Ikiwa kuna mtu anayepata shida ya maisha katika zama hizi, basi na Mzanzibari ni mmoja wao. Huyu ni mwenye mateso ya chini kwa chini ambayo bado dunia haijayaonu labda kutokana na msimamo wake wa kidini au kutokupata nafasi ya kujitangaza kwenye vyombo vya kidunia.

IMG-20150503-WA0085Mzanzibari mpaka leo anaendelea kuteseka na ataendelea kuteseka mpaka pale Mungu atakapomtakabalia dua yake na kumshushia uokozi, lakini dua si kupiga magoti pekee. Dua ni pamoja na kufanya kazi kukipata unachokiomba.

Mvua zimekuwa zikinyesha kila mwaka na maafa yake huweza kutabirika, lakini bado mvua hizo hazijapatiwa ufumbuzi na matokeo yake zinaendelea kuwaathiri wananchi wanyonge, zikiwatia hasara kila mwaka na wengi wao hawana uwezo wa kununua vitu vipya zaidi ya kuponea majokofu na majiko ya mitumba kutoka Uingereza.

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

Serikali inakuwa na haraka sana ya kuwalaumu waliojenga maeneo ambayo hayastahiki kujengwa yanapotokea majanga kama haya ya mvua kali na mafuriko. Lakini haitaki kukiri na wengi hawajui kama suala la viwanja vya kujenga ni tatizo kubwa kwa wanyonge. Kila vikatwapo viwanja vipya huishia mikononi mwa mawaziri, wakereketwa na watoto wa wakubwa haijalishi wana viwanja vingapi hapo kabla. Wakubwa na watoto wao bado wanaendelea kupata tena na wanyonge wakizidi kuendelea kujenga nyumba na kuanzisha vijiji na miji kwenye maeneo yasiyopimwa na yasiyopangwa.

Ama baadhi ya watu wamejenga katika sehemu ambazo ni hazina ya nchi na tayari hazina hizo zimeangamia kama vile Fuoni, Kidichi, Kwerekwe, Kisauni na Machui. Wacha nazi ifikie shilingi 3,000 kwa moja na Ramadhani hii inayotujia! Minazi mingapi imeangamia katika sehemu hizi? Mabonde mangapi ya mpunga sasa yanapandwa watu? Mashamba mangapi yenye rutuba yamekuwa miji ya kisasa badala ya kuwa na chanikiwiti cha mimea ya matunda na vyakula?

Mimi nimesahau hasa wapi ilipo barua yangu ya maombi kwani nimechoka niliwahi hata kumwendea Mansour Yusuf Himidi wakati huo akiwa waziri wa ardhi na majenzi, lakini wapi haikufua dafu. Nikashukuru Mungu mtoto miye wa mnyonge nikijipa moyo kuwa kama sikupata hapa nitapata huko mbeleni tuendako najua cha kuzikiwa sitokosa.

IMG-20150504-WA0002Nikupe kituko chengine cha wakubwa mbali na hilo la kujikusanyia wao viwanja utadhani ardhi yote watazikiwa wao peke yao. Wakubwa hawa hata wanapochukuwa hiyo ardhi kama iko karibu na makaazi ya wanyonge, basi huwa adha nyengine kwa wanyonge hao. Mfano ni mbunge wa Mpendae, Mohamed Turki, aliyejenga mtaro huko Mpendae huku wakaazi wanajiuliza maji ya mtaro huo yanaenda wapi? Tembelea uone maajabu ya mtaro huo unaomwanga zaidi siasa kuliko maji machafu.

Tayari mvua ya majuzi imeua wenzetu watatu. Kuna nyumba zaidi ya 350 zimebomoka. Kutakuja pia na maradhi ya mripuko yanayotokana na makaro na majaa yaliyokaa ovyo ovyo. Maana yake ni kuwa athari ya mafuriko haya itatuandama miezi kama si miaka kadhaa ijayo na pengine mafuriko mengine yanayokuja yatatukuta hata athari za haya ya sasa hatujamaliza kuzikabili. Na mzigo huo wote ni kwa raia mnyonge, Mzanzibari masikini. Si kwa kiongozi wala kwa tajiri.

Matajiri na wakubwa kwenye serikali hawana wasiwasi na mafuriko kama haya. Mheshimiwa ambaye akisimama kwenye jukwaa anawaambia wananchi nchi yetu ni changa na masikini, akirudi nyumbani anamuusia wanawe wa kiume Silima na Vuai waowe haraka ili apate kuwaona wajukuu angali na nguvu, na watoto wakiuliza watawaweka wapi wake zao, muheshimiwa humwambia mwanawe wa mwanzo Silima achukue nyumba iliyoko Mombasa Kwa Mchina na Vuai achukue nyumba iliyoko Chukwani na ile bado kuna ile ya Tunguu ambayo itakuwa ni ya bibi yao.

IMG-20150503-WA0089Sitanii. Hayo yanafanyika katika nchi hii hii changa na masikini, Zanzibar. Sisi wacha tuishie mabondeni na milimani ambako si kwamba tunajenga bila ya serikali kujuwa. Hapana. Tunalipa vibali na kodi zite za ujenzi. Tunaachiwa kusudi kisha kubwa tunachokisubiri kutoka kwa watawala ni zawadi ya kuingiliwa na majanjawidi tutakapoamua kudai haki yetu ya kupiga kura.

Namshukuru sana Mungu kunijaalia kuwa Mzanzibari. Naipenda Zanzibar lakini serikali na viongozi wake wanawachukulia wananchi wake kama watoto wa kambu, mbumbumbu, wazungu wa reli. Wito wangu kwa Wazanzibari ni kuwa tushikamaneni ili kulitoa joka kuu.

Na kama hilo halikuwezekana, basi wakubwa niwaombe kabisa kuwa mutuletee mipira ya kondomu, kwani majanjawidi yenu tunajuwa kuwa yako mazoezini Tunguu na Kinuni. Wakitoka huko, wanakuja hapa kututia Ukimwi. Akikupenda basi, kakutia ulemavu.

Hebu jiulizeni ni taifa gani duniani linalopanga mipango na kutumia pesa kuwatesa wananchi wake zaidi ya nchi hii changa na masikini?

Imehaririwa na Mohammed Ghassani

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.