Kila ushahidi upo bayana kwamba CCM Zanzibar ipo taaban na imezidiwa kisiasa kusiko kawaida. Imemalizikiwa na silaha zote hata ille silaha yake kuu ya kisiasa ya kujitia mbwembwe za kujinasibisha na alama za uasisi na kupigania uhuru wa Zanzibar kwa kuihodhi historia ya kimapinduzi na wanamapinduzi. Alama hizo tayari zimewapotea.

Maridhiano Zanzibar
Maridhiano Zanzibar

CCM imemalizikiwa na uwanja wa vita vya kisiasa hata ndani kambi zake yenyewe na kambi hizo sasa sio salama tena kwake. Kambi zake yenyewe zimegeukia badala ya kusaidia na kuiongezea nguvu. CCM imepigwa, imepigika, inashambuliwa, inaangukia pua.Wale askari muhimu ambao iliamini ni wenzake katika vita vya kisiasa ndio waliokamata silaha nzito nzito na kuimaliza. CCM imejeruhiwa imejeruhika, imevunjwa imevunjika. Inasubiri kukata roho huku ikiwa inajipa moyo. Inaendelea kupigana, huku inaashiria haitasalim amri. Pamoja na kukatwakatwa viapande vipande na kukosa kabisa huruma ya yeyote, haijaonyesha woga, inapapatua. Jee inakufa kifo cha kishujaa au kifo cha laana?

Na Ahmed Omar
Na Ahmed Omar

CCM imesaliti urithi wa wazee wetu, wana wa Afroshirazi, waasisi wa Taifa letu, ambao waliitakia mema Nchi yetu na watu wake. Wapigania ukombozi wa Nchi hii ambao uliwachukua muda mrefu na kila aina ya jitihada hadi kufikia kumwagana damu kutafuta usawa, hadhi, heshma na ustawi wa watu wetu. CCM imeamini katika utukufu wa tabaka tawala kuliko umma ulio nyuma yake. CCM imeamini kuhodhi rasilimali na kushibisha matumbo ya tabaka tawala na watoto wao na sio shida, njaa na umasikini wa raia uliokithiri kila pembe ya visiwa hivi.

CCM haikutahayari hata kuyarejea makosa makuu mawili yaliyotendeka huko nyuma na kuwa sababu kubwa ya wazee wetu akina Hayati Karume na Mzee Moyo kupigania ukombozi wa visiwa hivi. Miongoni mwa makosa Makuu yanayotajwa na wapigania uhuru hao wa Nchi hii ambayo yalilazimisha kuja kwa Mapinduzi ya kumwaga damu ni vile wanyonge kukosa ardhi pamoja na ubaguzi wa kikabila, kiasili na kingozi katika kufaidi raslimali za Nchi yetu tukufu.

CCM imeipora ardhi iliyokombolewa na waasisi na kuimilikisha kwa tabaka tawala, watoto wao, wajukuu wao na vilembwe vyao huku raia wakibaki kuwasilisha madai mahakamani na kulipia gharama za kesi zisizomalizika. CCM inawabagua wazanzibari na kuwaweka katika mafungu na madaraja. Hawa ni waswahili na hawa ni Waarabu, hawa ni wapemba na hawa ni waunguja, hawa ni weupe na hawa ni weusi, hawa ni wazanzibari halisi na hawa si wazanzibari halisi, hawa ni wenzetu na hawa si wenzetu.

Imekuwa ikitumia misingi ya makundi iliyoyajenga na kutunga lugha za kibaguzi kwa kundi moja dhidi ya jengine. Imekuwa ikitoa ajira kwa upendeleo kwa msingi wa makundi hayo. Imekuwa ikitoa huduma za kijamii kwa upendeleo pia kwa msingi wa makundi hayo. Imekuwa ikitoa nafasi za vyeo serikalini kwa upendeleo na kufanya unyanyasaji na mateso kadhaa wa kadhaakwa msingi wa makundi hayo.

Chama cha CUF kilichoingia katika ulingo wa siasa kiasi cha miaka 23 iliyopita na kupingana na dhulma zote zinazofanywa na CCM kwa miaka zaidi ya 38, kimeungwa mkono na wazanzibari kwa kiwango kisichomithilika. Hii ni kwa sababu wazanzibari wamefahamu kwa yakini kwamba Chama hichi ndicho kilicho mbadala wa usaliti wa CCM. Ndio Chama kinachobeba matumaini yao, ndicho kilichobeba mabango ya kurejesha hadhi, usawa, heshma na umoja wa wazanzibari kwa upande mmoja, na kurejesha mamlaka ya Zanzibar yaliyoporwa kupitia Muungano wa kinafiki uliyoiweka Zanzibar kifungoni kwa miaka 51, kwa maslahi ya matumbo ya tabaka tawala na aila zao.

Pamoja na upepo wa kisiasa kuthibitisha wazi wazi bila chenga, wasemavyo vijana, CCM bado inaendelea kufanya dhulma za aina mbali mbali. Bado inaendela kuwa dalali wa Zanzibar kwa hata yale mamlaka finyu yaliyobaki ambapo kama sio Chama cha CUF yangekuwa yameshakwenda na maji. Inaendelea kufanya ubaguzi kwa kauli na vitendo. Viongozi na wanachama wao wachache waliobaki walioshibishwa chuki kwa thamani ya elfu mbili, kofia na fulana, wanaimba nyimbo za kuwabagua wazanzibari kwa rangi zao, asili zao na rangi za ngozi zao na kujidhatiti bila woga kuwapachikia mabango katika vigingi vyao yanayobeba kauli mbiu zao za kibaguzi. Inaendela kuwapiga mafungu wazanzibari ili wachukiane, wahasimiane na wapigane. Pamoja na Maridhiano yaliyoletwa na Rais Mstaafu Amani Karume na Maalim Seif ya kufuta chuki na farka, bado CCM inatamani kurejea katika zama za Komandoo.

Inaendela kuwatesa watu wasio na hatia, kuwatia ulemavu, kuwafungulia mashtaka yasio na kichwa wala miguu na wengine kuwaua. CCM imetamani tena zama zake ilipowakatakata watu wasio na hatia kwa visu, nondo na mapanga. Imetamani tena zama zake ilipokuwa ikimimina risasi katika miguu, mikono, matumbo na vichwa vya wazanzibari na kuwauwa mamia kama kuku huku wengine wakibaki na matundu ya risasi na ulemavu wa kudumu kosa lao likiwa kupigania haki na uhuru wao wa kisiasa na kidemokrasia .

Imetamani zama zake za kuwanyima wazanzibari ajira, nafasi za masomo na nyadhifa za kiserikali kwa makosa yao au ya wazee wao kuwa na asili ya kisiwa cha Pemba au kutounga mkono siasa za CCM. Imetamani zama zake za kupanga mipango ya kimaendeleo na kutoa huduma za kimaendeleo kwa kuyatenga maeneo yasiyounga mkono siasa za CCM bila ya kujali huduma hizo zinagharamiwa na wazanzibari wote. CCM imechagua tena kurejesha uintarahamwe, uharamia na ukatili alimradi tu Chama hicho kikongwe na kilichoshindwa kukidhi matashi ya umma kinaendelea kubaki madarakani.

CCM inaonekana haihitaji khatima njema, khatima ya kishujaa na kiheshima kwa kujikomboa na kujisafisha kutoka katika vazi la dhulma ililolivaa. Bila shaka CCM sio tu haimo katika maandalizi ya kukabidhi madaraka ya uongozi na hatamu za dola ya Zanzibar kwa Chama kinachoungwa mkono na wazanzibari walio wengi, CUF, lakini pia haijiandai kusalimuamri dhidi ya vitendo vyake vya dhulma na kuwaomba radhi wazanzibari kwa maovu yote iliyowatendea katika kipindi cha miaka 38. CCM haionyeshi kama inahitaji kuaga kwa heshima na kupewa nafasi nzuri ya kukumbukwa katika historia ya siasa za Nchi yetu, bara la Afrika na ulimwengu, lakini pia viongozi wake kuenziwa na kuheshimiwa pale upepo mpya wa siasa za mabadiliko ndani na nje ya Bara la Afrika unaovuma kwa kasi utakapowaweka pembeni.

CCM Zanzibar ilipotea na kuwapoteza wazanzibari, sasa bila shaka inahitaji kutanabahi kufeli kwake na kuisaka khatima njema kwa haraka iwezekanavyo.

Hata hivyo haionekani kushughulika kufanya hivyo. CCM imeshafahamu kwamba inatoweka, hata hivyo imechagua kutoweka huku ikiwa inachiria damu za watu iliyowadhulumu kwa miaka mingi na inayoendelea kuwadhulumu. Viongozi wake wanaziba macho yao na masikio yao na hawataki kufahamu kwamba ulimwengu wa Kenya, ulimwengu wa Nigeria, ulimwengu wa Cote de Voire nk katika zama hizi ni sawa na ulimwengu wa Zanzibar.

Umma katika nchi mbali mbali barani Afrika uimechoshwa na dhulma za matabaka tawala yaliyosaliti fikra za wapigania uhuru wa bara hili na badala yake wao kuasisi falsafa zao mpya za wapigania matumbo yao na aila zao. Mabadiliko tayari yanavuma kila sehemu ya bara hili na umma uko tayari kwa lolote kama ambavyo wazanzibari nao wako tayari kwa lolote alimradi matashi ya umma yachukue mkondo wake Oktoba mwaka huu.

Hii ni saa ya mabadiliko barani Afrika na duniani kote. Matabaka tawala yaliyoshindwa kusimamia maslahi na matashi ya umma na kuleta neema kwa raia yanang’oka madarakani kwa kasi ya ajabu. Demokrasia na uhuru wa raia sasa vinachukua nafasi yake. Na hivi ndivyo ninavyoiona CCM Zanzibar.

Inang’oka ikitaka isitake hata ikatumia shehena yake yote ya silaha inazozimiliki. Naishauri iondoke kwa salama, kwa khatima njema na kwa heshima vyenginevyo kilicho mbele yake ni kifo kibaya Oktoba 2015 kilichoambatana na laana za wazanzibari wadhulumiwa.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.