Mambo yetu mengi yamevurugika na kutukosesha maendeleo na sasa ni wakati wa kufahamu kuwa ni nguvu na ushirikiano wetu ndio pekee utakaotusaidia kuyaweka sawa na kutupeleka kule tunakotaka.
Huo ndio uliokuwa wasia wa muasisi wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, Mzee Abeid Karume, katika hotuba zake mbalimbali tokea miaka ya mwanzo ya uhuru wa nchi yetu. Alituhutubia tushirikiane na tutumie nguvu za pamoja kupigana vita dhidi ya maadui wetu watatu: ujinga, maradhi na umaskini.
Wafanyakazi wa moja ya hoteli za kitalii visiwani Zanzibar.
Wafanyakazi wa moja ya hoteli za kitalii visiwani Zanzibar.

Miaka 51 sasa, lakini bado hali ni tete kwa kuwa maadui zetu hawa watatu wanaendelea kuimarika na kutuacha sisi tukiendelea kudhoofika. Udhaifu wetu umekithiri sana katika mapambano yetu, na hasa hasa upo katika ukosefu wa ajira nchini.

Na Ali Mohammed Ali
Na Ali Mohammed Ali

Laiti tusingekuwa na matatizo ya ajira, tungeushinda ujinga kwa kuwa kupitia ajira tungepata pesa ambazo kwazo tungesoma na kusomesha jamii iliyotuzunguka, tukapata elimu, tukaushinda umaskini na maradhi na kwa elimu tukafikia kiwango kizuri cha maendeleo kama tulivyoshuhudia katika nchi za wenzetu kama zile Scandinavia, China, Japan, na hata zile zinazojiita Asian Tigers kwa sasa.

Zanzibar imekuwa kitovu cha kufanyiwa majaribio ya mara kwa mara ya nadharia za mipango isiyo endelevu na sera zisizoendana na ukweli wa kiutafiti ambazo mara zote zimefanya ubora wa mambo yetu mengi yazidi kuporomoka. Kwa mtindo huo, taifa linaangamia kwa kupelekwa hatua moja mbele kisha hatua mbili nyuma ilhali ulimwengu wa utandawazi unasonga mbele kwa kasi na wala hautungojei.

Kwa ulimwengu wa karne hizi tulizonazo, ukitaka kufikia mafanikio ni lazima uwe una sera ya hicho kitu unachotaka kukifikia. Sera ya ajira ya Zanzibar iliyotolewa na Wizara ya Kazi, Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto mwaka 2009 haiwezi kulifikisha taifa hili popote.
Sera, kwa fasili yake, ni mpango wa yatakayotendwa katika sekta fulani au maelezo ya malengo na njia ya utendaji iliyochaguliwa kuyafikia malengo hayo. Kikawaida ya Sera huwekwa katika maandishi ili iwe ndio kiongozi cha maamuzi ya nini kifanyike. Sera zaweza kuainishwa kwa namna mbalimbali ikiwa ni pamoja na ngazi zake mbili: kwanza kubainisha masuala muhimu ya sekta fulani na kufafanua nia ya kisiasa ya kurekebisha au kuboresha vipengele mbalimbali vya mfumo wa sekta fulani (substantive policies) na, pili, kuweka wazi utaratibu au namna ya utekelezaji wa kilichobainishwa katika masuala muhimu – nani mtekelezaji, utekelezaji ufanyikeje, kipindi cha utekelezaji, na ni raslimali gani zitumike (procedural policies).
Hivyo sera ya ajira iliyokamilika na inayotekelezeka lazima iwe na ngazi zote mbili, yaani sera bainishi na sera namna. Haya ni mabawa mawili yanayotegemeana. Sera nyingi zimekua dhaifu na zisizotekelezeka kwa kukosa bawa la pili ambalo ni namna utekelezaji wa sera hiyo. Aidha yapo mambo kadhaa yanayofanya sera ifanikiwe, miongoni mwao yakiwa ni ushirikishaji kamili wa wadau wote wa sekta husika kuanzia hatua za mwanzo za uandaaji, utekelezaji na tathmini ya sera hiyo.
Wadau wa ajira kama sekta ni pamoja na serikali kuu na serikali za mitaa, wamiliki wa taasisi za binafsi na za umma, wazazi, walimu, wataalamu wa masuala ya ajira, wanasheria, wanafunzi, asasi zisizo za kiserikali, vyama vya siasa, jumuiya ya wafadhili, na wananchi kwa ujumla. Sera ya ajira itakuwa haijakamilika kama itapuuza kuwashirikisha kikamilifu wadau wote hao. Sera na mipango yoyote iitwayo ya taifa na mipango isiyozingatia ushirikishwaji wa kundi fulani la wadau ina walakini.
Sera ya Ajira ya Zanzibar ya Mwaka 2009 haikupitia ngazi hii ya ushirikishwaji kikamilifu wadau wa ajira ambao wameelezwa hapo juu. Nasema hivyo kwa kuwa mwaka 2013 – miaka minne baada ya kuanzishwa kwa sera hiyo – nilishiriki katika moja ya mikutano ihusianayo na ajira na ikatokea wengi wetu tukiwa ni wadau wa ajira hatukuwa tukiijuwa sera yenyewe, ambayo kimaandishi lazima niseme kuwa ni moja ya nyaraka zenye matumaini makubwa. Ingelikuwa tangu awali imewashirikisha wadau, basi ingelikuwa imeshaanza kuonesha matunda ya kutufikisha tunakotaka kama taifa.
Kwa mfano, katika tamko la sera hiyo ya ajira kupitia sekta ya utalii inasemwa kuwa: “Serikali itaweka mazingira mazuri yatakayohakikisha ongezeko la idadi ya wanawake na vijana wa Zanzibar wanaofanya kazi katika nafasi za utendaji katika ngazi zote ndani ya sekta ya utalii”. Tamko hili ndio kipengele kinachojulikana kama sera bainishi, kwamba serikali imeshabainisha jinsi ya kuongeza ajira kupitia utalii, lakini mkakati wake ambao ndio kipengele cha pili kijulikanacho kama sera namna ndio ambao haupatikani ama hautekelezeki.

Tuchambue kidogo hatua kwa hatua kwa kutumia mfano huu. Mkakati huu una sehemu tatu zilizoainishwa ambazo zinawezesha kufikia tamko hilo zikiwemo:

  • Ongeza hoteli za nyota tano na ubora wa huduma, na ajiri Wazanzibari katika hoteli hizo katika ngazi zote.
  • Endeleza utalii kwa madhumuni ya kuongeza ajira zaidi kwa wananchi na fedha za kigeni.
  • Ainisha vivutio vya utalii ili visaidie maendeleo ya utalii na upatikanaji wa faida kubwa kadiri iwezekanavyo.

Katika vipengele vitatu hivi, hapa tupigie mstari cha kwanza. Ni kweli wawekezaji katika sekta ya utalii wanaongezeka lakini sio kwa kazi iliyotarajiwa na sera hii. Zipo hoteli mpya kadhaa zenye hadhi ya nyota moja hadi tano, lakini mkakati wa sera hii ajira hautekelezwi kwa kuongeza ajira kwa Wazanzibari. Kwa ufupi, hakuna uwiano baina ya kuongezeka kwa hoteli na kuongezeka kwa ajira.

Kukwama kwa mkakati huo kunaonyeshwa katika takribani sheria zetu zote zinazosimamia ajira visiwani Zanzibar tangu ile ya Sheria ya Ajira Namba 11 ya Mwaka 2005, Sheria ya Uwekezaji Zanzibar Namba 11 ya mwaka 2004, Sheria ya Utalii Zanzibar Namba 6 ya Mwaka 2009 hadi Sheria ya Hifadhi ya Jamii Namba 2 ya Mwaka 2009.

Kwa mfano, sera hiyo haitekelezeki kupitia sheria inayosimamia Ajira ya Zanzibar Nambari 11 ya 2005, kwa kuwa, kwa mfano, katika sura ya tano kifungu nambari 29 (1), kunatolewa ruhusa kwa wakala wa ajira awe na leseni ili aweze kusambaza wafanyakazi kwa taasisi inayotafuta wafanyakazi, lakini kifungu hicho hakisisitizi kwamba raia wa Zanzibar ndio wapewe fursa hiyo ya ajira ili kuifanya sera hiyo itekelezeke.

Wakala amepewa ruhusa hiyo aliyopewa baada ya kukata leseni ya kumsambazia waajiri/mwekezaji, lakini ni mwajiri ndiye anayefungwa na kifungu nambari 36 (1) kinasema: “Hakuna Muajiri atakayeruhusiwa kuajiri mgeni isipokuwa: (a) endapo hakuna Mzanzibari mwenye sifa zinazotakiwa katika nafasi hiyo.”

Labda sera ingefanikiwa kupitia kifungu hiki, kwa kuwa kuna kipaumbele hapa alichopewa Mzanzibari na kwa kujenga imani kwamba kwa Zanzibar ya leo hakuna taaluma inayokosa mtu, lakini bado sera haitekelezeki kwa kifungu hiki hiki kwa kuwa amezungumzwa “mgeni” na neno mgeni kwa tafsiri iliyopo katika kifungu cha 3 (1) cha sheria hii ni: “muajiriwa yeyote ambaye si raia wa Tanzania.” Kwa maana hiyo muajiri ana khiari yake kuajiri Mzanzibari au Mtanganyika, maana neno “raia” katika kifungu hiki limetafsriwa kuwa ni “mtu yeyote ambaye ni raia wa Tanzania”.

Sasa kwa tafsiri hii ile azma ya kumwamuru muajiri atoe ajira kwa Wazanzibari ili kuifanya sera hiyo itekelezeke ni ngumu kwa sababu tayari maandiko ya kisheria yapo na yanajulikana. Hivyo ni vyema tunapoamua kutayarisha mipango endelevu kwa jamii na taifa letu tukakusanya mawazo ya walio wengi pamoja na kufanya tafiti za kutosheleza ili kuipa mipango yetu nafasi ya mafanikio. Vyenginevyo, tusilaumiane tukamsaka mchawi. Wachawi ni sisi wenyewe!

Imehaririwa na Mohammed Ghassani.

One thought on “Sera ya Ajira Zanzibar ndiye adui wa vijana”

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.