Kuna msemo kwamba “nia njema hairogwi”, lakini usemi huu tayari unabadilika ama, kwa usahihi zaidi, tunaubadilisha sisi wenyewe watu wa sasa. Watu wa zamani waliuamini msemo huu na hadi wanaondoka duniani walifanikiwa nao.

Rais Jakaya Kikwete akihutubia baada ya kuifungua rasmi hospitali mpya ya Kibweni.
Rais Jakaya Kikwete akihutubia baada ya kuifungua rasmi hospitali mpya ya Kibweni.

Miaka kadhaa iliyopita, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) iliweka nia ya kupunguza msongamano wa wagonjwa katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja, ndipo Kikosi chake cha Kuzuia Magendo (KMKM), ikaamua kujenga hospitali ya kisasa huko Kibweni, kando kidogo ya Unguja Mjini, ambayo ilifunguliwa rasmi na Rais Jakaya Mrisho Kikwete wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 4 Desemba 2014.

Na Ali Mohammed Ali
Na Ali Mohammed Ali

Ni kweli kuwa hospitali hiyo imekuwa kimbilio kubwa kwa wagonjwa kutoka maeneo mbalimbali ya kisiwa cha Unguja. Ndani ya kipindi hiki kifupi imeonesha umahiri kwa mujibu wa uwezo wa madaktari walionao zaidi ikisifikana kwa matibabu ya macho.

Lakini nia hii njema ya serikali yetu inaonekana sasa kuanza kurogwa, hasa kwenye suala la kuifanya hospitali hiyo kufikika na kutoa huduma kwa wote. Kama tunavyojua hali zetu za kimaisha za Zanzibar, ni asilimia chache ya raia wanaomiliki vipando vya moto kama usafiri na wachache zaidi ndio wenye uwezo wa kutumia usafiri wa kukodi. Maana yake ni kuwa idadi kubwa zaidi ya raia ni wale wenye uwezo wa ama kupanda daladala au njia nyengine za usafiri kama baiskeli, marikwama au miguu kufika hospitalini hapo.

Aliyekuwa Waziri wa Afya wa Zanzibar, Juma Duni, akihutubia kwenye ufunguzi wa hospitali mpya ya Kibweni.
Aliyekuwa Waziri wa Afya wa Zanzibar, Juma Duni, akihutubia kwenye ufunguzi wa hospitali mpya ya Kibweni.

Watu wanaotumia usafiri wao wenyewe na au wa kukodi wafikapo katika hospitali hii huzunguka upande wa nyuma kwenye lango kubwa ambapo huruhusiwa kuingiza magari yao na kuegesha bila malipo wala bughudha ya aina yoyote kutoka kwa walinzi wa eneo hilo. Hata wale waliokuwa wakitumia daladala hadi katikati ya mwezi wa Aprili 2015, hawakuwa wakipata kwani kuna vituo vya daladala pande zote za barabara.

Sasa kuanzia katikati ya mwezi Aprili 2015, daladala zimekuwa haziruhusiwi kusimama hapa kwenye vituo hivi. Vituo ambavyo hutumiwa zaidi na wagonjwa kwa sasa, wengine wakiwa mahamumu sana na hawana uwezo wa kukodi usafiri binafsi.

Bila ya shaka, serikali haiwezi kuwa haielewi kwamba daladala ni usafiri wenye sheria zake, ambazo moja ya sheria zake ni kushusha watu katika vituo vinavyotambulika kisheria. Ndio pia usafiri wa harakaharaka huwezi kumwambia dereva wa daladala akupelekee mgonjwa wako ndani ya hospitali wakati ndani kuna abiria wengine ambao pia wana haraka ya kufika waendako.

Kwa mantiki hiyo, zuilio hili la daladala kutosimama pale kwa sababu za kiusalama kwa kambi ya jeshi hilo la majini haliingii akilini, maana sote tunafahamu kwamba eneo lolote lenye kambi ambayo inaaminiwa kwamba inatunza usalama wa nchi kuna masafa yake maalum ambayo raia huwa hawatakiwi kuishi katika eneo hilo.

Rais Jakaya Kikwete akikata utepe kuashiria kuzinduliwa rasmi kwa hospitali mpya ya Kibweni.
Rais Jakaya Kikwete akikata utepe kuashiria kuzinduliwa rasmi kwa hospitali mpya ya Kibweni.

Lakini kwa kambi hii ya jeshi la wanamaji, limekosa masafa hayo tangu awali kwa kuwa kwake karibu sana na makaazi ya watu. Hivyo kama ni makosa yalifanywa tangu wakati kambi hiyo inaanzishwa, au kugawiwa viwanja vya watu kujenga baada ya kambi hiyo kuanzishwa.

Yawezekana yalitokea haya kwa yale yale makosa makubwa yanayotukabili ya kutokuwa na mashirikiano ya karibu baina ya mamlaka zetu wakati tunapoamua kuanzisha kitu ambacho kinazihusu mamlaka zaidi ya moja. Kwa kufanya hayo ndio kero kama hizi hutokea.

Rai yangu ya kwanza, jeshi la KMKM lisimamishe hatua yake ya kuzizuia daladala kusimama pale katika vituo vya Kibweni. Badala yake waweke ulinzi kuhakikisha usalama wa kambi unapatikana ili kuwapunguzia usumbufu wagonjwa wanaofikia hospitalini hapo kwa ajili ya matibabu. Kwa sasa, wagonjwa na wazee wanapata shida sana, kwani daladala zinasimama Kibweni Msikitini kama unatokea Bububu na kama unatokea Mjini, basi husimama kwenye duka la “ Madawa Spice” la zamani.

Rai yangu ya pili, KMKM iangalie mazingira mengine ya kuihamishia kambi hiyo, kwa kuwa kambi hiyo kwa sasa imekuwa karibu na majumba ya raia wa kawaida. Bado tunayo maeneo mengi ambayo ni mazuri kwa kambi yetu hiyo. Hili litaisadia kupunguza hasama baina ya raia waishio karibu na kambi hiyo na jeshi hilo.

Tukifanya hivyo, kutasaidia kuijengea misingi endelevu ile nia njema ya SMZ kuanzisha hospitali hiyo ya kisasa ya Kibweni.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.