zangu wa Kizanzibari na mazungumzo yetu yalikuwa zaidi katika masuala ya uchaguzi huu na hatima ya Zanzibar. Suali kubwa linalozuka – baada ya propaganda zote hizo na pia kuiangalia historia ya miaka 20 ya chaguzi nchini mwetu – ni namna gani upinzani umejipanga katika kulinda kura zao?

Kwanza, ninachokiona kwa sasa hakuna upinzani kama uliokuwapo zamani. Kwa sasa kuna wanamabadiliko kutoka kila sehemu ya wananchi wa Zanzibar na Tanzania nzima. Hii pekee ni sababu inayotosha ya kusema kwamba uchaguzi wa mwaka huu utakuwa tafauti kabisa na chaguzi zilizotangulia. Sababu hii ni muhimu sana kwa vile siasa za sasa zimebeba zaidi umoja kutoka makundi tafauti yenye nia moja ya mabadiliko visiwani mwetu.

Pili, wale wanaofikiri kwamba “wembe ni ule ule“, basi wajitathmini upya. Uchaguzi huu umeamsha zaidi ari ya wengi katika kusimamisha nguzo imara za mabadiliko kwa lengo la maendeleo. Huu ni uchaguzi wa kwanza unakaofanyika ukiwa umewagawa watu katika makundi mawili: la kwanza la wazalendo waliothubutu kusimama na umoja wa Wazanzibari na Watanzania wanaohitaji mabadiliko na la pili ni la wala nchi wachache wanaoendesha siasa za wagawe uwatawale milele.

Sioni kwamba hakuna mafanikio kwa miaka 20 tokea uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi ulipoanza, hasa kwa upande wa wanamabadiliko. Kushiriki uchaguzi usio wa haki na kuweza kushika asilimia 49.8 ya kura ni mafanikio makubwa yasiyobezeka hata yakibezwa. Vyama vingi nchini hupotea baada ya uchaguzi mkuu, lakini ukuwaji wa siasa za visiwani umezidi kuifanya kambi ya wanamabadiliko kujitokeza kwa wingi hadi kufika hapa tulipo sasa.

Kufikiwa kwa Maridhoano yaliyozaa serikali ya Umoja wa Kitaifa na kutupa katiba inayotamka wazi kwamba vyama vitakavyoweza kuvuna 10% ya kura katika uchaguzi vina haki ya kuwemo katika uongozi wa serikali, ni mafanikio makubwa ya kupigiwa makofi kwa kila mwenye upeo na kiu ya mabadiliko. Hatua ya mwisho kabla ya kubeba uongozi wa mabadiliko. Kwa hakika, mabadiliko haya yanazidi kuiweka Zanzibar kwenye historia yake ya kuongoza katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati.

Mageuzi ni hatua, na kwa miaka 20 wanamabadiliko wamekuwa na maendeleo makubwa kwa kila hatua kufikia katika kilele tunachokiona katika uchaguzi unaotukabili mwaka huu. Hatua ya kuweza kuvuna mamia ya wanachama kaskazini na kusini mwa Unguja imekuja kutokana na mafanikio ya chaguzi za nyuma na hasa kuutazama ushindi kama mchakato wa hatua moja baada ya hatua nyengine kuelekea kileleni.

Narudia. Mwaka 2015 si mwaka 1995. Tulipo sipo tulipotoka. Tukumbuke hili na litujaze mori kwamba kilele kimefika, nacho ni Oktoba 2015.

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar imekuwa kwa miaka yote hii ikitumia ujanja wa kunyakuwa ushindi kwa kujuwa ushahidi wa wizi haupo. Imekuwa ikijipanga zaidi katika hesabu za wapiga kura na namna inavyopokea matokeo majimboni yakiwa tayari yameshaharibiwa na kumtangaza mshindi kutokana na mahesabu hayo yaliyoharibiwa.

Mchakato wenyewe wa wizi wa kura ni mrefu unaoanza kwa kuzuia uandikishaji wa wapiga kura wakiwatumia masheha kama taasisi ya upendeleo katika uandikishaji, huku Tume yenyewe ikiwa ni ya wapenzi na wanachama wa watawala. Zoezi zima kuanzia chini mpaka juu limejengwa zaidi kama kituko cha demokrasia chenye lengo moja tu – kuhuisha ushindi wa watawala kwa njia itayohalalisha udhalimu mkubwa kwa wananchi.

Uchaguzi umekuwa kama mchezo wa bao, au kama vile mtuhumiwa mahakamani anayejulikana kwamba ametenda kosa lakini akaweza kushinda kesi kutokana na umahiri wa wanasheria wanaomuongoza. Huko nyuma, wengi walifikiri demokrasia ya nchini ni ya mwenye haki apewe. Ila miaka 20 ya vyama vingi imethibitisha kwamba ni mchezo unaopangwa na unaohitaji umahiri katika mikakati ya kuzuia hadaa.

Tumewasikia wanamageuzi wakipiga kelele na kutoa mifano mingi ya namna ushindi unavyoporwa, huku wananchi wenyewe wakichangia. Kwa mfano, kisiwani Pemba ni ngome kubwa ya wanamageuzi lakini unaposikia kuwa watu 12,000 wamo katika Daftari la Kupiga Kura lakini hawajajitokeza kupiga kura, unatambua udhaifu uko wapi. Au kwamba katika jimbo la Mtambwe analotokea Maalim Seif Sharif Hamad wa Chama cha Wananchi (CUF), kura zake ni chache kuliko za mgombea uwakilishi na ubunge wa chama chake ambao wameibuka washindi, unajiuliza inawezekanaje? Jawabu iko moja tu, nayo ni udhaifu wa huko nyuma katika ngome za wanamageuzi. Tukumbuke tafauti ya kura za mshindi na mshindwa kwenye uchaguzi ni 3000 tu. Lakini unaposikia watu 12,000 waliojiandikisha lakini wakapuuza kupiga kura katika ngome yako, unajiuliza kosa lilipo na unajuwa sasa ujipange vipi.

Vyovyote itavyokuwa, nguvu ya wanamageuzi ipo katika kujuwa jumla ya wapiga kura katika Daftari la Kudumu la Wapigakura. Huwezi kuongeza watu wakazidi idadi ya jumla ya wapiga kura katika daftari. Hivyo wizi wowote unaofanyika ni lazima uwapunguze wapiga kura wa wanamabadiliko ili uongoze wa kwako. La si hivyo, idadi ya wapiga kura itazidi ya jumla katika Daftari la Kudumu.

Sasa wanaofikiri kwamba wembe ni ule ule, wafikiri vizuri sana ila wawe tayari kuyakubali matokeo pale yatapozima matarajio yao. Mungu hasimami na udhalimu wa maisha, na ishara zipo kwamba pamoja na mikakati ya kuziba udhaifu wa majimbo yaliyo ngome za wanamageuzi, na Mungu pia kwa miaka 20 katuwekea hatua baada ya hatua kabla ya kufika kilele. Kheri haitaki papara, na tulipo sasa hasa baada ya kuwamo katika serikali ya umoja kumetufundisha zaidi kwamba sote ni binaadamu tunaoweza kufanya kazi pamoja hata tukitafautiana kimawazo. Somo kubwa kwa wanamabadiliko.

Msisitizo kwa sasa uko kwa wananchi wenyewe kuhakikisha kila mmoja wetu anajiandikisha kupiga kura. Mazungumzo yetu yaliishia kwa kukubali ukweli kwamba udhaifu upo katika wapiga kura wetu. Mmoja wa washiriki wa mazungumzo yetu anakiri kwamba yeye binafsi katika familia yake watu wanne hawakupiga kura wakiwa miongoni mwa waliojiandikisha. Mwengine anasema watu tisa katika familia yake hawakupiga kura wakiwa katika daftari la wapiga kura. Umuhimu mkubwa upo katika kuekeza katika elimu ya upigaji kura hasa katika ngome za wanamageuzi ili wafahamu kila kura moja ina nguvu ya kuhuisha mabadiliko.

Na mikakati yote Tume inayyoweka kusaidia watawala, katika suala la kutangaza mshindi Tume haina njia ya wizi wa moja kwa moja ikiwa mawakala watasimamia vizuri kila kura inayohesabiwa hasa katika kuangalia mpishano baina ya kura za wagombea uwakilishi, ubunge na mgombea wa urais.

Ndio nikarudia tena uchaguzi huu utakuwa wa mwanzo kufanyika ukibeba ari mpya baada ya kusoma udhaifu wa nyuma na kubwa nguvu za safu ya wanamageuzi walioamua kusimama na mabadiliko yanayohitajika.

Wanaosema wembe ni ule ule wanasema hivyo kwa woga na pia kujaribu kuchezea akili za wananchi na kuwakatisha tamaa wakijuwa kabisa wanaokata tamaa ndio miongoni mwa wale waliojiandikisha lakini wakaacha kupiga kura.

Wanaosema nchi hii haitatolewa na karatasi wajitazame vizuri ulimwengu wanaoishi na mabadiliko ya dunia yalivyo. Hawa ni wa kupuuzwa kwa vile nao lengo lao ni kupunguza ari ya wapiga kura wenye muamko wa mabadiliko.

Kama wewe ni mfuasi wa Team Mabadiliko, basi juwa kuwa mchango wako mkubwa ni kura yako. Hakikisha unalinda haki yako na kuhamasisha walio katika himaya yako wanajumuika na wanamageuzi katika kura ya kuikoa nchi kutoka dimbwi la maafa ya watawala wasiojielewa.

Pamoja tunaweza. Mapambano hayafanikiwa siku moja. Hivi nani aliefikiri kwamba serikali ya umoja wa kitaifa itasimama na kudumu kwa miaka mitano u kama katiba ya Zanzibar itapigiwa kura ya maoni na kushinda kwa asilimi kubwa? Au kama Makamo wa Kwanza wa Rais atakuwa ni Maalim Seif? Au hata kwamba Rais wetu ni Dk. Ali Mohamed Shein?

Tumesahau tulipotoka na vizingiti tulivyovuka tukafika tulipo? Waache walale na usingizi wa pono wa ati wembe ni ule ule, nasi tuwaambie kuwa hakuna refu lisilo na mwisho.

Aluta continua.

Imehaririwa na Mohammed Ghassani

One thought on “Kwa nini 2015 ni mwaka tafauti?”

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.