Waraka ufuatao umeandikwa na kijana mmoja wa jimbo la Tumbatu na kuchapishwa kwa mara ya kwanza kwenye mtandao wa Zanzibar Yetu. Ndani yake muna hoja kubwa juu ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tawala za Mikoa na Vikosi), Haji Omar Kheir, kuhusika na hujuma kwenye jimbo hilo ambalo yeye ni mwakilishi wake Barazani. Zanzibar Daima inauchapisha waraka kama ulivyo na kumtolea wito Waziri Haji ajibu tuhuma hizi dhidi yake.

Waziri Haji Omar Kheri
Waziri Haji Omar Kheri

“HUNADI mwenye kunadi, Wagomani, wa Mgambo na Wakokoni mtatangaziwa wanaume wote kuanzia miaka kumi kuendelea mfike klabu ya Nyota bila kukosa.

Ni kauli iliyozoeleka masikioni mwa wakazi wa Tumbatu Kichangani, hasa vijiji vya Gomani na Chwaka vinavyopakana – Gomani ipo kaskazini na Chwaka kusini. Sauti ya mpiga mnada, Bwana Kombo Simani, hutokea Msikiti wa Gomani.

Kwa wakazi wa mji wa Gomani, matangazo yakitokea Msikiti huu, wanajua ni miito ya watu kushiriki vikao vya mikakati ambayo, kwa masikitiko, mingi huwa ya kuhujumu Chwaka.

Klabu ya Nyota ni maarufu kwa vikao vingi vya kupanga mikakati ya kuonea wanakijiji wa Chwaka. Wakati kama huu wa kukaribia msimu wa uchaguzi mkuu vikao hufululiza.
Sasa vikao vimeanza kijijini Gomani, yalipo makazi ya Mwakilishi wa Tumbatu na ngome yake kuu kisiasa.

Kwa bahati mbaya, kila kinapofanyika kikao cha mikakati ya kisiasa, matunda yake huangukia kijiji chetu Chwaka, ngome ya Chama cha Wananchi (CUF). Nia ni kuhujumu wana-CUF.

Hujuma zinaandaliwa chini ya udhamini wa mwakilishi ambaye pia ni Waziri wa Nchi ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum, Haji Omar Kheri na Afisa Tawala Wilaya Kaskazini A, Muhammed Omar Hamad na kusaidiwa na vijana wa Gomani waliopata mafunzo katika vikosi vya SMZ na kubakia kisiwani Tumbatu badala ya kurudi kwao wakafanya kazi zao.

Kazi yao imekuwa ni kuandaa matukio ya kupachua bendera za CCM na kuchoma moto maskani za CCM na kutoa taarifa polisi ili Polisi wapate sababu ya kufika Chwaka na kukamata watu. Kwa mtindo huu wanalenga kupunguza kura za CUF.

Karibuni tu kijana Juma Haji Fumu (Juma Bwende Salmini) alichoma maskani ya CCM ya Mgambo madukani kwa Adam Ali saa 5:15 usiku akapiga kelele za “moto moto” likatokea kundi kubwa la vijana wa CCM ambao inaonekana walikuwa wamejiandaa vilivyo kutokana na wingi wao, na kupaza sauti “leo kitaeleweka makafu tutawaonesha.”

Walizunguka mji na punde wakaanza kuvurumusha mawe kwenye mapaa ya nyumba za wanakijiji Chwaka.

Fujo hizo ziliendelea kama robo saa alipotokea Sheha wa Shehia ya Gomani na kuwaamuru wananchi wakalale kwani hakuna ushahidi na mtu aliyedaiwa kuchoma moto maskani ya Mgambo, ambae wao walikuwa wakisema waliochoma ni watu wa Chwaka.

Kauli ya kuwataka waache fujo na kuhatarisha amani haikufaa kitu kwani majibu aliyopata ni kuambiwa kumbe Sheha ni CUF, hafai kwa vile hawajibiki inavyotakiwa.

Vijana wa CCM waliendelea na vurugu na uvamizi wa nyumba za watu wa Chwaka hadi kuichoma ya Salim Abdalla Salim, wakaivunja nyumba ya Juma Makame Karo na kuvunja mlango wa afisi ya jimbo la Tumbatu maarufu kama Cairo.

Baada ya watu kuamka, walipelekwa askari FFU wenye zana za kijeshi wakapambane na wakorofi. Walipewa taarifa kuwa ofisi ya Sheha wa Uvivini imevamiwa na Sheha amepigwa.

Walipofika Tumbatu walikuta mji upo shuwari, kila mtu na shughuli zake. Ni desturi kwa Tumbatu polisi hupewa habari na wakubwa kuwa kuna fujo ila kinyume chake kila askari wanapofika hukuta mji tulivu. Lengo huwa ni kuchochea watu wa Chwaka wakamatwe.

Polisi wakamhoji Sheha ambaye majibu yake yalikuwa hakuna fujo. Hata habari kuwa alivamiwa na kupigwa, aliikanusha.

Cha ajabu Polisi na waandishi wa habari walipelekwa maskani za CCM zilizodaiwa kuchomwa lakini hawakwenda nyumbani kwa Salum Abdalla ilikochomwa wala kwa Karo iliyovunjwa chumba kikiwa kozi tisa za matofali. Mali za wanaCCM ndio mali za wengine upuuzi.

Polisi wapo kwa ajili ya wapinza ni sio CCM.
Mambo hayakuishia hapo, walitafutwa vijana watano wa Chwaka na kusingiziwa kesi ya kuchoma maskani ambayo kiuhalisia ilichomwa na Juma Haji Fumu.

Wala polisi hawakuwa na barua ya Kituo cha Mkokotoni kama inavyotendwa siku zote CCM wa Gomani wakitaja tu majina ya vijana wa Chwaka yakafika Mkokotoni, basi polisi watafika Chwaka kuwakamata.

Hazikupita siku nyingi kijana wa Chwaka aliyekuwa Mkokotoni kwa shughuli zake alikamatwa na kuwekwa ndani siku mbili. Alitolewa kwa dhamana ya Sh. 100,000 bila ya kupelekwa mahakamani.

Muhamed Omar Hamad na Haji Omar Kheir walipoona hawajafanikiwa mbinu zao, ndio uliitishwa mkutano mwengine Gomani kwenye msikiti, alinadi mwenye kunadi “Wa Gomani, wa Mgambo, na Wakokoni vijana wa kiume mnatakiwa kufika klabu ya Nyota kwa mkutano muhimu” ajenda ziliwekwa wazi na huu ulikuwa mbaya zaidi kwani ajenda ya kwanza ni “Watu wa Gomani wasinunue bidhaa kwenye maduka ya Chwaka, wa Chwaka asikanyage Gomani kuanzia saa mbili ya usiku labda ambaye ana nyumba Gomani au ni kwao.”

Kali zaidi ilitolewa na msomi wa sheria Zanzibar University (ZU), Khamis Juma (Chombo) akisema “nyumba zote za watu wa Chwaka zilizoko kijiji cha Gomani zichomwe moto maana hazitakiwi kuwepo Gomani na hata watu wa Gomani wakiwa na michango yao, watu wa nyumba hizo hawashiriki maana sio watu wa Gomani kwa hiyo hazitakiwi kuwepo.”

Walipomtafuta wa kufanyiwa hivyo, hawakuafikiana, kila mmoja aliogopa kuja kumdhuru ndugu yake. Mbinu zao chafu zilipofeli ndipo wakamtuma kijana apachue bendera za CCM mchana kweupe ili wasingiziwe watu wa Chwaka. Kijana aliposhikwa na kuulizwa, alisema ametumwa na babake mdogo.

Ndipo usiku tarehe 6 Aprili jengo la ghorofa moja la Baraza la Vijana wa CUF lililojengwa kwa miti sura ya banda la kitalii, lilipochomwa moto na vijana watatu wa Gomani – mmoja askari wa Kikosi cha Mafunzo (KM), mmoja KMKM na mmoja Polisi ambao muda mwingi hubakia Tumbatu kutumika kutekeleza hujuma za CCM kijijini Chwaka.

Wamekuwa wapangaji hodari wa mipango ya fitina, mmoja akisikika akisema watachoma banda la Baraza la Vijana wa CUF kila wenyewe watapokimbilia kukata mikoko na kulijenga upya.”

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.